Nyuma ya pazia la uhalifu wa viongozi wa dini zanzibar

Status
Not open for further replies.

Jamhuri ya Zanzibar

Senior Member
Jul 17, 2012
126
195
  • Wazanzibari hawarudi nyuma katika agenda yao mbali ya vitimbi kadhaa.

Maridhiano ya wazanzibari hayakutoka Dodoma na kuna kila ushahidi kuwa hayakupata Baraka za Dodoma. Maridhiano ya wazanzibari hayakutoka kwa wahafidhina, maagenti wa Dodoma walioko Zanzibar na halkadhalika kuna kila aina ya ushahidi sio tu hayakupata Baraka zao lakini waliyapinga na wanaendelea kuyapinga kwa nguvu zao zote. Shabaha ya kupinga maridhiano ya wazanzibari na serikali ya Umoja wa kitaifa ni kujenga farka, fitna, chuki, ukabila, ugozi, chokochoko na uvunjifu wa umoja na mshikamano miongoni mwa wazanzibari ili shabaha ya wazanzibari kurejesha nchi yao yenye mamlaka kamili kitaifa na kimataifa isitimie. Lengo ni kwamba Dodoma (mkoloni mpya wa Zanzibar) aendelee kuitawala Zanzibar na maagenti wao (wahafidhina vibaraka wa Zanzibar) waendelee kujaza matumbo yao huku wazanzibari walio wengi wakiteseka ndani ya ardhi yao tukufu.

Lengo kuu la mtandao huu wa kupinga maridhiano ni kujaribu mbinu hii na ile ili kuizima nuru njema ya umoja wa wazanzibari ambayo ndio silaha pekee wanayoitegemea hivi sasa katika kuirejesha Jamhuri ya watu wa Zanzibar. Lengo ni lile lile linalopiganiwa kuwa wazanzibari wasambaratike, wagombane, wasiwe wamoja, wasiaminiane na wasisikilizane huku watanganyika wakiendelea kuiweka Zanzibar katika mikono yao. Wanamtandao wanafahamu kwamba wazanzibari wakiwa wamoja wanapata jukwaa la pamoja la kujadili na kusahau mawazo ya tofauti zao za kisiasa na huhisi machungu ya kudhalilika kwa nchi yao. Ukiwaondoa wazanzibari katika maelewano na umoja kwa kujenga mazingira ya kila upande uone bado sisi ni maadui kumbe baina yetu unafanikisha mpango wa kuwagawa katika agenda ya uhuru wao kutoka kwa watanganyika wanayoipigania.

Mbinu kubwa wanayotumia maadui hawa wa Zanzibar hivi sasa ni ile ya kuandaa matukio mbali mbali na kuyanasibisha matukio hayo na UAMSHO kwa upande mmoja na kwa upande wa pili wakifanya kila wawezalo kuziunganisha harakati za UASHO na zile za chama cha CUF na kuziundia harakati zote mbili picha ya uongo zionekane kuwa zipo chini ya mwamvuli mooja na amri moja. Lakini hebu tujiulize hivi hapa maadui hawa wa Zanzibar wamekuja na staili mpya? Haya ni mambo makongwe kabisa kwa Zanzibar ambayo yameshazoeleka. Kwa lugha nyengine hizi ni propaganda za kitoto kwa wazanzibari, hakuna jipya.

Siku ya tarehe 3 Machi 1996, enzi zile wazanzibari walipogawanywa na kutiwa chuki baina yao ilidaiwa na serikali kuwa mafiasa watatu wa usalama waliokuwa kwenye doria huko katika kijiji cha Shengejuu, kisiwani Pemba, walipigwa na kuporwa silaha na wanakijiji. Kwa sura ya kawaida ya uaskari ni vigumu kuaminika kwamba askari watatu wakiwa na silaha mikononi waporwe silaha zao wote watatu na wapigwe bila ya wao hata kujeruhi mtu yeyote au kujeruhiwa wao wenyewe. Muda sio mrefu, siku ya pili yake tu, kijiji hicho kilivamiwa na kiasi cha askari wapatao 300 wa kikosi cha FFU na jeshi la wananchi (JWTZ) waliokuwa wako kamili kivita. Unyama, mateso na vitendo vya kihuni walifanyiwa wananchi wa kijiji cha Shengejuu. Sio tu unyama huo walifanyiwa washukiwa, lakini pia mateso yaliwakuta watu wengi waliokuwa hawana hatia yoyote. Baadhi ya wanakijiji walipigwa hadi kuzirai, wengine waliibiwa mali zao kama vile kuku na mbuzi, maduka yaliporwa, wanawake walibakwa na watu wapatao 80 waliwekwa ndani. Kati ya watu hao 80, watu 30 waliachiliwa huru na waliobaki waliendelea kusota ndani kwa kipindi kirefu sana. Kiongozi mmoja mkuu wa SMZ wakati ule, aliwahi kufanya mkutano na waandishi wa habari kuelezea hali ya mtafaruku inayoendelea katika kijiji hicho cha Shengejuu, na hapa namnukuu moja ya kauli zake aliyoitoa kupitia kikao hicho“Sasa tunataka kuwafanya watu wajue kama serikali ipo”.
Katika enzi hizo wafuasi wa CUF walikuwa wakisingiziwa kuhusika na hujuma mbalimbali kama vile kuchomwa moto madarasa ya skuli, kupaka vinyesi kwenye kuta za skuli, kutia vinyesi kwenye visima n.k. Hizi bila shaka zilikuwa ni mwendelezo wa propaganda chafu za kisiasa zilizokuwa na lengo la kujenga picha ya uongo na kuhalalisha hujuma dhidi ya watu wasio na hatia. Waliokuwa wakifanya haya ni watu waliofundishwa vyema propaganda na siasa chafu za uchochezi. Wakitekeleza vitendo hivyo huku wakilindwa na askari polisi. Madhumuni ni kuendelea kupata fursa ya kuwatesa raia wasio na hatia kwa kuwapiga, kuwaweka gerezani na kuwaua. Waliokuwa wakifanya vitendo hivyo hawakujua kwamba walikuwa wanaonekana na wanafuatiliwa nyendo zao na hivyo kufahamika wao na waliowatuma.
Katika hatua nyengine Siku moja wanakijiji hao hao wa Shengejuu katika nyakati za usiku wakiwa katika doria yao ya kuangalia ni nani hasa wanaofanya vitendo hivi, walifanikiwa kuwafumania watu hao. Wakiwa wanaendelea na doria, wanakijiji hao waliiona gari yenye namba za usajili ZNZ-12633 inayomilikiwa na usalama wa taifa ikisimama kiasi cha umbali wa mita 100 hivi kutoka ilpokuwepo skuli ya Shengejuu (Soma kitabu cha Dr. Bakari, 2001 kiitwacho The democratization process in Zanzibar). Ghafla watu watatu waliokuwa na galoni la mafuta ya petroli walishuka kutoka katika gari hiyo. Haraka haraka wakamwaga mafuta na kuchoma baadhi ya majengo ya shule hiyo na kukimbia. Wanakijiji wakajitokeza ghafla na kuwazingira wahalifu hao. Lakini mara milio ya risasi hewani ikasikika na watu hao kuingia ndani ya gari yao na kukimbia. Wanakijiji waliwahi kuuzima moto huo. Ilithibitika kuwa watu waliofanya vitendo hivyo ni wanamaskani waliokuwa wakilindwa na wanausalama ndio waliokuwa wakitekeleza vitendo na hujuma zile kwa nia ya kukizulia chama cha CUF na kuwatesa raia bila ya hatia yoyote kwa maslahi binafsi ya kisiasa.

Maadui wa Zanzibar baada kuliona wimbi la kudai mabadiliko katika mfumo na muundo wa Muungano wa Tanzania linaongezeka wameamua kujipanga upya na kujaribu kuwasambaratisha wazanzibari ili wasifikie lengo lao kwa kupitia mbinu hizo zilizotumika huko nyuma za kuandaa uongo na kuupandikiza katika jamii. Bila shaka wakitarajia uongo huo utaweza kuzaa chuki na fitna miongoni mwa makundi mabali mbali yaliyoshika kamba ya pamoja kutafuta maslahi ya nchi yao na hivyo kuiwachia kamba hiyo na kusambaratika. Chuki ambazo zinajengwa hapa ni baina ya CUF na CCM kwa vitendo kama vile vya kuzichoma moto maskani za CCM na kuwasingizia CUF. Kuwatesa wafuasi wa CUF kwa visingizio mbali mbali kama vile kupambana na UAMSHO ili wafuasi wa CUF wakasirike na serikali na chao kwa kuwa CUF ni sehemu ya serikali hiyo. Wafuasi wa CUF wakikasirika dhidi ya chama chao itakuwa tayari umefanikisha kulisambaratisha kundi kubwa linashikilia engine ya kudai mabadiliko na hivyo kuliwacha kundi hilo likiwa dhaifu.

Maadui hawa wa Zanzibar wameunda makundi maalum ya uharamia, kuratibu na kutekeleza vurugu, kuchoma moto maskani za CCM, kucoma moto makanisa na kushambulia na kuwauwa viongozi wa dini ya Kikristo. Kuna taarifa za uhakika za kikao cha CCM mkoa wa Mjini magharibi kilichosimamiwa na mwenyekiti wake Borafia Silima cha kupanga hujuma za uchomwaji moto wa baa ya Mbawala. Kijana Salim Hassan Mahoja na wenzake watatu wote wakiwa ni MAJANJAWIRI walitumika kushiriki uchomaji moto wa baa hiyo. Kwa kuwa mmiliki wa baa hiyo alijua kua vitendo vya fujo vingeweza kupelekea baa yake kuchomwa, aliomba ulinzi mapema kutoka katika jeshi la polisi. Askari watatu waliokuwa na silaha bila ya sare walilala katika baa hiyo wakiwasubiri wahalifu pindipo baa hiyo ingevamiwa na kuchomwa. Vijana waliopangwa kuiripua baa hiyo Salim na wenzake walifika katika eneo la tukio usiku na kujaribu kutaka kuchoma moto baa hiyo kama walivyoagizwa. Bahati mbaya askari waliokuwa wamejificha ndani ya baa hiyo waliwashambulia kwa risasi za moto na kijana Salim akafariki hapo hapo huku vijana wenzake wawili wajeruhiwa kwa risasi. Maiti na majeruhi wote wakapelekwa hospitali ya Mnazi mmoja. Jambo hili limefunkwa halikusemwa wala halikuripotiwa katika vyombo vya habari.

Hivi sasa maadui wa umoja wa wazanzibari na wale wasiotamani kuiona Zanzibar inajitawala kutoka mikononi mwa watanganyika wamekuja na staili mpya ya kufikia agenda yao hiyo. Hii sasa ni kuipaka matope Zanzibar kwa kuijengea sura ya mbaya mbele ya jamii ya kimataifa. Wanamtandao wanavyoamini na bila shaka ndivyo ilivyo kuiingiza Zanzibar katika mgogoro na jamii ya kimataifa ni mtaji pekee wa kutafuta uungwaji mkono na ulimwengu na “mandate’ ya kuendelea kuiweka Zanzibar katika ukoloni wa Tanganyika.

Hivi karibuni kumeibuka vitendo vya kuwashambulia kwa risasi na kuwauwa viongozi wa dini ya Kikristo na kiislamu kwa kutumia bunduki na mapanga. Sheikh Fadhil Soraga alimwagiwa tindi kali na watu wasiojulikana. Hili ndio tukio la mwanzo katika kipindi hichi cha mfululizo wa matukio ya uhalifu kwa viongozi wa dini. Usiku wa tarehe 25/12/2012 Padri wa kanisa katoliki mjini Zanzibar Ambrose Mkenda alipigwa risasi na watu wasiofahamika akiwa anawasili nyumbani kwake ambapo watu hao waliokuwa wamepanda chombo aina ya vespa walimpiga risasi akiwa getini ndani ya gari akijiandaa kuingia nyumbani kwake maeneo ya Tomondo. Siku ya tarehe 16/02/2013 Padri Everist Mushi wa kanisa katoliki Zanzibar, alipigwa risasi kichwani na watu wasiojulikana na kufariki papo hapo asubuhi wakati akielekea kwenye ibada katika kanisa katoliki Beit el Raas Zanzibar. Kama ilivyokuwa kwa Padri Mkenda wauwaji wa Padri Mushi waliofanya tukio hilo walikuwa wawili na walikuwa wamepakizana kwenye pikipiki aina ya Vespa wakati padri huyo alikuwa kwenye gari lake. Tukio la mwisho hadi tunaandika makala hii ni kuuliwa kinyama kwa kukatwakatwa na mapanga shingoni Imamu wa Msikiti wa Mwakaje akiwa Shambani kwake Kitope.

Uchunguzi unaendelea lakini zipo dalili nyingi za kuyahusisha matukio haya na njama za kuijengea Zanzibar picha ya UGAIDI mbele ya jamii ya kimataifa. Wauwaji wanaonekana ni watu waliotumwa na mtandao maalum ili kutimiza agenda yao hii. Hapa hatuwezi kusema ni akina nani na nani lakini kwa mujibu wa kile kinachoendelea Zanzibar itoshe kuamini kuwa ni mipango maalum ya kuiteka nyara sauti ya umoja wa wazanzibari ambayo bila ya woga kutoka kwa wazanzibari wenyewe, viongozi wao wakuu na taasisi kadhaa za serikali yao kwamba wanataka mabadiliko kutoka katika mfumo wa sasa wa Muungano kwenda katika mfumo mpya wa muungano utakaoipatia Zanzibar mamlaka yake kamili kitaifa na kimataifa. Kwa kuwa kuna taasisi za dini ya kiislamu zilibeba agenda hii kwa ari na hamasa ya hali ya juu basi wanamtandao wanadhani itatosha kuwafanya mataifa makubwa kuamini kuwa mauwaji ya viongozi wa kikristo yapo nyuma ya harakati hizi za kudai Zanzibar yenye mamlaka kamili.

Wazanzibari wameishi na ndugu zao wa kikristo kwa karne nyingi sana huku utamaduni wa dini ya kiislamu ukiwa ni wenye kutawala Zanzibar. Katika kipindi chote hicho wakristo wamekuwa wakiwashimu waislamu kwa kila hali na hivyo waislamu hawakuiona haja wala sababu ya kuwabugudhi wakristo. Hata Askofu Shayo akizungumzia kadhia hii alipata kutamka “mimi nimeishi Zanzibar kwa miaka 20 sasa, sikupata kuona haya”. Haya ni mapya sana, haya ni mambo maalum katika agenda maalum. Haya si mambo ya kidini wala ugaidi bali ni vitimbi vinavyopangwa kiufundi vya kuhakikisha wazanzibari hawafikii lengo lao. Haya si mapambano ya waislamu dhidi ya wakristo wala wakristo dhidi ya waislamu ni agenda iliobebwa na wenyewe ambao wanajua vyema azma ya agenda hiyo.

Hebu tujiulize ni kwa nini mauwaji ya mtu mmoja ambayo si mauwaji ya kawaida kwa Zanzibar kwa ghafla sana yanaitwa “mauwaji ya ugaidi” na viongozi wa Tanganyika wanaojiita wa Jamhuri ya Muungano? Kuyaita mauwaji haya ugaidi ni kwa sababu aliyeuwawa ni Padri na hivyo iaminike kauliwa na waislamu? Kule Tanganyika watu kadhaa wamekua wakiuliwa katika kadhia kadha wa kadhaa hatujaona viongozi wa Tanganyika kuyaita matukio hayo kuwa ni ugaidi. Halkadhalika kule Tanganyika wazi wazi mapambano ya kidini yamekuwa yakifanyika na hadi kufikia mkristo kuuliwa na waislamu lakini hapasikiki kauli ya viongozi wa Tanganyika wakiitangaza Tanganyika kuwa ni pahala ambapo ugaidi unafanyika. Ni kwa nini Zamnzibar tu?

Tunaamini wataalamu wa ndani na wa nje watafanya kazi kwa umakini na wahaliu hawa kubainika. Lakini ukweli utabaki pale pale kwamba hizi ni njama maalum za watu maalum wenye nyadhifa maalum kuteka nyara agenda ya wazanzibari ya kujikomboa. Kama ni sulala la kuchunguzwa na kupatiwa majibu lingepata majibu lile na kutiwa tindi kali Sheikh Soraga na kupigwa risasi Padri Mkenda, matukio yote mawili yamenyamaziwa kimya hadi sasa. Hivi nchi hii ya Tanzania yenye vyombo vya ulinzi na usalama vya kila aina vinashindwa kuwakamata waliohusika na matukio haya? Havishindwi hata kidogo bali matukio yamefumbiwa macho kusudi kwa kuwa kuna mipango maalum nyuma yake.
 
Makala ndefu, but nimefanikiwa kuisoma yote...

1. Kwa nini unaamini chini ya muungano Zanzibar inatawaliwa?
2. Kama waliotekeleza mauaji ya Padre ni watu wanaotaka kuwachonganisha wazanzibar na jumuiya ya kimataifa, je, huo si ndi ugaidi wenyewe?
 
Status
Not open for further replies.
Back
Top Bottom