KWELI Rais Daniel Arap Moi alihudumu nafasi ya Urais bila kuwa na First Lady

Taarifa hii imethibitika kuwa ya kweli baada ya kufanya tathmini ya kina
Kuna kijiwe huku Bonyokwa tunapiga stori za kawaida kuhusu nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Sasa kuna jamaa kasema kuwa Rais wa awamu ya pili nchini Kenya, Hayati Daniel Arap Moi wakati anaingia madarakani hakuwa na mahusiano kabisa na hakutaka kujihusisha nayo kabisa. Nguvu kubwa alielekeza katika malezi ya watoto.

Jambo hili lilimfanya ahudumu miaka 24 ya urais bila kuwa na mke (First Lady) jambo ambalo halijazoeleka ulimwenguni, kwamba kuwe na mtawala asiye na mwenza.

_110751815_0e83d737-d47d-4ab7-bba2-fa2720b261ff.jpg

Daniel Toroitich Arap Moi (Google)
 
Tunachokijua
Daniel Toroitich Arap Moi alikuwa mwanasiasa wa Kenya aliyehudumu kama Rais wa pili wa nchi hiyo kuanzia 1978 hadi 2002. Ndiye mwanasiasa aliyehudumu kwenye nafasi ya rais kwa muda mrefu zaidi kuliko marais wengine nchini humo hadi sasa. Hapo awali, Moi aliwahi kuwa makamu wa tatu wa Rais wa Kenya kuanzia 1967 hadi 1978 chini ya Rais Jomo Kenyatta, na kuwa Rais kufuatia kifo cha rais huyo.

Maisha ya Ndoa
Lena Tungo Moi ndiye alikuwa mke wa Moi. Alizaliwa mwaka 1926, aliolewa na Moi mwaka 1950 na walijaliwa watoto wanane; wa kike watatu na wa kiume watano; wa kike ni Jennifer, Doris na June ambaye aliasiliwa; wa kiume ni Jonathan, Raymond, John Mark, Philip na Gideon.

Kwenye miaka ya 1960 na 1970, Lena Tungo Moi alionekana na kupendwa katika ulingo wa kisiasa, ambapo Moi alikuwa wa Rais, lakini hakuwahi tena kuonekana hadharani baada ya Moi kuwa Rais mwaka 1978.

Lena-Moi.jpg

Lena Tungo, Mke wa Moi (Google)
Citizen Digital, Jarida maarufu la Nchini Kenya kupitia makala yao ya Februari 4, 2020 lilifafanua mkasa ulioikumba ndoa ya Moi hadi kupelekea Lena asionekane tena hadharani.

"Katika wasifu wa 1998, The Making of an African Statesman, na Andrew Morton, Bw. Moi, kulingana na Sunday Nation, alikiri kwamba alikuwa na furaha kidogo kutoka kwa familia yake, akisema kwamba alihisi kukatishwa tamaa na kuvunjika moyo." lilinadika Jarida hilo

Aidha, Gazeti la The Monitor (2020) kupitia makala yake yenye kichwa cha habari "The untold story of Moi’s troubled family" familia ya Moi ilikuwa na Matatizo makubwa, hata watoto wake hawakuwa tayari kumpa ushurikiano kwenye masuala mbalimbali ya kifamilia na kiuongozi, hivyo muda wote alijihisi mpweke.

Baadaye, Moi alitengana na mke wake mwaka 1974 na talaka yao kukamilika mwaka 1979.

Pia, Moja ya sababu zinazotajwa kuwa chanzo cha kutengana ni kitendo cha Lena kukataa kucheza muziki na Mzee Kenyatta katika hafla moja ya Ikulu, wakati Moi alikuwa akicheza na Mama Ngina Kenyatta.

Kitendo hicho kilionekana kuwa fedheha kwa Moi, jambo lililomfanya atengane na Lena. Lena alikuwa Mkristo ambaye alikuwa na dhana kwamba kucheza muziki ni dhambi, hivyo, hakuwa tayari kufanya hivyo.

Katika kipindi chote, Lena hakuonekana hadharani mpaka Julai 2004 alipofariki dunia. Kifo cha Lena kilimuunganisha tena na mume wake. Alikuwa mke wa rais ambaye Wakenya hawakuwahi kumfahamu.

Uongozi na Kifo
Daniel Arap Moi alifariki dunia Februari 4, 2020 katika hospitali ya Nairobi alikokuwa amelazwa kwa takribani miezi mitatu akiwa na umri wa miaka 95.

Licha ya kuitwa dikteta na wakosoaji wake, Moi alikuwa akipendwa na wananchi. Hata hivyo, katika utawala wake, wapinzani hawakupata nafasi, baadhi yao waliwekwa kizuizini na hata wengine kuuawa.

Moi alihakikisha hakuna mtu anamyumbisha katika utawala wake. Aliwadhibiti wapinzani na wote waliokuwa tofauti naye. Alifuta mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1982 kabla ya kuviruhusu tena mwaka 1991.

Utawala wake wa miaka 24 ulijaa chungu na tamu kwa Wakenya. Siku anaondoka madarakani Desemba 2002, baadhi ya watu walifurahi kwa sababu walikuwa wamemchoka. Hata hivyo, anakumbukwa kwa kujenga mfumo imara wa elimu nchini humo.

Wakati wa utawala wake, Moi alifahamika kwa majina mengi, baadhi ya majina hayo ni kama vile Mtukufu Rais, Nyayo na Rais kwa bahati mbaya (accidental president). Alipenda kutukuzwa na mara nyingi kuonekana kwenye vyombo vya habari.
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom