RC D`Salaam kasi ni nzuri uhamisho Mabwepande

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
KATUNI%28620%29.jpg

Maoni ya katuni


Kaya 289 za waathirika wa mafuriko yaliyotokea jijini Dar es Salaam Disemba mwaka jana waliokuwa wamehifadhiwa kwenye makambi ya Mbweni JKT na baadhi waliokuwa kwenye kambi ya JKT Mgulani, juzi walihamishiwa rasmi kwenye makazi mapya katika eneo la Mabwepande,nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Mratibu Mkuu wa operesheni ya kuhamisha wakazi hao maeneo ya mabonde ya Msimbazi, Jangwani, Kigogo, Mkwajuni na kote mafuriko yaliposababisha kuyakimbia makazi yao, Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Said Meck Sadick, alisema kaya hizo zenye watu 750 zilihamishiwa Mabwepande na tayari wamekwisha kupewa viwanja vya kujenga nyumba zao upya.

Waathirika hawa wamekuwa wakiishi katika kambi za muda tangu mwaka jana mwishoni, kwanza mashuleni, kambi za JKT Mgulani, JKT Mbweni na Ubungo Maziwa, na ulikuwa ni moja ya mitihani ya serikali kuhakikisha kwamba agizo lake la kuwataka watu hao wahame katika maeneo hatarishi linatimizwa.

Jumla kaya 556 ziliyakimbia makazi yake mbali na hizo zilozohamishwa juzi, bado wengine wameendelea kuishi katika kambi ya JKT Mgulani na Ubungo Maziwa na mkakati ulioko ni kuhakikisha kuwa katika kipindi cha wiki moja, uhamisho huu unakwenda sambamba na kugawa viwanja na kuhakiki wamiliki wake kwa kuwapiga picha pamoja na familia zao na kupewa hati yake.

Kimsingi operesheni hii pamoja na maumivu ya wakazi wa mabondeni kupoteza makazi yao, hatua ya kupata viwanja vilivyopimwa ambavyo vitakuwa na hatia, ni ukombozi kwao hasa kwa siku za usoni.

Ni ukombozi kwa sababu sasa watakuwa wanaishi katika maeneo rasmi yanayotambulika, watakuwa na hati ambazo zinafaa kutumika kupata mikopo kutoka taasisi za fedha kwa ajili ya kujijenga kiuchumi. Ni hakika makazi ya mabondeni pamoja na kuwa ni nyumba zao za kuishi, kiusalama, kiuchmi na hata kijamii yalikuwa ni mzigo.

Tunajua juhudi za serikali ni kubwa kwani taratibu zote hizi za kupata viwanja, kupima na kuweka baadhi ya huduma muhimu kama kuchonga barabara, kuweka matangi ya maji na kuchimba visima, kusimika nguzo za umeme na kutandaza nyaya zimefanyika chini ya kipindi cha mwezi mmoja.

Ni kasi kubwa inayozidi sana juhudi za kuwasaidia waliokuwa waathirika wa mabomu wa Mbagala na Gongo la Mboto ambao licha ya janga lao kusababishwa na vyombo vya serikali, kwa maana ya jeshi, waliosota kwa muda mrefu zaidi kwenye mahema bila kujua hatma yao.

Kuna ahadi kwamba huduma nyingi za kijamii ikiwa ni pamoja na watoto wa waathirika kuanza kwenda shule kuanzia jana katika Shule ya Msingi Mabwepande na Sekondari na juhudi za kuongeza idadi ya walimu kwenye shule hizo, zinaendelea; sambamba na ongezeko la wanafunzi pamoja na ujenzi wa madarasa mapya, ahadi ya kujengwa kwa maduka makubwa katika kipindi kifupi kijacho.

Ni hakika kama wahenga walivyotuasa kwamba Roma haikujengwa kwa siku moja, kadhalika Mabwepande haitajengwa kwa siku moja, huduma zitapelekwa huko na hatimaye litakuwa ni eneo zuri la kushi watu likiwa lina kila kitu muhimu kwa maisha ya watu wake. Hili litahitaji subira hata hivyo.

La msingi kwa sasa ni moja tu, kwamba hatimaye serikali imetekeleza kauli yake kwa wakazi wa mabondeni ambao kwa zaidi miongo miwili sasa wamekuwa ni kero kwa baadhi ya viongozi wa serikali wanaoguswa kwa dhati na maisha ya wananchi. Sisi tunaipongeza pamoja na mapungufu yote yanayoweza kuelezwa katika iperesheni hii.

Kinachotakiwa sasa ni kwa wakazi wa mabondeni, hususani walioathirika katika mafuriko haya kutambua kwamba kwa hakika kinachotokea kwao sasa ni neema tu, kwa hiyo washikamane, wasikilize serikali inasema nini ili mwisho wa yote wapate kila aina ya masaada ambao utawezekana kwa nia ya kuwafanya wapate tena makazi ya kudumu bora zaidi kuliko kue mabondeni walikokuwa wanaishi.

Ni wito wetu kwa wote kuwa ule ujanja wa kuchangamkia viwanja na kuendelea kung’ang’ania eneo ambalo ama limelipwa fidia au limetangazwa kuwa ni hatari kuishi, safari hii hautalipa kwani serikali baadaye itapitisha greda kwenye maeneo yote ya mabondeni na kusambaratisha nyumba zote zilizojengwa kwenye maeneo hayo.

Sisi tunasema kwa hili tutakuwa nyuma ya serikali ili kuboresha makazi ya wakazi wa mijini, hasa Dar es Salaam ambayo inaongoza kwa kuwa mji umaokuwa kwa kazi sana ukanda huu lakini watu wake wengi wakiishi kwenye maeneo yasiopimwa rasmi kuwa makazi.




CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom