SoC01 Tuutokomeze Ukeketaji: Tubadili mbinu za kuutokomeza katika umri mdogo

Stories of Change - 2021 Competition

Dr Restart

JF-Expert Member
Jul 15, 2021
3,298
17,155
Februari 6 kila mwaka, dunia nzima huadhimisha siku ya kupinga Ukeketaji wa wanawake baada ya Baraza la Umoja wa Mataifa kuipitisha mnamo mwaka 2003.

Je, ukeketaji ni nini?
Ni kitendo cha kukata na kuondoa sehemu ya nje ya viungo vya uzazi wa mwanamke haswa kinembe.
Kitendo hiki hufanyika na mtaalamu wa jadi maarufu kama Ngariba.

Pamoja na jitihada nyingi za serikali na wadau mbalimbali katika kuutokomeza ukeketaji, lakini bado ukeketaji upo katika kiwango kikubwa. Na kama juhudi hazitaongezwa basi ukeketaji hautokaa uhitimike.

Mwanadamu ni kiumbe kilichojaliwa akili nyingi na Mwenyenzi Mungu. Unavyombana katika jambo moja ndivyo anavyozidi kutafuta namna ya kuliendeleza jambo husika katika njia nyingine. Ndivyo ambavyo imetokea kwa wanaofanya ukeketaji.

Kipindi cha nyuma, Ukeketaji ulikuwa ukifanyika kwa mabinti wanaotayarishwa kwa ajili ya ndoa. Lakini, baada ya serikali na wadau kupiga kelele pamoja na kuandaa sheria kali kwa wote wataohusika na 'unyama' huo basi walibadili mbinu za kuuendeleza.

Badala ya ukeketaji kufanyika kwa mabinti wakubwa basi sasa unafanyika kwa watoto wadogo kabisa ambao bado hawajajitambua. Hii ni kwa sababu, uwezekano wa mabinti kukataa kukeketwa wakishakuwa wakubwa ndiyo sababu haswa inayosababisha kuwaangukia mabinti wadogo.

Kinachofanya Ukeketaji kutofikia tamati ni kwa kuwa sababu za kuukataa hazijawashawishi haswa wanaoufanya. Sababu hizo zinakosa hoja hivyo kuonekana kwamba hazina mantiki na kuwapa nafasi ya kuendelea kuufanya.

Wataalam na serikali imekuwa ikitoa sababu za kupinga kwa kutaja athari za ukeketaji. Nitaeleza sababu hizo kwa ufupi na hoja za wanaoundeleza.

1. Ukeketaji huweza kusababisha kifo kwa damu nyingi kumwagika wakati na baada ya tendo. Wataalam wanadai kuwa Ukeketaji husababisha damu nyingi kumwagika. Na hivyo kuhatarisha uhai wa muathirika.

Hoja za Wakeketaji:
Miaka nenda rudi, wamekuwa wakiufanya. Haijawahi kutokea kifo kisababishwacho na Ukeketaji. Hiyo ni kutokana na ukweli kuwa hakuna mishipa mikubwa inayoweza kukatwa na kupelekea umwagikaji wa damu. Ngariba moja nilimuhoji akanieleza kuwa tangu akiwa binti mpaka sasa anapofanya Ukeketaji hajawahi kushuhudia kifo kilichosababishwa na kitendo hicho.

2. Ukeketaji husababisha maambukizi ya magonjwa ya zinaa kwa kushirikisha vifaa. Wataalam wanaamini kuwa kitendo hushirikisha matumizi ya viwembe na visu kwa watu wengi hivyo kufanya uwezekano wa maambukizi kuwa kikubwa.

Hoja:
Kila mtu hutumia wembe wake na kufanya uwezekano wa maambukizi kutokuwepo. Ngariba husafisha mikono yake punde akishamaliza kumkeketa binti mmoja kabla ya kuendelea na mwingine.

3. Maumivu makali wakati wa ukeketaji ni moja ya sababu za kupinga. Kwamba binti hupata maumivu makali sana.

Hoja:
Maumivu ni ya muda na kamwe hayadumu. Ni kama kuanguka na kukwaruzika ukucha kung'ooka. Utaumia sana lakini baadae hupoa.

4. Matatizo wakati wa kujifungua ni kawaida kwa wanawake waliokeketwa.

Hoja:
Wanawake wao wengi wanajifungulia nyumbani bila usaidizi wa Madaktari. Wakunga wa jadi hufanya hivyo bila ya changamoto yeyote juu ya upokeaji wa mtoto.

5. Uharibifu wa eneo la nje la uke kwa kuondoa kinembe wakati wa ukeketaji.

Hoja:
Siyo uharibifu kwa kuwa haimuathiri, ni kama mwanaume kuondolewa govi. Wanachombeza juu ya sera ya Usawa. Kila kifanyikacho kwa mwanaume pia kifanyike kwa mwanamke.

Athari zote zilizoelezwa hapo juu zina mantiki lakini hazishawishi wahusika kuachana nayo kabisa.

Je, nini kifanyike?
1. Serikali na wadau waanze kutoa sababu zenye mashiko. Sababu hizo ni;
a)Athari za kisaikolojia kwa waathirika. Kutokana na utandawazi, wanawake wanapoingiliana na mitandao hukutana na maumbile tofauti na yao. Hali hiyo huwasababishia maumivu makali kisaikolojia. Na kwa bahati mbaya sana tatizo hili haliripotiwi.

b)Unyanyapaa kwa kutoolewa na wanaume ambao hawapo tayari kuukubali hali halisi ya kuwa wamekeketwa. Kuna wanawake ambao hawajaolewa kwa sababu tu wenzi wao walitambua kuwa wamekeketwa. Na hata akiolewa, mumewe atachepuka kwa kisingizio kuwa hawana utamu kama wale ambao hawajakeketwa.

c) Kutopata ladha halisi ya mapenzi wakati wa kujaamiana. Ukweli ni kwamba kinembe kina nafasi kubwa sana katika kuleta msisimko wakati wa tendo la ndoa. Na kukosekana kwake kunapunguza msisimko na hivyo kutoleta raha.

2. Serikali itunge sheria kali sana kwa wale wote wataobainika kufanya ukeketaji. Mangariba pamoja na wazazi wote wawili wahusike katika adhabu hizo. Ngariba hawezi kumkeketa binti bila mzazi wake kuridhia. Hivyo wote wawajibike.

3. Ukaguzi wa mara kwa mara wa wanafunzi kipindi cha masomo yao. Kila mwanafunzi wanaporudi kutoka likizo wakaguliwe kama hawajakeketwa. Na kama wamekeketwa daktari aripoti kwa serikali na hatua za kisheria zifuate.

4. Kuwepo na zawadi kwa yeyote atakayeripoti tukio la ukeketaji kabla halijatokea. Hii itatoa motisha kwa jamii kulindana na hatimaye kuutokomeza.

5. Elimu na nguvu kubwa sana zielekezwe vijijini ambapo ndipo kuna kiwango kikubwa sana cha ukeketaji. Serikali iache kuandaa semina sehemu za mijini. Waingie huko kijijini kuwafikia walengwa wakubwa.


Mwisho, niipongeze serikali na wadau mbalimbali kwa jitihada zao nyingi katika kupambana na Ukeketaji. Lakini, jitihada za makusudi zinahitajika endapo tunataka kufikia tamati.

Tanzania bila Ukeketaji Inawezekana.
 
Back
Top Bottom