YEHODAYA
JF-Expert Member
- Aug 9, 2015
- 36,908
- 51,907
Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli awaapisha Mabalozi wateule wafuatao :-
1. Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi kuwa Balozi wa Tanzania Nchini Afrika Kusini
2. Dkt. Modestus Francis Kipilimba kuwa Balozi wa Tanzania Nchini Namibia
3. Profesa Emmanuel David Mwaluko Mbennah kuwa Balozi wa Tanzania Nchini Zimbabwe
4. Dkt. Benson Alfred Bana kuwa Balozi Tanzania Nchini Nigeria.
Hafla ya uapisho inafanyika Ikulu Jijini Dar es salaam.
Rais Magufuli awakataza Mabalozi kuaga aga ovyo ”Ikiwezekana ndani ya wiki 2 muwe mmeshaenda kwenye nchi mkatuwakilishe”
Rais Magufuli ameyabainisha hayo leo Januari 14, 2020, mara baada ya zoezi la kuwaapisha Mabalozi wa nchi nne ikiwemo Zimbabwe, Nigeria, Afrika Kusini pamoja na Namibia, hafla iliyofanyika Ikulu ya Jijini Dar es Salaam, na kumuagiza Waziri wa Mambo ya Nje kuhakikisha barua za Mabalozi hao zinapatikana haraka ili waweze kwenda kufanya majukumu yao waliyopangiwa.
“Ninajua siku za nyuma kulikuwa na tabia ya watu, akishateuliwa Ubalozi atakaa tena anazunguka maofisi kwenda kuaga kwa Rais, Waziri Mkuu, Waziri wa Mambo ya Nje wengine wanaenda hadi kwa Wakurugenzi na Wakuu wa Mikoa, ikiwezekana ndani ya wiki 2 muwe mmeshaenda kwenye hizo nchi ambazo mtatuwakilisha” amesema Rais Magufuli.
Walioapishwa leo ni Meja Jenerali Mstaafu, Gaudence Milanzi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Dkt Modestus Francis Kipilimba kuwa Balozi wa Tanzania nchini Namibia, Profesa Emmanuel David Mwaluko Mbennah, kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe pamoja na Dkt Benson Alfred Bana kuwa Balozi wa Tanzania nchini Nigeria.
=====
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 14 Januari, 2020 amewaapisha Mabalozi 4 aliowateua hivi karibuni kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Afrika Kusini, Namibia, Zimbabwe na Nigeria.
Walioapishwa ni Mej. Jen (Mstaafu) Gaudence Salim Milanzi anayekuwa Balozi wa Tanzania Pretoria - Afrika Kusini, Dkt. Modestus Francis Kipilimba anayekuwa Balozi wa Tanzania Windhoek – Namibia, Prof. Emmanuel David Mwaluko Mbennah anayekuwa Balozi wa Tanzania Harare – Zimbabwe na Dkt. Benson Alfred Bana anayekuwa Balozi wa Tanzania Abuja – Nigeria.
Baada ya kuwaapisha, Mhe. Rais Magufuli amewataka kuripoti katika vituo walivyopangiwa ndani ya wiki 2 kuanzia sasa na amewasisitiza kwenda kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, kwa kuzingatia maslahi ya Taifa hasa kiuchumi na kuwawezesha Watanzania kupata ajira katika fursa zilizopo katika nchi hizo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amewataka Mabalozi hao kufuatilia maeneo yote ambayo Mhe. Rais Magufuli alikubaliana na Waheshimiwa Marais wenzake alipotembelea nchi hizo hivi karibuni, na pia kuitangaza vyema Tanzania ambayo kwa sasa inapiga hatua kubwa katika maeneo mengi.
Hafla ya kuapishwa kwa Mabalozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Kabla ya kuwaapisha Mabalozi hao, Mhe. Rais Magufuli ameongoza kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
14 Januari, 2020