Ripoti UNDP: Tanzania imepanda viwango Maendeleo ya Binadamu

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,390
8,155
Tanzania imepanda katika viwango vya kimataifa vya maendeleo ya binadamu, imeeleza ripoti mpya ya Maendeleo ya Watu 2021/2022.

Imepanda kutoka nafasi ya 163 (alama 0.529) mwaka 2020 hadi 160 (alama 0.549) mwaka jana kati ya mataifa 191 huku ikiwa juu ya majirani zake sita wa ukanda wa Afrika Mashariki.

Ripoti hiyo inayotolewa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), imetumia vipimo vyenye maeneo yanayotofautisha ukuaji wa maendeleo ya watu katika ubora na idadi ya huduma za lishe, ubora wa elimu, maji safi, umeme, makazi, kinga ya vifo vya watoto, nishati ya kupikia na umiliki wa mali.

Hata hivyo, pamoja na kupanda kwa nafasi tatu, takwimu zinaonyesha bado Tanzania ipo kundi la mataifa 32 yenye kiwango cha chini cha maendeleo ya watu.

Katika kundi hilo, ipo juu ya majirani zake Uganda, Burundi, Msumbiji, Rwanda,Malawi na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu ripoti hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba alisema, “tulitakiwa kuwa juu ya nafasi hiyo kutokana na miradi mingi iliyofanyika kwa kuzingatia ubora na idadi kuanzia huduma za afya, elimu, sera zetu za kijamaa zinachechemua zaidi maendeleo ya wananchi kuliko mataifa ya sera za kibepari.”

Tutuba alisema ombaomba Tanzania anapata umiliki wa ardhi, mtoto anapata elimu bure na mkopo wa elimu ya juu, anapata huduma za afya bure na maskini anapata maji bure kupitia vikundi vya watumiaji maji.

“Sisi tuna taarifa zetu za kujipima, hatuna tafiti mbadala na siwezi kujua kasi ya mataifa hayo mengine,” alisema Tutuba.

Akizungumzia hilo, Profesa Humphrey Moshi kutoka Idara ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alitaja maeneo mawili yanayohitaji uboreshaji wa huduma ikiwamo kuimarisha ubora wa huduma.

“Tumekuwa na majengo ya shule, majengo ya vituo vya afya lakini hakuna vifaa kwa hiyo tuimarishe ubora.”

Pili, alisema kasi ya ukuaji wa uchumi ni ndogo kuliko kasi ya ongezeko la watu, hatua inayoathiri kasi ya maendeleo ya watu kutokana na ongezeko la mzigo mkubwa wa huduma.

“Wakati ukuaji uchumi wa China ukiwa asilimia 9.5, ongezeko la idadi ya watu wake kila mwaka ilikuwa kwa wastani wa asilimia 1.6 lakini sisi(Tanzania) ukuaji wa uchumi kwa sasa uko wastani wa 5.4 wakati ongezeko la watu ni wastani wa asilimia 3.2 kwa mwaka. Tofauti hii lazima tuwe chini katika ripoti (HDI).”

Profesa Moshi alisema kasi ya kushuka kiwango cha umaskini wa watu inakuwa ndogo hivyo uchumi unatakiwa kukua kwa angalau asilimia nane katika uwiano wa ukuaji wa watu kwa asilimia 3.2 nchini.

“Tuwekeze katika kilimo cha kisasa ili tukuze vipato vya wananchi wetu, kipato kikiongezeka, watakuwa na uwezo wa kujihudumia mahitaji ya msingi, pia Serikali iimarishe huduma za afya, elimu, umeme, majisafi kwa ubora unaohitajika.”

Ripoti hiyo iliyozinduliwa Septemba mwaka huu, inaonyesha mataifa 66 yako kiwango cha juu sana, 49 kiwango cha juu, 44 kiwango cha kati na 32 kiwango cha chini ikiwamo Tanzania.

Kati ya mwaka 1990/2021, mwenendo wa ukuaji wa maendeleo ya watu nchini umekuwa wastani wa asilimia 1.27, ikionyesha mabadiliko na mwaka 1990/2000 yalikuwa kwa asilimia 0.7, yakapanda kwa asilimia 2.16 mwaka 2000/2010 kabla ya kuporomoka tena kwa asilimia 0.98 mwaka 2010.2021.

Uwekezaji wa Serikali

Katika sekta ya elimu, Serikali ilianza kugusa kundi la watoto milioni 12 mwaka huu baada ya kuanza utekelezaji wa mradi wa Kuimarisha Ujifunzaji katika Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) utakaojenga madarasa 12,000 na shule salama 6,000 nchi nzima chini ya fungu la Sh1.15trilioni.

Kwa mujibu wa Tamisemi, utekelezaji wa mradi huo utakaoanza na Shule 1,000 ni wa miaka mitano na utaboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji, ujuzi na ubora wa walimu katika ufundishaji.

“Tumekuwa na mlundikano wa watoto. Mradi utaongeza watoto shuleni, kuongeza idadi ya wanaofaulu na itaongeza mwamko, tutakuwa na ushirikiano mkubwa na jamii,” anasema Ofisa elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Abdul Maulid mwenye shule 753 za mkoa huo.

Mbali na miradi hiyo, tayari kuna maelfu ya Watanzania wameanza kunufaika na huduma katika vituo vya afya nchini chini ya fungu la zaidi ya Sh100bilioni zilizotolewa mwaka 2021/22 kwa ajili ya kuendeleza mradi wa ujenzi wa vituo 304 vya afya.

Kati ya hivyo, vituo 52 vilianza kujengwa mwaka 2019/20, vituo 252 vilianza kujengwa 2021/22 na vituo 18 vimejengwa kwenye halmashauri zenye mapato madogo na vituo 234 vimejengwa katika tarafa zisizo kuwa na vituo vya afya na kata za kimkakati kupitia tozo za miamala ya simu.

Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania, Feddy Mwanga alipongeza juhudi hizo akisema zitasaidia kusogeza huduma kwa wananchi wengi hususani wajawazito wanaokabiliana na changamoto za kujifungua. Alisema idadi ya wajawazito kujifungua nyumbani imepungua hadi asilimia 40.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom