Njia sahihi ya kuzitumia hisia

Am For Real

Senior Member
Nov 21, 2023
168
466
Matatizo mengi tunayokutana nayo kwenye maisha, kwetu wenyewe na kwa wengine huwa yanaanzia kwenye hisia.

Tunafanya maamuzi fulani kwa kusukumwa na hisia na baadaye tunagundua hayakuwa maamuzi sahihi kitu kinachofanya tuingie kwenye matatizo.

Tunaweza kuzichukia hisia, lakini bila ya hizo, hatuwezi kufanya maamuzi yoyote, tunaweza kufikiri tutakavyo, lakini ili kufanya maamuzi, lazima kuwe na hisia zinazotusukuma.

Hivyo badala ya kuzilaumu hisia, tunapaswa kujua jinsi ya kuzitumia vizuri ili tufanye maamuzi bora na yenye manufaa.

Kwa kuanzia kwetu wenyewe, tunapaswa kujua ni hisia zipi zenye nguvu zaidi kwetu kwenye maamuzi ambayo huwa tunafanya.

Binadamu wote tunasukumwa na vitu viwili, tamaa ya kupata na hofu ya kupoteza. Hivyo unapaswa kujua ni kitu au vitu gani unataka sana, ambavyo uko tayari kufanya chochote kuvipata. Na pia kujua vitu gani hutaki kupoteza kabisa na hivyo uko tayari kwa lolote usivipoteze.

Lazima ujue kwa hakika maeneo hayo mawili kukuhusu wewe mwenyewe ili uwe makini mno wakati wa kufanya maamuzi.

Kwa mfano, kama unachotaka sana ni pesa, tena za haraka na zisizohitaji kuchoka sana, mtu akija kwako na fursa ya kutajirika haraka bila ya kazi utamsikiliza na kujikuta unashawishika na hata kukubaliana naye. Hata kama kuna makosa ya wazi kwenye kile anachokueleza mtu, hutaweza kuyaona kwa sababu hisia zako zinataka sana kile anachokueleza kiwe kweli. Hivyo ndiyo wengi wanaingia kwenye kutapeliwa.

Hivyo hisia zozote kuu zinazokusukuma wewe, unapaswa kuwa makini nazo mno, inapofika kufanya maamuzi, jua kabisa ni kipi kinachokusukuma sana na hapo jipe nafasi na muda wa kuangalia kitu kwa undani kabla ya kuamua. Lengo ni kuhakikisha hisia zako hazikuhadai ujidanganye mwenyewe, kwa kuona kile unachotaka kuona ambacho siyo kilichopo.

Upande wa pili ni kwenye hisia za wengine. Hatuwezi kuwashawishi wengine bila ya kugusa hisia zao. Tunaweza kuwapa ukweli wote ulivyo, lakini hilo halitawafanya wachukue hatua, ni mpaka tuguse hisia zao ndiyo wanachukua hatua.

Chukua mfano mzuri wa kitu ambacho kinauzwa na umekuwa unakihitaji ana, lakini huhangaiki nacho sana kwa sababu unajua kipo. Lakini siku unaambiwa kimebaki kimoja tu na kikiisha hakipatikani tena, unanunua mara moja, hiyo ni kwa sababu hisia zako za kupoteza zimechochewa, unachukua hatua ili usipoteze.

Unaweza kuona hii ni njia ya mkato ya kuwafanya watu wachukue hatua unazotaka, unachohitaji ni wewe kujua hisia zenye nguvu kwao na kuzitumia. Lakini nikupe tahadhari, unaweza kutumia hisia kumshawishi mtu yeyote afanye chochote unachotaka, lakini kama kitakuwa siyo chenye manufaa kwao, watakuchukia na kila mara watakukwepa.

Mfano unauza kitu ambacho mtu hana uhitaji nacho, lakini unajua hofu yake iko wapi, unatumia hofu hiyo kumfanya anunue, ananunua kweli, lakini baadaye anagundua alichonunua siyo sahihi na hakina manufaa kwake, atakuwa anakukimbia.

Hivyo unapaswa kujua kwanza kama mtu ni sahihi kwako, kama kile unachotaka afanye kina manufaa kwake na hapo ndipo utumie hisia. Usianze kutumia hisia kabla hujajua kama mtu ni sahihi na anachofanya kitakuwa na manufaa kwake.

Ukitumia hisia kumshawishi mtu kuchukua hatua yenye manufaa kwake, atafurahi sana baada ya kufanya hivyo na ataona jinsi gani alikuwa anajichelewesha, atakupenda na kuendelea kushirikiana na wewe.

Hisia ni kama moto, ukitumika vizuri unafanya mambo yenye manufaa, lakini ukitumika vibaya unaleta uharibifu. Kuwa makini na namna unavyotumia hisia, kwako mwenyewe na kwa wengine pia.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom