Serikali yakataa kuwalipa walimu 19,276

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,028
Serikali yakataa kuwalipa walimu 19,276

na Hellen Ngoromera
Tanzania Daima~Sauti ya Watu

SERIKALI imekataa kulipa madai 19,276 ya walimu wa shule za msingi, sekondari, vyuo vya ualimu na ukaguzi wa shule yenye thamani ya zaidi ya sh bilioni saba kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo wahusika kudaiwa kughushi nyaraka mbalimbali.

Uamuzi huo ulitangazwa jana jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mwantumu Mahiza, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu madai ya madeni ya walimu ya kiasi cha sh bilioni 16.4 yaliyowasilishwa serikalini na Chama cha Walimu Tanzania (CWT).

Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo kati ya madai hayo, 1, 754 ambayo yana thamani ya sh 1,174, 800,255.56 ambayo ni ya sekondari yalibainika kughushiwa, hayakupita kwa wakuu wa shule, hayakuwa na nyaraka halali pamoja na sababu nyingine wakati ya walimu wa shule za msingi yalikuwa 17,522 ambayo thamani yake ni sh 6,128,644,36.

Kutokana na sababu hizo Naibu Waziri huyo alisema wizara imeshaandika barua kwa wahusika na kuwa imewapa mwezi mmoja kuzifanyia marekebisha kasoro mbalimbali kuhusu mapungufu yaliyojitokeza katika madai yao na kuwa ikibainika kuna walimu walioghushi nyaraka kwa nia ya kuiibia serikali watachukuliwa hatua za kisheria ili kukomesha tabia hiyo.

‘Inatia shaka, kuna mwalimu mwingine alithubutu kufanya ujanja na kudurufu cheti cha kuzaliwa cha mtoto mmoja kuwa watoto watatu au zaidi tofauti lakini tuligundua baada ya kusahau kubadili baadhi ya namba katika vyeti hivyo, mwingine aliandika alisafirisha tani saba za mizigo wakati kwa taratibu tunaruhusu tani tatu tu ambazo nazo ni kilo nyingi sana, kuna mambo mengi yamefanyika jamani katika zoezi hilo”, alisema naibu waziri huyo.

Kwa upande wa madai ya walimu wa shule za sekondari, vyuo vya ualimu na ukaguzi wa shule ambayo yalishughulikiwa na makao makuu ya wizara hiyo na kuhakikiwa Oktoba 23 na makao makuu ya wizara hiyo na CWT, Mahiza alisema hadi kufikia Novemba 17 mwaka huu wizara ilipokea madai hayo yenye thamani ya sh 2,435, 686, 968.16 na kuyafanyia uhakiki.

Alisema katika kuhakiki madai 2,182 yenye thamani ya sh 1,260,886, 742.60 yaliyohusu posho za kujikimu, uhamisho, likizo, wastaafu na mambo mengine yalihakikiwa na kukubaliwa kisha kuwasilishwa Wizara ya Fedha na Uchumi (Hazina) Novemba 19 na kuwa kwa sasa malipo yameshaanza kufanyika.

Kwa upande wa madai ya walimu wa shule za msingi alibainisha kuwa hadi mwishoni mwa Novemba mwaka huu serikali ilipokea madai yenye thamani ya sh 17,930,141,892.00 kisha kuhakikiwa na timu ya uhakiki katika kila mkoa Novemba 10.

“Madai yaliyokubaliwa baada ya uhakiki ni ya sh 11,801,497,531.00. Jumla ya walimu waliowasilisha madai ni 51,688 na walimu 34,166 walilipwa madai yao, halmashauri zote isipokuwa Longido zilianza kufanya malipo Novemba 17 mwaka huu hadi kufikia Novemba 30 zilikamilisha kuwalipa walimu madai yao, Longido haikutumiwa kutokana na matatizo ya takwimu”, alisema naibu waziri huyo.

Aliongeza kuwa pamoja na madai hayo wizara imeendelea kupokea madai mapya yenye thamani ya sh 1,166,353,606.41 hadi kufikia Desemba 15 mwaka huu kati ya hayo madai yenye thamani ya sh 561,255,050.96 na kuwa madai yenye thamani ya sh 605,098,553.45 yameonekana kuwa na nyaraka pungufu au kutostahili kulipwa kabisa.

Akizungumzia changamoto zilizojitokeza katika zoezi hilo alisema kuwa baadhi ya walimu hasa katika Halmashauri ya Kigoma walighushi kwa kalamu viwango vya fedha wanazostahili kulipwa na wale waliobainika kughushi alisema wizara yake imewachukulia hatua.

Alisema kutokana na mambo mbalimbali yaliyojitokeza serikali kupitia viongozi wa mikoa na halmashauri imeweka mkakati wa kutembelea kila shule ili kukutana na walimu ana kwa ana kuhusu madai hayo. Aliongeza kuwa kwa sasa matatizo ya kila mwalimu yatashughulikiwa shuleni na ufumbuzi wake kupatikana hapo.

Sambamba na hilo, amewaagiza wakurugenzi kutozalisha madeni yoyote ya walimu kuanzia sasa kwa kuzingatia taratibu za utumishi wa umma zikiwemo kutohamisha watumishi wake kama hakuna fedha, kutoidhinisha masomo bila kuwepo kwa fedha katika bajeti na mambo mengine.

Pamoja na mambo mengine alibainisha kuwa serikali inaangalia uwezekano wa kuongeza fedha za kuendesha sekta ya elimu kwenye halmashauri.

“Serikali inaendelea kusisitiza bajeti za halmashauri (Elimu) kutoingiliwa na mamlaka zozote zinazoagiza kugharamia hudumza zisizo katika bajeti za halmashauri, wakurugenzi wa halmashauri zote nchini wameagizwa kuhakikisha wanazingatia stahili za watumishi wao katika mipango na bajeti za halmashauri zote na kufanya ukaguzi wa kila robo mwaka wa matumizi ya fedha za walimu fungu 507 ili kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa,” alisema naibu waziri.

Alitoa wito kwa walimu wote kwamba pamoja na kuidai serikali lakini pia wanatakiwa kuwa wakweli hasa pale wanapowasilisha madai yao.
 
Back
Top Bottom