Posho Yawakimbiza madaktari Wapya Temeke

Gurudumu

JF-Expert Member
Feb 5, 2008
2,349
261
Posho yawakimbiza madaktari wapya Temeke



na Nasra Abdallah




MADAKTARI wapya waliopangiwa kufanya kazi katika hospitali ya Temeke Dar es Salaam, hawajapewa posho zao kwa miezi mitatu tangu wafike hospitalini hapo jambo linalowafanya wengi wao kuacha kazi.

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Temeke, Silvia Mamkwe, alisema hayo wakati wa ziara ya Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi, aliyoifanya hospitalini hapo.

Alisema fedha hizo ambazo jumla yake ni milioni 50 kwa madaktari wote 50, hazijatolewa na Hazina hadi sasa jambo linalowafanya kushindwa kuwazuia madaktari kwenda kutafuta maslahi sehemu nyingine huku wengine wakifanya kazi chini ya kiwango.

Hata hivyo alisema pamoja na kufika kwa madaktari kumekuwepo na changamoto mbalimbali hasa za madaktari waliobobea katika magonjwa mbalimbali ambapo mpaka sasa waliopo ni saba kati ya 50.

Alisema hali hiyo hufanya daktari mmoja kuhudumia wagonjwa zaidi ya 30 jambo ambalo ni kinyume na maagizo ya Shirika la Afya Duniani (WHO), linalotaka daktari mmoja kuhudumia wagonjwa wasiozidi 20.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni uhaba wa vitanda kwa ajili ya kina mama kwa ajili ya kujifungulia ambapo mpaka sasa vipo 11 wakati watoto wanaozaliwa kwa siku hospitalini hapo ni kati ya 50 hadi 80.

Kwa upande wake Meya Masaburi, alimtaka kumpatia orodha ya madaktari hao ili kuweza kufuatilia malipo hayo ofisi ya Hazina kabla ya mambo kuzidi kuwa mabaya.

Kuhusu gari la wagonjwa ambalo awali Mganga Mkuu wa Hospitali, Amani Malima, alisema wanalitegemea gari moja la jiji ambalo linakaa hospitali ya Mnazi Mmoja.

"Hali hii haikubaliki hata kidogo kwani gari la wagonjwa ni muhimu sana kwa kila hospitali, kusubiria gari moja kwa hospitali tatu zote za wilaya ni hatari na tunaweza tukajikuta tunamsababishia mtu kifo ambacho kingeweza kuzuilika," alisema.

Hata hivyo kwa upande wa maabara alitaka wasimamizi wa kitengo hicho kuwa makini kwa kufuatilia kwani kinalalamikiwa kuwa ndiyo sehemu inayofuja dawa ambazo nyingi zinapatikana mitaani kiholela na hivyo kuipa serikali hasara.

Wakati madaktari hao wakilalamikia kuhusu kuwa na msongamano wa wagonjwa, pia Masaburi alimtaka Mganga Mkuu kuweka utaratibu wa masaa kwa kila mhudumu kumpatia huduma mgonjwa kwani hii itasaidia kuwabana wale wavivu ambao wamekuwa wakichukua muda mrefu kutoa huduma kwa mtu mmoja muda mrefu bila ya sababu.

My take: Hapa ni Dar es Salaam, huko mikoani hali itakuwaje? Je serikali inajali wananchi wake?
 
Back
Top Bottom