Tuwazomee wanaotaka DART wapewe wageni

Nyombesi

Member
Aug 19, 2014
53
5

Tuwazomee wanaotaka DART wapewe wageni

Na Mussa Mkama

Nimesoma kwa makini makala ambayo ilitoka katika gazeti moja la kila siku iliyoandikwa na anayejiita Mwandishi Wetu, iliyokuwa na kichwa cha habari “Serikali imebariki ufisadi wa UDA?” nimejiridhisha pasi na shaka kuwa mwandishi wa makala hiyo ni kuwadi wa watu ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakipinga kampuni ya wazawa ya Simon Group kuuziwa hisa za UDA.
Kwanza mwandishi huyo ameendelea na ‘wimbo’ uliopitwa na wakati wa madai ya kipuuzi kuwa uuzwaji wa hisa za UDA kwa Simon Group haukufuata taratibu na sheria, na pia kwamba haukuzingatia thamani halisi ya shirika hilo.

Ni bahati mbaya sana Mwandishi huyu na watu wa aina yake wamekuwa wakitumia taarifa za kuokoteza uchochoroni. Nataka nimwambie wazi Mwandishi huyu kuwa ni kupoteza muda kuhoji juu ya umiliki wa UDA kwasababu hakuna kinachoweza kubadilika kwani taratibu na sheria zote zilizingatiwa kikamilifu wakati wa uuzaji wa hisa za UDA kwa Simon Group.

Nataka nimwambie Mwandishi Maalum na watu wengine wanaodai kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa sheria na taratibu wakati wa ubinafsishaji wa UDA eti kwasababu Baraza la Mawaziri halikuhusishwa au kwamba hapakuwa na mwakilishi wa serikali wakati wa ubinafsishaji huo, hawajui walisemalo.

Maamuzi yote kuhusu ubinafsishaji wa UDA yalifuata na kuzingatia kikamilifu Memorandum and Articles of Association ya shirika hilo. Ikumbukwe kuwa UDA limesajiliwa na mamlaka ya usajili wa makampuni (BRELA) kama kampuni chini ya sheria ya makampuni (Cap. 212).

Sasa huo ufisadi unaodaiwa kufanywa na Simon Group uko wapi? Huko siyo kuchafua watu bila sababu za msingi? Kwanini wahusika hawaweki wazi ajenda yao ya kutetea maslahi ya mfanyabiashara rafiki yao anayeitaka UDA kwa udi na uvumba?

Lazima watanzania waelewe kuwa uamuzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuuza hisa zake kwa kampuni ya Simon Group ulikuwa haukwepeki. Ni ukweli usiopingika kwamba, kwa hali mbaya ya fedha iliyokuwa ikiikabili UDA kabla ya kuuzwa kwa kampuni ya Simon Group ni wazi shirika hilo lisingeweza kuendelea kusimama.

Shirika halikuwa na uwezo wa kujiendesha na wala serikali kuu na Halmshauri ya jiji la Dar es Salaam hawakuwa na uwezo wa kulikwamua kutoka kwenye matatizo ya kifedha yaliyokuwa yakilikabili.

Tangu mwaka 1985 wakati serikali ilipoipa Halmashauri ya jiji asilimia 51 ya hisa za shirika la UDA, Halmashauri ya jiji haikuwekeza mtaji wowote ndani ya UDA, na kadhalika serikali haikuendelea kutoa fedha kulisaidia shirika hilo , na tangu wakati huo UDA imekuwa ikipata hasara kubwa na kudidimia kiuchumi.

Mpaka kufikia Juni, 2010, UDA ilikuwa na limbikizo la hasara ya sh. 2,566,468,229, hivyo kulifanya shirika lianze kudidimia na kukosa uwezo wa kutimiza malengo yake ya kutoa usafiri bora na wa uhakika kwa wananchi wa Dar es Salaam .

Wakati Simon Group ilipouziwa UDA kulikuwa na mabasi kati ya 4-5 yenye kutembea barabarani, na kwa hali hii wananchi wa Dar es Salaam hawakuwa na manufaa yoyote wanayopata kutokana na uwepo wa UDA au umiliki wake kuwa chini ya serikali na Halmashauri ya Jiji, vyote hivi havikuwa na faida yoyote kwao.

Simon Group wameonyesha kwa vitendo dhamira yao ya kulifanya shirika la UDA litekeleze majukumu yake kikamilifu, wameonyesha dhamira yao ya kuwapatia wananchi wa Dar es Salaam usafiri bora na wa uhakika zaidi.

Mpaka sasa Simon Group tayari wamenunua mabasi zaidi ya 400 ambayo yapo barabarani jijini Dar es Salaam yakihudumia wananchi na mengine 600 yanaendelea kutengenezwa viwandani huko India na China. Je, huyu mwandishi maalum haoni dhamira hiyo ya Simon Group?

Umefika wakati sasa watanzania tuelezane ukweli. Watanzania wanapaswa kutambua ukweli kuwa shida ya wananchi wa Dar es Salaam siyo nani anamiliki UDA, shida ya wananchi wa Dar es Salaam ni usafiri bora na wa uhakika.

Wananchi wa Dar es Salaam wanataka kuona adha ya kugombea usafiri nyakati za asubuhi wanapokwenda kazini na jioni wanaporejea nyumbani inakoma mara moja, wanataka kuona watoto wao hawasumbuliwi tena na makondakta wanapokwenda na kurudi shuleni, wanataka kupanda basi kwa wakati wanaotaka na kufika makazini kwa wakati.

Aidha, tunapenda kumuuliza Mwandishi Maalum na watu wengine wanaopinga uuzwaji wa UDA, walikuwa wapi wakati shirika hilo lilipokuwa hoi kifedha na kuelekea kufirisika? Walikuwa wapi wakati UDA ikiwa imechoka na kushindwa kununua mabasi mapya na kubaki na mabasi manne tu tena machakavu na hivyo kushindwa kuwahudumia wananchi?

Walikuwa wapi wakati UDA ikiwa taabani kifedha kiasi cha kushindwa kujiendesha na kuwalipa wafanyakazi wake na kuamua kuuza au kukodisha baadhi ya mali na rasilimali zake kwa wafanyabiashara wa kigeni ambao baadaye walitaka kuuziwa shirika, na sasa wanawatumia watu wengine kupinga uuzwaji wa shirika baada ya kukataliwa kulinunua?

Kwanini watu hawa hawakuanzisha kampeni maalum wakati huo ya kuichangia UDA ili ikuze mtaji wake na iweze kujiendesha? Wanapata uzalendo leo wanapoiona UDA inanawiri baada ya kuchukuliwa na mwekezaji mwenye mapenzi ya kweli kwa nchi yake na watanzania wenzake? Huu kama siyo unafiki na choyo ni nini basi?

Huu ndiyo udhaifu wetu watanzania, tunapigana vita wenyewe kwa wenyewe kwa kuwanufaisha wageni. Kelele zote hizi kuhusu uuzwaji UDA zinatokana na ukweli kuwa aliyenunua ni mswahili, mtanzania mweusi ambaye kwa mtazamo wa wafanyabiashara wa kigeni hastahili kumiliki uchumi wa nchi yake.

Jambo la pili ambalo Mwandishi Maalum amelitilia nguvu katika makala yake ni kutaka UDA isipewe fursa ya kumiliki mradi wa DART kama itaomba. Kwa maneno yake mwenyewe mwandishi huyo angependa mradi huo wapewe wageni badala ya wazawa, aibu juu yake na anapaswa kuzomewa na kila mtanzania anayejitambua.

Hata hivyo kwa ufinyu wa akili na fikra mwandishi huyo ameshindwa kujenga hoja kwanini UDA wasipewe mradi huo.
Mwandishi huyo anadhani UDA inategemea huruma ya uzawa ili kupata haki ya kumiliki mradi huo, na ndio maana anasema katika makala yake kuwa serikali isiangalie uzawa wakati itakapotangaza zabuni ya kuendesha DART bali sifa za waombaji.

Kitu asichokijua ni kwamba UDA haijivunii uzawa tu bali sifa zingine ikiwemo uwezo wa kifedha na ushahidi wa hilo unaonekana wazi kwani UDA ya sasa ni tofauti kabisa na ilivyokuwa miaka mitatu iliyopita kabla ya kuuziwa Simon Group.

Halafu nataka kumpa taarifa Mwandishi huyu mbumbumbu kuwa serikali zote makini duniani zinawapa kipaumbele kwanza wananchi wake na wageni huangaliwa baadaye. Hata huko Ulaya na Marekani anakodai Mwandishi huyu kuwa matajiri wa kiarabu wanapewa nafasi, raia wa nchi hizo hupewa nafasi ya kwanza na hao wageni huangaliwa baadaye.

Kukimbilia kauli za kisiasa za Abbas Mtemvu ama Adam Malima badala ya kujenga hoja nani apewe mradi huo wa DART ni usahahidi mwingine kuwa mwandishi huyo hakuwa na hoja, ni kuwadi wa maadui wa kibiashara wa Kampuni ya Simon Group ambayo ni mwanahisa mkuu katika UDA.

Ni vema Mwandishi huyu mbumbumbu na kuwadi wa wageni aelewe kuwa serikali haiendeshwi kwa kauli za kisiasa, chuki na ubinafsi za mtu yeyote. Serikali haiwezi kuinyima zabuni UDA ya kumiliki DART kwa kuwasikiliza watu kama Mbunge wa Temeke Abbas Mtemvu au Naibu waziri wa Fedha Adam Malima.

Suala la zabuni ni la kanuni na utaratibu, ikiwa UDA wanakidhi vigezo kwanini wasipewe mradi huo? Au kwa vile ni waswahili wenzetu? Kuwa Mtanzania imekuwa nongwa!

Ieleweke kuwa uamuzi wa wamiliki wa dala dala mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mwenyekiti wa DARCOBOA Sabri Mabrouk wa kuunganisha nguvu na UDA ili kupata fursa ya kumiliki mradi wa DART ni uamuzi wa kizalendo na wa kuigwa na watanzania wote.

Watanzania tunapaswa kaungana kiuchumi ili tuweze kupata fursa si tu ya kumiliki DART bali kumiliki uchumi wa nchi yetu. Kama tutaweza kushinda zabuni ya kumiliki mradi wa DART itakuwa ni fursa nzuri kwa watanzania wote kwani fedha zote zitakazopatikana kutoka na mradi huo zitabaki hapa hapa nchini.

Ni vizuri watanzania wakaelewa kuwa UDA na wamiliki wa daladala wana mitaji mikubwa ambayo inawawezesha kushinda zabuni ya mradi huo. Kuungana haimaanishi kuwa hawana mitaji bali ni muhimu kwenye jambo kama hilo kushikamana pamoja kama watanzania dhidi ya wageni ambao watajitokeza kuomba zabuni ya kuendesha mradi huo.

Halafu kuna dhambi gani UDA kuunganisha nguvu na watanzania wengine kwa lengo la kumiliki uchumi wa nchi yao? Hivi ni dhambi viongozi wetu wa serikali kushuhudia na kuunga mkono jambo kama hilo?

Ni kipi kilichomsukuma mwandishi huyo kuwatukana Waziri Hawa Ghasia na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadick ni kushiriki kwao kwenye halfa ya utiaji saini mkataba wa UDA na wamiliki wa daladala au kuna lingine?

Mwandishi huyo anataka serikali kujitenga mbali na UDA kwa madai ya kizushi na umbeya kuwa uuzwaji wake ulikuwa wa kifisadi? Kwa hakika huu ni wendawazimu mkubwa. Hivi mtanzania mzalendo anapotumia fedha zake kuboresha huduma za usafiri na kuwekeza nchini mwake ni ufisadi huo?

Eti anahoji chanzo cha fedha za mtaji wa Mwenyekiti Mtendaji wa Simon Group Robert Kisena! Hii ni akili ya ajabu sana. Kwanini mwandishi huyu hajahoji utajiri wa hao wageni anaotaka wapewe mradi wa DART? Je, anajua mahali walikopata fedha hao wageni anaotaka tuwamilikishe mradi tulioujenga kwa fedha zetu?

Ni vema kibaraka huyu wa mabeberu wa Ulaya na Marekani akajipange aje na hoja zenye mashiko lakini siyo huu ujinga na upuuzi aliotuandikia. Nataka nimwambie kuwa huwezi kuzuia mvua isikunyeshee kwa viganja vya mikono. Hawezi kuzuia UDA na wamiliki wa dala dala wasipate mradi wa DART kwa fitna za kizushi na umbeya. Angoje aone nani atashinda zabuni ya mradi wa DART.

Mwisho.
 
Back
Top Bottom