Tujifunze Kombe la Dunia 2010

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
KATUNI%28205%29.jpg

Maoni ya katuni



Hatimaye michuano iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa ya Kombe la Dunia imeanza jana nchini Afrika Kusini. Michuano hii itakayofikia ukomo Julai 11, ni mikubwa kuliko yote ya soka duniani.
Sisi tunaona kwamba hii ni fursa ya aina yake. Historia haionyeshi kwamba hapo kabla, bara la Afrika liliwahi kupata bahati kama hii ya kuandaa michuano ya Kombe la Dunia.
Lakini, mwaka huu, licha ya kuwahi kuibuka mizengwe mingi kutoka kwa baadhi ya mataifa makubwa ya Ulaya, Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), chini ya uongozi wa rais wao Sepp Blatter, lilisimama kidete na hatimaye michuano hiyo ikaanza kwa kishindo jana nchini Afrika Kusini, katika ardhi ya Afrika.
Sisi tunaona kwamba hii ni bahati ya mtende kuota jangwani. Ni bahati ya pekee ambayo bara hili iliikosa kwa muda wote wa miaka 70 tangu kaunzishwa kwa michuano hiyo ya Kombe la Dunia.
Hata hivyo, wakati nasi tukiungana na Waafrika wengine katika kufurahia fursa hii adimu, tunaona kwamba kuna haja ya kuwakumbusha Watanzania wote, na hasa wanasoka, kwamba tusiishie kufurahia Kombe la Dunia bila kuambulia faida nyingine zaidi ya hiyo ya kicheko kitokanacho na burudani.
Tunaamini kwamba wachezaji wetu watapata mafunzo ya kutosha katika kipindi cha mwezi mzima, wakiiga mbinu za kucheza kitimu, nidhamu uwanjani, umakini wa kuzuia na kupachika magoli na kila zuri litakaloonyeshwa na wachezaji wa kiwango cha juu watakaoshiriki katika michuano hiyo.
Na ‘utamu’ wa michuano hii kwa wachezaji wetu unaongezwa na ukweli kwamba baadhi ya nyota watakaoshiriki, walishawahi kuja nchini na kucheza dhidi ya timu yetu ya taifa, Taifa Stars.
Kaka, Robinho, Maicon, Lucio na Ramires ni miongoni mwa wakali wa Brazil waliokabiliana na Taifa Stars wiki iliyopita. Drogba, Eboue, Kallou na Dindane wa Ivory Coast waliwahi pia kucheza dhidi ya Stars Januari 4 mwaka huu, kama ilivyo kwa mshambuliaji Samuel Eto’o Fils, Rigobert Song, Alexander Song na Geremi Njitap, waliowahi kutua nchini na kucheza dhidi ya Stars katika michuano ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Ghana mwaka 2008.
Kwa sababu hiyo, tunaamini kwamba wachezaji wetu watakuwa makini zaidi kufuatilia uchezaji wa wakali waliotuzidi katika viwango vya soka ili siku moja, nasi tuwe miongoni mwa mataifa yanayoshiriki fainali za Kombe la Dunia; badala ya kuwa mahiri katika kuchagua timu za kushangilia.
Mbali na wanasoka wetu, sisi tunaona kwamba hata viongozi wa klabu za soka na wale wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) watakuwa na la kujifunza kuhusiana na umakini wa hali ya juu katika kuandaa michuano mbalimbali. Waamuzi wa soka nao watakuwa na ‘darsa’ tosha la namna ya kuchezesha kwa haki na kujionea madhara ya kupuliza filimbi zao kwa upendeleo.
Tunaona kwamba mashabiki nao hawataambulia patupu. Watajifunza namna nzuri za kushangilia na kuzipa moyo timu zao. Wataona vilevile namna wenzao waliofika katika fainali hizo za Kombe la Dunia watakavyohimili shinikizo la kufungwa kwa timu zao.
Viongozi wa Serikali na waandishi wa habari za michezo halikadhalika. Nao hawatakosa la kujifunza kupitia michuano hii ambayo hufanyika mara moja kila baada ya miaka mine, sambamba na polisi na maafisa wa usalama ambao watajionea moja kwa moja kupitia televisheni jinsi wenzao wanavyofanya kazi katika viwanja vya soka.
Kwa mifano hiyo ya wale watakaonufaika kupitia fainali za Kombe la Dunia , ni wazi kwamba wadau wote watakuwa makini katika kufuatilia na kupata kitu fulani bora cha kuiga kwa manufaa ya soka letu katika siku za usoni.




CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom