Polisi `wanapotengeneza` ajali Songea hadi Mbambabay!

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
Ninalizungumzia eneo lenye uwakilishi wa wabunge kupitia chama tawala- Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Na katika hali ya kustaajabisha, miongoni mwa walio wabunge hao, si tu kwamba ni wawakilishi wa wananchi, bali wana ushawishi na nyadhifa za juu katika chama tawala, serikali na Bunge!

Yupo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mbunge wa Songea, Dk Emmanuel Nchimbi na Mkurugenzi Mkuu wa kikundi cha uhamasishaji cha CCM-Tanzania One Theatre (TOT), Kepteni John Damian Komba, Mbunge wa Mbinga Magharibi.

Pia yupo Mwenyekiti wa Bunge, Jenista Mhagama ambaye unapotoka mjini Songea na kufika eneo la Likuyu, unaelekea jimboni kwake. Barabara ni hiyo hiyo, inayotokea na kwenda kwa `vigogo’ hao.

Katikati ya viongozi na wawakilishi hao, unakuta lipo jeshi la polisi ambalo kwa mujibu wa sheria na kanuni, lipo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inayoongozwa na Dk Nchimbi. Nitajadili.

Kwa muda mrefu sasa, kumekuwa na ajali za nchi kavu na majini, zinazozidi kuchukua uhai wa watu na upotevu wa mali zinazosadikiwa kuwa katika thamani ya mabilioni ya Shilingi.

Ipo dhana iliyozoeleka kila vinapotokea vifo, watu ‘wanaangukia’ kusema, ‘ni mapenzi ya Mungu, Mungu alipenda, kazi ya Mungu haina makosa…’ na nyingine nyingi.

Ni kweli anapoamua Mwenyezi Mungu, hakuna mwenye nguvu ama mamlaka ya kuzuia, bali inatokea kwa kadri ya mapenzi yake yanayostahili na kupaswa kutumia.

Lakini yapo yanayotokana na uzembe wa kibinadamu, mengine yakitokana na sababu za hovyo zinazowahusisha watu wa hivyo hivyo kuzua mambo ya hovyo kama vifo vinavyotokana na ajali.

Hivi karibuni nilisafiri kwa kutumia usafiri wa umma, kutoka mjini Songea hadi Mbambabay. Ilinichukua takribani saa tisa njiani, kupitia barabara ambayo kwa sehemu kubwa haina lami.

Ukosefu wa lami haikuwa tatizo kwangu, kwa maana yapo maeneo mengi ya nchi yaliyo katika hali hiyo, na inapohojiwa, jawabu linakuwa rahisi kutoka kwa walio kwenye mamlaka husika, ‘suala hilo linashughulikiwa.’

Kilichonistua na kunisononesha kwa asilimia mia, ni uzembe unaofanywa na askari wa usalama barabarani baarufu kama trafiki, hali inayoweza kuibua huzuni iliyo kuu itakayotokana na ajali zitakazolitikisa nchi!

Unaposafiri kati ya Songea na Mbambabay, ukakutana na askari hao, kisha ukashuhudia jinsi abiria ‘wanavyosindikwa’ ndani ya basi, utashangaa, utasononeka, utashindwa kujiuzua kuhoji.

Mabasi yenye uwezo wa kuchukua abiria 55 hadi 60 yanabeba abiria wanakisiwa kuwa zaidi ya 120, yaani zaidi ya mara mbili ya uwezo wake.

Sitaki kuzungumzia kero ya upungufu wa mabasi yanayotoa huduma za usafiri kati ya maeneo hayo, kwa maana huo ni mjadala mwingine.

Lakini iwe iwavyo, hakuna sababu inayoweza kutumika kuhalalisha uovu kama kasumba na mazoea ya mabasi yanayosafiri kati ya Songea na Mbambabay, kujaza abiria ‘kupindukia’.

Unapowatazama watu ‘walioshonana’ wakiwemo watoto wadogo wasiokuwa na tiketi, lakini basi husika likapita kwenye vizuizi vya askari wa usalama barabarani pasipo kuchukuliwa hatua, unahoji, jeshi hili lina mamlaka ya kidaadili?

Unaweza kuhoji, hivi askari wa usalama barabarani waliopo kati ya maeneo hayo, walipitia mafunzo maalum pale Chuo Cha Polisi Moshi (CCP) na baadaye kusomea usalama barabarani?

Ama walikuwa wameketi vijijini kwao, wakiota moto na kuchoma mahindi ama kufanya shughuli yoyote, kisha wakachukuliwa tu na kuajiriwa moja kwa moja kwa ajili hiyo!

Kwa maana haiwezekani kwa askari wa usalama barabarani kama waliopo kati ya Songea na Mbambabay, washuhudie uvunjifu wa sheria na kanuni za sekta hiyo, wabaki ‘wanafumba macho’, ili iweje?

Basi lililobeba abiria ‘kupindukia’, linapopita mbele ya askari wa usalama barabarani, kisha abiria waliosimama, wakatangaziwa wachuchumae, halafu basi likaruhusiwa kuondoka, inatoa ‘picha’ gani kama si mazingira ya kuwepo rushwa?

Mabasi yanayojaza kupindukia, yakiwa katika hali isiyokuwa ya kuridhisha kwa ubora katika utoaji huduma ya usafiri, yanapita kwenye maeneo hayo yenye milima na mabonde.

Jiografia ya barabara hiyo inajijenga katika vilima, mitelemko na mabonde ambapo kila basi linapokuwa safarini, muda mrefu inakuwa kila abiria ‘kuililia’ nafsi yake, kwa maana wakati wowote linaweza kutokea la kutokea.

Hapo ndipo viongozi hasa wa serikali wakiwemo mawaziri kama Nchimbi, watabaki kutuma salaama za rambirambi na vyombo vya habari kuripoti, ‘fulani awalilia marehemu wa ajali Songea’! Aibu tupu!

Uzembe unaofanywa na askari wa usalama barabarani kati ya Songea na Mbambabay ni sawa na kushiriki kutengeneza ajali, kwamba pamoja na imani iliyojikita katika ‘ajali haina kinga’, lakini kwa wingi wa abiria unaweza kuwa sababu ya kizembe.

Sababu ya kizembe inayoshindwa kudhibitiwa na watendaji wazembe inaweza kusababisha ajali ya kizembe inayokamilisha kupoteza maisha ya watu na mali zao.

Kwa nini tunafikia huko? Nani wa kuwawajibisha askari wanaoshiriki uzembe unaotoa mwanya kwa mabasi yanayotoa huduma ya usafiri kati ya Songea na Mbambabay, kujaza abiria kupita uwezo wake?

Tuziepuke ajali kwa kudhibiti uzembe kama unaofanywa na baadhi ya askari wa usalama barabarani waliopo kwenye barabara hiyo.

Vinginevyo, uzembe wao utakuwa mauti kwetu.

Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE
. Anapatikana kupitia simu namba +255 754 691540, 0716635612 ama barua pepe; mgeta2000@yahoo.com.






CHANZO: NIPASHE

 
Back
Top Bottom