Republic Vs. Acp. Abdallah Zombe & 12 Others, Criminal Case No. 26 of 2006

Apr 26, 2022
64
100
Hello, leo nakuletea summary ya kesi maarufu ya mauaji, ambayo iliwahi kuitikisa Tanzania enzi hizo (2006). Ni kesi ya ‘Abdallah Zombe na wenzake 12.’

Hii ni summary (muhtasari au dondoo) kwa sababu kesi halisi ni ndefu sana, mathalani ya kwanza iliyosikilizwa Mahakama Kuu ina kurasa 230, wakati iliyotolewa kwenye rufaa na Mahakama ya Rufani ina kurasa 56. Hapa nimeandika vitu vya msingi tu, kama vile simulizi ya kilichotokea na uamuzi wa Mahakama, mambo mengine kama vile ushahidi uliotolewa na kila shahidi alisema nini nimeruka, ikiwa utataka kujua yote hayo ni vizuri kusoma kesi nzima.

Imeandaliwa na kuletwa kwako nami Zakaria Maseke - Advocate Candidate (0754575246 - WhatsApp).
zakariamaseke@gmail.com

Haaya ni baadhi ya mambo utakayojifunza kwenye hii Kesi.

1: Je, mtu kuwepo tu eneo la tukio bila kufanya kitu kingine zaidi, kunaweza kukufanya uwe miongoni mwa wakosaji?

2: Je, ukimshauri au kumuwezesha au kumsaidia mtu mwingine kutenda kosa, na akatenda, je na wewe utakua umetenda kosa?

3: Je, kama yule mtendaji kosa halisi uliyemshauri au kumuwezesha au kumsaidia kutenda kosa HAYUPO (hajashtakiwa), je wewe unaweza kutiwa hatiani peke yako?

4: Mwisho nitakupitisha kwa ufupi, position (sheria) ikoje kwa sasa kuhusu hayo maswali (kwa sababu hii kesi ni ya zamani kidogo - mwaka 2016 na leo ni 2022).

UTANGULIZI (INTRODUCTION):

Hii ni kesi ya mauaji ya watu wanne (wafanya bishara wa madini watatu na dereva tax mmoja), ambao waliuawa kikatili tarehe 14/1/2006 Dar es Salaam, kwa kile kilichodaiwa mwanzo na Polisi kwamba, walikuwa ni majambazi waliopora lori la biashara na kisha kujibizana kwa risasi na Polisi maeneo ya Sinza, walipojaribu kukamatwa.

Watu waliouawa ni:
1: Ephraim Sabinus Chigumbi
2: Sabinus Chigumbi Jongo
3: Juma Ndugu (dereva tax) na
4: Mathias Lunkombe

Hawa walikuwa ni wafanyabiashara wa madini, Mahenge, mkoa wa Morogoro.

Kufuatia mauaji hayo ya kikatili (brutal killings), Mheshimiwa Rais wa wakati huo akaunda Tume ya uchunguzi kuchunguza mauaji hayo. Katika kuchunguza, tume ilijikita kwenye vitu vifuatavyo:

(i) Kuchunguza chanzo na mazingira yaliyopelekea vifo vya watu wanne Sinza.

(ii) Kuchunguza kama kweli hao wafanya biashara (marehemu) wanne walihusika kwenye tukio la unyang’anyi (eneo la Sinza).

(iii) Kuchunguza na kutambua majina, makazi na shughuli za marehemu hao.

(iv) Kuchunguza busara au kiasi cha nguvu waliyotumia polisi, na

(v) Kumshauri Mheshimiwa Rais kuhusu tukio zima.

Tume ikatembelea maeneo mbali mbali, ikahoji mashahidi mbalimbali, wakiwemo polisi waliohusika pamoja na raia.

Ushahidi ukarekodiwa wakakusanya na vielelezo kadhaa.

-Tume ikapendekeza kesi ifunguliwe na kutokana na mapendekezo ya tume, kesi ilifunguliwa Mahakamani (Mahakama Kuu, Dar es Salaam).

- Maafisa 13 wa Polisi walishtakiwa kwa makosa ya kufanya mauaji kinyume cha kifungu cha 196 cha Sheria ya Kanuni ya adhabu (Penal Code).

- Maafisa hao ni wafuatao;

1: ACP Abdallah Zombe
2: SP Chiristopher Bageni,
3: ASP Ahmed Makele
4: PC Noel Leonard
5: WP 4593 Jane Andrew
6: CPL Nyangelera Moris
7: CPL Emmanuel Mabula
8: CPL Felix Sandy Cedrick
9: PC Michael Shonza
10: CPL Abeneth Saro
11: DC Rashid Lema
12: CPL Rajabu Bakari and
13: CPL Festus Gwabisabi.

Tuanze sasa kesi.

FACTS (STORI NZIMA IKO HIVI):

Tarehe 7-1-2006, Ephraim Chigumbi, Sabinusi Chigumbi na Protace Lunkombe walianza safari kutoka Mahenge kwenda Arusha kuuza madini.

Baada ya kuuza baadhi ya madini wakakaa Arusha mpaka 12-1-2006 wakaamua kurudi Dar es Salaam kutafuta wanunuaji wengine wa madini.

Baada ya kuuza baadhi ya madini Dar es Salaam, wakaenda Gereji ya Ilala kutengeneza gari lao. Gari halikutengamaa siku hiyo hiyo, wakaamua kukodi tax, wakaenda mpaka Sinza C.

Wakiwa wanajiandaa kuondoka Sinza, ikaja gari aina ya Toyota ikiwa na Polisi watano, wawili wako na silaha. Sabinus na wenzake wakakamatwa na Polisi, wakafungwa pingu.

Pia Polisi wakakamata begi lao lililokuwa na hela Tsh Million 5. Wakakamata na Pistol ya Sabinus ambayo alikuwa anaimiliki kihalali.

Mashahidi waliokuwepo wanasema hawakujua marehemu walipelekwa wapi baada ya kukamatwa.

Majira hayo hayo kulitokea pia unyang'anyi barabara ya Sam Nujoma. Kwa hiyo Polisi walikuwa wanafatilia wahusika wa tukio la unyang'anyi. Hivyo marehemu wakawa ndio washukiwa (suspects) wa kwanza.

Taarifa za kukamatwa kwao zikazagaa kwa marafiki na ndugu zao ambao walijitahidi kuwatafuta walipo bila mafanikio.

Baadaye, washukiwa wote wanne wakakutwa Hospitali ya Muhimbili wakiwa wamefariki.

KESI MAHAKAMA KUU:

-Jamhuri ilileta mashahidi 37.
-Washtakiwa wote walikana mashtaka, hivyo kesi ikaendelea kusikilizwa.

Mashahidi walisema waliona majeraha ya risasi kwa marehemu wote wanne nyuma ya shingo na alama kwenye miili yao. Ushahidi ambao baadae ulithibitishwa na report ya Daktari.

Daktari akasema kwamba chanzo cha mauaji hayo kilikuwa ni majeraha yanayotokana na kupigwa risasi.

Kwa mujibu wa polisi, walisema kwamba vifo vya washukiwa hao vilitokana na majibizano ya risasi kati yao na Polisi katika uzio (ukuta) wa shirika la Posta Sinza, wakati washukiwa wanajaribu kutoroka.

- Baada ya kesi kusikilizwa na kufungwa kwa upande wa mashtaka (Prosecution / Jamhuri), Mahakama Kuu ikaona kwamba washtakiwa watatu: PC Noel Leonard, CPL Nyangelera Moris na CPL Felix Sandy Cedrick, hawakuwa na kesi ya kujibu hivyo wakaachiwa huru.

- Wakabaki watuhumiwa 10.
-Kesi ikaendelea kusikilizwa upande wa washtakiwa (defense).
-Lakini wakati kesi inaendelea, mshtakiwa mmoja DC Rashid Mohamed Lema akafa.
- Hivyo wakabaki watuhumiwa 9 mpaka mwisho wa kesi.

Baada ya kuchambua ushahidi, Mahakama Kuu ikagundua kwamba, hakuna risasi zilizofyatuliwa kwenye ukuta wa shirika la Posta Sinza, wala hapakuwepo na majibizano ya risasi kati ya Polisi na Majambazi Sinza.

-Kwa hiyo hakuna mauaji yaliyotokea hapo (so the victims were and could not have been killed there).

-Kwamba tukio la unyang'anyi lilikuwa ni kweli, lakini marehemu hawakuhusika kwenye unyang'anyi huo.

-Mahakama Kuu ikaridhika kwamba hao wafanya biashara wanne waliuawa kikatili na chanzo cha kifo chao ilikuwa ni kupigwa risasi.

-Pia Mahakama Kuu ikajiridhisha pasipo na shaka (beyond reasonable doubt) kwamba wahanga waliuliwa msitu wa Pande na sio Sinza.

-Swali la msingi sasa, lilikuwa ni je, ni hawa washtakiwa ndio waliowaua?

-Baada ya kuchambua ushahidi uliopo, Mahakama Kuu ikasema hapana! Sio hawa washtakiwa walioua. Hakuna ushahidi wa moja kwa moja au wa kimazingira (circumstantial) unaoonesha kwamba kuna yeyote kati yao aliua.

Ushahidi unaokaribia sana, ni ambao ulikuwa unaonesha kwamba baadhi ya watuhumiwa, mfano mshtakiwa wa pili na wa tatu walikuwepo eneo la tukio na walishuhudia mauaji, lakini wao binafsi hawakuua.

Jaji akasema watuhumiwa hao wangeweza kutiwa hatiani kwa kusaidia na kuwezesha uhalifu, lakini kama wauaji halisi hawapo Mahakamani, kesi dhidi yao haiwezi kusimama, wanabaki tu kutiliwa mashaka makubwa, ambayo peke yake haitoshi kutia mtu hatiani.

Mathalani, kuhusu Mshtakiwa wa 2 (SP Christopher Bageni) ambaye Mahakama Kuu ilithibitisha kwamba alikuwepo kabisa eneo la tukio msitu wa Pande, na angeweza kuzuia uhalifu kufanyika lakini hakufanya hivyo, bado Mahakama Kuu ilimwachia huru, kwa sababu hapakuwa na ushahidi wowote unaoonyesha kwamba alishawishi, aliamuru au kusaidia mhalifu yeyote kufanya mauaji.

Mahakama Kuu ikasema, ushahidi uliopo inasemekana aliyefanya mauaji ni Cpl. Saad. Na huyo Cpl Saad aliyewapiga risasi marehemu hakuwa miongoni kati ya wale walioshtakiwa kwenye kesi Mahakamani wala hajajitetea.

Mahakama Kuu ikasema kwamba, kwa kuwa Cpl Saad sio miongoni mwa watuhumiwa, kwa hiyo hoja ya kuwatia hatiani washtakiwa wengine kwa kosa la kushawishi au kusaidia kufanya uhalifu pia haiwezi kuzingatiwa wakati anayedaiwa kuwa muuaji halisi hayupo.

Mwisho kabisa, Mahakama Kuu ikasema upande wa mashtaka (jamhuri) umeshindwa kuthibitisha kesi yao dhidi ya watuhumiwa pasipo na shaka yoyote (the prosecution has failed to prove their case against the accused persons beyond reasonable doubts).

MAHAKAMA KUU IKASEMA WATUHUMIWA WOTE HAWANA HATIA NA IKAWAACHIA HURU WATUHUMIWA WOTE TISA, HATA WALE WALIOKUWEPO ENEO LA TUKIO MUDA MAREHEMU WANAPIGWA RISASI.

-Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) hakuridhika, akakata rufaa Mahakama ya Rufaa.

-Mwaka 2013 kesi ikaenda Mahakama ya Rufaa.

MBELE YA MAHAKAMA YA RUFAA:

- Sasa wahusika (parties) ni DIRECTOR OF PUBLIC PROSECUTIONS (MWENDESHA MASHTAKA MKUU WA SERIKALI) Versus (dhidi ya) ACP ABDALLAH ZOMBE na wenzake nane (8), rufaa ya jinai, namba 358, 2013.

Hizi ni baadhi ya sababu alizotumia Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali kupinga maamuzi ya Mahakama Kuu:

1: Kwamba, Jaji wa Mahakama Kuu alijielekeza vibaya katika kutafsiri kanuni ya wanaoweza kuhusika kwenye kosa, dhidi ya mshtakiwa namba 1, 2, 3 na 8 (that, the learned trial judge misconceived the application of the principle of parties to the offence, hence he failed to apply it against the 1, 2, 3 and 8” respondents).

2. Kwamba Mheshimiwa Jaji alijielekeza vibaya kisheria kwa kuamua kwamba, kwa sababu mhalifu halisi aliyewafyatulia risasi marehemu hakushtakiwa, basi hawa walioshtakiwa hawawezi kutiwa hatiani kwa kosa la mfichaji wa muuwaji wa kukusudia (that the learned trial judge erred in law and fact in finding that since the actual shooter of the deceased was not charged with the respondents, they (respondents) could not be found guilty of accessory after the fact to murder).

Wakati kesi ya rufaa inaendelea, Jamhuri ikaomba kuwaondoa wafuatao:

1: Mshtakiwa wa nne PC Jane Andrew.
2: Mshtakiwa wa tano CPL Emmanuel Mabula.
3: Mshtakiwa wa 6 PC Michael Shonza.
4: Mshtakiwa wa 7 CPL Abineth Saro na
5 Mshtakiwa wa 9 CPL Festus Gwabisabi.

Wakabaki Washtakiwa wanne wafuatao:

1: Mshtakiwa wa 1 ACP Abdallah Zombe.
2: Mshtakiwa wa 2 SP Christopher Bageni
3: Mshtakiwa wa 3 ASP Ahmed Makele na
4: Mshtakiwa wa 8 CPL Hamis Bakari akachukua nafasi ya mshtakiwa wa 4.

Washtakiwa wote wanne wakiwa Mahakama ya Rufaa, wakakana tena kuhusika na mauaji ya hao wafanya biashara wanne.

Baada ya pande zote mbili (upande wa Jamhuri/Mashtaka na upande wa utetezi (washtakiwa) kuwasilisha hoja zao, Mahakama ya Rufaa ikaanza kuchambua ushahidi.

Mahakama ya Rufaa kwa kuzingatia ushahidi wa Daktari aliyefanya uchunguzi wa miili ya marehemu, ikajiridhisha kwamba hakuna shaka hawa wafanya biashara wanne walifariki kwa kupigwa risasi.

Kama ilivyokuwa kule Mahakama Kuu, pia Mahakama ya Rufaa ikaridhika kwamba, wahanga waliuawa kikatili (brutally killed). Na kwamba, yeyote aliyefanya mauaji hayo ALIDHAMIRIA kuwaua kabisa.

Lakini kwa kuwa Mahakama Kuu iliwaachia huru watuhumiwa wote, issue (swali la kujiuliza) ilikuwa ni je uamuzi wa Mahakama Kuu uko sahihi?

Mahakama ya Rufaa ikasema, Mheshimiwa Jaji wa Mahakama Kuu, alikosea kutafsiri kitungu cha 22 na 23 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Section 22 and 23 of the Penal Code).

Ambapo kifungu cha 22 kinaongelea wakosaji wakuu (principal offenders). Kifungu hicho kinasema hivi (nanukuu):

22(1) “Pale ambapo kosa limetendeka, kila mmoja wa watu wafuatao watachukuliwa kwamba ameshiriki katika kutendeka kwa kosa hilo na watakuwa na hatia, na wanaweza kushtakiwa kwa kutenda ambao ni (when an offence is committed, each of the following persons is deemed to have taken part in committing the offence and to be guilty of the offence, and may be charged with actually committing namely);”

(a) “kila mtu ambaye anafanya kitendo au ambaye anaacha kufanya kitendo ambacho kinasababisha kosa (every person who actually does the act or makes the omission which constitutes the offence)”

(b) “kila mtu ambaye anafanya kitendo au anaacha kufanya kitendo kwa dhumuni la kumuwezesha au kumsaidia mtu mwingine kutenda kosa hilo (every person who does or omits to do any act for the purpose of enabling or aiding another person to commit the offence)”

(c) “Kila mtu ambaye anamsaidia au anamshawishi mtu mwingine katika kutenda kosa (every person who aids or abets another person in committing the offence)”

(d) “Mtu yeyote ambaye anamshauri au anamchukua mtu mwingine yeyote kutenda kosa, katika mazingira yoyote anaweza kushtakiwa labda kwa kutenda kosa au kwa kushauri au kusaidia kutendeka kwa kosa (any person who counsels or procures any other person to commit the offence, in which case he may be charged either with committing the offence or with counseling or procuring its commission).”

(2) “Kupatikana na hatia ya kushauri au kusaidia kutendeka kwa kosa, kunafanya matokeo yale yale katika hali zote kama kupatikana na hatia ya kutenda kosa. (A conviction of counseling or procuring the commission of an offence entails the same consequences in all respects as a conviction of committing the offence).”

(3) “Mtu yeyote ambaye anasababisha mtu mwingine kutenda au kutotenda kitendo chochote cha namna ambayo, kama atakuwa amefanya kitendo yeye mwenyewe au kutofanya kitendo hicho kitapelekea kosa kwa upande wake, atakuwa na hatia ya kosa la namna hiyo hiyo na atapewa adhabu ile ile kana kwamba yeye mwenyewe ndiye ametenda kitendo hicho au ameacha kutenda

(A person who procures another to do or omit to do any act of such a nature that, if he had himself done the act or made the omission the act or omission would have constituted an offence on his part, is guilty of an offence of the same kind and is liable to the same punishment as if he had himself done the act or the omission).”

Mahakama ya Rufaa ikasema, hicho kifungu cha 22 kinafafanua ni akina nani ni wakosaji wakuu kwenye kosa. Lakini hakisemi kwamba mashtaka dhidi ya mshawishi hayataendelea hadi mtenda kosa halisi ashtakiwe kwanza.

Kwa sababu hao walioorodheshwa kwenye kifungu cha 22 ni wakosaji wakuu, haijalishi ni washawishi au watenda kosa halisi.

Hawashtakiwi moja kwa moja kama washawishi, ila mchango wao katika kutenda kosa hubainika wakati wa kutoa ushahidi. Hivyo ndo kifungu cha 22 kinavyosema. (Ilisema Mahakama ya Rufaa).

Sasa MAHAKAMA YA RUFAA ikaanza kumchambua mshtakiwa namba mbili (SP Christopher Bageni) ambaye MAHAKAMA KUU ilikataa kumtia hatiani kwa kosa la kushawishi au kusaidia kufanya uhalifu, kwa sababu tu anayedaiwa kuwa muuaji halisi (Cpl Saad) hakuwepo Mahakamani.

Mahakama ya Rufaa ikasema, kwanza SP Christopher Bageni ndo alikuwa Polisi mwenye cheo cha juu kati ya polisi walioenda Msitu wa Pande. Na yeye ndo alitoa amri kwa polisi walio chini yake.

Yeye ndo aliamuru hao wafanya biashara wanne (marehemu) wapelekwe msitu wa Pande, sehemu ambayo hakuna nyumba karibu na kwamba lengo la kuwapeleka huko ilikuwa ni ili kutekeleza mpango muovu uliopangwa bila kikwazo chochote.

Na kwamba, hao marehemu wanne waliuawa kwa uwepo na ridhaa ya mshtakiwa wa pili (SP Christopher Bageni) katika msitu wa Pande.

Pia, huyu mshtakiwa wa pili aliwadanganya Maafisa wa polisi walio wakubwa wake, kwamba wale marehemu wanne waliuawa katika majibizano ya risasi Sinza, akaonesha na kibweta cha risasi tisa zinazodaiwa kufyatuliwa eneo la Sinza, wakati ushahidi unaonesha zilifyatuliwa msitu wa Pande na Cpl Saad.

Pia watu waliokuwepo karibu na Ukuta wa Posta Sinza walikanusha kwamba hawakusikia majibizano yoyote ya risasi au tukio lolote lisilo la kawaida.

Mahakama ya Rufaa ikasema, Mshtakiwa wa pili hakuishia hapo tu, lakini pia akaonesha mahali ambapo majibizano hayo ya risasi anadai yalitokea. Na kwa kuzingatia maelezo yake hayo, mchoro ukachorwa. Huo uongo wake ukaitia nguvu kesi ya Jamhuri.

Mahakama ya Rufaa ikaendelea kusema kwamba, kwa mujibu wa kifungu cha 22(1)(b) cha Sheria ya “Kanuni ya Adhabu,” mtu ambaye anamuwezesha mtu mwingine kumuua mtu mwingine, na huyo mtu akawa ameuawa, mtu aliyefanikisha mauaji ana hatia ya kumuua huyo mtu kinyume cha sheria, haijalishi muuaji halisi hayupo.

Kwa kiingereza, Mahakama ya Rufaa ilisema hivi, “aperson who enabled another person to kill another person and that other person is actually killed, the person who facilitated the killing is guilty of unlawfully causing death of that person notwithstanding the absence of the actual perpetrator.”

Kuhusu mshtakiwa wa nne, Mahakama ya Rufaa ikasema, kwanza hakukataa kwenda Msitu wa Pande. Lakini alikana kuhusika na mauaji. Yeye anasema alipofika msitu wa Pande alibaki kwenye gari ila baada ya kusikia mlio wa bunduki alitoka nje ya gari kuangalia kuna nini, akaona mmoja kati ya wale wafanya biashara wanne anapigwa risasi na Cpl Saad na wengine wamelala chini wakiwa wameshapigwa risasi na kuuawa.

Pia (Mshtakiwa wa nne) anasema, asingeweza kufanya lolote pale kwa sababu mshtakiwa wa pili ambaye ana cheo kikubwa kuliko yeye alikuwa pale.

Sasa, swali la kujiuliza Mahakamani lilikuwa ni je, mshtakiwa wa Pili alishiriki kusababisha vifo vya wale marehemu wanne?

Mahakama ya Rufaa kwa kuzingatia mazingira ya tukio lenyewe, ikasema haijashawishika kuamini kwamba mshtakiwa wa nne alishiriki kuua.

Kwa sababu kwanza, ushahidi wake haukupingwa Mahakamani. Pili, hakuwa anajua wanaenda wapi na kufanya nini.

Kwa hiyo, kuwepo kwake tu eneo la tukio, bila kufanya kitu kingine zaidi, haitoshi kumhusisha miongoni mwa wauaji.

Mahakama ya Rufaa ikarejea maamuzi yake ya zamani kwenye kesi ya Jackson Mwakatoka na watu wengine wawili dhidi ya Jamhuri (Jackson Mwakatoka & two others V R.) ya mwaka 1990) TLR 17.

Ambapo Mahakama ya Rufaa ilisema “Uwepo pekee wa mtuhumiwa kwenye mauaji, akiwa hana lengo lingine pale, haitoshi kuhalalisha kumtia hatiani kwa mauaji (mere presence of the accused at a killing, he not having any objection thereto, is not enough to justify a conviction for murder)”

Kwa hiyo jibu la swali la je, mshtakiwa wa pili (2) alishiriki kusababisha vifo vya wale marehemu wanne, Mahakama ikajibu Hapana.

Kuhusu mshtakiwa namba moja (1), Mahakama ilisema hakuna ushahidi, wa moja kwa moja au wa kimazingira (direct or circumstantial), kumhusisha na mauaji, ingawa kuna mashaka makubwa sana juu yake (though there is a strong suspicion hovering over his head.)

Ushahidi muhimu kabisa ambao ungemhukumu ni wa mazungumzo ya simu kati yake na mshtakiwa namba mbili. Lakini mazungumzo hayo hayapo, walipofatilia Vodacom na CELTEL, wakaambiwa wamechelewa, muda wa miezi sita umeshapita, kwa hiyo kumbukumbu zimepotea.

UAMUZI WA MAHAKAMA YA RUFAA

Rufaa dhidi ya washtakiwa namba 1, 3 na 4 ikaonekana haina mashiko (has no merits), ikatimuliwa (dismissed), watuhumiwa wote watatu wakaachiwa huru.

Rufaa dhidi ya mshtakiwa wa pili (SP Chiristopher Bageni) ikaonekana ina mashiko, ikaruhusiwa na akatiwa hatiani kwa kosa la mauaji. Mahakama ya Rufaa ikatengua maamuzi ya Mahakama Kuu yaliyomwachia huru mshtakiwa wa pili (SP Chiristopher Bageni) na badala yake IKAMHUKUMU HUKUMU YA KIFO KWA KUNYONGWA (death by hanging). Hiyo ilikuwa tarehe 13-09-2016.

MAREJEO (APPLICATION FOR REVIEW)

Kwa kuwa Mahakama ya Rufaa ndio Mahakama ya juu na yenye maamuzi ya mwisho nchini Tanzania, ina maana huwezi kukata rufaa tena, njia pekee iliyopo ni kuiomba Mahakama ya Rufaa ifanye marejeo (review) ya kurejea maamuzi yake yenyewe, kuona kama yako sahihi.

Mwaka 2016, SP Christopher Bageni akaomba marejeo (review) Mahakama ya Rufaa. Mahakama ya Rufaa ikasema hana sababu zenye mashiko, ikatupilia mbali maombi ya marejeo ya Christopher Bageni, hivyo ile hukumu ya kunyongwa hadi kufa ikabaki pale pale. Hiyo ilikuwa 06-08-2019. (Kesi ya marejeo inaitwa “SP Christopher Bageni Vs Director of Public Prosecutions, Criminal Application no. 63/01, 2016”).

POSITION YA SHERIA KWA SASA.

Kimsingi, msimamo wa sheria bado ni ule ule mpaka leo. Mfano, kuhusu swali la kwanza, la je, mtu kuwepo tu eneo la tukio bila kufanya kitu kingine zaidi, kunaweza kukufanya uwe miongoni mwa wakosaji?

Jibu bado ni hapana! Kama ilivyoamuliwa mwaka 2016 na Mahakama ya Rufaa kwenye hii kesi (ya Abdallah Zombe), position bado ni hiyo hiyo.

Mfano ukirejea kesi ya hivi karibuni ya “Lidumula S/O Luhusa @ Kasuga dhidi ya Jamhuri, Rufaa ya Jinai (Criminal Appeal) namba 352 ya mwaka 2020,” ambapo mshtakiwa alishukiwa kuua kwa sababu tu alikuwepo eneo la tukio. Mahakama ya Rufaa bado iliendelea kusimamia msimamo wake kwamba, kuwepo eneo la tukio haimaanishi umeua.

Mahakama ya Rufaa ilionya kwamba, mara kadhaa kuna mkanganyiko kati ya kuwepo eneo la tukio na kushiriki kutenda kosa. Huo mkanganyiko kama ukiendelea utapelekea kutiwa hatiani kwa watu wasio na hatia. (Nanukuu kwa kiingereza, Mahakama ya Rufaa ilisema “Occasionally there happens confusion between presence at the scene of crime and participation in the commission of the offence. Such confusion, if allowed to prevail, may lead to conviction of innocent persons”).

Mahakama ikaendelea kusema, kinachoadhibiwa na sheria ni kushiriki kutenda kosa, lakini mtu kuwepo tu eneo la tukio hakumfanyi awe mhusika kwenye kosa. (“It is participation which is punishable by the law” but “mere presence at the scene of crime does not constitute one a party to an offence.”

-----MWISHO----

Angalizo: Position au maelezo haya ni kwa mujibu wa kesi na sheria zilizokuwa zinatumika mpaka siku ya kupost hili andiko. Hivyo unaposoma leo haya maelezo, soma kesi na sheria zilizopo sasa hivi, ili ujue utaratibu bado ni ule ule au la! Sheria zinarekebishwa na mpya zinatungwa kila siku.

Pia natoa angalizo, wale wazee wa kukopi machapisho ya watu na kuweka majina yenu. Ni kosa kisheria. Hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayejimilikisha andiko hili. Unaruhusiwa tu kushare lakini usibadili yaliyomo. Ni heri uanze kuandika ya kwako mpya.

Makala hii imeandaliwa na kuletwa kwako nami Zakaria Maseke (0754575246 WhatsApp). Advocate Candidate.
 
We mwenyewe umekopi na kupest. Tukishayasoma hayo zamani sana.
 
Back
Top Bottom