RAI YA JENERALI; Hatuwezi kuijadili Tanzania bila kuujadili Muungano!

Kiganyi

JF-Expert Member
Apr 30, 2012
1,242
765
KATIKA muktadha wa mjadala kuhusu kuandika katiba mpya, nimekuwa nikisema kwamba yapo masuala ya kikatiba ya aina mbili: aina ya kwanza ni yale ambayo, hata kama yanaumua hisia kali miongoni mwa wanasiasa, bado yanaweza kupata ufumbuzi wake ndani ya muda mfupi.


Aina ya pili ni ile ya masuala ambayo, hata kama hayaibui hisia kali miongoni mwa wanasiasa na watawala, lakini yana umuhimu mkubwa, ufumbuzi wake hauwezi kupatikana kirahisi au katika muda mfupi.



Aina ya kwanza, kama naruhusiwa kukariri yale niliyokwisha kuyasema, ni ile inayohusu matatizo ya kiutawala na yanayogusa mgawanyo wa madaraka katika ngazi mbalimbali za utawala.
Kuna mgawanyo wa madaraka baina ya mihimili mitatu ya dola (Utawala, Bunge na Mahakama); ukomo wa madaraka ya ofisi za watawala; ukomo wa madaraka ya Bunge; ukomo wa mamlaka ya Mahakama; maingiliano kati ya mihimili hiyo, na kadhalika.
Katika kuyaandikia vipengele vya kikatiba, masuala ya aina hii yatapatiwa majibu kwa kufuata utashi wa kisiasa wa wale walio madarakani pamoja na raia wenzao wenye ujuzi wa mambo na ari ya kuchangia katika maendeleo ya taifa lao.



Mara nyingi maoni yao yatatokana na ujuzi wa kitaaluma katika nyanja za siasa, sheria na historia, na jinsi wanavyoiangalia jamii wanamoishi na mahitaji yake ya wakati huo.
Wajuzi hawa watadurusu mifumo mingi duniani na katika historia, ili kuona kama wanaweza kujifunza namna wenzao walivyoshughulikia hoja zilizo mbele yao. Katika nchi nyingi za Jumuia ya Madola (Commonwealth), mara nyingi wataalamu watajikita zaidi katika historia ya kikatiba ya Uingereza na mfumo unaoitwa wa ‘kibunge”. Lakini wakati mwingine wataenda nje ya mfumo huo na kufanya majaribio ya kuchanganya dhana za mfumo wa kibunge na mfumo unaoitwa wa ‘kirais.’



Ndivyo tulivyofanya sisi kwa kuchanganya dhana hizo mbili, na ndiyo maana tumejenga ofisi zenye utata, kama ile ya ‘waziri mkuu’ asiyekuwa waziri mkuu kwa maana ya mfumo wa ‘kibunge.’
Wanaofuatilia masuala haya watajua kwamba waziri mkuu wa Uingereza ni kiongozi wa wabunge wa chama chake na serikali yake, lakini si bosi wa mawaziri wake. Anaitwa ‘primus inter pares’ (first among equals, ama kiongozi wa walio sawa).
Hata hivyo, inapobidi waziri mkuu achukue uamuzi au abebe lawama, yeye ndiye mkuu wa kufanya hivyo. Hawezi kumwachia malikia majukumu hayo.



Tutaona kwamba hiyo ni tofauti kabisa na jinsi tunavyoendesha mambo yetu kikatiba nchini, na mifano ya hivi karibuni imedhihirisha, kwa mara nyingine tena, utata wa ofisi ya waziri mkuu na mambo mengine yanayotokana na kuchanganya dhana hizi mbili.
Hata hivyo, mimi naamini kwamba haya ni mambo yanayowezwa kurekebishwa iwapo kuna utashi wa kisiasa na uangavu wa mawazo, na utambuzi wa uzoefu wetu kihistoria utakaotuwezesha kuona ni wapi tulipata usumbufu wa kimuundo na ni vipi tunaweza kurekebisha.



Haya ni masuala ya kimpangilio ambayo hayahitaji muda mrefu mno wala tafakuri ya kuchosha kuyapatia ufumbuzi. Utashi wa kisiasa na umahiri wa wajuzi wa mambo vinatosha kuyaangalia, kuyajadili na kuyaweka bayana, kuonyesha njia kadhaa zinazoweza kufuatwa, na hatimaye kuchagua njia mwafaka kwa wote, au kwa walio wengi kwa wakati tulio nao.
Tunaweza kuteua utaratibu wa ‘kibunge’ au ule wa ‘kirais,’ au tunaweza kuteua kuendelea na mseto wetu wa hivi sasa, pamoja na utata wake.



Wakati tukifanya hivyo, tunaweza pia kuamua mambo kama vile mawaziri kutokuwa wabunge; madaraka ya rais kupunguzwa na kukabidhiwa kwa asasi mahsusi; matokeo ya kura za rais kupingwa ndani ya kipindi kilichopangwa, na mambo kama hayo. Haya yote, na mengine kama haya, tunayamudu katika kipindi cha miezi 18.



Sasa tuangalie masuala ambayo ni mazito , nyeti na tata, ambayo yanahitaji tafakuri ya muda mrefu na ambayo hayatatuliki kwa watawala kuwa na utashi wa kuyatatua ama kwa wajuzi wa mambo kuwa na weledi na umahiri uliojipambanua.



Haya ni yala masuala ambayo yanahitaji maridhiano ndani ya jamii ambazo zinaweza kuwa na maslahi yanayokinzana, na wakati mwingine maslahi hayo yakiwa yamejenga uhasama ndani ya jamii hizo, hususan kwa sababu bado jamii hizo hazijapata, au hazijajitengenezea, wasaa wa kuyajadili kwa kina masuala muhimu.



Sina budi kuanza na suala la Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar, ambayo ndiyo Tanzania. Juhudi yo yote inayolenga kuwaambia wananchi kwamba wanaweza kuandika katiba mpya kujadili masuala yote yanayohusu nchi yao bila ya kujadili kwa kina sula la Muungano ni kazi bure.



Maana ya juhudi kama hizo ni sawa na kuwaambia watu wajadili kila kitu kadri wanavyotaka lakini wasiijadili Tanzania yenyewe, jambo ambalo halieleweki.
Katiba haina budi kusimama juu ya misingi ya aina ya Tanzania tunayotaka kuijenga, na hiyo ni pamoja na kile kinachoifanya Tanzania kuwa Tanzania, na hicho ni Muungano. Sasa inawezekana vipi kuijadili Tanzania kwa kutoijadili Tanzania?



Sote tunaelewa kwamba yapo maoni yanayopishana mno kuhusu Muungano kama muungano, na pia muungano kwa maana ya mifumo yake na michakato yake. Ni kusema kwamba wapo watu wanaoamini kwamba Mungano, pamoja na kwamba una matatizo kadhaa, ni jambo jema na ambalo linafaa kuendelezwa huku matatizo yake yakirekebishwa ili kukidhi maslahi ya wana-Muungano wote.



Wapo wanaoamini kwamba Muungano hauna haja ya kuendelea kuwapo kwa sababu mbalimbali. Wengine wanazitaja sababu hizo, na wengine hawautaki kwa sababu tu hawautaki.

Kisha wapo watu ambao wanauona Muungano kama kitu kilichopo na ambacho wamekizoea, lakini hawajui kama una manufaa au hauna manufaa, na wala hawaoni ni kwa nini watu wanasumbua akili zao juu ya jambo kama hilo.



Baina ya misimamo hii, naamini kwamba kila mmoja una mantiki yake, na si busara kuenenda kama vile upande mmoja lazima umebebwa na mantiki nzito zaidi kuliko mwingine. Busara inasema tuujadili Muungano, na tuujadili katika marefu na mapana yake na pia kina chake katika kila eneo.



Itakuwa hasara kubwa iwapo tutaingia katika zoezi la kuandika katiba mpya (kama kweli tumedhamiria kuandika katiba mpya, na si kugongagonga iliyopo) bila kujadili kwa kina asasi hii muhimu kuliko zote.



Kitakuwa ni kichekesho cha gharama kubwa iwapo tutajidai tumeandika katiba mpya halafu baada ya miaka miwili au mitatu tuanze kuunda tume, mara “Tume ya Bakari”, mara “Tume ya Yohana” eti “kuangalia kasoro za Muungano na kupendekeza marekebisho ya kuuboresha.”
Tume hizi tumeziona, mapendekezo yake tumeyasoma, lakini hakuna kilichobadilika kimsingi kwa sababu kila mara juhudi zilizofanyika zimekuwa ni za kupoza jazba, kutuliza hisia, “kufunika kombe”, kama wasemavyo Waswahili, ili “mwanaharamu apite”.



Kama kawaida yetu, tumekataa kufanya kazi ya kina, kazi ya kudumu, kazi ya mtazamo wa masafa marefu. Tuna haraka kama vile tuko katika mpito tukielekea kwingine, sijui wapi?
Hakuna sababu ya kukumbushana kwamba huu ni muungano wa nchi mbili zilizokuwa huru kabla ya kuungana. Ingawaje ni kweli kwamba walio wengi katika nchi yetu wamezaliwa chini ya Muungano, bado ni kweli pia kwamba hisia za u-Tanganyika na u-Zanzibari hazijatoweka moja kwa moja.



Zimekuwa zikichomoza mara kwa mara, na kila mara zikizimwa kwa njia ambazo hazikushughulikia masuala ya msingi yaliyojitokeza wakati huo. Tusipoujadili Muungano kwa kina, upana na urefu, kwikwi hizi zitaendelea kujitokeza kama kielelezo cha matatizo yanayofunikwa funikwa kila mara.


 
Copy and paste ...inaboa mkuu!!
Fanya ka-uchambuzi wako na kisha weka summary...itasaidia sana ktk majadiliano
 
sasa kwa mitazamao ya JF na Great Thinkers wake huyu Jenerali leo kaenda kinyume kwani hajawatukana Uamsho wala hajazungumzia kanisa kuchomwa moto wala hajawatukana CCM vizuri

lakini yote tisa kumi huyu ni jina lake la kati ni TWAHIR na hiyo ni very unfortunate hivyo pamoja na usomi wake na uchambuzi wake wa kina juu ya hili suala bado mbele ya waGALA ataonekana anawatetea wenzake tuuu

hana jipya

unfortunately discussions zetu zimeguuzwa kuwa that low
 
sasa kwa mitazamao ya JF na Great Thinkers wake huyu Jenerali leo kaenda kinyume kwani hajawatukana Uamsho wala hajazungumzia kanisa kuchomwa moto wala hajawatukana CCM vizuri

lakini yote tisa kumi huyu ni jina lake la kati ni TWAHIR na hiyo ni very unfortunate hivyo pamoja na usomi wake na uchambuzi wake wa kina juu ya hili suala bado mbele ya waGALA ataonekana anawatetea wenzake tuuu

hana jipya

unfortunately discussions zetu zimeguuzwa kuwa that low

Mkuu hilo jina ni laubaguzi mkubwa, ninyi watoto wa kijakazi!
 
Wakati tukifanya hivyo, tunaweza pia kuamua mambo kama vile mawaziri kutokuwa wabunge; madaraka ya rais kupunguzwa na kukabidhiwa kwa asasi mahsusi; matokeo ya kura za rais kupingwa ndani ya kipindi kilichopangwa, na mambo kama hayo. Haya yote, na mengine kama haya, tunayamudu katika kipindi cha miezi 18.
Hapa ninakubaliana na mwandishi hasa kwa hili la mwisho "la muda mfupi" wa kurekebisha kasoro za miundo yetu.
Itakuwa hasara kubwa iwapo tutaingia katika zoezi la kuandika katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - msisitizo wangu (kama kweli tumedhamiria kuandika katiba mpya, na si kugongagonga iliyopo) bila kujadili kwa kina asasi hii muhimu kuliko zote.
Lakini hapa hata mwandishi hakutaja muda ambao ungefaa, angalau kwa makisio, kujadili na kuandika katiba hiyo.

Kwa maoni yangu, kuhusu hilo la mwanzo, hata huo muda wa miezi 18 nahisi ni mingi sana, kwani tayari tunaelewa kila palipooza, tatizo letu ni kuwa tunashikilia uoza huo ili kukidhi mahitaji na utashi wa [wana]siasa (political interests na political will) kuliko mahitaji ya sera (policy needs) ya nchi na sio ya chama au vyama.

Vyovyote iwavyo, nadhani muda umefika kwa viongozi wetu kuacha upofu wa nyoyo zao na kuona ukweli kuwa Watanzania wameshakuwa vya kutosha kiasi hawataki tena kuburuzwa na maslahi ya wachache. Hapa sisemei chama bali ninasema kwa yeyote atakayekanyaga ikulu kwa maslahi yake na/au ya kikundi chake. Na watu wa kuwaogopwa zaidi ni hawa waliozaliwa ndani ya Muungano, ambao ndio idadi kubwa zaidi ya Watanzania wote, wenye umri wa kisheria kuanzia miaka 18 hadi 30, au kusema, waliozaliwa kuanzia mwaka 1977.

Katika hawa mna wasomi wakubwa waliotafrika kwa kukosa kazi, au wana kazi lakini hawalipwi kulingana na elimu yao, na ndio maana wengi huingia kwenye siasa kwani ndiko kwenye ulaji; kuna waliokosa elimu kwa sababu ya umasikini wa wazazi wao, waliomo vijiweni na mitaani wakihataraishwa maisha yao kwa kuiba kuku na kusekwa jela miaka 5 au kuuliwa hapo hapo na "wananchi wenye hasira," wakati baadhi ya watu wachache wenye umri wa baba na babu zao wanaikwangua nchi kutoka kila upande.

Hawa ndio idadi kubwa ya watoa maoni kuhusu katiba mpya. Kuwazuwia wasijadili Muungano ni sawa na kuzuwia njia ya mkondo wa maji; lazima maji hayo yatatafuta pengine pa kutokea. Mwanya mdogo utakaopatikana (na tayari huwa tunaona yanayotokea kwenye maandamano "ya amani" yanavyoishia kwa vurugu, uporaji na uharibifu wa mali - yanayotokea ZNZ na yaliyotokea
Morogoro:

Hayo yalielezwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Adolfina Chialo. Kamanda huyo alisema hayo akizungumzia vurugu hizo zilizosababisha uharibifu mkubwa wa mali, uporaji wa bidhaa madukani, kwenye baa pamoja na uchomaji wa matairi na kuziba barabara itokayo Kilombero
kwenda Mikumi - Chanzo HabariLeo
. Wanasiasa wasicheze na bomu la wakati.
 
Sioni Hoja mpya hapa. Muungano Wa Tanzania siyo kitu kipya. Muungano umejenga nchi inaitwa Jamhuri ya. Muungano wa Tanzania. Ukiandika katiba mpya lazima uanze na jina la nchi na mipaka yake. Nchi tunayo na mipaka yake inajulikana. Kinachotakiwa kujadiliwa siyo Kama muungano uwepo au usiwepo. Waliodai katiba mpya kwa nia ya kuvunja muungano walikosea mahesabu, badala ya kujumlisha wanatoa. Nchi iPo . Kinachotakiwa ni kujadiliana namna ya kuiongoza nchi yenyewe. Chombo gani kiwe na madaraka na. Wajibu gani. Je tuwe na serikali moja, mbili Kama inavyopenda CCM, tatu za cuf au kumi na. Zaidi za Chadema? Tukijibu hilo swali, kisha tuamue serikali iPi iwe na madaraka na wajibu upi. Kama Hoja ni kujadili muungano kwa nia ya kuuvunja hakuna haja ya Tume ya katiba kwa vile kura ya maoni inatosha kuuvunja , na kisha kila nchi ikaanzisha mchakato wa kkuanzisha katiba na hasa Tanganyika ambayo haipo kwa sasa. Kama hii siyo Shabaha, basi tujadiliane kuhusu katiba ya nchi ambayo iPo inayoitwa "Jamhuri ya muungano wa Tanzania".
 
Historia ya Muungano wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa inajaribu kupindishwa bila sababu za msingi.Hali hii ndiyo leo imepelekea machafuko yanayojiri huko Zanzibar.Kuna sababu gani ya kuzuia aina ya Muungano wautakao wananchi bila ya kuwa na maslahi binafsi kwa wanaoweka vizuzi hivyo.

Wakati mwingine makosa ya kiufundi yanayofanywa kwa makusudi na viongozi wetu yataigharimu nchi kwa kusababisha amani tuliyojivunia miaka dahari iliyopita kuyeyuka kama karatasi ya nylon ndani ya moto.Leo hii nafungua ukurasa huu ndani ya JF tujadili aina ya Muungano tuutakao kwa uwazi bila kumung'unya maneno.

Nichukue fursa hii kukaribisha michango yenu wana JF ilikuweza kulinusuru taifa letu na hatari iliyoanza kujiinua na kushika kasi.



Tukishirikiana kwa dhati hakika tutaweza na lengo letu litafanikiwa
 
Back
Top Bottom