Serikali yatishia kuzifuta taasisi zikiwemo za dini

MaxShimba

JF-Expert Member
Apr 11, 2008
35,772
4,054
9/2/2009

Serikali yatishia kuzifuta taasisi zikiwemo za dini

Na Salim Said


SERIKALI inakusudia kuzifutia taasisi 100 za dini nchini, kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yao na kutoa maelezo ya mabadiliko ya wadhamini wake katika mamlaka husika kwa muda mrefu sasa.

Kabla ya kutekeleza azma hiyo serikali kupitia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Ritta) imetoa notisi ya siku 30 kwa taasisi hizo kutoa sababu za kisheria za kushindwa kutekeleza majukumu yao, na kwamba zitakazoshindwa zitafutiwa.

Akitengua uamuzi wa serikali wa kufuta misamaha ya kodi kwa taasisi za dini nchini Juni mwaka huu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alionya pia kwamba, kuna baadhi ya taasisi zinaitumia vibaya misamaha hiyo na kuahidi kufuatilia na kuzichukulia hatua.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na kusainiwa na Kaimu Mkuu Utawala wa Usajili wa Ritta, Philip Saliboko, serikali imezitaka taasisi hizo kujielezea kisheria sababu za kushindwa kufanya kazi zao kwa mujibu wa usajili wao.

Aidha asilimia kubwa ya taasisi hizo zinamilikiwa na taasisi za dini ya kiislamu na chache zikimilikiwa na dini ya Kikristo.

Hivi karibuni kumekuwa na mvutano mkali baina ya serikali na taasisi za dini nchini, huku Waislamu wakivutana na serikali kuhusiana na hoja ya Mahakama ya Kadhi. Pia waraka wa Kanisa Katoliki umezua mjadala mzito katika jamii na serikali kwa jumla.

“Kwa kutumia Trustee Incorporate Act Cap. 318 R.E 2002 sehemu ya 23(1)(d) nimeridhika kwamba bodi hizi zimeshindwa kufanya kazi au majukumu yake na pia zimeshindwa kuleta taarifa za kutujulisha sababu za mabadiliko au kutojaza nafasi za wadhamini wao kwa muda mrefu,” alisema Saliboko.

Taasisi hizo ni pamoja na nyumba za kiibada (misikiti na makanisa), shule, hospitali, taasisi za kibiashara na huduma za kimisaada kwa jamii, vitoto vya kulelea mayatima na taasisi za fedha.

Alitahadharisha kwamba, zikipita siku 30 za notisi hiyo tangu ya kutolewa kwake atazifuta taasisi hizo, la sivyo zitoe sababu zinazokubalika kisheria.

Taarifa hiyo iliyoandikwa na kusainiwa na Saliboko Agosti 31 mwaka huu, pia imechapishwa kama tangazo katika baadhi ya magazeti ya kila siku nchini.

Alizitaja baadhi ya taasisi hizo kuwa ni pamoja na Masjid Taqwa Iringa, Masjid Nuur Same, Daarul Uloom Madrasat Sunniya, Masjid E. Amirul Ali bin Abutalib (A.S) Magomeni Dar es Salaam, Madrasatul Ally Badawwy Kondoa, Gofu Juu Muslim Group Tanga na Masjid Jumuiya El-Islaamiya Tambuka Reli Temeke.

Nyingine ni Masjid Munawwar na Madrasat Muhammadiya, Najah Islamic Center Kwale Dar es Salaam, Rungwe Education Trust Fund Tukuyu, Michael Tayari Relief Fund Mbeya, The Kondoa Education Trust Fund, Masjid Islamic Ikhwaan, Masjid Ibadhi Mwanga, Madrasatul Badawwy, Bodi ya Maendeleo ya Waislamu Shinyanga na Ludewa District Educational Trust Fund.

Pia zimo taasisi za Kirua Vunjo Development Trust Fund, Deeper Christian Life Ministry Tanzania, Baby Care Women Association (Bacana), Kasulu District Education Trust Fund, Tarime Rural Development Trust Fund, New Life Outreach, Prof. Justinian F. Rweyemamu Accountancy Fund, Inter Consult Employees Trust Fund na Faith Foundation.

Alizitaja nyingine ni Biirabo Rural Transforamation Scheme Trust Fund, Korean Methodist, Igunga Education Trust Fund, Children Education Programmes (Cep), Isangati Division Development Trust Fund na Alhajj Abdulrehman Hassan Charitable Hospital.

Nyingine ni pamoja na Masista wa Huruma wa Mtakatifu Vinsent, Institution of Religious Muslim School, Human Eye Foundation, Mama Clementina Foundation, African Sisters St. Agness Chipole, Diocese of Mbinga, Sunni Muslim Jamaat Charitable Hospital, Pentecostal Church of Dodoma Urban na Masjid Jamhuri Islamia Keko.

Hizo ni baadhi kati ya taasisi hizo 100 zilizoorodheshwa katika tangazo lililochapishwa jana katika Gazeti la Serikali la The Daily News.

Hata hivyo, Mwananchi haikufanikiwa kumpata Saliboko kupitia simu yake ya mkononi, ili kupata ufafanuzi zaidi kuhusiana na matatizo ya taasisi hizo. Habari zilizotolewa na mfanyakazi mmoja wa ofisi hiyo zilisema alikuwa kwenye mkutano.

“Aah, mimi siwezi kusema chochote kwa sababu tangazo limesainiwa na Saliboko na yupo katika kikao cha siku nzima, lakini tangazo linajieleza,” alisema Joseph Mwakatobe kutoka Ritta.

Imetoka Gazeti la Mwananchi
 
Ni kweli maana hizi taasisi nyingine zinatumia udini kwa ajili ya manufaa ya watu wachache kama misamaha ya kodi, Kuna baadhi zindiriki hat kushiriki katika biashara haramu ya dawa za kulevya. Wanajipatia misaada ambayo hawaitumii kama vile wanavyoomba kwa wahisani wao. Wakifutiwa hao itakuwa ni jimbo la maana sana.
 
Back
Top Bottom