Tujikite katika Mijadala na si Matusi kuelekea Uchaguzi Mkuu Octoba, 2015.

S.N.Jilala

JF-Expert Member
Jan 26, 2012
540
507
TUJIKITE KATIKA MIJADALA NA SI MATUSI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU, OCTOBA, 2105.

Na: Simon Jilala
20/8/2015

Je, ni kwa nini mashabiki/wanachama na hata wakati mwingine viongozi wa vyama vinavyoenda kushiriki katika uchaguzi mkuu October, 2015 hawajikiti kwenye hoja wakiwa ama wanahojiwa na vyombo vya habari au wakiwa majukwaani na hata wakiandika kwenye mitandao ya kijamii hawajadili kwa undani maswala ya Kijamii, Kiuchumi na Kisiasa zaidi ya jazba na matusi wakati mwingine?.

Kwa kifupi, wengi wamejikita katika propaganda zaidi, haya ndo mambo ya msingi ya kujadili kwa sasa au kuna mambo mengine muhimu tunatakiwa kuyajadili wakati huu kuelekea uchaguzi mkuu?. Kuna mijadala ipi ni muhimu wakati huu ambako kampeni zimekaribia kuanza?. Mimi nadhani; Mijadala ambayo ingetakiwa iwepo kwa muda huu kabla ya kampeni kuanza ipo sana. Kwa hiyo, nawaza kwa mapana kabisa kuwa mambo haya Sita ni kati ya mambo ya msingi ambayo wachambuzi, wananchi, na viongozi wa vyama wangetakiwa sana kuyajadili kwa upana wake.

1. Ilani za vyama vyote vilivyo na mgombea katika nafasi ya Urais.

Ilani ya vyama vyote ingetakiwa iwe iko wazi kabisa na wananchi wanayo. Mosi, ingesaidia sana kwa wananchi wetu kuanza kuisoma ili kuona uhalisia uliomo kwenye ilani ya vyama hivi vishiriki. Pili, ingesaidia sana kwa wachambuzi wetu kuanza kuchambua vyema ilani hizo kama kweli zinaendana na mahitaji ya wananchi wa Tanzania. Kwa sasa ni tofauti kidogo, kila kona tunajadili mambo ambayo ni kama mashabiki wa Mpira tu, yule kamla chenga mchezaji fulani badala ya kujikita katika hoja zenye mantiki.

Kusema kweli, sijasikia kabisa na wala sijaona ilani ya chama chochote ama kwenye mitandao zaidi ya kusema wameshatoa tayari ilani. Katika ilani, sidhani kama ni siri kuijua mapema ili wananchi waweze kuziona na kuzitafakari vyema na waweze kufanya maamuzi sahihi.

2. Uwezo wa kila mgombea katika kujenga hoja.

Hili nalo linagusiwa kidogo sana na wachambuzi wa maswala ya kisiasa, lakini angalau wanajaribu kuchambua kadri ya uwezo wao. Mimi naona haitoshi kusimama kwenye majukwaa na kutuhubiria kuondoa umasikini. Swali la msingi sana hapa ni; utauondoaje umasikini?, lazima swala la ilani ya chama hapa liwepo kwa uwazi kabisa. Lazima mgombea aijue ilani ya chama chake vizuri ili atuambie ni kwa namna gani ilani hiyo atafanikisha endapo atachaguliwa kuwa mgombea wa URAIS.

Pindi tukiona kuna hoja muhimu upande wa pili, wengi naona kwa sasa kama hatuna hoja anaanza matusi badala ya kutetea upande wake na ilani ya chama chake. Kwa nini wagombea wetu tusiwaandalia midahalo kama Kenya, U.S.A na nch zingine ili kuwaona mawazo yao maana nje ya ilani ya chama lazima mgombea tumjue uwezo wake wa kujenga hoja na kuelezea mambo ya nje na ndani kwa ufasaha kabisa.

3. Rekodi za kila mgombea kabla ya kugombea nafasi nyeti kabisa ya URAIS.

Hili nalo kidogo naona wengi wanaliongelea pamoja na wagombea wenyewe. Je, alishawahi kutiwa nguvuni kwa ajili ya wizi?. Je, kuna jambo gani mgombea alishawahi kulifanya hapa nchini kweli tunashawishika Watanzania kuona anafaa kuwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?. Je mgombea ni mvumilivu vya kutosha?, maana tukipata mgombea ambaye si mvumilivu na tukamuweka katika nafasi ya URAIS atatupeka ambako siko, haya yote yanahitaji mijadala ya wazi. Uzuri rekodi zipo, watu wangewajadili vyema pasipo kutoa lugha za matusi kwa kila mgombea ili kujua ni nani hasa atatufaa kati ya waliojitokeza.

4. Muda wa kujadili itikadi za kila vyama ndio huu.

Mijadala mingi muda huu ningetegemea tuanze KUTUJADILI kwa uwazi kabisa itikadi za vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi mkuu. Kwa mfano, tukisema CCM inafuata itikadi ya Mrengo wa Kijamaa, iko hivyo kinadharia na ki vitendo?, Je CHADEMA wanaposema wao wanafuata Mrengo wa Kati, wakifuata Ujamaa wa Kidemokrasia ( Wakichukua yaliyo mazuri) na Wakichukua pia yaliyo mazuri kutoka katika Uliberali.

Je, ni vipimo gani wanatumia kujua haya ya Ujamaa ni mazuri au mabaya na ya kiliberali kuna mazuri na mabaya?. Haya mambo yangeweza sana kupanua ubongo wa wananchi kuliko ushabiki mwingi wa mashabiki, wanachama na viongozi wa karibia vyama vyote uliojaa matusi, kebehi, na maneno ya kuokoteza kuhusu chama fulani badala ya mijadala ya ndani kabisa ili kujua kila chama kinataka kutupeleka wapi, au kimetutoa wapi. Je, kilikotutoa kinasitahili kutuongoza?. Kama hakisitahili ni kwa nini?.

5. Njia gani vyama vilitumia kupata wawakilishi katika nafasi za URAIS, Ubunge, na Udiwani?.

Kila chama unakuta kuna lawama ndani ya wanachama kuhusu utaratibu uliotumika kupata wawakilishi wa nafasi za ubunge. Haya mambo yangehitaji mijadala zaidi. Unakuta watu wanakuwa wakali kuwa utaratibu chama chetu kilifuata lakini hawataji kiundani ni utaratibu upi katika chama unatakiwa ufuatwe na kweli ulifuatwa?. Zaidi ya hapo, migongano mingi iko katika lawama kila chama, na hapo ndipo Msamiati ''KUKATWA'' umeibuka kwa kasi sana. Haya mambo tungekuwa tunayajadili kwa kina yangesaidia sana katika kupanua mawazo kuliko kuwa na wigo mfinyu katika namna chama chochote kinavyopata wagombea wa nafasi zake. Na mijadala ya wazi ingepunguza hata lawama ya kusema Mimi nimekatwa badala ya kujua hatua gani chama kinapitia kabla ya uteuzi wa mwisho?. Hii mijadala ingetusaidia sana kuwa na uelewa mpana kuelekea uchaguzi. Mkuu.

6. Tutawajuaje viongozi ambao si wala rushwa?

Swali hili pia lingehitaji mijadala mingi, maana kila kona katika kura za maoni tulisikia kuna baadhi ya wagombea tena wengi walijihusisha na rushwa kupata nafasi za kuteuliwa. Je, mianya ndani ya kutoa rushwa ndani ya chama itawezaje kuthibitiwa?. Kwa nini Jamii ya Kitanzania kwenye mijadala ya wazi wawe viongozi, wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanakemea rushwa lakini wakati mwingine wanapenda rushwa?. Kwa nini wananchi wanawachukia wala rushwa lakini wanapokea rushwa kutoka kwao na kuwachagua pia.

Kwa nini tumefika hapa tulipo katika maswala ya rushwa. Nini nafasi ya vyombo vya kudhibiti rushwa katika CHAGUZI zikifika?. Je, wanatenda katika haki au kuna upendeleo?. Mifumo ya rushwa itazibibwaje?. Haya mambo yanahitaji mijadala ya wazi na yenye kutoa majibu yaliyo bora na sahihi ili umma uweze kujifunza. Naamini, elimu ya uraia ina nguvu sana katika kumwelimisha Mwananchi wa kawaida.
 
Mbona hamutuelewi?Tunazidi kusisitiza miaka 53 ya uhuru umaskini unazidi. matadhi yanazidi.Ujinga unazidi.Mbona ardhi tunayo na watu tunao?kinachokosekana hapa ni sera nzuri na uongozi bora.Ulizia wazee wa n
Nyerere watakueleza hayo.Hata mjenge majukwaa. ya dhahabu.Mwaka huu hakuna atakayeendelea kusikiliza sera za kuendelea kutuibia.Mwanaume atajulikana october.
 
Mbona hamutuelewi?Tunazidi kusisitiza miaka 53 ya uhuru umaskini unazidi. maradhi yanazidi.Ujinga unazidi.Mbona ardhi tunayo na watu tunao?kinachokosekana hapa ni sera nzuri na uongozi bora.Ulizia wazee wa n
Nyerere watakueleza hayo.Hata mjenge majukwaa. ya dhahabu.Mwaka huu hakuna atakayeendelea kusikiliza sera za kuendelea kutuibia.Mwanaume atajulikana october.
 
Back
Top Bottom