Rais Magufuli anamuogopa Membe au watu wanamogopa kwa niaba yake?

blance86

JF-Expert Member
Aug 31, 2016
2,081
5,450
MAGUFULI ANAOGOPA KUPINDULIWA AU WATU WANAOGOPA KWA NIABA YAKE?

MWANAZUONI Dk Darren Schreiber wa tasisi ya utafiti ya UC San Diego, California, Marekani, akishirikiana wasomi wenzake, mwaka 2013, walitoa ripoti kuwa watu wa vyama vya Democratic na Republican hutumia ubongo tofauti na ndio maana marais watokanao na vyama hivyo hutofautiana namna ya kufanya uamuzi.

Utafiti huo waliupa jina la "Blue Brain and Red Brain", yaani ubongo wa bluu na mwekundu. Blue ni Democrats na Red huwakilisha Republicans. Dk Schreiber alisema kuwa ubongo wa bluu na mwekundu hudhihirika viongozi wanapofanya uthubutu.

Wakati Marekani ubongo na matumizi yake ni tofauti kwa vyama viwili, CCM ubongo na matumizi yake ni tofauti ndani ya chama kimoja. Kuna ubongo unaomfia Mwenyekiti, Rais Magufuli, tuwaite "Magufuli Brain", na wana CCM wanaojiona hawana chao, maarufu kama waliokatwa mikia. Tuwaite "Mkia Brain".

Julai 2016, Rais Magufuli alisema wana CCM waliohama na kurejea ni kama ng'ombe aliyetoroka na kurejea amekatwa mkia. Huwa tofauti na wenzake zizini. Ben Membe, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje, alisema hivi karibuni kuwa yeye na mfanyabiashara Rostam Aziz wamekatwa mikia. Membe na Rostam hawajawahi kuhama CCM.

Kumbe utambulisho wa waliokatwa mkia umekua. Hata ambao hawajahama lakini hawana chao kwa sasa, wanajiona wamekatwa mkia. Sasa tutembee na makundi hayo mawili; Magufuli Brain na Mkia Brain.

MAGUFULI BRAIN

Hawajulikani wanampenda sana Rais Magufuli au wanapigania ugali wao. Hawaeleweki kama wanaridhishwa na hali ya mambo ya nchi yanavyokwenda au wanalinda usalama wao. Ubongo wao humfia Magufuli liwake jua inyeshe mvua.

Ni rahisi kuwatambua wakizungumza mbele ya vipaza sauti au vyombo vya habari. Hutafuta namna yoyote mpaka wamsifie Rais Magufuli. Jamii ya Magufuli Brain imepanuka. Imefikia hatua bungeni Magufuli Brain wamejaa. Unashangaa Spika Ndugai anamsifia Magufuli mahali pa kuchomekea tu!

Mashirika ya umma yanatekwa na Magufuli Brain. Viongozi wao wakizungumza, bila kumsifia Rais Magufuli wanakosa amani! Mkuu wa Traffic, anaonya madereva wazembe, halafu anasema "Awamu ya Rais Magufuli hatutaki ajali", utadhani awamu nyingine ajali ziliruhusiwa!

Wanaharakati wameibuka, wanajiita watetezi wa Rais Magufuli. Magazeti yamechomoza, yanamtetea Rais Magufuli kwa gharama yenye kuifedhehesha taaluma ya habari.

Ndani ya Magufuli Brain kuna makundi matatu; la kwanza ni lile la waliokuwa wakifaidi mema tangu awamu zilizopita, lakini wameweza kucheza vizuri na upepo wa nyakati. La pili ni la ambalo walijiona hawana chao awamu za nyuma, sasa wanaona huu ni muda wao. Hawa nasikia wanajiita wa jalalani!

Kundi la tatu ni wana CCM wa usajili. Yaani wapinzani waliokuwa na vyeo lakini wakahamia CCM kumuunga mkono Rais Magufuli.

MKIA BRAIN

Tusizungumzie waliokimbilia fursa upinzani na kurejea CCM baada ya kuzikosa. Hao hawana uzani kabisa. Mkia Brain tunaowagusa hapa ni wale Membe alijinasibisha nao. Watu wazito waliokuwa hawagusiki awamu zilizopita, lakini sasa hawana chao.

Mkia Brain wapo katika makundi matatu; la kwanza wananung'unika na kusema sana mafumbo (Mfano Nape na Membe). La pili linahusu watu watulivu na wasio na papara (mfano January Makamba na Kinana). La tatu wao baada ya kujigundua hawana chao, wanajipendekeza, mfano Mwigulu na Bashe.

Membe alimsema Rostam kuwa amekatwa mkia lakini anataka kujifanya mtetezi wa Rais Magufuli. Ooh! Hapa Membe alituweka hadharani kuwa Rostam ni Mkia Brain ambaye anatengeneza maridhiano na Rais Magufuli.

HOFU YA MAPINDUZI

Kuna vita inapiganwa kati ya Magufuli Brain na Mkia Brain. Ajabu ya vita hii ni kama bondia anayepigana na mwenzake aliyefungwa mikono kwa nyuma. Magufuli Brain wanapiga, Mkia Brain hawaruhusiwi kujibu mapigo.

Magufuli Brain wanawatuhumu Mkia Brain na baadhi ya viongozi wa upinzani kuwa wanamhujumu Rais Magufuli. Mkia Brain wanatuhumiwa kuandaa mkakati wa kumdhibiti Rais Magufuli asigombee Urais mwakani.

Mwanachama wa CCM, Cyprian Musiba, anayejiita mwanaharakati huru na mtetezi wa Rais Magufuli, amekuwa msemaji mkuu wa tuhuma dhidi ya Mkia Brain. Yapo magazeti huwananga mno Mkia Brain kwa kuwaita majna mabaya.

Hivi karibuni, makatibu wakuu wastaafu CCM, Kinana na Yusuf Makamba, walitoa waraka wakilaani kuchafuliwa na Musiba. Wakasema inaoneka Musiba analindwa na mamlaka isiyohojiwa na yeyote.

Makamba na Kinana hawakutaja jina la Rais Magufuli wala hawakumshutumu popote. Isipokuwa walisema hawawezi kumhujumu Rais wakiwa nyumbani kwao, tena Rais wa chama chao. Ukisoma waraka vizuri, utaelewa kuwa walijitenga na tuhuma za kumhujumu Rais, wakataka umma umpuuze Musiba.

Baada ya waraka huo, aliibuka Bashe (Mkia Brain) na kuwashambulia Kinana na Makamba kuwa waraka wao ulilenga kumdhibiti Rais Magufuli asigombee Urais mwakani. Kwa nini Bashe alikimbilia kwenye Urais mwakani wakati hayakuwa maudhui ya waraka?

Makamba na Kinana wanalalamika Musiba anawachonganisha na Rais Magufuli. Anawajengea chuki ndani ya CCM waonekane wanahujumu chama na mwenyekiti wao. Bashe anasema waraka unajenga uhalali wa kumzuia Rais Magufuli asigombee Urais 2020. Hii ilitokea wapi?

Kwani Musiba ndio Rais Magufuli? Maana aliyeshutumiwa kwenye waraka ni Musiba. Au hiyo mamlaka inayomlinda Musiba ambayo imesemwa na akina Kinana ni Rais Magufuli? Inaonekana Bashe anajua zaidi!

Baada ya Bashe kuwashambulia Kinana na Makamba, Rais Magufuli amempa Unaibu Waziri wa Kilimo. Je, Rais Magufuli alifurahishwa na kauli yake kuwashambulia Kinana na Makamba? Tukumbuke kuwa Bashe ni Mkia Brain ambaye amefanya maridhiano. Mwaka juzi alilalama bungeni kuwa alitekwa na Usalama wa Taifa.

Sasa basi, kinachoonekana sasa hivi ni hiki; Musiba anawashambulia Mkia Brain akimtumia Rais Magufuli. Anasema anamtetea. Wanaoshambuliwa wanaibuka na kutaka Musiba apuuzwe, kisha wanahoji mbona hachukuliwi hatua?

Wanatokea Magufuli Brain, tena wabunge, wanamtetea Musiba kwa kutumia jina la Rais Magufuli. Bashe na Livingstone Lusinde wametumia jina la Rais Magufuli kumtetea Musiba. Hivyo, Magufuli Brain wanaona Musiba yupo sahihi na hapaswi kuguswa. Tena wanaona akiguswa Musiba ni kama kaguswa Rais Magufuli.

Kuna wakati Katibu Mkuu CCM, Dk Bashiru Ally, alimvaa Membe kwa sababu ya maneno ya Musiba pamoja na maandishi ya magazeti yenye kuitwa ya mkakati dhidi ya Mkia Brain pamoja na wapinzani. Bashiru kumvaa Membe kwa sababu ya maneno ya Musiba ilikuwa bahati mbaya au dhamira?

Tuulizane; hivi hizo hujuma zinazosemwa dhidi ya Rais Magufuli zipo au kuna watu wanaweweseka? Je, ni watu wanajitafutia thamani mbele ya Rais Magufuli kwa kumtisha kuwa anahujumiwa na anapangiwa njama?

Kwani Rais Magufuli naye anaamini na anaogopa hayo mapinduzi au kuna watu wanaogopa kwa niaba yake? Wanaosemwa wanataka kumpindua ni wana CCM, mbona hawashughulikiwi kwa vikao vya chama, badala yake wanakong'otwa na Musiba pamoja na magazeti ya mkakati?

Makamba na Kinana wamelaumiwa kwa nini wametoa waraka hadharani badala ya kufuata taratibu za chama. Mbona Magufuli Brain hawajawahi kuungana kumshambulia Musiba ili aache masuala ya chama yashughulikiwe ndani ya chama? Kosa la Musiba hawalioni ila la Kinana na Makamba wameliona? Mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu sio?

Hii hofu inatokana na nini? Watu wanatengeneza hofu isiyokuwepo? Kuna ambao wameona ulaji katika kuvujisha siri hewa na kuwapa watu uhusika ili waaminike kwa Rais? Swali kuu ni hili, je, Rais Magufuli anawaamini?

Hata Mkia Brain nao huweweseka. Juzi, Nape alisema watu wanaowaza Rais Magufuli hatagombea Urais CCM 2020 wanajisumbua. Je, aliamua kuongea kauli ya maridhiano au aliwananga watengeneza hofu isiyokuwepo?

Rostam pia alisema Magufuli ndio mgombea pekee wa Urais CCM 2020. Alimtaka Membe amuunge mkono Magufuli. Je, Membe ameshatangaza kuwania Urais mwakani au huwa ananong'ona? Rais Magufuli anamuogopa Membe au watu wanamogopa kwa niaba yake?

Ndimi Luqman MALOTO
 
Back
Top Bottom