TUMEKWISHA:Wizara, taasisi na halmashauri zakiuka Sheria ya Manunuzi

Kasheshe

JF-Expert Member
Jun 29, 2007
4,694
787
Kwa mtindo huu, mimi nimeshajikatia tamaa wazalendo wenzangu!!!! Tunafinga point watu wachache kumbe jamii nzima imeoza....

origina document should be this

Kwa hisani ya Habari Leo
Joseph Lugendo
Daily News; Saturday,March 21, 2009 @20:10
Wizara, halmashauri na taasisi mbalimbali za umma, zimegundulika kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004, imefahamika. Kwa mujibu wa Jarida la ‘Tanzania Procurement Journal' la Februari 28, mwaka huu, linalotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), Sheria hiyo imekuwa ikikiukwa katika vipengele ambayo hutumika kudhibiti karibu asilimia 70 ya matumizi ya fedha za Bajeti ya Serikali. Sheria hiyo imekiukwa katika ununuzi wa bidhaa na huduma mbalimbali kwenye ofisi 14 za umma zilizofanyiwa ukaguzi, zikiwamo wizara, taasisi za umma, halmashauri na ofisi za wilaya mbalimbali nchini katika ununuzi uliofanyika Mwaka wa Fedha 2007/2008.

Hata hivyo udhaifu huo wa kufuatwa kwa Sheria hiyo umeonekana kutofautiana katika ofisi hizo, ambapo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, ndiyo iliyoongoza kukiuka sheria hiyo katika asilimia 75 ya ununuzi wake. Ofisi nyingine zilizokiuka Sheria hiyo kwa sehemu kubwa ya ununuzi ni Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko ambayo imekiuka Sheria hiyo katika asilimia 72 ya ununuzi wake na Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo iliyokiuka Sheria hiyo katika asilimia 66 ya ununuzi. Ofisi iliyokiuka Sheria hiyo kwa sehemu ndogo ya ununuzi wake ni Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), iliyokiuka kwa asilimia 27. Nyingine ni Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA) asilimia 33, na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, asilimia 40.

Zilizokiuka Sheria hiyo kwa wastani ni pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani asilimia 43, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) asilimia 48, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Mawasiliano (TCRA) asilimia 53, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa asilimia 58, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili asilimia 60 na Wizara ya Sayansi na Teknolojia asilimia 64. Udhaifu huo, umegundulika baada ya kufanyika kwa ukaguzi wa maofisa wa PPRA katika ununuzi uliogharimu mabilioni ya fedha yaliyofanywa na ofisi hizo. Aidha katika jarida hilo, maofisa hao walionyesha vipengele ambavyo vimetia doa utekelezaji wa Sheria hiyo kwenye ofisi hizo.

Moja ya vipengele vya Sheria hiyo vilivyokiukwa ni, kipengele cha taratibu inayozitaka ofisi hizo kutangaza zabuni za ununuzi ili kukwepa ununuzi wa bidhaa unaofanyika kinyemela bila kuwa na ushindani au ‘kupeana'. Kwa mfano katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kati ya ununuzi wa bidhaa na huduma mbalimbali zipatazo 516 zikiwamo zabuni mbalimbali, ni zabuni saba tu, ndizo zilizotangazwa katika vyombo mbalimbali vya habari. Nyingine zilitolewa bila kutangazwa. Kipengele kingine kilichokiukwa ni cha kuitaka bodi ya zabuni na mamlaka stahili kuidhinisha ununuzi wa bidhaa na huduma kabla ya ununuzi huo kutekelezwa.

Kwa mujibu wa jarida hilo, katika Halmashauri hiyo ya Jiji la Dar es Salaam, kati ya zabuni na ununuzi wa bidhaa na huduma 516, ni saba tu zilinunuliwa baada ya kupata idhini ya bodi ya zabuni na mamlaka stahili. Aidha ukaguzi uliofanyika TRA, uligundua kuwa ofisa ambaye kwa nafasi yake ana mamlaka ya kuidhinisha ununuzi wa mahitaji yasiyozidi Sh milioni 50 kwa mwaka bila idhini ya bodi ya zabuni, aliidhinisha ununuzi wenye thamani ya Sh milioni 441, bila ridhaa ya bodi hiyo.

Pia ilibainika kuwa ununuzi katika baadhi ya ofisi hizo, umekuwa ukifanyika bila kuweka kumbukumbu sahihi. Kwa mfano katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kati ya ununuzi wa huduma na bidhaa 519, ni saba tu ambazo zina kumbukumbu katika mafaili ya halmashauri hiyo. Udhaifu mwingine uliobainika katika utekelezaji wa Sheria hiyo ni kwenye uundwaji wa Kitengo cha Ununuzi wa Umma (PMU). Katika baadhi ya ofisi, mkuu wa kitengo hicho amekuwa akiripoti kwa ofisa ambaye hawajibiki kimadaraka kuidhinisha ununuzi wa bidhaa na huduma zinazohitajika, tofauti na matakwa ya sheria kuwa mkuu wa kitengo hicho, anapaswa kuwajibika kwa ofisa anayeidhinisha ununuzi.

Kwa mfano, katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, mkuu wa kitengo hicho aliwajibika kwa mweka hazina wa halmashauri ambaye hana mamlaka ya kuidhinisha ununuzi wa bidhaa na huduma. Aidha katika Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, kitengo hicho kilikuwa hakijaanzishwa kabisa na katika Wizara ya Mambo ya Ndani na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), idara zilijiamulia kutekeleza ununuzi wa mahitaji yao bila kukipa taarifa kitengo hicho.

Hata hivyo jarida hilo limefafanua kuwa, kati ya February 16 na Machi 4, 2009, maofisa wa PPRA, walifanya ufuatiliaji wao kuangalia utekelezaji wa matakwa ya Sheria hiyo, ambapo iligundulika kuwa wastani wa ukiukwaji wa Sheria hiyo umekuwa ukipungua kwa baadhi ya ofisi za umma. Ofisi hizo ni pamoja na Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, ambako kiwango cha ukiukwaji wa Sheria kilipungua kutoka wastani wa ukiukwaji wa Sheria katika asilimia 76 ya ununuzi ya mwaka 2007 mpaka wastani wa asilimia 31 ya ununuzi wa mwaka huu.
 
Kwa nini kama sheria zinakiukwa wasichukuliwe hatuwa za kisheria na wahukumiwe? au hizo sheria zilizokiukwa hazina hukumu?
 
Back
Top Bottom