Fidel80
JF-Expert Member
- May 3, 2008
- 21,947
- 4,445
MKUU wa Intelijensia za Jinai katika Jeshi la Polisi nchini, Hussein Laisseri ametaka jamii kuwa makini na dada poa ambao hutumia udhaifu wa wanaume kuwalisha mihadarati na kuwaibia. Kauli hiyo ameitoa wakati akijibu hoja za gazeti hili kuhusu kuzagaa kwa maelezo kwamba wasichana hao hupora watu kwa staili ya kujipaka dawa hizo katika sehemu za miili yao zinazohusishwa na ngono. Alisema ingawa walioathirika huwa hawataki kusema, utafiti unaonesha kwamba matukio hayo yanaongezeka ingawa wanaofanyiwa huona haya kuzungumza. Laisseri, ambaye pia ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SAC), alimweleza mwandishi wa habari hizi, kuwa mazingira ya aina hiyo ya uhalifu pekee, yanatosha kumfanya mtendwa asiseme ukweli wa kilichomkuta na kuifanya ofisi yake ikose rekodi ya matukio hayo kama inavyopasa kuwa. Si unaona kwamba ni matukio ya aibu? Sasa unatarajia kuna mtu atasimama na kusema alikuwa na mama au dada poa, halafu akaleweshwa na kuibiwa kwa njia hiyo? Alihoji. Kila anayewasilisha madai ya kuibiwa fedha nyingi katika mazingira yasiyoeleweka, hueleza kuwa waliofanya hivyo ni wahalifu anaohisi kuwa ni majambazi au wezi wa kuwinda, hatuwezi kulazimisha mtu aseme kuwa alitendwa na mtu wake, hata kama ilikuwa hivyo, hadi ushahidi uthibitishe na si hisia, alisema Laisseri. Aliwataka wanaokumbwa na kadhia hizo, wasifanye siri, bali walieleze Jeshi la Polisi ili wasaidiwe. Kwa mujibu wa utafiti, wengi wa wanaofanya wizi wa kutumia mihadarati, si wasimamao kando ya barabara, bali ni wenye vijiwe maalumu katika hoteli kubwa hasa kwenye huduma za kasino. Dili zao si za fedha ndogo na wala hawalengi watu wa kipato cha kudunduliza. Hawaangalii sura wala mavazi ya wanayemlenga. Zaidi, wanapima fungu la fedha wanazoweza kuiba na kuendeleza maisha yao, alisema mmoja wa waliopata kukutwa na tukio la aina hiyo, ambaye hata hivyo alidai fedha zake hazikuibwa zote kwa kuwa alikabidhi sehemu kubwa kwa msimamizi wa kaunta katika hoteli aliyokwenda kujirusha Dar es Salaam. Alidai kwamba aliingia chumbani na dola 1,000 za Marekani na baada ya kushituka usingizini ikiwa ni mchana wa siku ya pili, hakuzikuta wala kumwona binti aliyekuwa naye. Ninachojua alivaa wigi refu na nguo za heshima. Anazungumza Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa na Kinyaturu. Alinibembeleza
nikafanya hivyo na sijui kulitokea nini kwani nilipoamka siku ya pili, sikumwona wala fedha zangu, lakini sikumweleza yeyote niliishia kulipa fedha ya chumba ya siku mbili, alisema. Lakini, baadhi ya wafanyakazi wa kasino za Dar es Salaam walidai kwa nyakati tofauti kuwa wizi wa aina hiyo kwao si kitu kipya, kwa sababu ndio unaotumiwa na machangudoa wanaofahamika kwenye hoteli zao kila wakati. Hivi unafikiri wanawake wote unaowaona kwenye kasino ni wafanyakazi au wacheza kamari kweli? Nenda kaunta utajionea mambo, kwa sababu wanakuja na Sh 3,000 tu za kadi za kuchezea kamari, halafu wanatega mingo' (wanasubiri wateja) kwenye mashine za katikati, huku wakijinadi kwa kuzungusha macho na kubadili mitindo ya kusimama. Wanawaliza sana Wazungu, wafanyabiashara wakubwa, mawaziri na watu wengine wenye umaarufu, wanaokuja kunywa bia na mvinyo kwenye kaunta za hoteli zetu. Na si unajua tena masharti ya humu? Yaliyotokea ndani ni ya ndani, hivyo tunakaa kimya tu na kuwashangaa, alisema mfanyakazi wa kasino iliyo katikati ya Jiji la Dar es Salaam. Mfanyakazi mwingine wa kasino hiyo alisema aliukuta wizi wa aina hiyo katika kasino za Kampala, Uganda, lakini baadaye akaona ukiigwa na machangudoa wachache nchini na kuchukulia kuwa jambo la kawaida. Sasa unatarajia nini, mtu kaacha mkewe au mumewe nyumbani na kuja kusaka changudoa kwenye kasino, acha aleweshwe, tena sasa hivi wanakoleza chuchu tu na kujizolea fedha. Wengine bila aibu wanatutuma tuwashawishie wanawake hao na sisi tunafikisha ujumbe, kwa sababu tunaamini bila wao (machangudoa) biashara haichangamki na ukifuatilia kwa undani, utagundua kuwa hiyo ndiyo sababu inayofanya wasifukuzwe na uongozi wa kasino wanayoingia, licha ya kujulikana kuwa ni wezi, alisema mfanyakazi huyo. Mikoa inayotajwa kuongoza kwa matukio ya aina hiyo ingawa hayajaripotiwa ni Mbeya hasa wilayani Kyela na Chunya, Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Mwanza, Singida na Arusha. Chanzo:Polisi yahadharisha wapenda ngono