Tanzania ni nchi ya ushabiki wa vijambo vidogo

dosari

Member
Oct 7, 2016
81
84
Hivi karibuni Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2017-2018 imepitishwa na Bunge. Kilichomo kwenye Bajeti ni kuwa Mtanzania maskini atatozwa kodi ya barabara ya umiliki wa gari na pikipiki hata kama hana vyombo hivyo.

Sababu ni kwamba Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, imeamua kufuta kodi za barabara kwa magari na pikipiki, badala yake wamiliki wa vyombo hivyo watalipa kupitia mafuta ya petroli na diseli ambayo yanapandishwa bei.

Mbaya zaidi ni kuwa mpaka mafuta ya taa nayo yanapandishwa bei. Lengo kuu ni Serikali kukusanya mapato mengi zaidi, kuliko kiasi ambacho kilikuwa kinapatikana awali kupitia kuwatoza wamiliki wa magari.

Bajeti hiyo imepitishwa na Bunge. Hakuna mbunge ambaye hamiliki gari. Hivyo, wabunge ni sehemu ya wanufaika wa unafuu wa kodi za barabara kwa vyombo vyao vya moto.

Wabunge walishangilia sana. Ushangiliaji wa wa wabunge ulikuwa ni usaliti mkubwa kwa wananchi. Ni kwa sababu asilimia zaidi ya 95 ya wananchi wanaowawakilisha bungeni hawana vyombo hivyo vya moto.

Hivyo, kumuongezea mwananchi bei ya mafuta kwa sababu ya kufidia kodi za barabara ni kumuonea. Mbunge wake alipaswa kusimama imara kupinga hilo.

Kuongeza bei ya mafuta ni kuongeza gharama za maisha kwa upana zaidi. Nyongeza hiyo ya mafuta itamfikia mwananchi wa chini atake asitake.

Mtumiaji wa mafuta ya taa nyumbani kama nishati yake ya mwanga na kupikia, anakwenda kuyaona machungu ya kodi ya barabara iliyohamishiwa kwenye mafuta.

Wamiliki wa mabasi ya masafa marefu na ndani ya miji wakishaona machungu ya nyongeza ya bei za mafuta, nao watataka kumbebesha mwananchi wa kawaida mzigo huo. Wataomba kupandisha nauli, kwa hiyo Mtanzania maskini ndiye ataumia.

Wamiliki wa saluni ambao wanamiliki jenereta ndogo ambazo huwawezesha kuendelea na kazi kipindi cha matatizo ya umeme, nao watalazimika kubeba mzigo wa kodi ya barabara.

Kimsingi hili ni jambo ambalo lilipaswa kubeba uzito wa kitaifa kuelekea kupitishwa kwa Bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha. Hata hivyo, wananchi walikaa kimya kama vile haliwahusu.

Nyakati ambazo uchumi wa mwananchi mmoja mmoja unaporomoka, biashara nyingi zimefungwa na zinaendelea kufungwa kwa sababu Mtanzania amepoteza uwezo wa kununua kwa kiasi kikubwa.

Nyakati ambazo hoteli nyingi zimegeuzwa mabweni na watu wengi wamepoteza ajira, hivyo kuongeza mlundikano wa watu wasio na ajira, wakati huohuo Serikali inaongeza ugumu wa maisha kwa wananchi.

Usisahau kuwa bei za bidhaa za chakula zipo juu na Bajeti ya Serikali haioneshi kuja kumpoozea gharama mwananchi, bali inakuja kuongeza.

Hayo ni mambo ambayo Watanzania walipaswa kuifanya mitandao ya kijamii izidiwe nguvu kwa Tanzania kutokana na wingi wa malalamiko. Mabaraza ya mitaani yalipaswa kutikisa kila upande wa nchi.

Hoja ilikuwa moja tu; ni kwa nini Mtanzania maskini abebeshwe mzigo wa gharama za watu wenye unafuu mkubwa wa maisha? Watanzania walitakiwa kuwa wakali sana katika hili.

Tunaweza kuacha hilo, tushike lingine ambalo ni kauli ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliyotoa bungeni kuwa wabunge waliopinga Bajeti wasipewe fedha za maendeleo.

Hii ni kauli ambayo pengine ingetolewa na mbunge chipukizi, siyo mwandamizi tena Spika wa Bunge ambaye Bunge lililopita alikuwa Naibu Spika na kabla ya hapo alipata kuwa Mwenyekiti wa vikao vya Bunge.

Tunaweza kuachana na ukongwe wa ndani ya Bunge alionao mtoa kauli, turejee kwenye mantiki ya kauli; mtu akipinga Bajeti ndiyo aadhibiwe kwa kunyimwa fedha za maendeleo?

Huo ni uongozi wa wapi? Kuleta mfumo wa kukomoana siyo uongozi wa Serikali na ni kinyume na muktadha unaoleta mgawanyo wa mihimili mitatu ya dola.

Mbunge anapaswa kupinga Bajeti kama anaona haifai. Hata hivyo, demokrasia ya Bunge inaelekeza wengi wapewe, hivyo kura zinapopigwa, wanaounga mkono Bajeti wakishinda, baada ya hapo inakuwa Bajeti ya wote, maana ndiyo iliyopitishwa.

Huwezi kusema Bajeti iliyopitishwa ni kwa ajili ya waliounga mkono, na walioipinga watakuwa na Bajeti yao. Bajeti ni moja, inapopitishwa inakuwa ya wananchi wote.

Ni kama uchaguzi, Rais hawezi kuchaguliwa na wote, lakini baada ya kushinda anakuwa Rais wa wote nchi nzima. Vivyo hivyo kwa wabunge, madiwani, wenyeviti wa mitaa na vijiji, hawawezi kupigiwa kura na wote, ila wakishinda wanakuwa viongozi wa wote.

Hivyo, kauli ya Ndugai kuwa wabunge waliokataa Bajeti wanyimwe fedha za maendeleo ina udhaifu mkubwa. Na ifahamike kuwa fedha husika si za wabunge wala Serikali, bali za wananchi.

Kuwanyima fedha wabunge, maana yake watakaoteseka ni wananchi ambao ndiyo wamiliki wa fedha husika. Zaidi, itakuwa ni kupingana na demokrasia.

Serikali inakwenda bungeni na mipango yake ya kukusanya fedha na kuzitumia katika mwaka husika wa fedha. Wabunge wanasikiliza na kuchagua kukubali au kukataa. Mwisho kabisa wengi wanashinda. Hapo hakuna sababu ya kuwekeana vinyongo.

Mpaka hapo utaona kuwa kauli ya Ndugai ilipaswa kuamsha hasira za wananchi ambao walipaswa kuja juu, kuhoji maoni ya Spika wa Bunge ambayo yanachafua mfumo wa demokrasia.

Kinyume chake, wananchi wamekuwa kimya, utadhani kauli ya Ndugai haina athari yoyote kwao. Katika mitandao ya kijamii, watu hawahoji. Ndugai anapata wakati mzuri katika kipindi ambacho alipaswa kukiona kigumu kutokana na matamshi yake.

MSHANGAO WANGU

Kwa siku mbili mfululizo, Watanzania wamejikita kwenye mjadala kuhusu kiungo mkabaji wa Klabu ya Tottenham Hotspur ya Ligi Kuu ya England, Victor Wanyama, kupewa hadhi kwa jina lake kupewa mtaa, Sinza, Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam.

Malumbano yamekuwa ni kwa nini Wanyama raia wa Kenya, apewe jina la mtaa, wakati Tanzania ina mastaa wakubwa na hawajawahi kupewa hadhi hiyo?

Straika wa Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta ndiye anatajwa zaidi, kwamba ingekuwa bora kama Mbwana angeanza kupewa hadhi hiyo.

Wanaopinga Wanyama kupewa jina la mtaa wanajenga hoja kuwa kama ni kigezo cha kucheza soka Ulaya, hata Mbwana anacheza kwenye bara hilo.

Watetezi wa Mbwana wanakwenda mbali zaidi na kueleza kuwa nahodha huyo wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, mwaka jana alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora Afrika kwa wachezaji wa ndani.

Kipindi Mbwana anatwaa tuzo hiyo, alikuwa anacheza Klabu ya TP Mazembe ya DRC. Baada ya hapo ndipo alisajiliwa Genk ya Ubelgiji.

Kwa hoja hiyo na kwa kuongezea Utanzania wake, ndipo watetezi wa Mbwana wanaibuka kwa nguvu kubwa na kuhoji; Wanyama kaifanyia nini Tanzania mpaka apewe jina la mtaa?

Nikikwepa kidogo malumbano kuhusu uhalali wa Wanyama kupewa mtaa, nabaki kwenye mshangao; je, Watanzania waliona sawa kwa wingi wao kutawala mitandao ya kijamii kwa hoja za Wanyama?

Wakati wakijadili suala Wanyama kwa nguvu kubwa, walishindwa kutumia hata robo yake kuhoji ongezeko la gharama ya maisha kwa Serikali kupandisha bei za mafuta.

Watanzania hawakushituka kabisa Ndugai aliposema wabunge waliokataa Bajeti wanyimwe fedha za maendeleo. Badala yake wameshituka sana katika suala la Wanyama kupewa hadhi ya mtaa kupewa jina lake.

Ni hapo ndipo unawaona Watanzania wenye kupenda vijimambo vyepesi na kuvishikia bango. Mambo mazito yenye kugusa moja kwa moja maisha yao ya kila siku wanayapa kisogo kama vile hayawahusu.

Kumbe aliyesema Tanzania ni nyepesi sana kuitawala alilenga mwamko mdogo wa Watanzania katika kuhoji mambo ya msingi na kuyabeba yaliyo mepesi.

Watu ambao wanakabiliwa na changamoto nyingi zinazowakita moja kwa moja kwenye maisha yao, lakini wanaacha kuhoji, badala yake wakaijaza mitandao ya kijamii kwa kila aina ya matamshi ya kuhoji uhalali wa Wanyama kupewa jina la mtaa.

Haina maana kuwa suala la Wanyama halina umuhimu, isipokuwa umuhimu huzidiana. Kuwepo au kutokuwepo kwa mtaa unaoitwa Wanyama hakuwezi kukupunguzia bei za bidhaa sokoni na madukani.

Suala la Wanyama au Mbwana kupewa jina la mtaa linahusu heshima kwa mchezaji husika na nchi yake. Jina la mtaa ni kumbukumbu ya miaka mingi ijayo. Hivyo, si vibaya kuwa na mjadala, lakini isiwe mjadala mkubwa kuliko wa kuhoji kupaa kwa mfumuko wa bei za bidhaa.

Kwa Tanzania, yenye kufaa kujadiliwa kidogo ndiyo hujadiliwa zaidi, halafu yenye kustahili mjadala mpana huwa hawayajadili kabisa. Ni kama vile hawana habari nayo au hayawahusu.

SASA NAMI NITIE NENO

Tanzania na ukubwa wake, mitaa na barabara ni nyingi mno. Ni uhakika kuwa huwezi kujaza majina ya watu mashuhuri mpaka kuyamaliza.

Hivyo basi, baada ya Wanyama, wengine pia wanaweza kupewa mitaa na barabara ili zisomeke kwa majina yao.

Kuhusu suala kwamba Mbwana alistahili kabla ya Wanyama, litumike kuzindua mamlaka za nchi kutambua thamani za mashujaa wa taifa ili hadhi zao zilindwe.

Binafsi nimpongeze Meya wa Ubungo, Boniface Jacob, kwani uamuzi wake wa kumzawadia Wanyama jina la mtaa umeileta nchi kwenye mjadala wa kutambua na kuthamini mashujaa wa taifa.

Kumbe sasa, wananchi wengi wanapenda Mbwana abebe jina la mtaa au barabara lakini sauti zao hazikusikika mpaka Meya Jacob alipoupa jina mtaa wa Wanyama.

Kumbe sasa mashujaa wa Taifa la Tanzania wanapaswa kukumbukwa na kuenziwa kwa namna mbalimbali, ila hakuna presha iliyotoka mpaka mtaa ulipopewa jina la Wanyama.

Kumbe sasa, uamuzi wa Meya Jacob kumpa Wanyama jina la mtaa, ulipaswa kuchukuliwa chanya, baada ya hapo nchi ijielekeze kwenye kuwapa hadhi mashujaa wake.

Je, bila Meya Jacob kumpa Wanyama mtaa, nani angeanzisha vuguvugu la kutaka Mbwana na mashujaa wengine wapewe mitaa na barabara? Miaka nenda rudi mashujaa wa taifa hili wanachukuliwa kawaida tu.

USAHIHI WA KUMPA WANYAMA MTAA

Wanyama anacheza ligi ya soka inayotazamwa zaidi ulimwenguni, Ligi Kuu ya England. Vilevile Wanyama anachezea timu ambayo imemaliza msimu ikitoka nafasi ya pili.

Kwa hadhi ya Wanyama katika ulimwengu wa soka na jinsi alivyofika Dar es Salaam na kukubali kujumuika kwenye mpira wa Ndondo, ni wazi amejishusha sana.

Jina la Wanyama katika mtaa uliopo Sinza, ni tangazo kubwa kwa kitongoji hicho, Manispaa ya Ubungo na Jiji la Dar es Salaam. Meya Jacob alipaswa kupongezwa kwa ubunifu wake.

Kitendo cha Wanyama kupewa mtaa na mazingira aliyokabidhiwa ndiyo kivutio zaidi. Wapo wanasoka daraja la Wanyama hufika Tanzania kwenye mbuga za wanyama, lakini huwa hawataki hata kusema kuwa wapo Tanzania.

Kumpata Wanyama aliyefanya yote kuonesha anaipenda na anajivunia kuwepo Tanzania, ni jambo jema.

Lipo swali kwa nini apewe Mkenya na si Mtanzania? Hili swali najibu hivi; Barabara yenye umbali wa nusu kilometa inayopita Ikulu ya Nairobi hadi geti kuu la Ikulu, inaitwa Barabara ya Jakaya Kikwete.

Heshima iliyoje? Barabara ambayo inapitisha magari kwenda ofisi kuu ya umma nchini Kenya imepewa jina la Jakaya Kikwete ambaye ni Rais wa Nne wa Tanzania.

Kikwete alikwenda Kenya kuzindua barabara hiyo mwaka 2015, wakati huo akiwa bado Rais. Hiyo maana yake ni kuwa Rais wa Kenya kila anapotoka na kurudi Ikulu, lazima apitie Barabara ya Jakaya Kikwete.

Utaona kuwa hadhi ambayo Kikwete amepewa Kenya wakati nchi hiyo ikitawaliwa na Uhuru Kenyatta, inafuatia uungwana ambao Tanzania iliuonesha ilipoibadili jina Barabara ya Old Bagamoyo na kuipa jina la Rais Mstaafu wa Kenya, Mwai Kibaki.

Wakati Old Bagamoyo inabadilishwa jina kuwa Mwai Kibaki, watu wengi walipinga, lakini Wakenya wakaonesha kuwa wao wakipewa hawasahau, wakaipa Barabara ya Ikulu yao jina la Jakaya Kikwete. Awali, Barabara hiyo ilikuwa ikiitwa Mlimani.

Maana yake ni kuwa Wanyama kupewa heshima ya mtaa Tanzania ni ufunguo wa kidiplomasia na ujirani mwema dhidi ya Kenya. Inawezekana Mbwana, Ali Kiba, Nasibu Abdul 'Diamond Platnumz', Ambwene Yessayah 'AY' au mwingine yeyote wa Tanzania kutokea kupewa heshima kubwa Kenya.

Mitaa ya Tanzania ni mingi na majina mengine hata hayavutii. Hakuna sababu ya kuvutana kwa mtaa mmoja. Mtaa wa Wanyama uwe chachu kwa mashujaa wa Tanzania kukumbukwa na kupewa hadhi itakayodumu.

TAFAKARI YA MASHUJAA

Mwaka 1968, Mtanzania John Akhwari, aliwaduwaza Wazungu katika mashindano ya Olimpiki, alipokimbia kilometa 23 akiwa ameumia mguu na kuchanika vibaya.

Katika mbio za marathon kilometa 42, Akhwari aliumia akiwa kilometa 19. Hata hivyo, alipambana na maumivu yake mpaka alipomaliza mbio hizo. Olimpiki ya mwaka huo ilifanyika Jiji la Mexico, nchini Mexico.

Ujasiri na kujituma huko ndiko kulikowasisimua Wazungu, wakampa zawadi ya fedha ambazo mwenyewe husema zilitosha kubadili maisha yake, lakini aliyekuwa waziri wa michezo wa Tanzania wakati huo alimdhulumu.

Akhwari mpaka leo video yake akikimbia peku kumaliza marathon akiwa ameshaumia mguu, huoneshwa kutoa hamasa kwa wengine kujituma mpaka mwisho, lakini mwenyewe nchi yake ilishamsahau japo yupo hai.

Pigeni kelele mashujaa waliodhulumiwa na viongozi, siyo kulilia mtaa wa Wanyama. Akhwari aliwamaliza Wazungu alipoulizwa aliwezaje kukimbia kilometa 23 akiwa ameumia mguu? Alipojibu: "Nchi yangu Tanzania ilinituma nije nikimbie kilometa 42, siyo nianze kilometa 42 na kuacha."

Baada ya hapo sasa fungueni mjadala kuhusu maajabu ya Filbert Bayi na rekodi yake kwenye mbio za Jumuiya ya Madola, akabeba na medali ya dhahabu lakini Tanzania anachukuliwa poa tu.

Unaweza pia kustaajabu maajabu ya Juma Ikangaa na uwezo wake katika riadha miaka ya 1980, kisha tafakari miaka yote hiyo, eti leo ndiyo Watanzania wanamkumbuka baada ya Wanyama kupewa mtaa Sinza.

Ndimi Luqman MALOTO
 
Siku dereva wa lori atakapo toa jina la mtoto wake au bashite street wanaandamana na kumpongeza mzalendo analinda mitaa ya nchi wasipewe wageni
 
Tatizo madhara ya kutokua na Elimu bora mkuu ndio maana unaona Bunge linaweza kupitisha sheria za kukandamiza wananchi bila kujua athari zake mbeleni...,machinga na mamalishe walipe kodi huku mchimba madini mpaka atangaze faida ndio atalipa kodi..wengi wamesoma kwa kukariri kwa hiyo uhalisia wa kilichopo kichwani hamna kitu ni bora hata asie na Elimu kabisa Tanzania ana uelewa kidogo...
 
Sasa ni lipi jema waungwana.? Mlitaka nini kifanyike na serikali hii ndo mridhike? Hebu pitieni bajets za nchi zingine ndo mtajua tz ina nafuu kiasi gani?
 
Sasa ni lipi jema waungwana.? Mlitaka nini kifanyike na serikali hii ndo mridhike? Hebu pitieni bajets za nchi zingine ndo mtajua tz ina nafuu kiasi gani?

Umesoma mada ukaelewa??

In short hakuna jema tatizo ni kwamba iyo nchi mang'ombe ni wengi sana
 
Hakuna kitu najutia kama
Kuzaliwa nchi ya mafisad
Tanzania

Bora ngezaliwa kenya nkakimbizana na alhshababu
Tu
 
Back
Top Bottom