SoC03 Tuamke tuchukue nafasi zetu

Stories of Change - 2023 Competition

Lai leo

New Member
Jul 18, 2023
2
2
Jamii inatarajia kuona maendeleo katika kila eneo hasa kwa vizazi vijavyo.Wazazi wanajitahidi kuhakikisha watoto wao wanapata elimu bora na mahitaji muhimu ya kila siku,hata wale wenye kipato cha chini hawako nyuma kuhakikisha watoto wao hawabaki nyuma kielimu.

Katika ulimwengu huu wa teknojia, sayansi na maendeleo ya kasi,Watanzania hatuko nyuma kuhakikisha tunaenda sawa na wengine duniani kufikia pale mataifa yaliyo endelea yalipofikia.

Wazazi wanawapeleka watoto wao shule kwa matarajio ya kufuta ujinga na kujifunza mambo kadha wa kadha ambayo wazazi na walezi wanaamini yanapatikana katika elimu kupitia mfumo wa elimu n mtaala ambao tunao hivi sasa hapa nchini Tanzania.

Inapaswa kwa wazazi na walezi kujiuliza kama ni kweli watoto wao wanajifunza shuleni hata yale ambayo baadhi ya wazazi na walezi hawana muda wa kuwafundisha shuleni.

Je, vipi kuhusu watoto wanaokaa shuleni na kurejea nyumbani wakati wa likizo pekee?Wanapata elimu kuhusu maisha kwa ujumla na kujitambua wao na mabadiliko ya miili na hisia zao?Kwa sehemu kubwa jibu ni hapana na wameachwa wajifunze na wajue wenyewe kuhusu maisha na nini wanapaswa kufanya.

Watoto wa kike na wa kiume wanapaswa kuandaliwa kwaajili ya leo na kesho kwa ujumla na sio ki elimu pekee bali pia kwa kujuzwa wanatakiwa kufanya nini ili kujenga taifa la baadae lenye nidhamu, heshima na hofu ya Mungu na haitoshi tu kuwaambia waende kwenye nyumba za ibada bila kuwaeleza kwa uwazi juu ya ulimwengu wa kidigitali tulionao hivi sasa.

Binafsi nadhani umefika wakati wa mfumo wa elimu wa Tanzania kuweka vipindi maalumu katika masomo ya kila siku shuleni ambavyo vitafundisha kuhusu kuwa mwanaume na kuhusu kuwa mwanamke katika dunia hii yenye changamoto nyingi sana.Ni jambo la kuhuzunisha sana kusikia jinsi ambayo wavulana wanalawitiwa na wasichana wanavyopata mimba katika umri mdogo.

Tunaweza kuendelea kusema haya yote yanasababishwa na utamaduni wa kigeni na kwetu haupo lakini ukweli ni kwamba tunakwepa kutatua tatizo na kutafuta visingizio kwasababu sio wageni wanayafanya kwetu bali ni sisi kwa sisi.

Serikali inapaswa kujua kwa dalili hizi kizazi kinachofuata baada ya hichi kitakuwa na hali mbaya kimaadili kuliko hiki cha sasa kama isipochukua hatua madhubuti ili kunusuru kina baba na kina mama wa baadae.

Kufumba macho na kutupa lawama upande wa pili hakuwezi kutengeneza kizazi bora kijacho.Wazazi nao wanatakiwa kuwa wazazi kweli kweli na kukaa chini na watoto wao kwa uwazi bila kisingizio chochote kile na kuwaeleza ukweli wa dunia hii ya sasa.

jukumu la baba na mama kuongea na watoto wao kuanzia ngazi ya chekechea na kuwaambia jinsi ya kujitambua na kujua kusudi la maisha yao.

Viongozi wa dini nao wanatakiwa kufundisha haya mambo kwa uwazi ili kunusuru kizazi cha sasa na kinachokuja,nyumba za ibada zifundishe yanayotokea bila msukumo wa vyombo vya habari kwa kuwa vitabu vitakatifu vimekataza.

Yakemewe haya kwa nguvu kama mambo mengine yanavyotiliwa mkazo katika nyumba zetu za ibada.Vijana wakijua nafasi zao na wajibu wao katika jamii watafanya yanayowapasa na hizi habari za kulawitiana na na mimba za utotoni na mengine mengi ya kusikitisha yatapungua kwa kiasi kikubwa.Mvulana hawezi kukubali kulawitiwa kwasababu yoyote ile na msichana vivyo hivyo.

Serikali, wazazi, walezi,viongozi wa dini na jamii kwa ujumla,umefika wakati muafaka wa kuandaa watoto wetu kwa ajili ya leo na kesho yenye manufaa kwao.

Tukishirikiana kwa pamoja katika kuwafundisha na kuwaelekeza huku tukiwa tunawasikiliza tutajenga taifa lililo bora na lenye misingi imara. Sote tukichukua nafasi zetu na kuzitumia vizuri lazima tutakula matunda mema ya malezi bora tuliyopanda kwa watoto wetu.

Tuondoe uzembe na tamaa zilizokithiri, ubinafsi na kutokuwa na kiasi ambavyo vimetawala mioyo ya wengi kwa sasa kwasababu ni tishio kubwa kwa taifa letu kwani vinazidi kudidimiza misingi ya taifa letu bora.

Vyombo husika vikifuatilia kwa makini na kuchukua hatua kali bila kujali cheo au nafasi aliyonayo mtu katika jamii dhidi ya wahusika wanao wapa mimba na kulawiti watoto tutapiga hatua kubwa katika kuandaa taifa la kesho.

Jamii ikiondoa ubinafsi na kuona watoto wote ni wa jamii nzima,hakuna boda boda ambaye atamrubuni msichana wa shule, hakuna mwalimu ambaye atathubutu kumlaghai mwanafunzi awe wa kike au wakiume na kumtendea ukatili wa kijinsia, hakuna baba mtu mzima ambaye atadiriki kufanya ngono na wasichana wadogo wala kuwalawiti wavulana wadogo kama atawachukulia kama wa kwake binafsi, hakuna kumbi za starehe ambazo zitaruhusu watoto wadogo chini ya miaka kumi na nane, hakuna mfanya biashara ambaye atathubutu kuuza vileo kwa wote walio chini ya umri, hakuna viongozi wa serikali watakao puuza kufuatilia na kukemea tabiae hizi chafu, hakuna mhudumu wa afya ambae atapindisha ukweli pale atakapotakiwa kutoa taarifa sahihi za vipimo vya kitaalamu.

Tushirikiane kwa pamoja kujenga taifa la kesho bora kuliko la leo.Serikali, wazazi, walezi na jamii kwa ujumla tufanye wajibu wetu kila mmoja kwa nafasi yake kutokomeza mmomonyoko wa maadili ambao umekithiri kwa sasa.
 
Back
Top Bottom