SoC04 Tanzania Tuitakayo: Je, tupo tayari kwa AFCON 2027?

Tanzania Tuitakayo competition threads

Damaso

JF-Expert Member
Jul 18, 2018
1,662
2,219
Septemba 27, 2023 huko Cairo, Misri katika Kikao cha Kamati ya Utendaji ya CAF walitangaza kuwa Tanzania, Kenya pamoja na Uganda watakuwa wenyeji wa michuano ya Afcon 2027. Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ya 2027, ambayo pia inajulikana kama AFCON 2027 au CAN 2027, imeratibiwa kuwa ni toleo la 36 la mashindano ya kandanda ya Afrika yanayoandaliwa kila baada ya miaka miwili na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF). Itaandaliwa na Kenya, Tanzania na Uganda mwezi Juni na Julai 2027.​
1714718196488.png

Picha kwa hisani ya Goal.com
Tanzania kuandaa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kunaibua furaha kubwa kwa taifa. Walakini, ukitazama kwa karibu utaona changamoto kubwa ambazo zinaweza kuzuia mashindano yenye mafanikio namna hii kuwa mazuri. Makala hii inahoji kuwa wakati Tanzania yetu ikiwa ina bashasha kubwa, ila kuna mapungufu makubwa ya kimiundombinu, vikwazo vya uwekezaji, na masuala ya usalama tukiwa tunajiandaa na michuano ya AFCON 2027.
1714718741313.png

Picha kwa hisani ya Bin Zubeiry Sports.
Kwanza, ukweli mchungu miundombinu ya sasa ya michezo ya Tanzania haikidhi mahitaji ya mashindano ya hadhi ya kimataifa kama vile AFCON. Ukosefu wa viwanja vyenye uwezo wa kubeba umati mkubwa wa mashabiki ambao unaotarajiwa kwa mechi za AFCON ni jambo linalotia wasiwasi mkubwa sana. Wakati Tanzania inajivunia viwanja vya kuvutia kama (Lupaso) Benjamin Mkapa, Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid, pamoja na Jamhuri Dodoma na kadhalika. uwezo Lupaso unaweza kubeba mashabiki 60,000 na ni pungufu ya kiwango kilichopendekezwa cha 80,000 kwa fainali za AFCON. Kuboresha viwanja vilivyopo au kujenga vipya kutahitaji uwekezaji mkubwa na wakati, jambo ambalo linaweza kuwa dogo kwa kuzingatia ratiba ya matukio ya 2027.
1714718837626.png

Picha kwa hisani ya Dar24.
Upungufu na ubora mdogo wa viwanja vya mazoezi na uhaba wa hoteli za ubora wa juu italeta changamoto kwenye michuano hii. AFCON inahitaji viwanja vingi vya mazoezi na malazi ya kupumisha timu, maofisa, na wanahabari. Na kitu cha ajabu ambacho hata TFF imekaa kimya ila inafahamu kuwa ni changamoto ni kwamba viwanja vingi vya mikoani ni viwanja vya CCM, yaani CCM Kirumba MWanza, CCM Kambarage (Shinyanga), CCM Samora (Iringa), CCM Jamhuri (Morogoro) na kadhalika, viwanja vingi vipo chini ya CCM. Sio kitu kibaya ila maendeleo ya viwanja hivi yanategemea mifuko ya chama na sio tena serikali, wala TFF au vyama vya soka mkoa. Uwepo wa viwanja vizuri kwa ajili ya mazoezi ni sehemu muhimu katika kukidhi mahitaji ya mashindano haya. Mifano ya mashindano ya awali ya AFCON ilionyesha umuhimu wa miundombinu. mwaka 2017, Gabon, taifa mwenyeji, lilikabiliwa na ukosoaji kwa viwanja vyake ambavyo havikukamilika na mapungufu ya viwanja vya mazoezi. Hii ilisababisha kuchafuliwa kwa kiasi kikubwa kwa sifa ya mashindano hayo.
1714719142814.png

Picha kwa hisani ya The Citizen Tanzania.
Pili, vikwazo vya miundombinu ya usafiri vinaweka kivuli katika utayari wa Tanzania. Kuhakikisha usafiri bora kwa wachezaji, mashabiki, na maafisa ndani ya miji mwenyeji na kati ya viwanja vya mechi ni suala muhimu sana. Miundombinu ya sasa ya uchukuzi ya Tanzania, hususani mtandao wake wa barabara, inaweza kuleta changamoto katika kushughulikia utitiri wa wageni na mahitaji ya mashindano haya. Kuboresha mifumo ya usafiri kunahitaji uwekezaji mkubwa na mipango ya muda mrefu. Kama tu barabara zinafungwa kwa sababu ya mafuriko, au msafara wa Mkuu wa Mkoa, je tunao uhakika kuwa wageni wana uwezo wa kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha bila tatizo? TFF na serikali mkae chini mjiulize vizuri, je tupo tayari kwa ajili ya Afcon 2027? au ndo bora Afcon 2027 ije na iende?

Katika matukio ya michezo yote, jambo la msingi, ni miundombinu thabiti na imara ya matibabu iliyo na vifaa tiba vya kushughulikia dharura zinazowezekana ni muhimu. Ndani na nje ya uwanja, je Wizara ya Afya ipo tayari kushughulikia dharura za wageni? Kama tu vituo vya afya havina wataalamu wa kutosha, je mtaajiri watu ili kufidia upungufu uliopo katika vituo vya afya. Serikali inaonesha kuwa Tanzania imepiga hatua katika baadhi ya sehemu hususani kushughulikia dharura za watu muhimu tu wenye wadhifa, wasiwasi kuhusu uwezo wao wa kusimamia mahitaji ya mashindano makubwa ya kimataifa unaendelea kuonesha shaka kubwa.
1714719346588.png

Picha kwa hisani ya UEFA.com
Tatu, wasiwasi kuhusu hali ya uchumi wa taifa inazua maswali kuhusu utayari wa Tanzania. Uzoefu mdogo katika kuandaa matukio makubwa ya michezo unaweza kuwa kikwazo kikubwa. Lakini kuandaa mashindano ya ukubwa wa AFCON kunahitaji utaalamu katika ugavi, teknolojia ya habari na mawasiliano, usimamizi wa matukio, na uratibu wa washikadau. Uzoefu mdogo wa Tanzania katika eneo hili unaweza kusababisha changamoto zisizotarajiwa, endapo kila kitu kitasimamiwa na serikali kuanzia A mpaka Z, turuhusu sekta binafsi kufanya kazi pamoja na serikali.
1714719480672.png

Picha kwa hisani ya Altezza Travel.
Tunahitaji kupata wafadhili. Kupata ufadhili wa kutosha kulipia gharama kubwa zinazohusiana na kuandaa AFCON ni kikwazo kikubwa, haswa kama serikali bado inaendelea kuweka vikwazo katika shughuli za wafadhili hawa. Kuvutia wafadhili na kusimamia fedha za mashindano kunahitaji mkakati thabiti na watu wenye moyo wa utendaji kazi sio wapigaji. Bila kuwa na mpango madhubuti wa kifedha, kuandaa AFCON kunaweza kuleta changamoto kubwa katika rasilimali za Tanzania haswa kwa Arusha na Dar es Salaam.

Kwa kumalizia, wakati shauku na bashasha kubwa ikiwa kwa watanzania, ila kupewa wenyeji wa kuandaa AFCON ni jambo gumu sana sio suala jepesi, Misri walipokuwa wenyeji wa Afcon 2019 na kupata sifa ya kuwa bora haikuwa bahati mbaya. Uongozi wa Rais Abdel Fattah El-Sisi akiwa pamoja na Waziri wa fedha, Mohamed Maait pamoja na Waziri wa Usafirishaji Kamel Al-Wazir. Hawa wawili walifanya kazi nzuri sana mpaka tukaona mpangilio mzuri wa malazi na vyakula. Hoteli kama Al Masa Hotel, pamoja na Triumph Plaza Hotel zilipata wageni wengi lakini gharama zao zilisanifishwa ili kuruhusu wageni kuhudhuria michezo yote.​
1714719730791.png

Picha kwa hisani ya Forbes.
Rai yangu Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro fanya ukae na wenzako kina, Prof. Makame Mbarawa, Mhe Hamad Masauni, pamoja na Dr. Mwigulu L. Nchemba mjadiliane kuhusu ugeni mkubwa ambao unakuja hivi karibu hapa kwetu nyumbani Tanzania. Tanzania inaweza kuhakikisha kuwa ndoto yake ya AFCON 2027 inatimia wakati imejiandaa kweli kweli kung'ara kimataifa.​
Tanzania Tuitakayo: Je tupo tayari kwa Afcon 2027?
 
Nimepata kitu kuhusu mpira (ambao kiukweli siujui kiundan) na uandaaji wa mashindano.

Na ndiyo kazi yangu huku stories of change. Kujifunza mawazo mapya. Ahsante.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom