Maboso
JF-Expert Member
- Feb 18, 2013
- 5,164
- 5,761
TAARIFA KWA UMMA
MAKALA YA GAZETI LA MWANANCHI YA TAREHE 21-07-2015 YENYE KICHWA CHA HABARI "MTANDAO WA RUSHWA MAHAKAMANI HUU HAPA"
NAFASI YA VYOMBO VYA HABARI MAKALA MAALUM YA GAZETI LA MWANANCHI LA TAREHE 21/07/2015 UK. 25 - 26
Mahakama ya Tanzania inatambua nafasi ya vyombo vya habari katika kuwafikishia wananchi habari na kuwaelimisha. Vile vile tunatambua nafasi ya kipekee ya vyombo vya habari katika kukosoa utendaji wa taasisi za umma na binafsi. Kwa kutambua hilo Mahakama imeunda jukwaa la mahakama na vyombo vya habari (Judiciary- Media forum)
USHIRIKIANO WA MAHAKAMA NA VYOMBO VYA HABARI
Katika kudhihirisha dhamira yake ya kushirikiana na vyombo vya habari ili kuboresha huduma na utoaji habari, tarehe 3/12/2014 Mahakama iliandaa kongamano la kujadili changamoto zinazoikabili pamoja na nafasi ya vyombo vya habari. Kongamano hili lilihusisha wahariri wa vyombo vyote vya habari. Katika kongamano hilo, pamoja na mambo mengine, tulikubaliana yafuatayo:-
- Kuimarisha ushirikiano kwa kupeana taarifa muhimu
- Mahakama kutoa ufafanuzi wa masuala yasiyoeleweka kwa waandishi wa habari ili kuepusha upotoshaji
- Kushirikiana katika kujengeana uwezo wa kuandika habari za mahakama.
UTEKELEZAJI WA MAKUBALIANO
Mahakama inatekeleza makubaliano haya kwa kutoa taarifa na maelezo ya kina kuhusu masuala mbalimbali hasa ya kesi zinazoendelea mahakamani. Mahakama inafanya hivyo kwa ufanisi zaidi pale ambapo mtaka taarifa anataja namba ya kesi na mahakama ilipo kesi au mtumishi anayelalamikiwa. Bila kutolewa kwa taarifa hizi ni vigumu kwa mahakama kuchukua hatua.
2. UMUHIMU WA TAARIFA HII
Katika gazeti la Mwanachi la tarehe 21/07/2015 ukurasa wa 25 na 26 kulikuwa na habari yenye maneno "Mtandao wa rushwa Mahakamani huu hapa." Katika habari hiyo Mwandishi ametoa tuhuma kwamba kuna rushwa Mahakamani kwa kutolea mifano kama ifuatavyo:-
2.1 Bw. Muhidini Ngulumwa, anashitakiwa kwa jinai katika Mahakama ya Mwanzo Magomeni lakini mlalamiko hafiki Mahakamani kwa miaka mitatu sasa ambapo pia aliombwa rushwa ya shilingi laki tano.
- Bi. Kuruthum Majjid, alitoa rushwa ya laki moja ili Polisi wamkamate mtuhumiwa. Mtuhumiwa alifikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Mogomeni ambapo amepewa dhamana lakini haudhurii Mahakamani kwa muda wa miezi kumi na tatu sasa.
- Bw.Abdallaha Majata, kesi yake inazungushwa mahakama ya Mwanzo Mbagala kwa madai kuwa uchunguzi haujakamalika na kwamba kuna mshauri wa Mahakama anamwomba wamalize kesi nje ya Mahakama.
- Bi. Halima Abdan, ametoa fedha polisi na Mahakamani kuwezesha ndugu yake apewe dhamana bila mafanikio. Mwandishi hakutaja Mahakama ilipo kesi husika.
- Bw. Claudiana Mbazigwa, amepoteza milioni moja na laki nne katika jitihada ya kumdhamini ndugu yake katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo bila mafanikio.
- Bw. Abdallh Mpondela amepoteza laki tano akijaribu kumdhamini ndugu yake bila mafanikio Mwandishi hajataja Mahakama ilipo kesi husika.
- Bw. Laizer Kaanan ametoa shilingi laki sita katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo ili kumdhamini ndugu yake bila mafanikio.
3.0. UFUATILIAJI WA TUHUMA
Mahakama imeguswa na kusikitishwa na tuhuma hizi. Kwa vile kesi katika Mahakama husajiliwa kwa nambari za usajili kwa ajili ya utambulisho, na kwa vile katika Makala Mwandishi hataji namba za kesi na kwa kuzingatia uzito wa habari yenyewe, Mahakama imeanza uchunguzi juu ya tuhuma hizi kwa hatua zichukuliwe na Idara ya Ukaguzi wa Huduma za Mahakama na Maadili kwenda ofisi za gazeti la Mwananchi (tarehe 22/7/2015) kupata taarifa zitakazowezesha kuchukuliwa hatua.
Hadidu za rejea zifuatazo zilitumika:-
- Kufahamu iwapo mwandishi wa makala anafahamu anuani au namba za simu za walalamikaji ili wasaidie kutoa taarifa zaidi ikiwa ni pamoja na nambari za kesi kwa ajili ya uchunguzi na hatua zifaazo.
- Kufahamu iwapo mwandishi wa makala anafahamu nambari za kesi za matukio aliyoandika.
- Kufahamu iwapo mwandishi anawafahamu au ana anuani au namba za simu za wazee wa baraza aliohojiana nao.
- Kufahamu iwapo mwandishi alipata namba za simu ya askari aliyezungumza na Halima Abdan baada ya kuunganishwa na mzee wa baraza.
- Kupata maelezo ya aina ya uchunguzi aliofanya mwandishi ili kujiridhisha na ukweli wa habari.
4.0. MATOKEO YA UCHUNGUZI
Katika ofisi za gazeti la Mwananchi Ofisa wa ngazi za juu wa Mahakama alikutana na Bw. Joster Mwangulumbi ambaye ni Mhariri wa Habari za uchunguzi. Bw. Joster alimfahamisha Mkurungenzi Msaidizi mambo yafuatayo:-
- Mwandishi wa makala hayo (Bi. Kalunde Jamal ) yuko safarini na asingepatikana kwa mahojiano lakini alimpigia simu wakaongea kuthibitisha masuala kadhaa.
- Mwandishi wa makala ni mwandishi wa habari za Mahakama na katika kufanya kazi zake alipata malalamiko aliyoyatolea taarifa ofisini akatakiwa kufanya uchunguzi na matokeo ya uchunguzi ndiyo yaliyochapishwa.
- Katika ufuatiliaji Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Mwanzo na Wilaya hawakuwa tayari kuzungumzia na kufafanua malalamiko hayo.
- Ofisi za gazeti na Mwananchi na mwandishi wa makala hawafahamu nambari za kesi zinazolalamikiwa, anuani na hata namba za simu za walalamikaji waliotajwa. Pia hawana namba za simu za wazee wa baraza au askari polisi aliyewasiliana na Halima Abdan na kwamba hawawezi kupata anuani au namba za simu hizo.
Mapungufu haya yanaleta mashaka juu usahihi wa taarifa zilizoandikwa katika makala hayo. Licha ya upungufu wa dhahiri ambao hauiwezeshi Mahakama kuchukua hatua zozote, katika toleo la tarehe 22/07/2015 gazeti hili lilitoa tahariri yenye kusisitiza yaliyomo katika makala yenye utata ila yenye kuvutia.
5.0. HARAKATI ZA MAHAKAMA KUBORESHA
5.1. HATUA ZA KUBORESHA HUDUMA
Mahakama inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha huduma zake. Mahakama pia kama Taasisi ya Umma iko tayari na imekwisha toa fursa kwa wadau kutoa maoni yao kuhusu namna ya kuboresha huduma zake kupitia matangazo kwenye magazeti Mwananchi la tarehe 29/5/2015 na Mtanzania la tarehe 03/6/2015 ambapo maoni yanaendelea kupokelewa. Mahakama pia iko tayari kukosolewa kwa njia zote halali kwa lengo la kuboresha huduma, ili mradi taarifa hizo ziweze kusaidia kuchukua hatua kwa sasa na kuwa kama chachu ya mabadiliko/mageuzi yanayoendelea ndani ya Taasisi hii muhimu ya uendeshaji wa Nchi yetu.
5.2. WITO KWA WANANCHI NA WADAU
Ili kuondoa kero zilizobainishwa na gazeti la Mwananchi, Mahakama inatoa rai kwa gazeti la Mwananchi au mtu yeyote mwenye taarifa sahihi kuipatia ushirikiano ili kupata nambari za kesi zilizolalamikiwa na mahakama zilikofunguliwa.
Kwa lengo hilo la ushirikiano Mahakama inaomba wale wote waliotajwa katika makala iliyochapishwa tarehe 21/07/2015 kuhusu mtandao wa rushwa Mahakamani (Kama wapo) ambao ni Muhidini Ngulumwa, Kuruthum Majjid, Abdallah Majata, Halima Abdan, Claudiana Mbazigwa, Abdallah Mpondela na Laizer Kaanan wafike Makao Makuu ya Mahakama, Mahakama ya Rufani ya Tanzania, No 11409 Kivukoni Front, waonane na Mkurungenzi Msaidizi wa Malalamiko katika Idara ya Ukaguzi wa Huduma za Mahakama na Maadili ili watatuliwe kero zao. Inasisitiza tena ili kuondoa rushwa, maadili yasiyofaa huduma suala la uwazi wa utoaji huduma na kuboresha mawasiliano ni muhimu kuanzia tarehe 6 Desemba, 2014.
Mahakama imeweka namba ya simu Na. 0752- 500 400 ambayo inapokea malalamiko, maoni na mapendekezo ya wananchi na wadau mbalimbali kwa njia ujumbe mfupi na mitandao ya kijamii (WhatsApp, na barua pepe info@judiciary.go.tz)
Matokeo ya utaratibu huu ni mafanikio makubwa ambayo Gazeti la Mwananchi ingeyatumia pia kwa manufaa ya Wananchi, kwa kutoa ushahidi na taarifa kamilifu.
"PAMOJA TUNABORESHA HUDUMA"
IMETOLEWA NA:
MTENDAJI MKUU
MAHAKAMA YA TANZANIA