The Buzwagi Saga: Karamagi aenda kusaini Mkataba wa ULAJI London

mugongo *2 lete hoja za Karamagi. Acha kuyeyusha, tupo makini na tunatizama pande zote!!!

FD
 
Kwa hilo Nampa Heshima yake; ukiondoa chuki yake (aliyoionyesha dhahiri) dhidi ya Chadema, napenda kuongeza kuwa mawazo tofauti ndio hufanya maamuzi kuwa ya busara zaidi. Hatuko hapa kudanganyana kwamba wote tunachukia kilichoendelea bungeni; wapo wanaona ni sahihi kilichofanyika kama mugongo na wengine niliopata kuwasikia, wapo pia wanaona sio sahihi (kama wengi wana Jambo) lakini vyovyote vile tunavyotofautina ni lazima tuwe makini kuweka hoja mbele na ubinafsi nyuma. Hongera Mugongo kwa kutokuwa mwepesi wa kujibu tuhuma binafsi; natumai utaendeleza na hoja.

Sijasoma hoja za Field Marshall ES juu ya hili...yupo vacation nini?

Haswa mtu wangu!
 
Ninadhani kuwa hayo mashirika 60 yasiyokuwa ya kiserikali hayashabikii chama chochote.

Inawezekana wasishabikia chama chochote moja kwa moja, lakini wana wajibu na haki ya kuunga mkono harakati za mabadiliko na hoja za msingi zinazotete nchi hata kama zimetolewa na chama cha siasa. Again, hawa watu wa NGO ni binadamu wenye utashi na sioni ni kwa nini wasichague upande katika siasa kama ambavyo wanaweza kuwa na uchaguzi katika mambo mengine katika maisha. Hata nchi zingine sio jambo la ajabu kuona taasisi fulani ya kiraia ikishabikia na kuunga mkono chama cha siasa dhidi ya kingine. Why should be a sin in TZ? haya mambo ya kutenganisha siasa na NGO, na hii slogan ya non-political ndio inayofifisha kustawi kwa demokrasia ya vyama vingi katika nchi yetu. Sasa watu wanaofanya kazi serikali tunasema wasishabikie vyama, watu wa taasisi za kiraia nao tunasema no, hivi ni akina nani hao ambao tunawaachia hivi vyama vya siasa? Halafu wakipewa akina Makamba ukatibu mkuu tunashangaa?
 
Nyani,

Hata mie ninaenjoy presence yake maana kama utakumbuka vizuri enzi za business times.... this guy anaresemble character moja hivi ambayo kwa sasa ninaitunza.

Mie siko vexed by whatever the heck anafanya ila napush to the limit ambayo atarudia kufanya yale aliyofanya kipindi kile alichokumbwa na kashfa ya wizi wa mitihani....

.....tih teh tih teh tih teh.....

Waandishi bongo wanamaslai ya kisiasa. Kwa kuangalia waandishi (walioula) kwa kukabidhiwa wilaya na sehemu nyingine, nadhani hii ni tatizo!
 
Comimg to the issue of not doing research. Hivi ni mbunge gani anayeweza kusimama kifua mbele kujinadi kuwa yeye anafanya research zaidi ya ZITTO KABWE. Zitto sio mbunge kasuku kama tuliowazoea. Kama kuna kitu kinachompa nguvu kifikira ni hili la kujisomea na kufanya research. Actually researching ndio hobby yake kubwa zaidi ya siasa.

Wajanjawajanja ndio wanapenda kutumia neno la research kupunguza uhalali wa hoja makini wakati wao ndio mabingwa wa kutoa hoja za kikasuku.

Ni ajabu kwa wabunge waliokimbilia kudai kuwa KARAMAGI hajadanganya kuhusu maslahi ya taifa katika mkataba wakati hata huo mkataba wenyewe hawajauona. Halafu wana guts za kumhukumu Zitto kuwa hajafanya research.

Nina wasiwasi hii yote ya kumsimamisha Zitto ubunge inaweza ikawa mbinu ya maadui wa MTANDAO ndani ya CCM kusabotage legitimacy ya JK kwa wananchi. Kama wamefanya hilo kwa mpango maalum ama bahati mbaya lakini ni wazi wamefanikisha hilo. Wametumia mbinu ya kuua ndege wawili Zitto na JK kwa jiwe moja.

Sijui nini kitakachofuata dhidi ya Zitto lakini ni wazi kwa JK wameshafanikiwa.

Tanzanianjema

Nakupa tano ndugu, wabunge wengi wa ccm hata elimu hawana, niimesoma cv zao nyingi ni certificate in ---- 3m0nths sweden or botswana nk,na ukada mwingi mwisho ubunge hatimaye uwaziri kwa njia ileile ya kubebana, sasa how do you expect wafanye research ya mambo? kwanza na uzee(majority) hata uwezo wa kufikiri hawana, isitoshe hata mikataba yenyewe wakipewa wasome hawata ielewa. hii ndo athari ya bunge letu, hawajui hata wanachosupport
 
Huyu bwana mudhihiri mudhihiri msameheni hana kosa kwanza
hata elimu yake ni ndogo na inamtosha ye na familia yake ndio maana yuko dar muda wote akijua ubunge ni wa familia yake,,hata sasa anapoangaika na shule pale open..kisa kahahidiwa cheo fulani
ni moja ya matokeo ,,,ma prof kuleni vichwa washenzi kama hawa
wawe na adabu,,pili jamani kweli tutafika kwa style hii jamani haya
mungu tumwachie mwenyewe natumaini anaona yote na kwajina la yesu ipo siku wananchi tutachoka mheshimiwa jakaya kikwete na familia ya El mtakapoamini kumbe mungu yupo,,,tutachoka nakuamua jambo msiloamini kutafuta haki zetu

Huyo Mudhihir nyie muacheni tu, acheni tu akatalie dar, hivi kwa mama yake (kwao) mmepaona? tangu aanze kuwa madarakani na kubebwa kote angeshweza hata kumjengea mama yake a decent house kwa kipato tu halali, lakini kama hata hilo kashindwa unadhani akili yake ni nzuri? uswahili na uhuni umemzidi, shame on him! selfish.
 
Hoja ya mheshimiwa Zitto, nitaiweka hapa.

MAELEZO YANGU KUHUSU HOJA YA KUUNDWA KAMATI TEULE YA BUNGE KUCHUNGUZA MAPITIO YA MIKATABA YA MADINI NA MAZINGIRA YA KUSAINIWA KWA MKATABA (MDA) MPYA WA MADINI WA BUZWAGI KULIKOFANYWA NA WAZIRI WA NISHATI NA MADINI MHESHIMIWA NAZIR KARAMAGI (MB) HUKO UINGEREZA MWEZI FEBRUARI 2007.
{Kanuni 104(2)}

1. Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa kunipatia fursa ya kuleta hoja hii hapa kwenye Bunge lako Tukufu kwa mujibu wa kanuni zetu za Bunge. Kuletwa kwa hoja hii, bila kujali maamuzi ya kuhusu hoja yenyewe, ni ishara tosha ya ukomavu wa demokrasia yetu ambayo inakuzwa na mijadala ya Bunge lako Tukufu. Nakupongeza kwa dhati kabisa kwa juhudi zako za kuliimarisha Bunge letu na kujenga muhimili imara wa ulinzi wa demokrasia ya vyama vingi nchini kwetu.

2. Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 16/7/2007 mara baada ya hoja ya Waziri wa Nishati na Madini kuamuliwa na Bunge lako Tukufu nilisimama mahala pangu na kutoa taarifa ya kukusudia kuleta hoja ya kuunda kamati teule ya Bunge. Nilisema kama ifuatavyo (kwa mujibu wa kumbukumbu sahihi za Mijadala ya Bunge), ninanukuu ‘…… naomba kutoa taarifa rasmi …… kwamba nakusudia kuleta hoja ya kuunda Kamati Teule kuchunguza mkataba mpya wa Madini ambao Waziri wa Nishati na Madini ameusaini bila kuzingatia maagizo ya Rais (wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) ya kupitia mikataba ya Madini aliyoyatoa mbele ya Bunge lako tukufu tarehe 30 Desemba, 2005. Mwisho wa kunukuu.

3. Mheshimiwa Spika, nimeshawasilisha hoja yangu hii kwa maandishi kwa Katibu wa Bunge na sasa nawasilisha rasmi katika kikao hiki cha Bunge kwa uamuzi. Nimezingatia kanuni 104 (2) katika kuwasilisha hoja yangu.

4. Mheshimiwa Spika, katika maelezo yangu niliyowasilisha Bungeni wakati wa mjadala wa Hotuba ya Waziri wa Nishati na Madini siku ya tarehe 16/7/2007 nilihitaji maelezo kutoka serikalini katika masuala makuu mawili yafuatayo:

i. Kusainiwa kwa Mkataba mpya wa wa Madini wa mgodi (mradi) wa Buzwagi kati ya serikali na Kampuni ya Barrick na sababu za mkataba huo kusainiwa nje ya nchi, London Uingereza na vilevile kwa nini mkataba huo umesainiwa wakati bado serikali inafanya durusu (review) ya mikataba kufuatana na maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndugu Jakaya Mrisho Kikwete.
ii. Kuondolewa kwa kipengele katika sheria ya kodi ya mapato ya mwaka 1973 kuhusiana na asilimia 15% ya ‘capital allowance on unredeemed qualifying capital expenditure’ bila ya kibali cha Bunge lako Tukufu.

5. Mheshimiwa Spika, wakati akijibu hoja zangu Waziri wa Nishati na Madini alijenga hoja zake kama ifuatavyo,

a. Kusainiwa kwa Mkataba wa Mgodi (Mradi) wa Buzwagi.

6. Mheshimiwa Spika, Wakati akijibu hoja yangu kuhusiana na suala la Mkataba mpya wa mgodi wa Buzwagi, Waziri wa Nishati na Madini amenukuliwa na kumbukumbu za majadiliano ya Bunge akisema kama ifuatavyo, nanukuu,

“Mheshimiwa Spika, katika tathmini ya Migodi, Mgodi wa Buzwagi ni marginal mine ambao uhai wake si wa muda mrefu. Bila ya kutumia fursa ya sasa ya bei ya Dhahabu uwekezaji wake usingeweza kuwa wa faida. Hata hivyo, Mkataba wa Buzwagi hauna mapungufu yaliyokuwamo kwenye mikataba ya zamani”. Mwisho wa kunukuu.

7. Mheshimiwa Spika, Kwanza kabisa napenda nilikumbushe Bunge lako Tukufu kuwa Rais alikwishapiga marufuku kusainiwa kwa mikataba mipya ya Madini mpaka hapo sheria za madini zitakarekebishwa. Akisoma hotuba ya Wizara ya Nishati na Madini mnamo tarehe 17/7/2006, Waziri wa Nishati na Madini Mheshimiwa Ibrahim Msabaha alilitaarifu Bunge kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amezuia kusainiwa kwa Mikataba mipya ya Madini. Nimeambatanisha Hansard ya siku hiyo kama uthibitisho wa kauli hiyo. Sasa inakuwaje Waziri wa Nishati na Madini kwenda kinyume na maagizo ya Rais? Tena nje ya Nchi?

7. Mheshimiwa Spika, Licha ya Marufuku hiyo ya Rais, mapitio ya mikataba ya madini ni mchakato ambao mwisho wake ni kuletwa kwa sheria ya madini hapa Bungeni na kuifanyia marekebisho ili kuiboresha na kuondoa mapungufu. Hivyo, mpaka hapo sheria itakaporekebishwa ndipo tutasema tumemaliza zoezi la kupitia mikataba ya madini na hivyo kusaini mikataba mipya na makampuni yote ya madini yaliyopo nchini na yatakayokuja kuwekeza.

8. Mheshimiwa Spika, suala ambalo linanipelekea kuomba kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kuchunguza mkataba huu mpya ni kuhusu uharaka uliopelekea Waziri wa Nishati na Madini kusaini Mkataba huu. Sheria ya Madini bado haijarekebishwa, je Waziri anatumia vigezo gani kusema mkataba mpya wa Buzwagi aliousaini London hauna mapungufu?

9. Mheshimiwa Spika, Waziri wa Nishati na Madini aliliambia Bunge lako Tukufu kuwa Buzwagi ni marginal mine. Vile vile Waziri anasema kuwa Kampuni ya Barrick inamiliki migodi mitatu tu kupitia kampuni zake tanzu ambazo ni Bulyanhulu Gold Mine, North Mara Gold Mine na Pangea Minerals Limited Tulawaka. Kwa maelezo haya ya Waziri Karamagi, Buzwagi sio Mgodi.

10. Mheshimiwa Spika, hoja hii ya kuwa Buzwagi sio mgodi inashabihiana kabisa na hoja ya Kampuni ya Barrick kwamba Buzwagi ni Project. Taarifa ya kampuni hii ya ‘Barrick Gold Corporation-Global operations-Africa- Buzwagi, inaonesha kuwa Buzwagi ni mradi. Taarifa hii ninaiambatanisha katika hoja hii.

11. Mheshimiwa Spika, taarifa ya Barrick Annual Review 2006 inasema ifuatavyo katika ukurasa wa 23, ninanukuu. “A major milestone was reached in February 2007 when we signed a mineral Development Agreement (MDA) with the Tanzanian government. In 2007, we expect to complete a detailed construction design and receive EIA approval”.

12. Mheshimiwa Spika, suala ambalo vile vile linanisukuma kuomba Bunge lako Tukufu kuunda Kamati Teule ni kwamba, iwapo Buzwagi sio mgodi bali ni mradi, ni kwa nini tumesaini Mineral Development Agreement (MDA) mpya? Kwa kuwa Pangea Minerals Tulawaka ndio inaonekana kumiliki mradi huu, Je serikali imefanya marekebisho tu ya MDA na kampuni ya Barrick?. Naomba Kamati Teule ichunguze ni nini kilichosainiwa, marekebisho ya mkataba wa Tulawaka au MDA mpya ya Buzwagi?

13. Mheshimiwa Spika, Buzwagi inashika nafasi ya pili kwa uwekezaji wa Barrick katika migodi hapa nchini. Wakati kampuni hii inawekeza dola za kimarekani 400 milioni katika Buzwagi, imewekeza dola za kimarekani 600 katika Bulyanhulu. Je ni kwa vipi Buzwagi iwe marginal mine wakati uwekezaji wake unashinda uwekezaji wa Tulawaka na North Mara?

14. Mheshimiwa Spika, chini ya kifungu cha 47 cha Sheria ya Madini ya Mwaka 1998 (Na.5/98), pamoja na mambo mengine kinataka leseni yeyote isitolewe mpaka taarifa ya mazingira iwe imetolewa na kuruhusu mgodi kuendelea na kazi.

15. Mheshimiwa Spika, wakati Waziri wa Nishati na Madini ameweka saini Mkataba wa Buzwagi juma la mwisho la mwezi Februari 2007, Baraza la Mazingira nchini limetoa kibali (Environmental Impact Assessment- EIA approval) tarehe 11 mwezi Mei 2007. Ni kwa nini Waziri wa Nishati na Madini Mheshimiwa Nazir Karamagi alisaini MDA ya Buzwagi na Kampuni ya Barrick kabla Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC) halijatoa ruhusa? Kulikuwa na haraka gani? Maslahi ya Taifa yalizingatiwa?

16. Mheshimiwa Spika, Sheria ya Madini, niliyoitaja hapo awali, imeunda Kamati ya Ushauri ya Madini (Mining advisory Committee). Kabla ya Waziri kusaini mkataba wowote ni lazima apate ushauri kutoka kamati hii. Kwa taratibu za Kiserikali, kama kamati ikimshauri Waziri na Waziri akakataa ushauri huo, inampasa Waziri atoe sababu ni kwa nini anakataa ushauri. Je Waziri alifuata ushauri wa kamati ya Ushauri ya Madini kuhusiana na wakati mwafaka wa kusaini Mkataba huu?

17. Mheshimiwa Spika, inawezekana kabisa MDA ya Buzwagi kusainiwa Uingereza sio tatizo. Kwa mfano, Mwaka 2006 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilisaini mikataba kadhaa. Ni mingapi kati ya Mikataba hii imesainiwa nje ya nchi? Nini madhara ya kisheria kwa Mkataba kusaniwa Uingereza? Je Mkataba umeandikwa “signed in London ……..” au “signed in Dar es Salaam …..? Kamati Teule ya Bunge ndio chombo pekee kitakachoweza kutoa majibu ya maswali haya.

18. Mheshimiwa Spika, suala hili ni suala la Kitaifa. Halina hata chembe ya itikadi za kivyama. Ninaamini wabunge wataamua kwa maslahi ya Taifa letu. Uundwaji wa Kamati Teule ya Bunge kuchunguza mapitio ya mikataba ya madini na mazingira ya kusainiwa kwa mkataba mpya wa Buzwagi yatatoa msaada mkubwa kwa azma ya Rais wetu ndugu Jakaya Mrisho Kikwete ya kuona rasilimali za madini zinafaidisha nchi yetu.


b. Kuhusiana na asilimia 15% ya ‘capital allowance on unredeemed qualifying capital expenditure’

19. Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini amenukuliwa na kumbukumbu za majadiliano ya Bunge akisema, ninanukuu “..….kwa hiyo pamoja na kwamba ninamheshimu sana Mheshimiwa Kabwe Zitto na sote tunamheshimu ni msomaji mzuri, lakini wakati mwingine lazima kuangalia vitu gani unasoma. Ni kwamba kipengele hiki cha sheria kililetwa hapa Bungeni mwaka 2001 kwenye Bajeti kikabadilishwa…..” Mwisho wa kunukuu.

20. Mheshimiwa Spika, katika kuandaa hoja yangu hii, ilinibidi kupitia upya kumbukumbu za majadiliano ya Bunge ili kujiridhisha na maelezo ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini, maelezo ambayo mimi nililitaarifu Bunge lako tukufu tarehe 16/7/2007 kuwa sio sahihi.

21. Mheshimiwa Spika, Kumbukumbu hizo zinaonesha kwamba, sheria ya fedha ya mwaka 2001 (Finance Act. No.14 ya 2001) ilifanyiwa marekebisho kadhaa ikiwemo marekebisho ya sheria ya madini kifungu cha 87 ambapo kifungu kidogo cha (3) cha kifungu cha 87 kiliongezwa. Kifungu kidogo hicho kinasema, ninanukuu

‘(3) The provisions of subsections (1) and (2) shall not apply to any person who, immediately before the first day of July, 2001 was not the holder of a mineral right granted under this Act’

22. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 87 cha Sheria ya Madini ya mwaka 1998 (No.5/1998) kinazungumzia Mrahaba wa Madini (Remission and deferment of royalties). Hivyo, kama sheria ya fedha ya mwaka 2001 haikubadili kipenge hiki, Mheshimiwa Waziri ametoa wapi jibu aliloliambia Bunge?

23. Mheshimiwa Spika, suala hili linahusu haki, kinga na madaraka ya Bunge kwa mujibu wa sheria namba 3 ya 1988.

24. Mheshimiwa Spika, hata hivyo katika hotuba ya Waziri wa Fedha Mheshimiwa Basil Mramba, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti mwaka 2002, tarehe 13 mwezi Juni, alizungumzia kipengele hiki. Ninaomba kunukuu sehemu ya hotuba ya Waziri wa Fedha Mhe. Basili Mramba

“Amendment to the Income Tax structure, (44) Mr. Speaker, in this area I propose to take the following measures:
(v) I propose to reinstate the additional 15 percent capital allowance on unredeemed qualifying capital expenditure as set out in the Mining Act. No. 5 of 1998”….. Mwisho wa kunukuu.

25. Mheshimiwa Spika, nilipopitia sheria ya fedha ya mwaka 2002 nimekuta sehemu ya 8 inazungumzia mabadiliko katika kodi ya mapato ya 1973. Na hata katika ukurasa wa kwanza wa sheria hii (Arrangement of Contents), sheria ya Madini haitajwi.

26. Mheshimiwa Spika, maelezo haya ya Waziri wa Fedha ya mwaka 2002 yanaonesha dhahiri utata wa kipengele hiki. Ni kwa vipi kifungu cha sheria ambacho hakijafutwa kirejeshwe?

27. Mheshimiwa Spika, tuchukulie kuwa maneno ya Waziri ni ya kweli. Je kwa nini makampuni ya Madini ambayo yameingia Mkataba na serikali kuanzia Julai mosi 2001 hayajaanza kulipa kodi ya mapato?

28. Mheshimiwa Spika, utata huu ambao umegubika sekta hii ya madini unaweza kufafanuliwa na Bunge lako tukufu kupitia Kamati Teule. Kamati teule ya Bunge ichunguze upitiaji wa mikataba hii na kuona kama kuna vitendo vyovyote vya uvunjifu wa sheria za nchi na kupotea kwa mapato ya Serikali na ufisadi.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kutoa hoja.



…………………………….
KABWE ZUBERI ZITTO (MB)
JIMBO LA KIGOMA KASKAZINI



Nampongeza sana huyu kijana kwa ujasiri wa hali ya juu.
Nitaweka ya kagamagi baadae ili tuweze kuchambua moja baada ya nyingine ,tumalize kwanza hii ya zitto the great to me.

ya Karamagi:
MAONI YA SERIKALI KUHUSU HOJA YA KUUNDWA KAMATI TEULE YA BUNGE KUCHUNGUZA MAPITIO YA MIKATABA YA MADINI NA MAZINGIRA YA KUSAINIWA KWA MKATABA (MDA) MPYA WA MADINI WA BUZWAGI KAMA ILIVYOWASILISHWA NA MHESHIMIWA KABWE ZUBERI ZITTO

Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kuchangia kwa niaba ya Serikali hoja ya kuundwa Kamati Teule ya kuchunguza Mkataba Mpya wa Madini wa Mgodi wa Buzwagi.

Mheshimiwa Spika, mtoa hoja amejielekeza katika masuala makuu mawili ambayo anadai wakati nayaelezea, aidha sikuwa sahihi au nilidanganya.

Kwanza, Licha ya maelezo ambayo nilikwisha yatoa kwa niaba ya Serikali juu ya kuondolewa kwa kipengele katika Sheria ya Mapato ya mwaka 1973 kuhusiana na Nyongeza ya asilimia 15 kwenye Mtaji wa Uwekezaji ambao Haujarejeshwa kwa kila mwaka (Additional capital allowance of 15% per annum applied to the balance of unredeemed qualifying capital expenditure) Mhe. Kabwe Zitto anaendelea kusisitiza kuwa kuondolewa kwa kipengele hicho kulifanyika bila ya kupata kibali cha Bunge.

Mhe. Spika, Katika kujaribu kuthibitisha hoja yake, Mheshimiwa Zitto amenukuu kumbukumbu za Bunge ambazo zinaonyesha marekebisho yaliyofanyika kwenye Sheria ya Fedha ya mwaka 2001 (Finance Act. No. 14 of 2001), kwa kutaja marekebisho ya Sheria ya mwaka 1998 ya madini kifungu cha 87 ambapo kifungu kidogo cha (3) cha fungu la 87 la Sheria ya Madini liliongezwa.

Mheshimiwa Spika, naomba Bunge lako tukufu litambue kuwa hapa Mheshimiwa Kabwe Zitto anachanganya Sheria mbili tofauti; Sheria ya Madini ya Mwaka 1998, na Sheria ya Kodi ya Mwaka 1973.

Mheshimiwa Spika, Kipengele kinachozungumziwa hakiko chini ya Sheria ya Madini ya mwaka 1998 bali kipo chini ya Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 1973. Ukweli kuhusu suala hili ni kwamba kipengele hiki cha Nyongeza ya asilimia 15 kwenye Mtaji wa Uwekezaji ambao Haujarejeshwa kiliondolewa na Bunge kupitia Sheria ya Fedha ya 2001. Kama Mheshimiwa Zitto angesoma kwa uangalifu “Finance Act No.14 of 2001” aliyoinukuu angebaini kuwa marekebisho ya kipengele hiki yalifanyika katika fungu la 16B ya Jedwali la Pili la Sheria ya Mapato ya Mwaka 1973 na siyo fungu la 87 la Sheria ya Madini ya mwaka 1998 kama anavyodai Mhe. Kabwe Zitto.
Naomba kunukuu marekebisho kama yalivyoletwa Bungeni kwa manufaa ya Bunge lako Tukufu.

16B. Paragraph 16 of the second schedule to the
Principal Act is amended.

(a) by deleting the definitions of the words “additional capital allowance” and qualifying capital expenditure” which appear in sub-paragraph (1) of paragraph 16.

(b) By deleting the definitions of word “expenditure” and substitution for it the following definition.

“expenditure” means the sum of prospecting capital expenditure and development capital expenditure incurred in the United Republic by any person carrying on mining operations.

Maana ya mabadiliko haya ni kwamba fungu la 18 (1) la Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 1973 linaloweka masharti ya kipengele cha nyongeza ya asilimia 15% kwenye mtaji wa uwekezaji ambao haujarejeshwa liliondolewa.

Baada ya Bunge kupitisha marekebisho hayo, matokeo yake yalikuwa kwamba Bunge liliafiki kuondolewa kwa 15% ya additional capital allowance on unredeemed qualifying capital expenditure bila ya kujali mikataba ambayo baadhi ya makampuni ya madini yalikuwa yameingia na Serikali kwa mujibu wa fungu la 10 la Sheria ya Madini ya mwaka 1998 kabla ya mabadiliko haya.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua kwamba mikataba ambayo Serikali iliingia na kampuni za madini kabla ya mabadiliko ya sheria hiyo ilikuwa inaifunga (binding) Serikali kutofanya mabadiliko ya sheria ambayo yataondoa vivutio vya kodi vilivyokuwepo wakati mkataba unatiwa saini, Serikali ilileta mapendekezo kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2002 (The Finance Act, 2002) ambayo yalipitishwa na Bunge ili kurekebisha kasoro hiyo.

Mheshimiwa Spika, maana ya mabadiliko hayo ni kwamba 15% additional capital allowance on unredeemed qualifying capital expenditure ilirudishwa kwa makampuni ya madini yaliyoingia mkataba na Serikali kabla ya tarehe 1 Julai 2001. Ndio sababu migodi iliyokuwa na mkataba na Serikali kabla ya tarehe 1 Julai, 2001 ilieendelea kuwa na kivutio 15% additional capital allowance on unredeemed qualifying capital expenditure hata baada ya kuondolewa kwa fungu hilo.

Mheshimiwa Spika, ili kuthibitisha kauli yangu, nawasilisha kwako nakala ya Hansard ya tarehe 14 Juni, 2001 na nakala ya Ibara ya 16 ya Finance Act No.14 of 2001 ilivyowakilishwa Bungeni ili igawiwe kwa Mtoa hoja na Waheshimiwa Wabunge wengine watakaotaka kujiridhisha na ukweli huu. Mheshimiwa Spika, Serikali makini kama ilivyo Serikali yetu, haidanganyi. Uthibitisho huu ni kielelezo tosha kuwa mtoa hoja ndiye aliyelidanganya Bunge na Watanzania waliomsikiliza kwa kutokuwa makini na kauli yake Bungeni.
Mheshimiwa Spika, Pili Mhe. Zitto anahoji kusainiwa kwa mkataba mpya wa Madini wa mgodi (mradi) wa Buzwagi kati ya Serikali na kampuni ya Barrick na uhalali wa Mkataba huo kusainiwa mjini London, Uingereza. Vile vile, Mhe. Zitto anahoji kwa nini Mkataba huo umesainiwa wakati Serikali bado inafanya durusu (review) ya mikataba ya Madini kufuatia maagizo ya Rais.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la Mkataba kusainiwa Uingereza, kama nilivyolielezea Bunge lako Tukufu wakati nahitimisha hoja ya Makadirio ya Matumizi ya Wizara yangu kwa mwaka wa fedha 2007/08, mkataba huo uliandaliwa Tanzania na wataalamu wetu na ukapitia taratibu zote zinazopaswa kufuatwa ikiwa ni pamoja na kuidhinishwa na Kamati ya Ushauri ya Madini (Mining Advisory Committee) na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Mhe. Spika naomba kuwasilisha kwako vielelezo vya ushahidi wa kauli yangu hii. Vile vile uamuzi wa kuingiza mradi wa Buzwagi kwenye miradi ya Barrick Gold Corporation ambayo ni kampuni mama ulihitajika kufanyika kabla ya Machi, 2007, vinginevyo fursa ya uwekezaji katika mradi huu ingepotea.

Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa maandalizi yote ya kusaini mkataba yalikamilika nikiwa ziara ndefu ya nchi za nje, niliona si busara kuhatarisha uwekezaji wa mradi huu jambo ambalo lingeathiri maslahi ya Taifa. Faida inayotarajiwa kutokana na Mgodi wa Buzwagi katika kipindi cha uhai wake ni pamoja na:

• Mrabaha na kodi nyingine zinatarajiwa kufikia kiasi cha USD198.9 milioni.
• PAYE USD50.3 milioni.
• Ujenzi wa laini ya umeme na matumizi ya Umeme USD30 milioni.
• Kununua huduma mbalimbali za wakati wa kujenga miundombinu mingine kwenda mgodini, ujenzi wa mitambo na wakati wa uzalishaji USD568.4 milioni.
• Jumla ya mapato yote yatakayoingia kwenye uchumi wa Taifa katika kipindi cha uhai wa mgodi yanatarajiwa kufikia takriban USD818.3 milioni.
• Mgodi unatarajia kutoa ajira katika fani mbalimbali kwa jumla ya watu 696 watakaopata ajira ya kudumu. Kati yao, 630 au asimilia 91 watakuwa Watanzania; ikiwa ni pamoja na maafisa waandamizi.
• Mgodi utaongeza mapato ya taifa ya fedha za kigeni kutokana na mauzo ya madini nje.
• Mgodi utaendeleza miundombinu ya kiuchumi na kijamii, hasa huduma za jamii kama vile shule na zahanati katika maeneo yanayozunguka mgodi.
• Kufunguliwa kwa mgodi huo kutafungua fursa nyingine za kiuchumi katika maeneo mengi.

Mhe. Kabwe Zitto anauliza kwenye mkataba kipengele kinasema mkataba umewekwa saini London au Dar es Salaam?

Mheshimiwa Spika, Format ya mkataba wa Madini wa Buzwagi hauna kipengele anachokiuliza Mhe. Kabwe Zitto. Hiki si kitu cha ajabu kwa mikataba ya siku hizi ambapo mkataba unaweza kusainiwa na pande zaidi ya mbili zikiwa nchi tofauti. Mkataba unaweza ukasainiwa upande mmoja na ukatumwa kusainiwa na upande mwingine nchi nyingine.

Mhe. Spika, Mhe. Kabwe Zitto anahoji kama kabla ya kusaini Mkataba wa Buzwagi nilifuata Sheria inayonitaka kwanza kupata ushauri wa Kamati ya Ushauri ya Madini. Kama nilivyokwisha sema mkataba ulipitia taratibu zote zinazohitajika ikiwa ni pamoja na kupata baraka za Kamati ya Ushauri ya Madini. Kivuli cha idhini ya Kamati hiyo nimekwisha wasilisha kwako kama kielelezo cha kuthibitisha kauli yangu.

Mheshimiwa Spika, Mhe. Zitto anazungumzia eti maagizo ya Rais yalikiukwa, kauli anayoitoa bila ya kutafakari maagizo hayo yalikuwa ya aina gani. Mhe. Rais aliagiza mikataba yote ya madini (MDAs) kufanyiwa mapitio ili kubaini maeneo yanayoweza kurekebishwa kwa faida ya pande zote mbili - Nchi na Wawekezaji (win-win situation). Kamati iliundwa kwa ajili hiyo na baada ya kukamilisha kazi iliyopewa, iliwaSilisha mapendekezo yake Serikalini tarehe 14 September, 2006. Baadhi ya mapendekezo ya Kamati hiyo yalitumika katika majadiliano na makampuni ya madini yenye mikataba ya zamani. Mafanikio ya majadiliano hayo niliyataja kwenye hotuba yangu wakati nawasilisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ya mwaka 2007/08 kuwa ni:

• Kuondoa nyongeza ya asilimia 15 kwenye mtaji wa uwekezaji ambao haujarejeshwa (15% additional capital allowance on unredeemed qualifying capital expenditure). Hatua hii itawezesha kampuni hizo kukomboa gharama zao za uwekezaji mapema na hivyo kuweza kulipa kodi ya mapato (corporation tax).

• Kulipa kiasi cha Dola za Marekani 200,000 kwa mwaka kwa Halmashauri zinazohusika na migodi hiyo. Halmashauri zinazonufaika na malipo hayo ni Tarime, Kahama, Nzega, na Biharamulo.

• Kampuni ya Barrick Gold Corporation imekubali na imeanza kulipa Dola za Marekani milioni 7 kila mwaka kama malipo ya awali ya kodi ya mapato ya kampuni hadi migodi yake itakapoanza kulipa kodi stahili.

• Kampuni ya Resolute (Tanzania) Limited imeondoa kipengele kwenye mkataba wake kilichokuwa kinairuhusu kutokulipa kodi ya mapato kwa wafanyakazi wake wa kigeni. Kuondolewa kwa kipengele hiki kutailazimu kampuni hii kulipa takriban Dola za Marekani milioni 2.2 kila mwaka kama malipo ya kodi ya mapato. Katika mwaka 2006/07, kampuni hiyo imelipa Dola za Marekani milioni 2.3.

• Kampuni ya AngloGold Ashanti inayomiliki mgodi wa Geita imekubali kulipa kiasi cha Dola za Marekani 200,000 kwa mwaka kwa Halmashauri ya Wilaya ya Geita. Aidha, majadiliano katika maeneo mengine ya mkataba wake, yanaendelea.


Hivyo Mhe. Spika si kweli kuwa zoezi la kudurusu mikataba ya madini bado linaendelea.

Mheshimiwa Spika, nilisema kuwa mkataba mpya kuhusu Buzwagi hauna mapungufu yaliyokuwemo kwenye mikataba ya zamani – Ikiwa na maana kuwa kwa kutumia ushauri wa Kamati niliyoitaja hapo juu, mkataba wa Buzwagi umeboreshwa kwa maslahi ya Taifa ukilinganisha na mikataba ya zamani. Naomba ninukuu baadhi ya vipengele vilivyoboreshwa:

• Depreciation ya gharama ya uwekezaji ni asilimia 80 mwaka wa kwanza, na baadaye asilimia 50 miaka inayofuata, katika Mikataba (MDAs) ya awali depreciation allowance ni asilimia 100 mwaka wa kwanza.
• Withholding taxes zimeongezwa kiwango kama ifuatavyo:-
o Technical services kodi ya zuio itakuwa asilimia 5 badala ya asilimia 3 zilizoko kwenye Mikataba (MDAs) ya zamani na hii ni kwa kila malipo yanayozidi asilimia 2 ya gharama za uzalishaji.
o Service fee kwa ajili ya gharama za utawala itakuwa asilimia 15 ikilinganishwa na asilimia 3 za Mikataba (MDAs) ya awali na hii ni kwa gharama ya uzalishaji.
• Kuna masharti kuhusu kununua bidhaa na huduma mbalimbali hapa nchini.
• Kuna masharti kuhusu kuchangia mfuko wa uwezeshaji (empowerment fund) kupitia Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, USD125,000 kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, utaona kuwa kuna vipengele vilivyowekwa kwenye mkataba huu ambavyo utekelezaji wake utafanyika baada ya kuleta bungeni mapendekezo ya kurekebisha vifungu husika kwenye Sheria inayohusu mfumo wa kodi katika Sekta ya Madini.

Mheshimiwa Spika, Mhe. Kabwe Zitto anasisitiza kuwa zoezi la kudurusu mikataba bado linaendele. Mtoa hoja labda anachanganya tena Zoezi la kudurusu mikataba na zoezi linaloendelea la kudurusu Sheria ya Madini ya mwaka 1998 na Sheria zinahusu mfumo wa kodi katika Sekta ya Madini kitu ambacho ni kipana zaidi na kinawahusu wadau wote yaani, Wawekezaji wakubwa, Wawekezaji wadogo na wote wanaojihusisha na utafiti katika Sekta ya Madini. Akielewa hili, atabaini kuwa maagizo ya Rais yalitekelezwa kikamilifu na matokeo yake yameishaanza kujitokeza kama faida nilizozieleza hapo juu.

Mheshimiwa Spika, Mhe. Kabwe Zitto anahoji kama Buzwagi ni Mradi (project) au ni Mgodi (mine). Nafikiri hili ni suala dogo ambalo naamini ni la uelewa tu. Hadi sasa mradi wa Buzwagi haujafikia hadhi ya kuitwa mgodi. Kama ilivyo miradi yeyote, Buzwagi utapata hadhi ya kuitwa mgodi baada ya Waziri wa Nishati na Madini kutoa leseni ya uchimbaji, ujenzi wa mgodi kukamilika na shughuli za uchimbaji kuanza.Mgodi wa Buzwagi kuwa ni Marginal Mine (Mgodi mdogo na faida ndogo)

Mheshimiwa Spika, nilisema kwamba katika tathmini ya migodi, mgodi wa Buzwagi ni marginal mine ambao uhai wake si wa muda mrefu na kwamba bila ya kutumia fursa iliyokuwepo hususan bei kubwa ya dhahabu, uwekezaji wake usingekuwa wa faida.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Nishati na Madini ilifanya uchambuzi wa taarifa ya uwekezaji katika mgodi wa Buzwagi na kuonekana kuwa mgodi huo ni marginal project na ukianza kuendelezwa wakati huu ambapo bei ya dhahabu ni kubwa, wastani wa zaidi ya Dola za Marekani 600 kwa wakia, ndiyo utatoa marginal profit na kuwezesha mwekezaji kuendeleza mradi wa Buzwagi hadi kufikia hadhi ya kuwa mgodi.

Mheshimiwa Spika, Mhe. Kabwe Zitto anasema kuwa Mgodi wa Buzwagi hauwezi kuitwa Marginal mine kwa kigezo kuwa utashika nafasi ya pili kwa Migodi inayomilikiwa na kampuni ya Barrick Gold Corporation kwa kulinganisha moja kwa moja gharama za uwekezaji kati ya mgodi wa Bulyanhulu uliofanyika miaka ya tisini na mgodi wa Buzwagi unaotarajiwa kujengwa mwaka ujao – 2008.

Mheshimiwa Spika, Mtoa hoja inaelekea anazungumzia suala la utaalamu wa fedha ambalo inaonyesha wazi hana ujuzi nalo. Hata hivyo, Mhe. Spika, mtu haitaji kuwa mtaalamu ili kuelewa kuwa kama mwekezaji alitumia thamani ya dola za Kimarekani milioni 600 kujenga mgodi wa Bulyanhulu miaka kumi iliyopita, akitaka kujenga mgodi kama huo kwa sasa thamani yake itakuwa kubwa maradufu. Mhe. Spika labda kwa manufaa ya Bunge lako tukufu, naomba nitoe ufafanuzi wa ziada ili kuonyesha kuwa gharama za uwekezaji sio kigezo pekee cha kupima ubora wa mgodi.

Mheshimiwa Spika, Vigezo vingine vinavyotumika kujua ubora wa mgodi ni pamoja na mashapo yaliyopo na kiwango cha upatikanaji wa dhahabu kwa tani ya miamba(ore grade per tonne). Kiwango cha upatikanaji wa dhahabu katika mgodi wa Bulyanhulu ni wastani wa gramu 11 za dhahabu kwa tani ikilinganishwa na Buzwagi ambapo ni gramu 1.8 za dhahabu kwa tani. Mashapo yaliyopo Bulyanhulu ni kiasi cha wakia milioni 12 inayoweza kuchimbwa kwa miaka 25 wakati Buzwagi ni wakia milioni 2.5 inayoweza kuchimbwa kwa miaka 10. Kutathminiwa mgodi wa Buzwagi kama Marginal mine ni swala la kitaalamu lenye takwimu za wazi ambalo halipingiki wala halipindishwi.

Tuhuma kwamba Sheria imevunjwa kwa kusaini Mkataba kabla Baraza la Mazingira kutoa Environment Impact Assessment – EIA Approval

Mheshimiwa Spika, Mhe. Zitto amenukuu kifungu cha 47 cha Sheria ya Madini ya mwaka 1998 kinachotaka leseni yeyote ya uchimbaji Madini isitolewe mpaka taarifa ya mazingira iwe imetolewa.

Mheshimiwa Kabwe Zitto anachanganya tena vitu viwili tofauti, yaani Mkataba wa Madini na Leseni ya Madini. Mkataba wa Madini kati ya Serikali na Kampuni za Madini unaingiwa chini ya kifungu cha 10 cha Sheria ya Madini ya mwaka 1998 na hicho ndicho kitu cha kwanza kinachoanzisha mchakato wa uwekezaji. Hivyo, tathmini ya Mazingira (Environmental Impact Assessment Study) inafanywa baada ya mwekezaji kuwa na mkataba. Mwekezaji anaweza kuomba leseni ya uchimbaji wa madini wakati wowote lakini hawezi kuipata mpaka awe na kibali cha Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC).

Kwa maneno mengine, kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 1998, Maombi ya Leseni ya Uchimbaji wa Madini (Mining Licence) lazima yaambatane miongoni mwa mambo mengine na tathmini ya Mazingira kuhusu mradi huo (Environmental Impact Assessment Study). Mpaka sasa Leseni ya Uchimbaji kwa mradi wa Buzwagi bado haijatolewa. Kwa kupata kibali cha Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC), mwekezaji atakuwa ametimiza sharti mojawapo la kupata leseni.

Mheshimiwa Spika, Naomba nitumie fursa hii kumshauri Mhe. Kabwe Zitto ajielimishe zaidi juu ya sheria zinazosimamia Sekta ya Madini hapa nchini. Vile vile namshauri Mhe. Kabwe Zitto kujiepusha na hulka ya kutoa kauli nzito ambazo hazikufanyiwa utafiti wa kutosha kama hili analodai kuwa Serikali imevunja sheria za nchi na kulidanganya Bunge wakati ni yeye mwenyewe hajajielimisha vya kutosha kuhusu sheria anayoizungumzia kuwa imevunjwa.

Mheshimiwa Spika, mtoa hoja amedai kuwa suala analolizungumzia eti ni la kitaifa na halina hata chembe chembe za itikadi za kivyama. Pamoja na kuwa hoja alizozitoa hazina ushahidi wowote, tayari hoja hizo zimekwisha dakwa na kubebewa bango na Mwenyekiti wa Chama chake cha CHADEMA na wamezigeuza kuwa propaganda ya kisiasa kupitia vyombo vya habari. Labda angalizo analolitoa Mhe. Kabwe Zitto, analilenga kwa Chama chake mwenyewe.

Mhe. Spika, Kuna msemo wa kiingereza usemao, No Research No Right to Speak – (Bila Utafiti huna haki ya Kuzungumza). Hivyo vile vile Chama Makini Kinahitaji kufanya Utafiti kabla ya kujihusisha na mambo ya kuzua.

Mheshimiwa Spika, Hoja ya Mhe. Kabwe Zitto imeonyesha mapungufu makubwa ya tafsiri ya sheria anazozinukuu na vifungu anavyo vilenga ili kuthibitisha kuwa Serikali imelidanganya Bunge. Ni dhahiri hoja yake imejengwa katika mazingira ya uzushi yenye malengo makuu mawili, kwanza kuchonganisha Bunge na Serikali na pili ni kuwapotosha wananchi juu ya sheria zinazotungwa na Bunge lako tukufu kwa nia ya kujitafutia umaarufu usiokuwa na msingi (cheap popularity).

Mheshimiwa Spika, mtoa hoja anaomba Bunge lako tukufu kuunda Kamati Teule ya Bunge ili Kamati imfanyie kazi ya kuhalalisha mambo ya kuzua au kumsaidia kumfafanulia sheria ambazo yeye mwenyewe kashindwa kuzielewa. Mhe. Spika, hii si kazi ambayo Bunge hili linaweza kutumia fedha za walipa kodi kuifanya. Tabia ya namna hii ikiruhusiwa kuendelea inaweza kulipunguzia Bunge lako tukufu heshima na hadhi yake.

Mheshimiwa Spika, tarehe 16 Julai, 2007 mara baada ya makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kupitishwa na Bunge, Mheshimiwa Kabwe Zuberi Zitto alisimama na kutoa tuhuma nzito kwangu kama Waziri wa Nishati na Madini kuhusiana na mkataba mpya wa Buzwagi.

Akinukuliwa na Hansard ya tarehe 16/07/2007, Mheshimiwa Kabwe Zitto alisema nanukuu “ kutokana na majibu ya Mheshimiwa Waziri kuhusiana na Mkataba mpya wa Mgodi Buzwagi ambao Mheshimiwa Waziri ameeleza maelezo ambayo siyo sahihi, amedanganya na ameeleza vitu ambavyo kwa kweli sivyo ambavyo vipo katika Mkataba ambao ameusaini” mwisho wa kunukuu.

Kutokana na tuhuma hizo, Mheshimiwa Zitto kwa kutumia Kanuni ya 104(1) ya Bunge, alitoa taarifa rasmi ya mdomo ya kusudio la kuleta hoja ya kuunda Kamati Teule kuchunguza mkataba mpya wa Madini wa Buzwagi. Leo ametoa hoja aliyoitolea taarifa, lakini mbali ya kujikanganya kwenye sheria alizodai zimevunjwa, hajaonyesha wazi pasipotiliwa mashaka wapi nililidanganya Bunge.

Mheshimiwa Spika, Tuhuma Mhe. Kabwe Zitto alizozitoa kwangu kama Waziri mwenye dhamana ya Wizara ya Nishati na Madini na kudakwa na vyombo vya habari ameniathiri mimi binafsi kwa kunichafulia jina langu bila sababu za msingi kwa kutoa taarifa za uzusi tena uzushi wa hatari. Nina hakika wewe mwenyewe Mhe. Spika pamoja na Waheshimiwa Wabunge wenzangu mtakuwa mashuhuda jinsi magazeti mbali mbali yalivyokuwa yakitoa vichwa vya habari vyenye kutoa lugha za kejeli kwangu kutokana na tuhuma Mhe. Kabwe Zitto alizozitoa hapa Bungeni.

Mheshimiwa Spika, Kwa vielelezo na maelezo ya Serikali niliyoyatoa, sasa naomba kupitia kwako kuliomba Bunge lako tukufu vile vile liangalie vielelezo alivyovitoa Mtoa Hoja kama vipo ili liweze kupima na kuamua ni nani mwongo – ni nani aliyelidanganya Bunge – mimi au Mhe. Kabwe Zuberi Zitto.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
 
Heshima yenu wana jambo. Nafikiri kilichotokea kwa wale wenye kuona mbali walishajua kuwa huyu zitto lazima afanyiwe hivyo maana amekuwa mwiba mchungu kwa serikali.

Jamaa hoja yake iko wazi ila imegeuzwa chini juu na hawa wasanii. Nafikiri inabidi kuwa na chombo cha kukata rufaa ili ionekanew kosa liko wapi. Maana mtu anakubali kuwa alisign mkataba nje harafu zitto anaungiwa kwa kusema uongo upi?

Hapa nafikiri inabidi zitto aamue liwalo na liwe aombe rufaa kwani kilichofanyika si fair na kama hakuna rufaa then hizo sheria za bunge inabidi zipitiwe tena.

Nampongeza zitto kwa ujasiri maana yataka moyo kwa bunge letu lililojaa CCM uongee na usikike!

Leo nimemsikiliza mwanasheria mmoja kwa jina Alex smth akiongelea na kuchambua suala la zitto clouds fm pamoja na kanuni zilizotumika kumsimamisha . Amekiri kuna upindishwaji wa hizo kanini na kwamba kifungu kilichotumika kumhukumu zitto hakimaanishi adhabu hiyo entirely especially kwa kuwa hakupewa muda wa kutosha kutoa utetezi ( ikimaanisha hata kuonana na wanasheria wake ili wajadidi PO's za issue nzima. Hata hivyo kamaliza kwa kusema bado anaweza kulipeleka suala hili mahakama kuu kama bunge halitoi mianya ya rufaa. Wataalamu wa sheria watupe mwanga zaidi juu ya hili.
 
Mimi bado nashindwa kuelewa hii kesi ilivoendeshwa Waziri ametoa hoja yake na Zito katoa hoja yake. Wazungu wanasema Waziri alikuwa na burden of proof and to his credit amefanya hivyo na Zito alikuwa na burden of rebutall amefanya hivyo pia .... Mpaka sasa sielewi ni nani alikuwa Judge na nani alikuwa Juror katika hii kesi na jee walifika vipi conclusion kwamba the defendant (Zito)amesema uongo ? Nadhani ili ni swali muhimu ambalo linastahili majibu.

Jamani sijapata kuona kesi kama hii , yaani kwa kuwa waziri ametoa ushahidi basi mnasema mtu mwingine ni muongo, kwa ajili ya cheo chake au ? Ndio maana idea ya kuundwa tume ina make sense kwani ni tume pekee ambayo ingeweza kutoa huo uamuzi ! Huu ni ukikwaji wa sheria za nchi .

Pili kuna hili swala ambalo Spika amezungumzia juu ya mikataba kwamba wabunge hawawezi kuwa na access na hiyo mikataba kwa sababu wengine wanaweza kuitumia kwa manufaa yao binafsi ! what kind of crap is this? Tunatakiwa tujiulize wabunge ni kina nani na jee wanarole gani katika nchi yetu , na utamwambiaje mtu apitishe bajeti ya wizara bila ya kujua contents ya hiyo mikataba ? kama kweli tuko serious na kuleta maendeleo katika nchi yetu basi ni lazima tuondoe hizi red tapes.

Halafu kuna ishu moja mgogongo amejaribu kusema ya kuwa Tanzania haitaendelea kwa sababu viongozi hawajui role wanazo play , mfano chadema wanaenda kumpokea zito kwa sababu ametoa hoja bungeni which is part and parcel of his job. Nadhani Mugongo anachoshindwa kuelewa sababu ya kumpokea ni kuonyesha kuchukizwa na maamuzi maonevu na ya kiyachama aliyofanyiwa kijana huyu besides kwa nini Mugongo aoni viongozi wa serikali wanavyokimbizana kama kumbi kumbi kila mara muungwana anapoivascodagama hii dunia. Mugongo angalia kila mara kikwete anavyotoka safarini ,wawziri mkuu, mawaziri mbali mbali , mkuu wapolisi & Jeshi , mkuu wa mkoa wanavyomiminika kumpokea ...hilo mugongo ulioni..

Na suala la Spika kusema wabunge ni wanya biashara ni matusi makubwa kwa wabunge as well as wananchi waliowachagua , spika anaquestion integrity ya wabunge ..sasa sababu ya kuwaapisha ilikuwa ni nini ? na jee mawaziri sio wafanyabiashara? Those are legitimate questions that merit answers!
 
Angalieni hoja zote mbili hapo juu mtumie hekima zenu kuamua, acheni kupindisha pindisha, kila mtu atoe maoni yake na kwanini anasema hivyo. Na hiyo iwe ime kuwa based na hoja za hapo juu tuuu!!!

FD
 
Ha Ha, Yaani nilikuwa biz sijaangalia mtandao, nimeshindwa kuamini yaliyotokea.

Yaani bunge LETU "TUKUFU" limefanya haya maamuzi?

Ningependa niwe mbunge siku moja, watanitambua.

Haki ya nani hatuna BUNGE, Shujaa ZITO kasimamshwa kisa kutetea masrahi ya nchi?

Kama watapata kura zetu 2010 itabidi nijinyonge 2, no way mambo haya kutendeka mbele ya machoni yangu.

Yaani hapa nilipo BP juu
 
Sasa wanabodi hapa nimewawekea kila kitu kuanzia hoja ya Zitto, majibu ya Karamagi, michango ya wabunge wote wakiwamo wa CCM na wapinzani, hoja ya Mudhihir, michango na kila kilichotokea.. na hapa nampa faida aliyetaka kujua alichosema Malecela alisema hivi>:

"Mheshimiwa Spika, kwanza ningependa nichukue fursa hii kusema naunga mkono hoja mabyo imetolewa na ndugu yetu Mheshimiwa Mudhihir. Ninaunga mkono hoja hii na ninataka niseme hili kwa uchungu sana kwamba Bunge hili lazima liwe Bunge lenye heshima ambayo tumeachiwa tangu miaka mingi iliyopita. Mimi sijapata kukuta debate ikawa kama ya leo. Na lilipoanzia, kwanza yeye alianza kusema Waziri amelidanganya Bunge hili. Sasa wengine tunajaribu kusema labda tunasema Karamagi, hapana, siyo Karanmagi, ni Waziri wa Jamhuri ya Muungano wa Taznania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo hili alilolisema, kwanza limemdhailisha Waziri, limedhalilisha Serikali. Pili, linaleta hisia kwamba Mawaziri wa Chama cha Mapinduzi waongo. Na wana-CCM, tukumbuke, tunapoapa tunasema “nitasema kweli…”

WABUNGE FULANI: Daima.

MHE. DR. JOHN S. MALECELA: Hapa tumeona Mheshimiwa Karamagi akaisema kweli na wote hapa katueleza na tukaamini na tukakubali kwamba kweli hakudanganya Bunge hili. Kwa hiyo, mimi ningependa kwamba katika hili tusiwe na huruma kwa sababu wanasema “mdharau mwiba ataota nini…?”

WABUNGE FULANI: Tende.

MHE. DR. JOHN S. MALECELA: Sasa huu mwiba tuuondoe leo. Wengine watasema kwamba ooh labda hii itampa sifa kwa watu, hapana! Tusipomuadhibu, kwa watu itaonekana Serikali ya CCM, Mawaziri wa CCM wanasema uongo kwenye Bunge ambayo si kweli. Hii ni Serikali ambayo imechaguliwa na Mheshimiwa Rais Kikwete, Serikali tunayoiamini chini ya Waziri Mkuu Mheshimiwa Edward Lowassa. Na kweli, tuseme kweli kwamba Serikali yetu kila mara inajitahidi. Mawaziri wanapojibu hapa, wanajitahidi kweli kweli, kutoa mambo ya kweli na wakiona haitoshi, huwa wanasema au tuwafuate tuwaongezee au wanasema watatuandikia barua baadaye. (Makofi)

Makeshimiwa Spika, kwa kweli baada ya kusema hayo, mimi ningewaomba Wabunge wote pamoja na hata Wapinzani kwamba….shauri yenu, mimi mradi naomba tu, cha hakika sibembelezi! Ila ninachosema yeyote atakayepita katika njia ambayo Kabwe amepita, lazima tumuadhibu na kwa hiyo nakubalina na hoja ya Mheshimiwa Mudhihir kwamba Kabwe aadhibiwe na ni leo. Mheshimiwa Spika, Asante! (Makofi)"
 

Attachments

  • ZITTO_KARAMAGI_DEBATE.doc
    376.5 KB · Views: 174
Angalieni hoja zote mbili hapo juu mtumie hekima zenu kuamua, acheni kupindisha pindisha, kila mtu atoe maoni yake na kwanini anasema hivyo. Na hiyo iwe ime kuwa based na hoja za hapo juu tuuu!!!

FD

Fikiraduni,

Wewe sasa unalazimisha tembo afanye gymnastics. Ukiondoa Kitila, katika hawa jamaa hakuna mwenye intellectual stamina ya kupitia documents zote mbili na kuchambua hoja kwa hoja. Hapa ukileta headline ya Kulikoni ndio wao wanajitumbukiza. Mwanakijiji akisema kaonge na Meddy Mpakanjia utaona wanajitumbukiza enthusiastically. Kwahiyo, pole mkubwa.

Ngoja tusibiri a pageant ya mapokezi. Interesting precedent tunaiweka. Na watu wanasahau hapa kwamba Bunge, hili hili la CCM, lilimsimamisha Idi Simba at one point. Na bado akaingia Dar kwa mapokezi.
 
Pili kuna hili swala ambalo Spika amezungumzia juu ya mikataba kwamba wabunge hawawezi kuwa na access na hiyo mikataba kwa sababu wengine wanaweza kuitumia kwa manufaa yao binafsi ! what kind of crap is this? Tunatakiwa tujiulize wabunge ni kina nani na jee wanarole gani katika nchi yetu , na utamwambiaje mtu apitishe bajeti ya wizara bila ya kujua contents ya hiyo mikataba ? kama kweli tuko serious na kuleta maendeleo katika nchi yetu basi ni lazima tuondoe hizi red tapes.

Na suala la Spika kusema wabunge ni wanya biashara ni matusi makubwa kwa wabunge as well as wananchi waliowachagua , spika anaquestion integrity ya wabunge ..sasa sababu ya kuwaapisha ilikuwa ni nini ? na jee mawaziri sio wafanyabiashara? Those are legitimate questions that merit answers!


Rufiji

Chukua 5 na Mungu akubariki...
 
Fikiraduni,

Wewe sasa unalazimisha tembo afanye gymnastics. Ukiondoa Kitila, katika hawa jamaa hakuna mwenye intellectual stamina ya kupitia documents zote mbili na kuchambua hoja kwa hoja. Hapa ukileta headline ya Kulikoni ndio wao wanajitumbukiza. Mwanakijiji akisema kaonge na Meddy Mpakanjia utaona wanajitumbukiza enthusiastically. Kwahiyo, pole mkubwa.

Ngoja tusibiri a pageant ya mapokezi. Interesting precedent tunaiweka. Na watu wanasahau hapa kwamba Bunge, hili hili la CCM, lilimsimamisha Idi Simba at one point. Na bado akaingia Dar kwa mapokezi.

Unajua nini kuhusu intellectual stamina ya memba hapa? Most people here hawakuiba mitihani kama wewe ( as far as I know) na usianze kujikomba kwa Kitila....

Wewe umechambua hoja gani zaidi yakuleta issue za kulikoni kuhusu uhusiano wa AC na Zito and the like.....

Groupies wengine bwana..... Keep making my day.
 
Fikiraduni,

Wewe sasa unalazimisha tembo afanye gymnastics. Ukiondoa Kitila, katika hawa jamaa hakuna mwenye intellectual stamina ya kupitia documents zote mbili na kuchambua hoja kwa hoja. Hapa ukileta headline ya Kulikoni ndio wao wanajitumbukiza. Mwanakijiji akisema kaonge na Meddy Mpakanjia utaona wanajitumbukiza enthusiastically. Kwahiyo, pole mkubwa.

Ngoja tusibiri a pageant ya mapokezi. Interesting precedent tunaiweka. Na watu wanasahau hapa kwamba Bunge, hili hili la CCM, lilimsimamisha Idi Simba at one point kwa wizi. Na bado akaingia Dar kwa mapokezi.

Kwahiyo, perhaps kuna precedent kwa mapokezi ya thieves and ****** who are sanctioned by the Parliament.
 
Fikiraduni,

Wewe sasa unalazimisha tembo afanye gymnastics. Ukiondoa Kitila, katika hawa jamaa hakuna mwenye intellectual stamina ya kupitia documents zote mbili na kuchambua hoja kwa hoja. Hapa ukileta headline ya Kulikoni ndio wao wanajitumbukiza. Mwanakijiji akisema kaonge na Meddy Mpakanjia utaona wanajitumbukiza enthusiastically. Kwahiyo, pole mkubwa.

Ngoja tusibiri a pageant ya mapokezi. Interesting precedent tunaiweka. Na watu wanasahau hapa kwamba Bunge, hili hili la CCM, lilimsimamisha Idi Simba at one point. Na bado akaingia Dar kwa mapokezi.

Nimeshagundua, hawana hoja, kweli Kitila namkubali ingawa sio Chadema mimi.

FD
 
Back
Top Bottom