SoC02 Tuwekeze zaidi kwa watoto na vijana kwa maendeleo ya Tanzania ya baadaye

Stories of Change - 2022 Competition

Philombe Jr

New Member
Apr 24, 2021
4
3
TUWEKEZE ZAIDI KWA WATOTO NA VIJANA KWA MAENDELEO YA TANZANIA YA BAADAE

Nianze na methali maarufu ya samaki mkunje angali mbichi,hivyo ndivyo tunavyotakiwa tufanye nchini kwa kutumia rasilimali watu tukiegemea zaidi kwa watoto na vijana kwa ajili ya Tanzania ya baadae. Kwanini watoto na vijana kwasababu katika umri wao tunaweza kuwabadili kupitia maarifa bora ambayo tutawapa na kupata wataalamu bora sana kwa maendeleo ya Tanzania. Kupitia umri wao kama tutawekeza kwa nguvu zote Tanzania yetu itakuwa bora. Uwekezaji gani sasa tufanye kwa hili rika?

Uwekezaji ambao naulenga hapa ni wa kiafya na kimaarifa kuanzia mtoto anazaliwa hadi kufikia kupata elimu.

Serikali kushirikiana na Wizara ya Afya wanatakiwa kushirikiana kuhakikisha mazingira salama ya mtoto tangu anazaliwa hadi anafikia kupata elimu ya awali. Wizara ya Afya kwa dhati sana izidi kuendelea kutoa elimu kwa wazazi kabla ya kuzaa na baada ya kuzaa na kuhakikisha watoto wanazaliwa katika mazingira mazuri na kupata huduma zote za kiafya, kukaa pamoja na wazazi na kuwaeleza mahitaji mazuri ya mtoto ili awe na afya njema ni jambo zuri sana mana mtoto huyu ni nguvu kazi kwa taifa letu. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali iwekeze kwenye maarifa kupitia kwenye taasisi zetu kama vile shuleni na vyuoni.

Serikali inapaswa kuwekeza nguvu nyingi kwa ajili ya kulitayarisha wimbi la nguvu kazi ambalo litakua na msaada kwa Tanzania ya baadae. Serikali inapaswa kushirikiana na wadau mbali mbali wa elimu katika kuhakikisha wanatoa elimu iliobora kwa ngazi zote. Tunapaswa kuwekeza kwenye ujuzi bora na sahihi kwa nyakati sahihi, lazima tukae na kutathmini mfumo wetu wa elimu na kujiuliza elimu hii itaweza kuinufaisha Tanzania baada ya miaka fulani?

Elimu hii itaweza kutoa wahandisi, madaktari, wanasheria, wanasayansi, viongozi na wataalamu mbali mbali waliobora na wenye uzalendo katika kulikuza taifa letu? Jibu hapa lina ukakasi kwasababu tunaona elimu yetu bado haijawa na ubora tangu elimu ya awali. Idadi ya wanafunzi ni wengi ukilinganisha na madarasa, miundombinu ya elimu ni kidogo pamoja na wakufunzi wakiwa wachache.

RAI YANGU JUU YA UWEKEZAJI KWA WATOTO NA VIJANA

Serikali kuwekeza zaidi kwenye Afya ya mtoto.

Kwa pamoja tushirikiane kwenye kutoa elimu na kuhamasisha kuhudhuria klinik pale mzazi anapopata ujauzito. Wizara zizidi kuwahimiza wazazi na kutoa elimu ili tu watoto waweze kuwa na maendeleo mazuri kabla na hata baada ya kuzaliwa. Kwasababu mtoto ili baadae aweze kupokea maarifa vizuri ya msingi na hata ya baadae inachangiwa hata na ukuwaji wake tangu mdogo, hivyo mazingira bora ya ukuwaji yanachangia sana mtoto baadae kuja kuwa na uwezo mzuri wa kujifunza. Kuhamasisha wazazi kuwapatia chanjo watoto na kuhimiza kuhudhuria klinik na kuwapa mafunzo basi kutachangia watoto kuzaliwa wakiwa na afya njema.

Serikali kuja na mpango wa kuboresha miundombinu ya maeneo yanayotolewa elimu.
Tunaweza kuweka malengo na mipango ya miaka 5-10 kwamba kufikia mwaka 2030 tuwe tumeshajenga mfano madarasa laki 2 Tanzania nzima. Serikali inapaswa kuweka mipango ili kuweza kupata madarasa yalio mengi ambayo yataweza kuwaweka wanafunzi na kusoma katika mazingira yalio mazuri.

Tunashuhudia uwingi wa wanafunzi nchini kwenye madarasa tunaona kwamba kwa kweli wanafunzi hawapati elimu kabisa kama inavyotakiwa ndio mana watoto wengine huishia njiani. Wito wangu serikali ishirikiane na wadau mbali mbali waje na mpango huu viongozi wa mikoa mbali mbali kushirikiana na wananchi waje na mradi wa "Jenga Darasa" basi hakika tutakua na miundombinu mingi sana ambayo wanafunzi wataweza kusoma kwenye mazingira yaliomazuri.

Kuwatengeneza wataalamu mbali mbali huanzia kwenye mazingira ya darasani hivyo madarasa yakiwepo mengi watoto watapata kuelewa na wote kwenda safari moja kuliko uwingi wa wanafunzi ambao wachache tu huelewa nini kinafundishwa.

Serikali kuhakikisha inatoa nguvu kazi ya wakufunzi waliobora kabisa kwa ajili ya kutoa elimu iliobora.
Mradi mwengine wa kuwekeza ni kwenye kutoa wakufunzi ambao wanamapenzi na ukufunzi. Wakufunzi bora ni maslahi mazuri ya Taifa kwasababu watahakikisha malengo ya taifa kupitia mitaala yake inafikiwa kwenye kiwango kinachotakiwa. Kuwapa mara kwa mara elimu na maarifa mapya ili kuzidisha maarifa ni jambo ambalo nalipendekeza. Wakufunzi wafundishe stadi laini kama uvumilivu na uwajibikaji kama kawaida inavyokua uwalimu ni wito hivyo waweze kwa pamoja kufanikisha malengo ya taifa kwenye elimu ili mwanafunzi anapotoka kwenye hatua moja kwenda nyengine awe ameweza kujifunza na kupata maarifa yenye ubora zaidi.

Serikali kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwa mashirika binafsi kwenye Elimu.
Wawekezaji binafsi wa ndani na kutoka maeneo mbali mbali duniani wahamasishwe watiwe moyo kwa kuwekewa mazingira yaliobora ili waweze kuwekeza zaidi kwenye Elimu. Hali hii itachangia kuienga mashule na kuweza kuzalisha wanafunzi waliobora kwenye hatua mbali mbali za elimu. Mazingira mazuri ya uwekezaji nchini yanachangia watu mbali mbali kuwekeza nchini kwa kujenga miundombinu ya kutoa elimu jambo ambalo lina tija kwa Taifa letu.

Serikali kuwekeza na kutilia nguvu kwenye ujuzi sahihi kwa nyakati sahihi.
Ujuzi ambao tunapaswa kuwekeza ni ujuzi ambao taifa litafaidika kwa kubadilika kwenye uzalishaki na pia kwenye ujuzi ambao utasaidia watu waliokuwepo na hata wanaokuja, utasadia wanafunzi ambao wapo shuleni na vyuoni na hata waliomaliza. Pia tuwekeze kwenye kutoa ujuzi ambao mhitimu ataweza kujiajiri au kuwaza mitazamo mengine tofauti na serikali.

Tunataka Tanzania ya kiteknolojia, Tanzania ya maendeleo baada ya kipindi fulani ili kufikia huko hatuna budi kuwandaa watoto wetu kwenye ujuzi sahihi kwa nyakati hizi tulizonazo. Tunataka Tanznia yenye nguvu kazi ambayo itakuja na mabadiliko kuanzia ngazi ya chini hadi juu Hayo yatafikiwa baada ya nyakati fulani kama Tanzania itatoa ujuzi sahihi kuanzia tangu Elimu ya awali hadi vyuoni. Wanafunzi wote wa Tanzania lazima watayarishwe kwenye misingi ya kiteknolojia na ya Ujasiriamali. Baada ya kupata elimu ya msingi ya awali ya kusoma na kuandika, na kupewa maarifa kupitia masomo ya darasani hadi kupata elimu ya ubobezi chuoni basi tuhakikishe kwenye safari hiyo mwanafunzi anafundishwa masomo ya Tehama na Ujasiriamali.

Serikali kuwekeza kwenye elimu ya juu
Elimu yetu ya juu inatakiwa kupitiwa baadhi ya fani zinazotolewa kwasababu bado hazimpi kijana chaneli mbali mbali za kuangalia ili aweze kujikwamua kimaisha. Katika elimu ya juu tunapaswa kumjenga mwanafunzi kwa kumpa maarifa ambayo yanaweza kumuacha kwenye kufikiria lazima muajiri awe serikali na kumuelekeza kwamba hata yeye anaweza kutafuta fursa kupitia utatuzi mbali mbali wa matatizo yaliokuwepo kwenye jamii zetu. Serikali kupitia mavyuoni na kukagua fani itasaidia watu kusoma fani sahihi kwa nyakati sahihi.

Nahitimisha kwamba kwa maslahi mapana ya taifa hili hatuna budi kutengeneza rasilimali watu kwa kuwapa mazingira mazuri ya kusoma. Hali hii kwa kushirikiana na wakufunzi tutapata nguvu kazi kwa uwingi ambao wataweza kujiajiri na kuajiriwa ila kwenye kufanya kazi kwenye kiwango kilichobora. Serikali ihakikishe inataoa elimu iliobora kwa wazazi ili mtoto azaliwe salama, kupatikane miundombinu mingi kwa kutolea elimu na wakufunzi watayarishwe kwa ajili ya kusomesha kwa kutoa elimu iliobora.
 
Back
Top Bottom