Sahani ya ubwabwa wa Manji ina shombo

Mzito Kabwela

JF-Expert Member
Nov 28, 2009
18,857
7,617
NILIPOSIKIA kuwa rafiki yangu Yusuf Manji amejitosa kuwa mfadhili wa klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam na amemwaga mamilioni ya fedha kwa ajili ya usajili wa wachezaji na mambo mengi lukuki kusaidia klabu hiyo, nilicheka sana kimoyomoyo kwa sababu nilijua kuwa sasa ngoma imepata mpigaji.

Namjua Manji, nilijua ataipiga ngoma hiyo hadi ipasuke!

Nilisita kucheka hadharani kwa hofu ya kutolewa ngeu na manazi wa Yanga, ambao sikuwa na mashaka hata kidogo kuwa habari hiyo ya Manji kujitosa kuifadhili klabu yao ilikuwa sawa na kuhakikishiwa maisha bora kwa klabu yao katika uhai wote wa ufadhili wake. Hivyo kitendo cha mimi kucheka iwe kwa mazuri au mabaya hadharani, lazima pia kingepata majibu mazuri au mabaya, ikiwa ni pamoja na kutolewa ngeu.

Niliwaacha Wanayanga waendelee na furaha yao ya kupata mfadhili mwenye utajiri uliopitiliza, niliwaacha wafurahie kupata mtu wa kuwasaidia kutimizia shida za klabu yao, ilhali wana uwezo wa kuzitimiza wenyewe.

Niliwaacha ili nipate muda wa kucheka vizuri kutokana na hatua hiyo nzuri, lakini yenye gharama zake ya rafiki yangu Manji. Niliwaacha kwa sababu sikuwa na shida nao! Nilijua nitazungumza na mfadhili wao, iwe kupitia simu zetu za viganjani au ana kwa ana, kwa sababu sisi ni marafiki.

Na nitangulie kuonya mapema kuwa ninaposema Manji ni rafiki yangu, ninamaanisha hivyo, wala asitokee mtu wa kufikiri vinginevyo.

Mimi na Manji ni marafiki kweli, kwani wakati mwingine huwa ‘tunagonga glasi’ pamoja huku tukibadilishana mawazo, ingawa katika siku za karibuni tumepotezana. Na hii ni kwa sababu ya majukumu mazito tuliyonayo.

Nilipokutana na Manji tulizungumza mengi, yeye aliniambia ya kwake na mimi nilimwambia ya kwangu, yalikuwa mazungumzo mchanganyiko, tulizungumza ya uongo na ya kweli.

Bahati mbaya ni kwamba, hili la yeye kujitosa kuifadhili Yanga tuliligusia kidogo sana kwa yeye kunipa mikakati yake ya kumwaga mabilioni ya shilingi katika klabu hiyo ya mtaa wa Jangwani na Twiga.

Kwa tambo ambazo mimi hupenda kuziita za kijivuni, aliniambia anatarajia kutumia sehemu kidogo ya ukwasi wa kutisha alionao, kuifanya klabu hiyo kuwa moja ya klabu bora na maarufu barani Afrika na baadaye duniani. Aliponiambia hivyo, nilicheka sana hadi akanishangaa.

Nakumbuka aliniuliza kwa nini ninacheka sana, nikacheka tena, na yeye akacheka. Nikajua nimemuacha. Anacheka kwa sababu hajui kwa nini ninacheka! naye nikamfanyia kama Wanayanga. Nikamuacha.

Tangu wakati huo hadi sasa, nimekuwa nikicheka kila ninaposikia hadithi za Manji na mamilioni yake jinsi anavyojitoa kwa moyo wa upendo, lakini wenye kutiliwa shaka kuisaidia klabu ya Yanga. Sikuwa na mpango wa kusitisha kicheko changu, kwa sababu nilikuwa bado naburudika na midundo hiyo ya Manji ya Yanga, lakini leo nimeamua kununa, sitacheka tena katika hili kwa faida ya Wanayanga na Manji mwenyewe.

Ninaamini wengi hawajui kwa nini nimekuwa nikicheka katika kipindi chote hicho bila kueleza sababu.

Nilifanya hivi ili kutoa nafasi kwa Wanayanga kumpa Manji anachokitaka na yeye kuwapatia wanachokitaka. Hilo linaelekea kutimia, sasa naeleza kwa nini nilikuwa nacheka.

Mosi; nilicheka sana niliposikia Manji amejitosa kuifadhili Yanga na Wanayanga wamempokea kwa nderemo na vifijo, kwa sababu niliamini ufadhili wake haukuwa wa bure kama ilivyokuwa ikielezwa na baadhi ya watu. Niliamini kuwa Manji ameamua kujiingiza Yanga kwa sababu alilenga kupata kitu, tena kitu kikubwa.

Nilihisi kuwa Manji lazima anatarajia kupata manufaa zaidi kuliko mamilioni anayotumia kwa Yanga. Nasisitiza tena ni rafiki yangu, tunajuana.

Sikuwa na punje ya mashaka kuwa Manji ameamua kutumia mamilioni yake kujitumbukiza Yanga ili awe na sauti ndani ya klabu hiyo, ili Wanayanga wafuate matakwa yake, ili dunia imtambue kuwa naye yupo na bila shaka awe na kundi kubwa la wafuasi wanaomtegemea, ambalo atalitumia kutimiza matakwa yake.

Kucheka huku pia kulikuwa kwa mshangao kwa Wanayanga, ambao binafsi ninaamini kuwa baadhi yao hadi sasa hawajui kuwa rafiki yangu huyu ni mfanyabishara kama walivyo wengine, hivyo si jambo rahisi kumwaga sehemu ya utajiri wake pasipo kutarajia kupata chochote, iwe fedha nyingi zaidi ya alizomwaga, sifa na hata wafuasi wa kumlamba miguu.

Sina shaka hata kidogo kuwa Manji alijiingiza Yanga kibiashara zaidi. Anachotaka Yanga ni kuitumia kuzalisha mabilioni, ndiyo maana anamwanga mamilioni kwa sasa.

Na ili afanikiwe, anawapa Yanga wanachotaka kwa sasa, ili na wao waje wampe anachokitaka wakati muafaka utakapofika.

Historia ya Manji katika sehemu nyingi alizotia mguu wake kwa mbwembwe za kutoa misaada inaonyesha hivyo, kuwa hutumia ndoano ya misaada ili kuwanasa malimbukeni ‘hohehahe’ ambao akishawalevya kwa mamilioni yake, huwatumia kupata anachokitaka.

Kwa wasiolijua hili kuhusu Manji, waniulize, nitawaambia. Huyu ndiye rafiki yangu Yusuf Manji, bilionea kijana ambaye mapenzi yetu ni ya msimu.

Pili; nilicheka sana kusikia Manji anamwaga mamilioni kwa Wanayanga wakiwemo wachezaji ili wale washibe, wawe na miili yenye misuli ya kutosha kupambana na wachezaji walioshiba tangu wakiwa wadogo wanaocheza kandanda lenye akili huko ‘duniani’, wakati baadhi ya watumishi wake tunahemea nao vibaba vya unga Uswahilini. Sikuamini masikio yangu, ilikuwa habari ya kufurahisha sana. Kwamba, baba anapeleka chakula kwa jirani wakati wanae wana njaa!

Ilikuwa ni habari mpya na ya kufurahisha kwa rafiki yangu kwenda kutoa mamilioni kwa ajili ya kukarabati jengo la klabu ya Yanga, kwa kuliwekea hadi viyoyozi wakati baadhi ya wanaomzunguka, wakimsaidia kukusanya mabilioni anayoingiza na sehemu yake kuyamwaga kwa Wanayanga, wakiishi Uswahilini kwenye vibanda vilivyochoka mno. Vinavyoudhi kuvitazama kwa macho.

Nilicheka kwa sababu nilijua, Wanayanga hawajui kuwa Manji anakarabati jengo lile na kuwaonjesha utamu wa utajiri wake, ili wampe anachokitaka. Nacho ni ubwana dhidi yao. Hivyo ndivyo ilivyo, kwani katika klabu ya Wanajangwani, sasa kuna bango limeandikwa ‘Jeshi la Manji’. Kwa tafasiri yangu kwa bango hilo, wachezaji na wanachama wa Yanga sasa ni Jeshi Manji.

Sote tunajua jinsi Yanga ilivyo na mashabiki wengi, hivyo Wanayanga wote wakiwa jeshi la mtu mmoja, huyo anaweza kuwa na jeshi kubwa kuliko majeshi yetu ya Ulinzi na Usalama.

Kwa tafsiri nyingine iliyonijia kichwani ni kwamba Manji anataka kuogopwa kwa kuwa na jeshi kubwa, anataka kuwatisha maadui zake kwa kuwa na jeshi kubwa.

Nadhani amefanikiwa, kwa sababu Wanayanga sasa wanamtimizia anachotaka kwa gharama ya pilau na kulipiwa tiketi za kuingia Uwanja wa Taifa kuiona Brazil. Ana akili sana rafiki yangu huyu.

Na simlaumu kwa hili, analistahili, kwa sababu wenye klabu yao wamekubali kumpa anachotaka, baada ya yeye kuwapata wanachokitaka. Anastahili kuitwa bwana na Wanayanga kuwa watwana wake, wamekubali wenyewe kuwa wao ni jeshi lake.

Utukufu na ukuu ni wake dhidi ya Wanayanga. Akikohoa jeshi lake linatikisika. Niliyajua haya ndiyo maana nikawa nacheka sana.

Tatu; nilikuwa nawacheka viongozi wa Yanga waliokuwa wakishangilia ujio wa rafiki yangu huyo katika klabu yao, kwa sababu nilijua badala ya kuwa viongozi watakuwa waongozwa. Nilijua baada ya Manji kuanza kuabudiwa na wanachama na wachezaji kutokana na misaada anayowapa, viongozi watake wasitake, nao watalazimika kumuabudu.

Nilijua hili litatokea, lakini litaleta mtafuruku kwa sababu ya imani niliyonayo kwa baadhi ya viongozi wa klabu hiyo, kuwa si wote watakaokubaliana na hatua ya kuwa watwana wa bilionea huyu. Akili zangu zilinilazimisha kuamini kuwa wapo wenye akili kuliko yeye, ambao wangetumia mwanya wa kuwa karibu naye kuchuma kisha wakaangalia mbele.

Na hiyo ndiyo sababu kuu ya kucheka sana siku alipokuwa akinipa mipango yake dhidi ya klabu hiyo kuwa anakusudia kutumia ukwasi wake kuinyanyua.

Nilijua lazima watamliza. Watatumia fedha zake kujineemesha huku wakikwamisha mipango yake. Nilijua ipo siku atajutia nafsi yake kwa kujiingiza katika klabu hiyo!

Anayebisha katika hili atizame mfano hai wa mkutano wa Jumapili Juni 6, uliohudhuriwa na maelfu ya Wanayanga ambao walionjeshwa ‘harua’ na Manji na wao wakalazimika kufanya alichokitaka.

Iman Madega, mmoja wa viongozi wa Yanga ambaye sina shaka anajua janja ya Manji na amekuwa akimuwekea kauzibe katika mipango yake mbalimbali, licha ya kufaidi mamilioni yake akiwa katika wadhifa wa mwenyekiti wa klabu, alijikuta akizomewa na wenzake huku Manji ambaye hajawahi kunidokeza kama alishacheza hata mpira wa makaratasi, akishangiliwa. Madega ilikuwa lazima azomewe na sababu nimeishaieleza kuwa Yanga wanapaswa kumpa Manji anachokitaka kama yeye anavyowapa wanachokitaka.

Sababu nyingine iliyokuwa ikinichekesha ni ugomvi. Nilijua fedha za Manji badala ya kuleta amani ya kudumu katika klabu na kuisaidia kusonga mbele kimaendeleo, zitawagombanisha na kuifanya klabu hiyo irudi nyuma kwa kiwango kikubwa kimaendeleo ya soka.

Niliamini kabisa kuwa wakati utafika ambapo bilionea huyu atakapokuwa akitaka kutekelezwa kwa matakwa yake, lakini yatakuwa yakipingwa na baadhi ya Wanajangwani. Vita itaibuka baina ya wanaomuunga mkono na wasiomuunga mkono.
Charles Mullinda



Kwa sababu ya historia ya mashabiki wengi wa soka nchini ni tegemezi, huishi kwa kutegemea wafadhili wa klabu au mapato ya klabu yenyewe, ambao wako radhi kumwaga damu ili wapewe ubwabwa bila kujali kama wanaiua klabu yao kwa sinia la ubwabwa na nyama. Watapambana hadi tone la mwisho la jasho lao na yeyote atakayekuwa akimpinga bilionea huyu kijana. Na katika mapambano hayo, nina hakika watwana wa Manji watashinda na yeye atapata anachokihitaji.

Vita hii sasa inakaribia, kwani iwapo Manji ataendelea na kinachodaiwa kuwa mpango wake wa kuitaka nembo ‘logo’ ya klabu hiyo, ambayo sina shaka hata kidogo kuwa anaitaka kwa malengo yake binafsi, wanaopinga mpango huo, mbali na Madega, watatoana ngeu na wanaomuunga mkono.

Na Manji akishapata anachokitafuta Yanga, nina hakika ataitosa kwa staili yake ile ile ambayo amekuwa akifanya katika baadhi ya maeneo ambayo amekwishatia mguu wake. Kwa wanaodhani natania katika hili, hawa nawaambia wasubiri tu, wataona.
 
Hakuna Jipya. Haya yalitokea kwa Simba/Dewji ana Yanga/Gulamali ambaye alitaka hata picha yake iwekwe kwenye kadi za Uanachama za Yanga! Lililo kubwa na kusikitisha ni kwamba Watanzania hatujivunzi ama ni Wavivu sana wa kujivunza kuwa Hakuna Cha Bure Duniani. Njaa Yetu Inatuua wenyewe!
 
.............paragraph zote hizo 42 zingeweza kuwa condensed into 6 or 7 maana ni blaah blaah tupu!!! Kama kuna point basi imejificha sana!!!! Anayoyafanya manji kwa yanga ndio tunayoyafanya watanzania (kupitia serikali mufilisi ya c.cm) kwa wazungu so hamna jipya hapa!!! Kama manji amekunyima ulaji somewhere sometime,haituhusu!!!!
 
Back
Top Bottom