Pierre alikuwa Burundi, na Burundi ilikuwa Nkurunziza; Shetani mstaarabu na malaika pekee atakaye kumbukwa

Comred Mbwana Allyamtu

JF-Expert Member
Jun 28, 2016
348
847
PIERRE ALIKUWA BURUNDI, NA BURUNDI ILIKUWA NKURUNZIZA; SHETANI MSTAARABU NA MALAIKA PEKEE ATAKAYE KUMBUKWA.

Na. Comred Mbwana Allyamtu.
Thursday-18/06/2020
Arusha City, Arusha - Tanzania.

Taifa la Burundi ni nchi iliyokuwa ikiongozwa kifalme toka huko nyuma mpaka pale ufalme ulipo koma rasmi tarehe 28/11/1966, pale mfalme wa mwisho Ntare V Ndizeye alipo pinduliwa na mnadhimu mkuu wa jeshi kipindi hicho Kanali Michel Micombelo, na kuifanya Burundi kuwa jamuhuri rasmi tarehe 29.11.1966.

Mfalme wa kwanza wa Burundi aliitwa Ntare I Kivimira Savuyimba Semunganzashamba Rushatsi Cambarantama ambae alikuwa mfalme wa Burundi toka mwaka 1680 hadi 1709, alikuwa ni mtu kutoka ukoo wa nasaba ya Ntwero, ndio mtu anayetajwa kuwa mfalme wa kwanza wa Burundi, hata ikulu mpya ya nchi hiyo iliyo jengwa hivi karibuni imepewa jina la "Ntare Rushatsi" kuenzi heshima yake.

Kihistoria Burundi ilianzisha utawala wake rasmi mwaka 1680 na Mfalme Ntare I Kivimira Savuyimba Semunganzashamba Rushatsi Cambarantama akawa mfalme wa nchi hiyo ambayo kipindi hicho iliitwa Urundi, ufalme huo ulitawala Burundi kutokea mji wa kifalme uliyo itwa Muravya, ambao ni eneo la makazi rasmi ya wafalme (Mwami) wa Burundi.

Hivyo basi......

Huyu Ntare Rushatsi Cambarantama historia na simulizi inaeleza ni mtu kutoka Buha (Kigoma ya sasa), kutoka huyu Ntare l Rushatsi Cambarantama mpaka Ntare V Ndizeye Mfalme wa mwisho wa Burundi wamepita jumla ya wafalme (Mwami) 17 nchini Burundi, yani toka mwaka 1680 mpaka tarehe 28.11.1966.

Kwahiyo sasa......

Ufalme wa Burundi uliendelea kuimarika na kuenea eneo kubwa zaidi kipindi cha ufalme wa Mwami Ntare IV Rutaganzwa Rugamba aliyetawala tangu mwaka 1796 hadi 1850, mfalme huyu aliweza kupanua mipaka ya ufalme wake hadi kushika sehemu kubwa ya eneo la leo ambalo tunaiona Burundi ya sasa.

Hivyo basi...........

Wazungu wa kwanza waliofika Burundi walikuwa ni wapelelezi kutoka Uingereza ambao ni Richard Burton na John Hanning Speke ambao waliwasili eneo la ufalme wa Urundi mwaka 1854, wapelelezi hawa awakuandika chochote kuhusu utawala huu wa Urundi, hata baada ya Mkutano wa Berlin mwaka 1885 Wajerumani ambao walichukua Burundi ikiwa ndani ya koloni lao la Tanganyika, hawakujua ya kwamba falme za Burundi na Rwanda zilikuwepo ndani ya eneo walilotengewa kulitawala, walikuja kulitambua hilo baadaye.

Hivyo...........

Mwaka 1894 Mjerumani wa kwanza kabisa kufika Burundi alikuwa ni Oskar Baumann, huku kikosi cha kwanza kabisa cha ulinzi wa majeshi ya Ujerumani kiliwasili Burundi mwaka 1896, mkoa huo wa kaskazini wa Ujerumani waliuteua kuwa chini ya mwakilishi mkazi (Representative resident) katika mji wa Gitega ambaye hakuhusika na mambo ya utawala wa ndani.

Wakati ule eneo hilo la Burundi lilijulikana kwa jina la "Urundi", eneo hilo lilikuwa ni mkoa wa kaskazini wa koloni la Ujerumani ulio jumuisha ndani Rwanda (Ruanda) na Bukoba chini ya eneo la Tanganyika.

Kwahiyo..........

Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, Burundi pamoja na Rwanda ilikabidhiwa kwa Ubelgiji kwa niaba ya Umoja wa mataifa baada ya Ujerumani kunyang'anywa kama adhabu ya vita, eneo hilo alikabidhiwa Ubelgiji likiwa linaitwa Ruanda-Urundi, kimsingi Wabelgiji nao waliendelea na mfumo wa Wajerumani walio uacha wa kumwachia Mwami mamlaka makubwa, Ubelgiji waliiweka Ruanda-Urundi chini ya serikali ya Kongo ya Kibelgiji, hivyo maamuzi yote ya uongozi yalitoka Léopoldville (sasa Kinshasa).

Lakini baadaye walianza kuweka wawakilishi wao Bujumbura (wakati huo ikiitwa Usumbura) na kuingilia zaidi mambo ya utawala na uchumi huku wakiwapendelena sana jamii ya Watutsi ambayo ndiyo ilikuwa ikitoa wafalme yani mwami nchini humo, hivyo Wabelgiji waliwapendelea zaidi Watutsi na kupalilia zaidi chuki za kikabila, jambo hili lilikuja kuzaa matabaka ya kijamii baina ya Watutsi na Wahutu mpaka kipindi cha harakati za uhuru liliendelea kuwagawanya Warundi na kuzidisha uhasama wa kikabila kati ya makabila hayo mawili.

Sasa basi...........

Tangu uhuru, Burundi imeongozwa na watawala 10 (wafalme 2 na marais 8), Saba kati ya hawa 10 tayari wamekufa, na 3 bado wanaitumikia serikali kama maseneta wa kudumu, na 4 wamekufa, 5 wamekufa nje ya nchi wakati 2 wamemefia nchini Burundi, kati ya hao 10, ni 5 waliozikwa nchini Burundi na 1 alizikwa nje ya nchi, huku 1 hakuna mtu anayejua kaburi lake mahali lilipo.

Wakati Burundi inapata uhuru siku ya Jumatatu Julai 1962 ilikuwa inaongozwa na Mfalme Mwambutsa IV Bangiricenge, miaka mitatu tu baadaye, yani usiku wa Oktoba 18-19, 1965, kasiri la Mfalme Bujumbura lilishambuliwa na askari ambao walikuwa wanajaribu kumuua mwami katika jaribio la mapinduzi, Mungu alimlinda Mfalme Mwambutsa IV Bangiricenge hawa kufanikiwa kumuua, akatoroka kwa msaada wa askari wengine.

Baada ya shambulio hilo, Mfalme Mwambutsa alitoroka na kwenda Uswizi, kwanza alitorokea Dar es Salam ambapo ndipo alipo pata usaidizi wa kuelekea Uswizi.

Katika mapinduzi yale ya usiku wa tarehe 18 na 19 mwaka 1965 na ambacho wachambuzi wengi hawakielezi na hata ambacho Warundi wengi hawajui ni kwamba, Mfalme Mwambutsa IV Bangiricenge alipinduliwa na mwanae aliyeitwa Prince Samuragwa Karoli Ndizeye kwa msaada wa vikosi vilivyoongozwa na Kanali Michel Micombero.

Kwamba......

Mfalme Mwambutsa, ambaye alipinduliwa na mwanae hakuwahi kuiona tena Burundi hadi alipokufa Aprili 26, 1977 huko Geneva, Uswizi, ambapo alizikwa huko huko kwenye makaburi ya Meyrin, wakati Mfalme Mwambutsa IV Bangiricenge anakufa aliacha wosia ambao aliilalamikia nchi yake ya Burundi na utawala wa kijeshi juu ya kumsaliti kwa kumuua wanawe kipenzi Ludoviko Rwagasore (Waziri Mkuu wa kwanza wa Burundi) na mwanae Karoli Ndizeye kumpindua kwa kulaghaiwa na jeshi, kwa sababu hizo aliandika wosia kwamba iwapo atakufa basi asizikwe nchini Burundi.

Hata hivyo.......

Mnamo mwaka wa 2012, serikali ya Burundi ilitaka mwili wake urudishwe ili mabaki ya mwili wake uzikwe Burundi, serikali ya Uswizi ilikubali kufukua mwili kuurejesha Burundi, hata hivyo mwili ulifukuliwa na kukaa miezi kadhaa lakini baadae ukazikwa tena huko huko Uswizi, kufatia pingamizi kubwa kutoka kwa watetezi wa haki za umiliki wa wosia kudai kuwa aliacha wosia wa mwili wake usizikwe nchini Burundi hivyo walitaka uheshimiwe.

Huyo mfalme Mwambutsa IV Bangiricenge, alizaliwa Machi 13, 1911, na kufariki dunia asubuhi ya alhamisi ya tarehe 26.4.1977 akiwa na umri wa miaka 66.

Sasa.......

Huyu Prince Ndizeye nae alikuwa ni mtoto wa Mfalme Mwambutsa IV Bangiricenge, na alikuwa mdogo wa Prince Ludoviko Rwagasore kwa baba yake, Prince Karoli Ndizeye alichukua madaraka mnamo Julai 08, 1966 kwa kushirikiana na wanajeshi wakiongozwa na Kapteni Michel Micombero, hata hivyo Prince Karoli Ndizeye alifanikiwa kufanya mapinduzi ya kumuondoa baba yake mzazi ambayo alikuwa amelenga kumuua japo akumuua baada ya Mwami Mwambutsa IV kufanikiwa kutoroka.

Mnamo Jumatatu, Julai 1966, Karoli Ndizeye alitwaa ufalme wa Burundi kwa jina la Simba wa tano, yani Ntare V, wakati Mwami Ntare V Karoli Ndizeye akisimikwa ufalme alikuwa na umri wa miaka 19 tu, waswahili wanasema lenye shari lina laana, laana ya kumpindua baba yake kwa taama ikamrudia, kwani na yeye alipinduliwa miezi 4 tu toka asimikwe kuwa mfalme wa Burundi.

Jaribio la kumpindua Ntare V Karoli Ndizeye lilifanyika Novemba 28, 1966, alipokuwa katika ziara ya kikazi huko Léopoldville (sasa Kinshasa) Kongo, Mfalme Ntare V Karoli Ndizeye akiwa amepumzika katika hoteli iliyoitwa Maxwell hoteli jioni moja ya Novemba 28 alishambuliwa na askari wake wa ulinzi alie enda nao ziarani walio pokea maelekezo kutoka kwa Waziri Mkuu Kanali Michel Micombero.

Mpango wa kupinduliwa Karoli Ndizeye ulipangwa Bujumbura wiki mbili kabla na Kanali Michel Micombelo kwa kuwashirikisha maaskari kadhaa,(hili ntalieleza wakati mwingine katika makala itakayo muhusu mbabe wa mapinduzi Burundi Michel Micombelo), baada ya shambulio lile dhidi ya Karoli Ndizeye kule Kinshasa alifanikiwa kuwatoroka askari wake na kutoka Kinshasa, alikimbilia Brazaville kisha Logos alafu baadaye akakimbilia Ujerumani ambapo alipata hifadhi ya kisiasa huko.

Hivyo basi..........

Alipo kuwa huko Ujerumani alishughulisha na biashara, mwaka 1972 akaja Uganda kibiashara, wakati huo Uganda ya Idd Amin ilikuwa na urafiki na Michel Micombelo hivyo serikali ya Iddi Amin ikamkamata Ntare V Ndizeye Machi 1972, aliwekwa kizuizini kwa kosa la kupanga njama Uganda za kuipindua serikali ya Michel Micombelo nchini Burundi, hivyo Karoli Ndizeye March 23 akakabidhiwa kwa Rais Michel Micombero kule Bujumbura. Karoli Ndizeye alifungwa kwenye gereza lililo karibu na uwanja wa ndege wa Gitega katika mji wa Gitega.

Akiwa kizuizini aliteswa na kunyimwa chakula siku kadhaa mpaka alipo dhoofu kimwili akahamishiwa kwenye kambi ya makomando battalion ya 6 ambapo huko aliuawa kwa kupigwa risasi, ilikuwa ni Aprili 29, 1972, baada ya kuuwawa mwili wa Mfalme Ntare V haukuwahi kupatikana mpaka sasa wengine husema mwili wake ulikatwa katwa vipande na kutupiwa simba kama kitoweo, huku wengine wanasema alizikwa kwenye shimoni la pamoja huko Gitega, wengine pia wanasema mwili wake ulitupwa katika shimo la choo karibu na makao makuu ya kambi ya kijeshi batallon ya 6 mjini Gitega.

Huyu Mfalme Ntare V Karoli Ndizeye alizaliwa Desemba 2, 1947, na kuuwawa Aprili 29, 1972.

Turudi sasa Bujumbura.....

Wakati Burundi inapata uhuru mwaka 1962 kama nilivyosema huko nyuma ilikuwa inaongozwa na wafalme na mawaziri wakuu, waziri mkuu wa kwanza alikuwa ni Ludovick Rwagasole ambae aliuawa mwaka 1961 siku chache kabla ya sherehe za uhuru wa nchi hiyo, waziri Mkuu na kiongozi wa tatu wa nchi ya Burundi alikuwa ni Kanali Michel Micombero, aliyeingia madarakani Novemba 28, 1966 hadi Novemba 1976, alipo pinduliwa na Meja Jenerali Jean-Baptste Bagaza.

Huyu Michel Micombelo ndiye aliye upindua ufalme wa Ntare V Karoli Ndizeye na kuwa rais wa kwanza wa Burundi ambaye aliitangaza Burundi kuwa Jamhuri rasmi tarehe 29.11.1966, aliitawala Burundi kwa miaka 10 mpaka alipo pinduliwa mwaka 1976 na mjomba wake Meja Jenerali Jean-Baptste Bagaza, na kukimbilia mkoani Ngozi ambapo huko ngozi majeshi tiifu ya Bagaza yalimkamata na kumuamuru kuondoka nchini Burundi, Michel Micombelo alikimbilia nchini Somalia na kupewa hifadhi ya kisiasa na Rais Siad Barré.

Akiwa ukimbizini huko Somalia Micombero aliendelea kusoma uchumi katika chuo kikuu cha Mogadishu, baada ya kuhitimu masomo mwaka 1982, Micombero aliomba kurejea Burundi kuishi maisha ya kawaida, lakini Rais Bagaza lakata, Micombelo aliendelea kuishi huko Somalia mpaka mauti yalipo mfika Julai 16 1983.

Serikali ya Somalia iliomba kuurudisha mwili wa Micombero, ili uzikwe nchini kwake Burundi, lakini utawala wa Rais Jean-Baptste Bagaza ulikataa kuruhusu mwili wa Micombero kulejeshwa nchini Burundi, lakini baadaye Meja Jenerali Jean-Baptste Bagaza alikubali kwa masharti kwamba mazishi ya Micombelo yata hudhuriwa na watu wachache, na hakutokuwa na misa yoyote kitaifa, mwisho Micombero alizikwa nyumbani kwake katika wilaya ya Rutovu katika mkoa wa Bururi.

Hivyo basi................

Huyu Kanali Jean Baptiste Bagaza aliye pewa jina la "Igikunda Amaraso" yaani Mpenda damu, aliwekwa madarakani na serikali ya Ufaransa kwa sababu mwaka 1973 serikali ya Ufaransa ilimsaidia Major General Juvenile Habyalimana kumpindua Baba wa Taifa la Rwanda Gregory Kayibanda, hivyo Wafaransa walitaka kudhibiti mataifa yote yaliyokuwa yanazungumza kifaransa, hivyo wakaonelewa waweka vibaraka katika nchi za Rwanda na Burundi.

Jean Baptiste Bagaza alikuwa ni rais wa pili wa Burundi kuanzia mwaka 1976 mpaka mwaka 1987 huyu nae alipinduliwa na Major Pierre Buyoya, mbabe wa kivita na raisi wa kipindi kirefu nchini Burundi, huyu alikuwa raisi wa wa Burundi kuanzia mwaka 1987 baada ya kumpindua Jean-Baptste Bagaza mpaka mwaka 1993 alipo shindwa kwenye uchaguzi Mkuu wa kwanza wa kidemokrasia nchini Burundi wa mwaka 1993 ulio muweka madarakani raisi Muhutu wa kwanza Melchior Ndadaye.

Hata hivyo................

Baadae mwaka 1996 Pierre Buyoya alirudi tena kutawala Burundi kijeshi baada ya machafuko ya kisiasa nchini humo kufuatia kifo cha Melchior Ndadaye tarehe 21/10/1993.

Uchaguzi wa rais wa mwaka 1993 ulio muingiza Melchior Ndadaye madarakani ulifanyika kufatia msukumo wa muda mrefu wa kushika madaraka na kusababisha machafuko ya mara kwa mara baina ya Watutsi na Wahutu, ilibidi Rais Pierre Buyoya aitishe uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi nchini Burundi mwaka 1993 ili Warundi wamchague Rais wanayemtaka.

Katika uchaguzi huo Pierre Buyoya wa chama tawala cha cha muda mrefu UPRONA ambaye alikuwa anatetea kiti chake, aliangushwa na Melchior Ndadaye wa chama cha FRODEBU kwa kupata 32% dhidi ya 65% alizopata Ndadaye, Melchior Ndadaye akawa Rais wa kwanza Mhutu na Rais wa kwanza aliyechaguliwa kidemokrasia nchini humo.

Lakini.............

October 21 mwaka 1993 likafanyika jaribio la mapinduzi lilo beba uasi ndani yake, Melchior Ndadaye akauawa katika mapinduzi yaliyoongozwa na wanajeshi wa battalion ya11 mjini Bujumbura iliyokuwa ikiongozwa na wanajeshi wengi watutsi, Mapinduzi hayo yalisababisha kifo cha Melchior Ndadaye na viongozi kadhaa 16 walio kuwepo ikulu siku hiyo pamoja na kupelekea vifo vya watu zaidi ya 100,000 wengi wao wakiwa Wahutu.

Baada ya Melchior Ndadaye kuuawa François Ngeze akateuliwa kuwa Rais wa mpito wa nchi hiyo, akaongoza kwa siku sita tu na kukabidhi madaraka kwa mwanamama Sylvie Kinigi aliyekuwa Waziri Mkuu kwenye serikali ya Melchior Ndadaye, Kinigi nae akaongoza kwa miezi minne hadi February 1994 akakimbia kufatia vitisho vya kuwawa, kufatia hali hiyo Bunge la nchi hiyo likapiga kura na kumpitisha aliyekuwa Waziri wa kilimo Cyprien Ntaryamira kuwa Rais wa mpito kuongoza nchi hiyo ili kuivusha kwenye mkwamo wa kisiasa.

Cyprien Ntaryamira akaongoza kwa siku 60 tu kabla ya kuuawa baada ya ndege aliyokuwa amepanda na mwenzie Juvénal Habyarimana wa Rwanda kutunguliwa mjini Kigali usiku ule wa April 06 mwaka 1994 wakitokea Arusha kwenye usuluhishi, baada ya kuuawa kwa Ntaryamira, ilibidi Spika wa bunge la nchi hiyo Sylvestre Ntibantunganya aapishwe kuwa Rais aongoze hadi uchaguzi mwingine utakapofanyika, lakini nae alipinduliwa July 2 1996 na mbabe wa mapinduzi nchini Burundi Meja Jenerali Pierre Buyoya aliye tawala mpaka mwaka 2002 alipo lazimishwa kujiuzulu kumpisha Domitien Ndayizeye ili aunde serikali ya mpito kufatia makubaliano ya kuanza mazungumzo ya amani ya kumaliza machafuko ya muda mrefu nchini Burundi, yaliyo kuwa yakisimamiwa na Tanzania

Katika kipindi hiki ndio Pierre Nkurunzinza aliibuka na kujulikana kwenye siasa za nchini Burundi, Pierre Nkurunziza aliibuka baada ya kuzaliwa kwa vikundi kadhaa vya kiasi vilivyo kuwa vinaongoza mapambano dhidi ya Watutsi ili kuwakomboa Wahutu nchini Burundi, huyu Nkurunziza alikuwa ni askari wa kikosi cha waasi cha CNDD, kilicho anzishwa wa Leonard Nyangoma akishirikiana na Hussein Radjab mwaka 1994, waasi hawa waliweka ngome yao huko Uvira, kwenye jimbo la Kivu ya kusini mashariki mwa DRC, kikundi hicho mwanzoni kilipo anza kilikuwa na askari zaidi ya 30,000 na kilikuwa na nguvu sana kulinganisha na vikundi vingine vya waasi kama FNL-Perpehutu.

Hivyo basi...............

Pierre Nkurunziza alijiunga na kikosi cha waasi cha CNDD kwa mara ya kwanza August 1995, wakati huo Nkurunziza alikuwa na umri wa miaka 31.

Pierre Eustache Ngabisha Nkurunziza ni nani?..........

Pierre Nkurunziza alikuwa ni Mhadhiri msaidizi (Assistant Lecturer) kwenye Chuo kikuu cha Bujumbura (Kiriri university) kabla ya kuingia kwenye kundi la waasi la CNDD, lakini alipoteza kazi kufuatia machafuko ya mwaka 1993 baada ya kuuawa kwa rais wa kwanza Muhutu Melchior Ndadaye.

Pierre Nkurunziza alizaliwa tarehe18 Desemba 1963, mjini Bujumbura katika familia ya kabila la Wahutu, wenye asili ya mkoa wa Ngozi, Nkurunziza alisoma shule ya msingi kwenye mkoa wa Ngozi, baba yake aliitwa Eustache Ngabisha ambae aliwahi kuwa mbunge tangu mwaka 1965 hadi mwaka 1970, Mwaka 1971 baba yake Nkurunziza aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa (Gavornor) huko Gatara kaskazini mwa Burundi, Lakini aliuawa kwenye mapigano ya mwaka 1972 wakati wanajeshi wa kihutu walipojaribu kuipindua serikali ya Micombero na kusababisha machafuko yaliyo pelekea Warundi wapatao 400,000 wengi wao wakiwa Wahutu kupoteza maisha.

Nkurunziza alilelewa pamoja na ndugu zake wengine 7 watano kati yao waliuawa wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe ya mwaka 1993, na kubakiwa na dada yake 1 tu.

Kwahiyo sasa............

Wakati Pierre Nkurunziza anajiunga na waasi wa CNDD alikuwa na uchungu wa kuipoteza familia yake kutoka na chuki za kikabila baina ya Watutsi na Wahutu, alipo sajiliwa kwenye kikosi cha waasi cha CNDD alianza kama kuruta kwenye kikosi cha mapigano cha CNDD, kutokana na elimu yake nzuri na bidii jeshini alipanda vyeo haraka hadi kufikia Kanali ndani ya muda mfupi.

Hadi mwaka 2000 Nkurunziza alikuwa ni miongoni mwa viongozi waandamizi wa CNDD, hivyo februari 17 alimuita Evariste Ndayishimiye rafiki yake na mwanafunzi wake aliye mfundisha Chuo kikuu cha Bujumbura kujiunga na CNDD, hata hivyo mwaka 2000 ulitokea mpasuko ndani ya CNDD, viongozi wa juu walipishana mitizamo, Leonard Nyangoma alitaka kikundi hicho kilinde maslahi ya wahutu tu, lakini Hussein Radjab alitaka maslahi ya watutsi pia yazingatiwe ili kikundi hicho kiungwe mkono na pande zote mbili yani Wahutu na Watutsi.

Lakini hawakukubaliana, hivyo Nyangoma alidai kuwa falsafa ya kikundi hicho ilikua kupigania wahutu na si watutsi, Kufuatia mvutano huo kikundi hicho kiligawanyika na kuzaliwa vikundi viwili, yaani CNDD kilichoongozwa na Leonard Nyangoma mwenyewe kikiwa na askari 8,000, na CNDD-FDD kilichoongozwa na Hussein Radjab kikiwa na askari 22,000, kutokana na mpasuko huo Pierre Nkurunzinza na kijana wake Evariste Ndayishimiye wakachagua kujiunga na CNDD-FDD cha Hussein Radjab.

Toka hapo kikosi cha waasi cha CNDD-FDD kiliendelea kupata nguvu na uungwaji mkono mkubwa kutoka makundi mbalimbali ya watu na wanasiasa wakubwa nchini Burundi, wakati wa mazungumzo ya amani mjini Arusha yaliyo anza mwaka 2001 awali CNDD-FDD ilikataa kushiriki, lakini mwaka 2004 ilikubali kushiriki kuunda serikali ya mpito ya nchi hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Domitien Ndayizeye.

Hivyo basi.............

Viongozi wa juu wa kikundi hicho ikabidi wakae na kukubaliana namna ya kugawana madaraka, Ndayishimye akapangwa kuwa Mnadhimu Mkuu wa jeshi katika serikali ya mseto, Adolphe Nshimirimana awe Mshauri wa Rais kuhusu ulinzi, Hussein Radjab awe mgombea Urais kwenye uchaguzi wa 2005 na Pierre Nkurunzinza awe Mwenyekiti wa chama, kwa kuwa CNDD-FDD ilikuwa ina-transform kutoka kwenye kikundi cha waasi kwenda chama cha siasa, Hussein alikataa kuwa mgombea Urais, Alitaka aendelee kuwa Mwenyekiti wa chama angalau kwa miaka mitano ndipo agombee Urais.

Kwahiyo basi...................

Nafasi ya urais alimpa Pierre Nkurunziza kwa makubaliano kuwa yeye akijenge kwanza chama na Pierre agombee urais, na baada ya miaka mitano Pierre arudi kujenga chama na Hussein agombee urais, mpango ukakamilika na wakatoka msituni, askari wote 22,000 waliokuwepo msituni wakapewa nafasi katika jeshi la nchi hiyo katika mchakato wa kuchanganya majeshi kuunda jeshi la umoja wa kitaifa.

Lakini baada ya Pierre kushika madaraka akanza mzozo na Hussein Radjab, Mwenyekiti wake wa chama, Mwaka 2007 akaagiza Hussein Radjab akamatwe kwa madai kuwa katika moja ya hotuba zake alimkashifu na kumuita chupa tupu, Hussein Radjab akakamatwa na kushtakiwa, mwaka 2008 alipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka 13 jela, akafungwa katika jela ya Mbimba iliyopo jijini Bujumbura.

Mwaka 2010 Pierre aligombea na kushinda kwa awamu ya pili wakati Hussein Radjab akiwa jela, Lakini mwaka 2015 alipokuwa anakaribia kumaliza muhula wake wa pili Hussein Radjab alitoroka gerezani, Inadaiwa alitoroshwa na jeshi la nchi hiyo japo jeshi lilikanusha madai hayo, Mpaka leo haijulikani alitorokaje katika gereza hilo lililokua na ulinzi mkali sana, baadhi usema kuwa kutoroka kwa Hussein Radjab ilikiwa ni mbinu ya Nkurunziza, ili atakapo toroshwa na jeshi akiwa nje huko ufichoni auwawe ili kuweza kuondoa kikwazo hicho, japo fununu hizi azijawahi kupatiwa ushahidi popote.

Pierre Nkurunziza iligombee kwa awamu ya tatu kwenye uchaguzi wa mwaka 2015, Pamoja na kupata upinzani mkubwa ndani na nje ya nchi yake lakini aligombea, taarifa zinaeleza kuwa alihofia Hussein anaweza kuwa Rais wa nchi hiyo na kulipiza kisasi, Hivyo ili kujiweka salama ilimlazimu kugombea tena na kuendelea kubaki madarakani.

Mwaka 2015 lilifanyika jaribio la mapinduzi Pierre akiwa ziarani nchini Tanzania, inadaiwa jaribio hilo lilikua na mkono wa Hussein na liliongozwa na Mnadhimu mkuu wa Jeshi la nchi hiyo Meja Jenerali Godefroid Niyombare ambaye huko nyuma amewahi kuwa Mkurugenzi wa shirika la Ujasusi la Burundi (SNR), Lakini jaribio hilo lilizimwa na Niyombare alikamatwa na kuwekwa kizuizini huko Bujumbura, baadhi ya askari walioshiriki jaribio hilo waliuawa, Hussein Radjab mwenyewe alikanusha kuhusika kivyovyote vile na tukio hilo alipohojiwa na gazeti la Liberation la nchini Ufaransa.

Mwaka 2016 Hussein alihojiwa na BBC na kusema anaendesha vuguvugu la kudai mabadiliko akiwa nje ya nchi hiyo, hata hivyo inadaiwa Pierre alijiapiza kuwa hataondoka madarakani hadi amtie mbaroni Hussein Radjab.

Utawala wa Pierre umeshutumiwa kwa matumizi ya nguvu na kuongoza nchi hiyo kwa mkono wa chuma, December mwaka 2015 shirika la Human Right Watch liliripoti mauaji ya kinyama ya wakosoaji wa serikali, taarifa hiyo ilisema baadhi ya wakosoaji wamekuwa wakikatwa shoka kichwani, au kuchomwa moto wakiwa hai na kisha kuzikwa katika makaburi ya pamoja, March mwaka 2016 makaburi kadhaa ya halaiki yaligundulika nchini Burundi lakini serikali ilikanusha tuhuma za kutesa watu, kuwaua na kuwazika humo.

Shirika la kutetea haki za binadamu la IPHR la nchini Ubelgiji linadai kuwa watu zaidi ya 600,000 wamegeuka wakimbizi kipindi cha utawala wa Pierre, vifo zaidi ya 20,000 vimetokea na familia zaidi ya 1,000 zimepoteza ndugu zao ambao hadi leo hawajulikani walipo, kikosi cha chama cha CNDD-FDD kiitwacho Bonalikule kinalaumiwa kutekeleza mauuaji ya raia na watu walio mpinga raisi Pierre Nkurunziza.

Hii Bonalikule iligeuka kuwa dola, ilitumiwa na Nkurunziza kuwa nyamazisha wapinzani wake wa ndani ya chama na nje ya chama, baadae Nkurunziza aliwashughulikia viongozi wote wa juu wa chama chake cha CNDD-FDD alio wakuta msituni mwaka 1995 kutia ndani Adolphe Nshimirimana aliye uwawa na vikosi vya usalama wa Burundi mwaka 2018 Nyumbani kwake, kwa kutuhumiwa kumsaliti Pierre Nkurunziza.

Hata hivyo............

Burundi walifanya uchaguzi Mkuu siku ya Jumatano ya tarehe 20.05.2020, uchaguzi ule ulikuwa ni hatua nzuri katika afya ya demokrasia ya Burundi lakin wachambuzi wengi waliona uchaguzi ule kutokuwa na matumaini kwa Warundi, Uchaguzi huo ulikosa matumaini kwa sababu ulibeba sura ya maigizo, dhahiri ni uchaguzi uliofanyika kutuliza munkari ya kidiplomasia kuliko kutii matakwa ya wananchi au kwa ajili ya masilahi ya Warundi.

Kwanini nasema hivyo...................

Ni kwasababu sehemu kubwa ya uchaguzi ule ulibeba sura ya maridhiano kati ya masilahi ya Rais anayemaliza muda wake, Pierre Nkurunziza na diplomasia ya Burundi kwenye uso wa kimataifa, ili ionekane angalau Burundi inafanya uchaguzi wa kidemokrasia.

Iko hivi................

Kabla ya uchaguzi wenyewe kufanyika tarehe 20 may 2020, miezi 4 nyuma yani Januari 21, mwaka huu, Bunge la Burundi lilipiga kura na kupitisha kwa asilimia 98 mambo makuu manne ambayo ni *Mkataba mnono kwa raisi Nkurunziza* (marehemu kwa sasa).

Mambo hayo ni.....

1-, Nkurunziza atalipwa kiinua mgongo dola 530,000 (sawa na Sh1.22 bilioni) mara baada ya kuondoka madarakani.

2-, Nkurunziza atalipwa mshahara wa Urais maisha yake yote, kwa sasa mshahara wa Rais wa Burundi unaotambulika ni dola 47,000 (Sh108 milioni) kwa mwaka, hivyo Nkurunziza alitaka kila mwezi alipewa Sh9 milioni. Hata hivyo, inadaiwa kiasi hicho kinatamkwa kimaigizo tu, kwani malipo ya urais Burundi yana posho nyingi ambazo haziandikwi, hili Iilipitishwa kisheria kuwa mshahara huo uwe wa milele, utawahusu marais wastaafu watakaongia madarakani kwa njia ya kidemokrasia.

3-, Nkurunziza atajengewa makazi ya kifahari ambayo ataishi miaka yote baada ya kuondoka madarakani, pamoja na kwamba haikufafanuliwa kwenye muswada uliopitishwa kuhusu aina ya makazi ya kifahari atakayojengewa Nkurunziza, lakini inanong'onwa kuwa Nkurunziza ametaka yawe yenye kukaribiana na Ikulu ya Burundi.

Inaelezwa kuwa Nkurunziza hakupendekeza makazi yake yawe na ukubwa kama Ikulu mpya, lakini angalau yakaribie.

4-, ilipitishwa kuwa baada ya Nkurunziza kuondoka madarakani, hataitwa Rais Mstaafu, bali atafahamika kama Kiongozi Mkuu wa Nchi (The Supreme Leader) au Muongozaji Mkuu (The Supreme Guide), cheo hicho ni kikubwa mno, mfano wa karibu wa nchi yenye Rais na Kiongozi Mkuu ni Iran, Kuna Rais ambaye ni Mkuu wa Serikali na Ayatollah (the supreme leader) ambaye ni Mkuu wa Nchi na mwamuzi wa mwisho kuhusu nchi.

Kwa kawaida, Kiongozi Mkuu wa nchi ndiye anakuwa Amiri Jeshi Mkuu, hivyo, endapo Nkurunziza atakuwa Kiongozi Mkuu wa Burundi mwenye mamlaka kamili, maana yake ataendelea kubaki kiongozi mwenye uamuzi wa mwisho kuhusu Burundi kama mfalme, ili kuhalalisha hilo mapema Machi 2018, mabadiliko ya Katiba ya chama tawala cha Burundi CNDD-FDD yalitambulisha cheo cha Kiongozi Mkuu wa chama na Nkurunziza alipitishwa kuwa kiongozi mkuu wa milele.

Katiba ya Burundi ya mwaka 2005, ilipitisha cheo cha Useneta wa milele kwa wakuu wa nchi wastaafu, Nkurunziza akaona useneta ni cheo kidogo, akapimdua meza akataka awe Kiongozi Mkuu wa milele nchini Burundi, ila kwakua Mungu apangiwi akampangua jumla Pierre Nkurunziza, baada ya kuwa kiongozi mkuu wa nchi, Mungu akamfanya kuwa buriani wa milele.

Pamoja na juhudi zote za Nkurunziza kutaka kusalia mamlakani kugonga mwamba baada ya Mungu kupangua, hatimae dunia ilitangaziwa ghafla kifo cha Pierre Nkurunziza tarehe 9/06/2020 kilicho tokana na shambulio la moyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya serikali ilisema kwamba Nkurunziza alifikishwa hospitali ya Karusi kwa ajili ya matibabu kufatia kudondoka alipo kuwa akitazama mechi ya mpira wa kikapu mkoani Karusi, muda wote huo toka kulazwa kwake kulikuwa na usiri mkubwa hadi taarifa ilipo tolewa rasmi tarehe 9.06.2020 kuutangazia umma kifo chake, duru za siri zilieleza kuwa Pierre Nkurunziza alifariki toka tarehe 8.06.2020 siku moja kwabla ya kutolewa taarifa rasmi.

Kifo cha Nkurunziza kimebaki na nadharia nyingi, wapo wanaodai kuwa kifo cha Nkurunziza kina uhusiano na Ugonjwa wa Covid 19 kwa sababu mke wake ana huo ugonjwa na mitaa ya uswahilini kama Buyenzi na Nyanzalac ndio habari inayo pewa kipao mbele, lakini pia wapo wanao amini kuwa kifo cha Nkurunziza kina tokana na shambulio la moyo kama irivyolipotiwa na serikali ya Burundi.

Pia wengine hudai kifo cha Nkurunziza kinatokana na ujasusi wa mrithi wake Evarist Ndayishimiye kamzimisha mapema kuepuka asimuingilie kiutawala kutoka na kile kilichoitwa "Mkataba mnono wa Nkurunziza na dola", lakin wengine uhusisha kifo cha Nkurunziza na kutimia Siku zake za mwisho hivyo huamini kwamba siku zake zimefika na hamna namna.

Lakini wengine uhusisha kifo cha Nkurunziza na kupewa sumu na majasusi kutoka Rwanda(Red Tabara) kutokana na uhasama kati yake na Jenerali Paul Kagame.

Wengi huipa nguvu hoja hii hasa kutokana na maelezo kadhaa kufichuliwa na Meja Gakwerere kutoka Rwanda, huyu Gakwerere ni afisa mstaafu wa kikosi cha usalama wa taifa wa Rwanda anae ishi uhamisho kufatia kutofautiana na raisi Paul Kagame.

Ngoja tuipe nguvu nadharia hii ya kupewa sumu tuone..............

Utawala wa Rwanda umekuwa na uhasama na utawala wa Pierre Nkurunziza kwa muda mrefu, tangu mwishoni mwa mwaka 2013, wakati Paul Kagame alipoamua kujihusha na siasa za Burundi, Serikali ya Nkurunziza iliishutumu Rwanda kupenyeza majasusi wake ili kufuatilia nyendo za Pierre Nkurunziza ikiwa ni pamoja na kupenyeza majasusi wa Rwanda kwenye taasisi za serikali ya Burundi.

Kwa mujibu wa Gakwerere anaeleza kuwa Burundi ilikuja kujua kuwa inachunguzwa na Rwanda baada ya kuzima mpango mkubwa wa kumwangamiza Nkurunziza wa tarehe 13 Mei, 2015 baada ya jaribio la mapinduzi kushindwa, ambalo lilitokea wakati Nkurunziza alipo kuwa na viongozi wenzake wa Afrika Mashariki, jijini Dar es Salam Tanzania ambapo viongozi hao Rais Jakaya Kikwete, Rais Museveni, Rais Peter Nkurunziza na Paul Kagame walikuwa wakijadili juu ya mkwamo wa kisiasa nchini Burundi.

Gafla zikaja taarifa za Nkurunziza kupinduliwa huko Bujumbura taarifa hizo viongozi hao walizipata wakati walipo kwenda mapumziko kwajili ya chakula cha mchana, Baada ya chakula cha mchana, waliporudi kuendelea na mkutano wao, kwa mshtuko wa viongozi wengine, Paul Kagame aliwaambia Rais Jakaya Kikwete na Rais Museveni kwamba Peter Nkurunziza sio tena Rais wa Burundi, hivyo Nkurunziza hatakiwi kuwa kwenye chumba cha mikutano kama kiongozi wa Burundi, Kagame alidai kuwa Nkurunziza amepinduliwa hivyo wangejadili muktadha wa kuyaunga mkono mapinduzi ya kijeshi nchi Burundi.

Wakati Kagame akiwashawishi maraisi wenzake wakubaliane na yale mapinduzi ya kijeshi nchini Burundi, pia Jenerali mstaafu James Kabarebe ambaye ndie alikuwa mpangaji na mratibu mkuu wa operesheni ya mapinduzi kule Burundi alikuwa amemuhakikishia bosi wake Paul Kagame kwamba operesheni hiyo imefanikiwa kutokana na kusukwa vyema na Brigedia Jenerali Willy Rwagasana ambae kwa sasa ni mkuu wa walinzi wa rais, ambapo wakati huo alikuwa Kanali Lt na mkuu wa kikosi cha karibu cha ulinzi wa Paul Kagame.

Hivyo basi............

Brigedia Jenerali Willy Rwagasana alikuwa akiwasilisha taarifa za mapinduzi ya kijeshi Burundi yaliyo kuwa yakiongozwa na Meja Jenerali Niyombare kwa bosi wake James Kabarebe alafu Kabarebe anampatia taarifa hizo Kagame kuhusu yale yaliyokuwa yakifanyika nchini Burundi.

Bila woga, wala aibu raisi Paul Kagame alisisitiza kwamba Rais Nkurunziza hawapaswi kuwa kwenye chumba cha mikutano, na mada iliyo paswa kuzungumza ni namna gani wamsaidie Nkurunziza juu ya jinsi gani ya Nkurunziza kuweza kuondoka kwa amani yeye na familia yake pasipo kudhuliwa na jeshi lakini mapendekezo yote ya Kagame Rais Jakaya Kikwete na Rais Museveni waliyakataa na kusisitiza kwamba Rais Nkurunziza bado ni rais halali wa Burundi, na jumuia ya Afrika Mashariki itahakikisha njama hizo za mapinduzi hazifaulu.

Baada ya kuona aungwi mkono Paul Kagame alisimama na kuwambia maraisi wenzake kwamba anaondoka kwakua wao wameshindwa kusikiliza kile ambacho Warundi wanataka, na wanaweza kuendelea na mazungumzo yao bila uwepo wake.

Paul Kagame na timu yake waliondoka kwenye chumba cha mkutano na kurejea Kigali kusherehekea mapinduzi ya Burundi, hata hivyo mapinduzi yale yalishindwa na Nkurunziza kurejea madarakani kama nilivyosema uko awali, toka hapo Kagame amekuwa akitumia shilika lake la kijasusi la DMI (Detective Military intelligence) kutaka kumuua Nkurunziza.

Mwaka 2015, duru za ndani zilimtaadhalisha Nkurunziza juu ya mipango ya kutaka kuuwawa kwake, taarifa hizo zilipenyezwa na maafisa usalama wa Urusi kwenda kwenye shirika la kijasusi la Burundi (SNR) Kuanzia mwaka 2015, kufatia taarifa hizo, walimuonya Nkurunziza kutokuondoka nchini na kuwa makini kwa kila hatua, hata hivyo Nkurunziza hakuwahi kuondoka Burundi isipokuwa mara moja tu yani tarehe 20 Julai 2017, alipo kutana na Rais John Magufuli wilayani Ngara, kaskazini magharibi mwa Tanzania, hii ilikuwa safari yake ya pekee nje ya Burundi tangu mapinduzi ya Mei 2015 yaliyoshindwa hadi siku anapoteza maisha.

Toka hapo shirika la kijasusi la Rwanda limekuwa likipenyeza ujasusi wake nchini Burundi mpaka subuhi ya Ijumaa, Mei 22, 2020, akaunti za vyombo vya habari vya kijamii zinazoendeshwa na Kurugenzi ya Ujasusi ya Rwanda (DMI) ilipo anza kuchapisha taarifa za mke wa Nkurunziza, Denise Bucumi Nkurunziza kuugua Covid 19 na kusafirishwa kwake kwenda Kenya, lakini pia Jumamosi, ya tarehe 23 Mei 2020, Rwanda ndio nchi ya Kwanza duniani kujua kifo cha Nkurunziza kabla hata ya Warundi wenyewe.

Pia Gakwerere anaeleza kuwa Kagame na serikali yake walipata taarifa za ugonjwa wa Nkurunziza mapema kuliko hata maafisa wa serikali ya Burundi.

Hivyo basi...............

Gakwerere anasema kuwa kifo cha Nkurunziza kinatokana na hujuma za kijasusi za Rwanda kutokana na Kigali kufahamu kwa undani yaliyokuwa yakiendelea katika ikulu ya Ntare Rushatsi kuliko hata maafisa usalama wa Burundi.

Kutokana na hoja hizo ebu tujiulize maswali yafuatayo kuhusu hizo nadharia zingine....................

1) Inawezekana vipi Nkurunziza kufa kwa mshtuko wa moyo kama inavyo elezwa na taarifa kutoka kwa serikali ya Burundi wakati Nkurunziza alikuwa ni mtu wa mazoezi ya mwili kila siku na wala hakuwahi kulalamika kuhusu tatizo la moyo maisha yake yote.

2) Inawezekana vipi Nkurunziza kufa kwa Covid 19? wakati yeye na familia yake walikuwa wanafanyiwa vipimo kila baada ya siku 4 kwenye ikulu ya Ntare Rushatsi.

Ukijiuliza maswali haya unaweza kuelewa hasa kifo cha Pierre Nkurunziza, Shetani mstaarabu na malaika pekee atakaye kumbukwa nchini Burundi ambae ameuacha mkataba mnono mno........

Lakini mwisho wa safari ndio mwanzo wa safari nyingine, hii ina maana kwamba mwisho wa safari ya Pierre Nkurunziza ndio mwanzo wa safari ya Meja Jenerali mstaafu Evariste Ndayshimie, sasa taifa la Burundi lipo chini ya Evariste Ndayshimie ama awe shetani mstaarabu au maraika muovu.

R.I.P Pierre Nkurunziza na Aluta Continua Meja Jenerali mstaafu Evariste Ndayshimie.

CREDITS/ACKNOWLEDGEMENTS
----------------------------------------------------------
1- Robert Patrick Fati Gakwerere kupitia blogi yake- rpfgakwerere.org.
2- Liquman Mloto kwenye andiko lake la Nkurunziza aacha uraisi ili awe mfalme.
3- Kjell Erickson, kitabu cha "The princess of Burundi"
4- History of Burundi since descent, Kelvin shillington.
5- The History of Africa by Kelvin Shillington.
6- The German East Africa Company, or Deutsch-Ostafrikanische Gesellschaft with dealing with German interests in Tanganyika, Burundi, and Rwanda. Maxwell Maurice.

Ukinakili kazi zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
Wako Mjoli wa Historia na diplomasia ya ulimwengu.

Ndimi: Comred Mbwana Allyamtu
Copyrights of this article reserved
written by Comred Mbwana Allyamtu
•Napatika Kwa mawasliano
Comred Mbwana Allyamtu
Kwa Tanzania
+255679555526.
+255765026057.

Kwa Rwanda
+250733153930
+250788214234

Kwa DRC
+243 977 860 824
Email- mbwanaallyamtu990@gmail.com

Copyright 2020, All Rights Reserved.

Maktaba Kuu
FB_IMG_1592497841225.jpeg
View attachment 1482833
FB_IMG_1592497617879.jpeg
IMG_20200618_232924_526.jpeg
FB_IMG_1592497739577.jpeg
FB_IMG_1592320983291.jpeg
FB_IMG_1592496368217.jpeg
Burundi-Briefing-3April2020.jpeg
FB_IMG_1592357643073.jpeg
 
Kitu kimoja kama hutojali epuka au punguza hizo.

Hivyo basi
Kwa hiyo

N.k nadhani unakumbukia miaka ile kidato cha pili tunafundishwa kuandika essays. Achana nayo. Tupe mtiririko wa kawaida.

Pili nakupa pongezi kufuatilia kwa ukaribu historia mbalimbali hasa hasa za afrika. Napenda sababu unapenda kujifunza na kushare na wengine.
 
Hapo Burundi ardhi ya nchi hiyo inaonekana huwa inapenda kunywa
damu...yaaani mimi hata wanifuate wanieleze kuwa wamenichagua niwe mtawala wa hilo taifa sikubali

wewe nchi gani. viongozi wanapinduana pinduana tu kama vile mchezo wa mieleka..mbaya zaidi. nawashangaa. hao waliokuwa wana kubali kuteuliwa. ili. wakaimu madaraka yaani kabisa unaona. mwenzio ametoka kupinduliwa na kuuwawa then unateuliwa ukaimu madaraka na wewe unakubali 😃
 
Hapo Burundi ardhi ya nchi hiyo inaonekana huwa inapenda kunywa
damu...yaaani mimi hata wanifuate wanieleze kuwa wamenichagua niwe mtawala wa hilo taifa sikubali

wewe nchi gani. viongozi wanapinduana pinduana tu kama vile mchezo wa mieleka..mbaya zaidi. nawashangaa. hao waliokuwa wana kubali kuteuliwa. ili. wakaimu madaraka yaani kabisa unaona. mwenzio ametoka kupinduliwa na kuuwawa then unateuliwa ukaimu madaraka na wewe unakubali 😃
Kagame anaisumbua east africa sana.
 
Back
Top Bottom