Rajab Diwani: Kamanda wa Vijana

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,922
30,271
RAJAB DIWANI KAMANDA WA VIJANA

Nimekuwa na kawaida siku hizi kuwa kila ninapoona picha ya mtu maarufu katika wazalendo waliopigania uhuru wa Tanganyika nitafungua kitabu cha Abdul Sykes kutazama nimeandika nini kuhusu mzalendo huyu.

Baada ya kusoma yale niliyoandika nitayaweka mtandaoni watu wasome na kupata kumjua zaidi mzalendo huyo.

Pamoja na yale niliyoona katika kitabu kama nina mengine ambayo sikuandika katika kitabu nitayaongeza kuhifadhi historia kamili ya nyakati za kupigania uhuru.

Rajab Diwani alikuwa fundi seremala Mtaa wa Congo wakati harakati za kudai uhuru zinaanza na ni katika watu wa mwanzo kuingia TANU na kuwa karibu sana na Julius Nyerere.

Rajab Diwani alihudhuria mkutano wa kwanza wa TANU Ukumbi wa Arnautoglo akiwa na Abdul na Ally Sykes, Dossa Aziz, John Rupia, Julius Nyerere, Mshume Kiyate, Max Mbwana, Jumbe Tambaza, Juma Waziri, Rashid Ali Meli, Clement Mtamila, Frederick Njiliwa, Iddi Faiz Mafungo, Schneider Abdillah Plantan, Iddi Tulio, Marsha Bilal na Denis Phombeah aliyekuwa Menaja wa Arnautoglo.

Mkutano huu haukuzidi watu 20.

Haya kaeleza mwenyewe Rajab Diwani katika gazeti la Uhuru katika kumbukumbu ya miaka 20 ya chama cha TANU mwaka wa 1974.

Katika picha za mwanzo za mikutano ya TANU Rajab Diwani anaonekana juu ya jukwaa akiwa na Julius Nyerere, Bi. Titi Mohamed, John Rupia, Zuberi Mtemvu na viongozi wengine wa TANU.

Rajab Diwani alikuwa mhamasishaji hodari kwani alijaaliwa kipaji cha kuzungumza yeye akiwalenga vijana kuingia TANU kupigania uhuru wa Tanganyika.

Kwa ajili hii Rajab Diwani alikuwa karibu sana na vijana wa Bantu Group na mwaka 1958 baada ya mkutano wa Kura Tatu Tabora, Bantu Group ilipobadilika na kuwa TANU Youth League Rajab Diwani akawa kama vile katengenezewa jeshi la askari wa miguu yaani "Infantry."

Rajab Diwani akawa kamanda wa vijana katika TANU na akaja kujulikana kwa jina la Kamanda wa Vijana hadi katika siku za uzee wake.

Jeshi hili la Rajab Diwani lilitumika vizuri katika uhamasishaji umma na halikadhalika katika kupambana na wale walioonekana kuwa wapinzani wa TANU.

TANU Youth League ikawa na nguvu ya kuweza kuibeba TANU mgongoni na kuipeleka popote pale ilipoelekezwa.

Rajab Diwani alikuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya TANU na kwa nafasi hii yake akawa kiungo kati uongozi wa juu wa TANU na jeshi lile la vijana wenda kwa miguu.

Kuna wakati TANU Youth League walijiona sawa na Police Constable wakajipa madaraka ya kuingia popote palipo na rabsha kurejesha amani na utulivu.

Lakini hii TANU Youth League ya Rajab Diwani haikuwa na mafunzo yoyote ya sheria wao wakitegemea magwanda yao ya kijani na hamasa zao.

Juu ya haya TANU Youth League ilijijenga na ikawa sehemu muhimu ya jamii katika mitaa mingi ya miji mikubwa ya Tanganyika.

Lakini pia walikuwapo watu walilolikebehi jeshi hili wakiliona kama kundi la vijana wengi wao wakorofi wakitumika tu bila kujijua.

Ukweli lakini ulikuwa TANU Youth League ilikuwa tofauti sana na Bantu Group na hii inawezekana kwa sababu ya kuwa na jeshi linalovaa unifumu kwani unifomu hujenga nidhani kwa jeshi lolote.

Askari ndani ya unifomu anakuwa tayari anatambulika anakotoka tofauti na "ragtag."

Bantu Group lilikuwa kundi la vijana waliojikusanya wenyewe nje ya TANU kisha wakajiambatanisha kuisaidia TANU katika propaganda na uhamasishaji umma.

Hawakuwa wanapokea amri au maelekezo yoyote kutoka uongozi wa TANU.

Lau kama hakuna popote ambako Bantu Group walifanya fujo kuhatarisha amani nchini lakini vile vibweka vyao vya kuvaa magunia na kubeba mapanga na mashoka katika mikutano ya TANU yalikuwa mambo ya kutisha.

Joseph Nyerere mdogo wake Julius Nyerere alikuwa mmoja wa viongozi wa TANU Youth League na hii ikasaidia kuipa nguvu na mwelekeo jumuiya hii.

Rajab Diwani ndiye aliyewakabidhi vijana wa Dar-es-Salaam ulinzi wa mji siku ya uhuru tarehe 9 December 1961.

Rajab Diwani aliwaambia vijana hawa kuwa TANU inawakabidhi usalama wa nchi wao wahakikishe kuwa uhuru unapokelewa kwa amani na utulivu.

Uhuru huu ulikuja na changamoto za kusikitisha.

Ingawa Rajab Diwani alikuwa karibu na Nyerere hadi kifo chake lakini kwa ndugu zake hali ilikuwa tofauti sana.

Hali hii ilijidhihirisha katika mazishi yake.
Lakini hiki ni kisa kingine.

Huyu ndiye Rajab Diwani aliyefatana na Nyerere katika safari yake ya kwanza kuitangaza TANU Southern Province mwaka wa 1955 na hakuachana na Nyerere hadi alipofariki.

336786739_157823327180050_4161552920417344365_n.jpg

Rajab Diwani
 
Nimesoma moja ya nyuzi humu jamvini kuwa huyu Diwani na yule mwalimu wa madrassa ya Bukoba walitumika sana katika kuiiua EAMWA na kuanzisha Bakwata
 
Nimesoma moja ya nyuzi humu jamvini kuwa huyu Diwani na yule mwalimu wa madrassa ya Bukoba walitumika sana katika kuiiua EAMWA na kuanzisha Bakwata
Babu..
Mwalimu wa Bukoba jina lake Adam Nasibu.

Kweli walikuwa mstari wa mbele wakisaidiwa na vyombo vya serikali.

Ulikuwa msiba mkubwa.
EAMWS ilikuwa inajenga Chuo Kikuu.

EAMWS ikavunjwa na ndiyo ukawa mwisho wa miradi yote ya elimu iliyopangwa na Muslim Congress mwaka wa 1962.

Sheikh Hassan bin Ameir Mufti wa Tanganyika akakamatwa na kufukuzwa nchini.
 
Back
Top Bottom