SoC03 Rasilimali zetu ziwe Neema, na si laana kwa Watanzania

Stories of Change - 2023 Competition

Tukuza hospitality

JF-Expert Member
Jul 30, 2022
243
615
Utangulizi
Nimesoma machapisho mbalimbali kuhusiana na utajiri wa Afrika, nikagundua Bara la Afrika ni Tajiri kuliko mabara yote duniani. Tumebarikiwa kwa Ardhi kubwa yenye rutuba; na yenye rasilimali nyingi.

Sasa utajiuliza, kwa nini Bara la Afrika pamoja na utajiri wake ni maskini kuliko mabara yote? Swali hili lingeulizwa miaka ya 1880, jibu lingekuwa rahisi sana; sababu ni watu wake kukosa ELIMU! Hiki ndio kipindi kijana msomi, Dr. Karl Peters kutoka Ujerumani alikuja Tanganyika, akakutana na Chifu Mangungu wa Kilosa, ambaye yeye pamoja na wasaidizi wake hawakusoma; lakini kijana huyu aliweza kuingia naye mkataba, uliopelekea kuachia himaya yake na hadhi yake kwa Wajerumani.

Kwa wakati huu, tukiwa karne ya 21, ambapo unaweza kusema ni enzi ya utandawazi, ambapo nchi zote za Afrika (ikiwemo Tanzania) ni huru na zina wasomi wa kutosha kwa kila sekta; jibu la swali hili ni gumu, na pengine kila mtu anaweza kuwa na jibu yake. Kwa upande wangu, jibu ni NAKISI ya UADILIFU na UZALENDO, hasa kwa watu waliopewa dhamana ya uongozi katika nchi hizi!

Katika Makala haya, napenda kujikita zaidi katika swala la madini na gesi asilia.

Madini ni nini? Kwa mujibu wa Wikipedia ya SW, Madini ni dutu mango inayopatikana duniani kiasili. Madini huwa na tabia maalumu ya kikemia, si mata ogania na mara nyingi huwa na muundo wa fuwele (kristali). Kuna takriban madini 4,000 yaliyogunduliwa duniani

Gesi Asilia ni nini? Kwa mujibu wa tovuti ya “renovablesverdes”, Gesi asilia ni mafuta ambayo, kama makaa ya mawe au mafuta, huundwa na hidrokaboni, mchanganyiko wa molekuli zinazoundwa na atomi za kaboni na hidrojeni.

Madini Yaliyopo Tanzania
Kwa mujibu wa Tume ya Madini Tanzania (2023), kuna madini ya metali ambayo ni dhahabu, chuma, silva, shaba, “platinum”, “nickel” na bati; Madini ya mawe: kama almas, “tanzanite”, rubi, “garnet”, “emerald”, “spinel”, “tourmaline”, “alexandrite” na “sapphire”; Madini ya viwandani: “kaolin”, “phosphate”, chokaa, “gypsum”, “diatomite”, “bentonite”, “vermiculite”, chumvi, na mchanga wa fukwe; Madini ya kujengea: kokoto na mchanga; na Madini ya nishati: kama makaa ya mawe na urani.

Kielelezo Na. 1: Ramani ya Tanzania Inayoonyesha Baadhi ya Madini
Madini Tz.png

Chanzo: Google: “Tanzania Chambers of Mines”

Gesi Asilia

Kwa mujibu wa BBC News Swahili (Oktoba 3, 2019), serikali ya Tanzania imegundua maeneo mengine mapya manne tofauti yenye gesi asilia, yana uwezo mkubwa wa kutoa futi trilioni 5.2 zenye ujazo mraba na hivyo kufikia jumla ujazo wa futi trilioni 62.7.

Hata hivyo, kwa mujibu wa “BBC News Swahili”, Waziri wa Nishati alisema ni asilimia moja pekee ya gesi asilia iliogunduliwa iliyotumika katika kipindi cha miaka 15 iliyopita.

Kielelezo Na. 2: Mtambo wa Kuchakata Gesi Asilia
Mtambo wa Kuchakata Gesi Asilia Tz 4.png

Chanzo: BBS Swahili News (Juni 13, 2022)

Tunaweza Kunufaika Kiuchumi na Madini na Gesi Asilia

Kuanzia kipindi cha serikali ya awamu ya tatu cha Rais Hayati Benjamin Mkapa (1995 hadi sasa), tumeshuhudia wawekezaji mbalimbali katika sekta za madini na gesi asilia, lakini, kwa mtizamo wangu, Watanzania tumenufaika kidogo sana. Nilitarajia uwekezaji mkubwa na wa kimkakati katika sekta hizi ungezalisha ajira nyingi, ungepunguza mfumuko wa bei, na pengine kodi ambazo ni kero kama zile za ardhi na majengo zingefutwa (kama ilivyofutwa kodi ya maendeleo katika kipindi cha serikali ya awamu ya tatu).

Hali hii haina tofauti na ya nchi ya Nigeria, ambapo kwa mujibu wa ukurasa wa faceook wa Dotto Rangimoto (Aprili 20, 2016), Nigeria ndiye mzalishaji mkubwa zaidi wa mafuta barani Afrika, lakini wananchi wake takribani milioni 186 wanaishi katika umasikini mkubwa.

Hata hivyo, kuna matumaini ya kunufaika na rasilimali hizi; kwani kwa mujibu wa DW (Aprili 18, 2023), Serikali ya Tanzania ilitia saini mikataba yenye thamani ya Dola milioni 667 na makampuni matatu ya Australia tarehe 17 Aprili, 2023 kwa ajili ya uchimbaji wa madini adimu yaliyogunduliwa Tanzania; ambapo Tanzania itanufaika na asilimia 16 katika kila mradi.

Pia, kwa mujibu wa Habarileo (Februari 23, 2023), WIZARA ya Nishati imebainisha kwamba Machi 2023, serikali inatarajia kusaini mkataba wa kuanza Mradi wa Kuchimba Gesi Asilia katika eneo la Bahari Kuu Kusini mwa Tanzania wenye thamani ya shilingi trilioni 70.

Kama mikataba imeandaliwa vizuri kwa kuzingatia masilahi ya pande zote (wawekezaji na Tanzania), na ikasimamiwa vizuri, tunaweza kushuhudia mapinduzi makubwa ya kiuchumi.

Uporaji wa Rasimali za Afrika Ulianza Zamani, hata kabla ya Ukoloni
Kwa mujibu wa BBC Swahili Media (Novemba 9, 2022), Mwishoni mwa Karne ya 15 himaya inayojulikana kama Ufalme wa Congo ilitawala sehemu ya Magharibi ya Congo, na sehemu za majimbo mengine ya kisasa kama vile Angola. Na wakati Wafanyabiashara wa Ureno walipowasili kutoka Ulaya katika miaka ya 1480, waligundua kuwa walikuwa wameingia kwenye nchi yenye utajiri mkubwa wa asilii. Walifanya kila wawezalo kuharibu nguvu yoyote ya kisiasa au kiasili ilioweza kupunguza masilahi yao ya utumwa au biashara.

Taarifa inaendelea kusema, Pesa na silaha za kisasa zilitumwa kwa waasi, ambapo majeshi ya Congo yalishindwa, wafalme waliuawa, wasomi walichinjwa na kujitenga kulihimizwa. Kufikia karne ya 16, ufalme huo uliokuwa na nguvu ulikuwa umegawanyika vipande vipande katika hali isiyo na kiongozi, huku vita vya wenyewe kwa wenyewe vikiripotiwa. Watumwa, waathirika wa mapigano haya, walichukuliwa na kusafirishwa hadi Marekani. Takriban watu milioni nne walipelekwa kwa nguvu kwenye mdomo wa Mto Congo. Meli za Uingereza zilitumika kufanya biashara hiyo huku miji ya Uingereza na wafanyabiashara wake wakitajirika kwa rasilimali za Congo ambazo hawakuziona.

Hitimisho
Ni vizuri Watanzania tukafahamu historia hii ya uporaji wa rasilimali zetu (ambao hata Tanzania umefanyika, japo sii kwa kiasi kikubwa kama Congo), ili tuwe makini sana pale tunaoingia mikataba ya uwekezaji kati yetu na haya makampuni, mengi yakitoka katika mataifa yaliyotutawala, kwa sababu naamini kwamba hawana nia njema na sisi katika mali zetu.

Marejeo
BBS Swahili News (Juni 13, 2022), Makubaliano ya Gesi Asilia Tanzania - Matumaini Mapya ama Kaa la Moto Lingine Sekta ya Nishati?

BBS Swahili News (Oktoba 3, 2019), Tanzania Yagundua Gesi Zaidi katika Sehemu Nne Tofauti - Je Raia Wanafaidika Vipi?

BBC Swahili Media (Novemba 9, 2022), DR Congo: Je Taifa Hili Limelaaniwa na Utajiri Wake?

DW (Aprili 18, 2023), Tanzania Yasaini Mikataba ya Madini na Kampuni za Australia

Habarileo (Februari 23, 2023), Mambo Yaiva Mradi wa Gesi Asilia

Madini - Wikipedia, kamusi elezo huru

Provincial Government and State Authority in South Africa on JSTOR

County Government Structure in Kenya
 
Tukizitumia vizuri rasilimali zetu, utegemezi wa misaada kutoka nje ya nchi utakuwa historia; badala yake tutakuwa taifa linalotegemewa kwa kutoa misaada kwa nchi mbalimbali duniani!
 
Kuna haja ya kuwekeza zaidi kwenye rasilimaliwatu, watu wapitishwe kwenye historia yetu, na kutizamishwa katika vizazi vingi vijavyo kuhusiana na rasilimali hizi tulizojaliwa. Tunahitaji wawekezaji kutoka nje ya nchi, lakini ni lazima tuwe na mikataba inayozingatia masilahi ya pande zote, na kuhakikisha hakuna upande wowote unaokandamizwa kwa namna yoyote.
 
Back
Top Bottom