Sababu sugu zinazopelekea uchumba kuvunjika

Peter Mwaihola

JF-Expert Member
Jun 23, 2022
227
333
Si mara moja au mbili umewahi kusikia wachumba wametengana hivyo kukatisha ndoto yao ya kuwa wanandoa. Uchumba kuvunjika ni moja ya masuala yanayozungumzwa na kuikumba jamii kila kukicha ingawaje watu huchukulia kama ni kawaida na ni maamuzi ya wahusika.

Wakati mwingine watu hupatwa na mshtuko na kuumizwa pindi wanaposikia watu fulani wameachana au kugombana.

Maumivu yanayowapata wale wanao sikia huwa ni maumivu ya matamanio yao kutaka kuona uchumba wa wahusika unazaa ndoa mwisho familia iliyo imara mpaka kifo.
Kuna mwaka magazeti ya burudani yaliuza sana kwa kuandika udaku juu ya kuvunjika kwa uchumba Kati ya msanii chipukizi wa Marekani wakati huo Justin Biber na msanii mwenzake Selena Gomez.

Sio kwamba watu Walikua wanapenda udaku hapana bali wengi walipenda uhusiano wa wahusika hivyo walikuwa wanatamani kuona wanaoana rasmi.

Tuachane na huko ughaibuni tuje hapa kwetu ardhi ya Bongo unakumbuka nini kuhusu Alikiba na Jakate mwogelo, na una maoni gani juu ya kilichotokea kwa juma Jux na Vanessa Mdee?

Hiyo ni mifano kiduchu niliyokupa ili tutafakari kwa pamoja nini hupelekea uchumba kuvunjika.

Niliwahi kuzungumza na kijana ambae alinieleza masikitiko yake juu ya mchumba wake wa zamani ambaye ameolewa mtaa wa pili lakini angali bado anampigia simu akimuomba waendelee kuwasiliana kwakuwa bado anampenda akidai kuwa hakupenda kumuacha ni maisha tu.

Sababu ya kwanza inayotoka kwa kijana aliyekumbwa na mkasa huu anasema ni hali ya kiuchumi kwakua yeye hakua tayari kuoa kwa wakati ule aliomba ajipange ili baadae mambo yakikaa sawa apate kumuoa binti huyo.

Anadai kuwa baada ya miaka mitatu ya uchumba alisikia fununu kuwa mchumba wake yupo mbioni kuolewa na mwanaume wa mtaa wa pili lakini akapuuzia na akaja kuamini pale aliposikia kuwa ameolewa na hapatikani kwenye simu.

Sababu hii inagusa pia upande wa pili wa jinsia ya kike pale mwanamke anapokosa mahitaji fulani binafsi ndani ya familia yake hivyo anaona kimbilio ni kuolewa na akiona mchumba alienae hana muelekeo wa kuoa hivi karibuni basi huamua kuolewa na mwingine ambae yupo tayari kuoa hata kama hakumpenda kwa dhati wala kuwa na malengo naye.

Kadhalikia hali ya uchumi wa familia za wahusika huweza kuchangia kuvunjika kwa uchumba, kwa mfano kuna wanawake hawapendi kuolewa na wanaume masikini na kuna wanaume hawataki hata kusikia kuoa mwanamke anae tokea familia ya watu masikini. Pia sababu hii ya hali ya kiuchumi huhusisha tamaa ya fedha na ufahari.

Utengano wa kijiografia na kukosa mawasiliano, ikitokea wahusika wametengana kijiografia na mawasiliano kati yao yakawa hafifu basi kuna hatari kujisahau na kuanza kuishi maisha ya upekee pasipo kufikiriana wala kuona haja ya kutafutana hata kwa simu mwisho uchumba huvunjika.

Kigezo cha umri, muda mwingine uchumba huvunjika kutokana na kuwepo kwa msukumo wa kufikiria kusonga kwa umri hasa kwa jinsia ya kike ambapo wanawake wengi hufikiri kuwa kadri umri unavyoenda thamani yao hupotea hivyo huwashinikiza wachumba wao kuwaoa haraka na wakishindwa huwaacha na kuolewa na wanaume wengine walio tayari kuoa kwa wakati huo.

Shinikizo la wazazi, kumekuwa na tabia baadhi ya wazazi kuwashinikiza watoto wao kuoa au kuolewa na Watu fulani kwa sababu mbalimbali za kijamii hali hii huwaweka njia panda watoto hao hivyo huamua kuachana na wachumba wao wa awali na kufuata matakwa ya wazazi wao.

Kutofautiana kwa mitazamo ya kimaisha, hii ni sababu mojawapo ambayo hupelekea uchumba kuvunjika pale ambapo wahusika hutofautiana juu ya masuala mbalimbali ya maisha yao ya baadae ikiwemo wapi wataishi, namna gani watajenga familia yao na kuendesha maisha yao.

Ikitokea mmoja akawa hapendi kabisa mtazamo wa mwenzie akajaribu kunishawishi abadili ikashindikana basi uchumba huo upo hatarini kuvunjika.

Msukumo wa nje, muda mwingine watu hukatisha uchumba kwa kusikiliza maneno ya marafiki hasa yale ya umbea na utani wa vijiweni hivyo hukosa imani na wachumba wao huanza kuwaona watu wasiofaa na kuvutia tena kwa ajili ya ndoa.

Udini, ukabila na ubaguzi mwingine ni miongoni mwa sababu zinazotajwa kuwa sugu katika kupelekea uchumba kuvunjika kwani huwa inatokea mtu hataki kuolewa au kuoa kabila fulani kwahiyo akigundua mchumba wake ni wa hilo kabila basi humuacha.

Tabia binafsi za wahusika mfano ukorofi ulevi na zinginezo pia huchangia kuvunjika kwa uchumba katika jamii.

Suala la uchumba ni suala linalo husisha mambo mengi mtambuka hivyo linatajwa kuwa hatua ngumu kuivuka kuliko hata ndoa yenyewe hivyo wahusika wanatakiwa kuelewa mazingira yanayowazunguka na kuwa imara wakati wote ili kufikia malengo yao.

Peter Mwaihola kitaaluma ni mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii.
 
Back
Top Bottom