SoC03 Siku ya Nyerere (Oktoba 14) iwe kielelezo cha uchapaji kazi wa Baba wa Taifa letu na sio alama ya uvivu (Kukaa Nyumbani) wa Mtanzania

Stories of Change - 2023 Competition

Ramon Sanchez

JF-Expert Member
Oct 9, 2022
767
1,829
Habari za wakati huu ndugu zangu wote.

Kufanya kazi kwa bidii ni jambo muhimu sana ambalo sote tunahitaji maishani mwetu. Haiwezekani kufikia malengo fulani makuu bila kufanya kazi kwa bidii.

images (22)_1.jpeg

(Picha kwa hisani ya mtandao wa Google)​

Kwa maneno mengine ninaweza kusema ya kwamba, mtu asiyefanya kazi hawezi kupata chochote ikiwa anataka kukaa tu na kusubiri miujiza mingine. Kwa upande mwingine, mtu anayeendelea kufanya kazi kwa bidii kila wakati hakika atapata mafanikio makubwa maishani.

Kufanya kazi kwa bidii ni muhimu na historia imethibitisha hilo mara kwa mara. Mtu kama Bill Gates alikuwa akifanya kazi kwa saa nyingi kwa siku na alisinzia kwenye meza yake ya ofisini akiwa tu na vitabu vyake kama mto wake wa kulalia.

Vile vile, waziri mkuu wa zamani wa India, marehemu Jawaharlal Nehru alikuwa akifanya kazi kwa saa 17 kwa siku na siku saba kwa wiki. Hakufurahia likizo yoyote. Kiongozi wao mwingine mkuu, Mahatma Gandhi alifanya kazi siku nzima ili kupata uhuru wa nchi yao wa India.

Hivyo basi, tunaona kwamba ufanyaji wa kazi kwa bidii uliwalipa watu hao wote. Mtu lazima awe macho kila wakati kufanya kazi kwa bidii kwani inaweza kukusaidia kufikia ndoto zako. Kama tunavyosema, mwanadamu amezaliwa kufanya kazi.

images (22).jpeg

(Picha kwa hisani ya mtandao wa Google)​

Tunapofanya kazi kwa bidii maishani, tunaweza kufikia chochote na kushinda kikwazo chochote. Zaidi ya hayo, tunaweza pia kuishi maisha bora tukijua kwamba tumejitolea kwa kila kitu na kujitolea kwa uwezo wetu wowote kwa kazi yoyote tunayofanya.

Ndugu zangu watanzania, ni nani anaifahamu nchi moja kubwa ya kutokea katika bara la Amerika ya Kusini inayojulikana kwa jina la Brazil? Je, unaposikia neno Brazil, ni kitu gani chema huja kwa haraka haraka katika kichwa chako? Kwa wale vijana waliozaliwa miaka ya hivi karibuni ngoja niwasaidie jibu la hili swali pasipo kuwapotezea muda.

images (20).jpeg

(Picha kwa hisani ya mtandao wa Google)​

Kama wewe umekuwa ni mfuatiliaji wa muda mrefu wa matukio makubwa ya hapa duniani bila shaka utakuwa unakubaliana na mimi ya kwamba neno Brazil linashabihiana moja kwa moja na umahiri wa kusakata kabumbu wa timu ya taifa ya wanaume wa nchi hiyo almaaruf kama "Seleção".

Kama mchezo wa kandanda ulivyo kwa vijana wale wa kutokea maeneo ya misitu minene ya Amazon, ndivyo jinsi kaliba ya uchapakazi na kujituma ilivyowahi kuwa kwa Julius Kambarage Nyerere Waziri mkuu na Rais wa kwanza wa nchi ya Tanganyika.

Kama Mwalimu Nyerere alikuwa mchapa kazi, kwanini watanzania wanamuenzi kupitia uvivu (Mapumziko ya "Nyerere Day" Oktoba 14)? Hii kasumba ya kupenda kukaa kaa nyumbani na vijiweni kwa kisingizio cha "Nyerere Day" badala ya kwenda kuwajibika ofisini tumeitoa wapi? Kama baba yetu wa Taifa hakuwa hivi, sisi watoto na wajukuu wake hii vinasaba tumerithi kutoka kwa nani?

images (21).jpeg

(Picha kwa hisani ya mtandao wa Google)​

Mwalimu alikuwa kiongozi mwenye mvuto wa akili na uadilifu mkubwa, aliunganisha nchi na utambulisho wa kitaifa kutoka kwa makabila zaidi ya 120, yaliyounganishwa na lugha yao ya Kiswahili na maelewano ya kijamii yaliyojengwa juu ya misingi ya maadili, amani, haki, umoja na kujitolea.

Wakati nchi nyingine za kusini mwa Afrika zilipolazimishwa kuingia katika vita vya ukombozi ili hatimaye kufikia lengo la kuwa huru, Tanzania ilitoa msaada wa kisiasa, mali na kimaadili hadi uhuru na utawala wa ndani wa wazawa walio wengi ulipopatikana mwaka 1975 (Msumbiji, Angola), 1980 (Zimbabwe), 1990 ( Namibia) na hatimaye, 1994 (Afrika Kusini).

images (24)_1.jpeg

(Picha kwa hisani ya mtandao wa Google)​

Nyerere alifuata maadili ya uongozi, demokrasia na ubinadamu katika bara zima na, pamoja na viongozi wa nchi nyingine chache za Kiafrika zilizokuwa huru mwaka 1963 kama vile Nigeria na Ghana, wakaanzisha Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), ambao baadaye ulikuja kuwa Umoja wa Afrika.

images (23).jpeg

(Picha kwa hisani ya mtandao wa Google)​

Kwanini shughuli katika ofisi za serikali zisifanywe kwa muda wa saa zile zile rasmi (saa 8 kwa siku) ili kumuenzi Mwalimu kwa vitendo? Au kwanini siku ya "Nyerere Day" watanzania wasifanye kazi kwa muda wa saa tisa (saa 8 za siku zote jumlisha moja la ziada) ili kuendeleza "legacy" hii njema ya baba wa taifa letu?

Nyerere alikuwa Rais wa kwanza wa Tanzania ambaye alisisitiza kuitwa kwa cheo cha Mwalimu tu baaasi. Ndio, Nyerere alikuwa ni mwalimu na moja kati ya shule alizofundisha ni pamoja na Sekondari ya Pugu. Nyerere aliupenda saaana Ualimu na alikataa vyeo, marupurupu na kufurahia maisha ya anasa na rahisi hata kama alikuwa raia namba moja na Rais wa Tanzania. Mwalimu alipostaafu, alirudi katika kijiji chake kidogo ili kuishi maisha ya kawaida mno na rahisi pamoja na kuhudhuria Misa Takatifu kila siku ya jumapili.

Alipokuwa Rais, Nyerere alishiriki Misa Takatifu popote alipokuwa, na wakati wa Misa, angependelea kuchanganyika na watu wengine kwenye viti. Mara kwa mara alienda kwenye Ushirika Mtakatifu na alikataa kusindikizwa na polisi pamoja na ving’ora. Iwapo angelazimika kujipanga ili kupokea Ushirika Mtakatifu - angefanya hivyo kwa moyo mkunjufu na bila kujikweza.

HITIMISHO: Kufanya kazi kwa bidii hutufundisha nidhamu, kujituma na kujitegemea. Kupitia kufanya kazi kwa bidii pekee tu ndipo tunaweza kufikia malengo ya maisha yetu. Hivyo, sote tunapaswa kufanya kazi kwa bidii na sio kuendekeza kasumba ya uvivu kwa kujificha katika mwamvuli wa "Nyerere Day"..
 
Back
Top Bottom