Njia nyingine ya kupinga hukumu na tuzo ya Mahakama iliyotokana na maridhiano yenu ni kufungua Kesi mpya

Apr 26, 2022
64
100
Jinsi ya kuipinga hukumu na tuzo Iliyofikiwa kwa Maridhiano Mahakamani

Ikiwa Mahakama imeandika hukumu na kutoa tuzo (decree) kutokana na makubaliano yenu wenyewe, lakini baadae wewe ukataka kupinga hayo makubaliano kwa sababu mbalimbali, Je, utatumia njia gani kuhakikisha yale makubaliano yanafutwa au kutenguliwa?

Soma hii kesi alafu utajua cha kufanya.

Ni kesi ya Mohamed Enterprises (T) Limited V Masoud Mohamed Nasser, Civil Application No. 33 of 2012.

Imefasriwa na kuletwa kwako nami zakariamaseke@gmail.com
(0754575246 WhatsApp)
(Advocate Candidate).

FACTS (STORI YA KESI)

- Tarehe 1 June, 2010, Kampuni ya Mohamed Enterprises (T) Limited ilifungua kesi ya madai Mahakama Kuu kumshtaki Masoud Mohamed Nasser kudai dollars kadhaa za Marekani.

- Mwisho wakafikia na kuandaa makubaliano (consent agreement) ambayo watayapeleka kusajili Mahakamani.

- Tarehe 23 May, 2011, wakapeleka Mahakama Kuu, hati ya makubaliano yao (Deed of Settlement) kuomba yasajiliwe.

- Maombi yakakubaliwa na makubaliano yao yakasajiliwa na JAJI MWARIJA, J., Ikawa sasa ni kama TUZO (DECREE) rasmi iliyotolewa na Mahakama yenyewe. Na hapo kesi inakuwa imeisha.

- Lakini cha ajabu, tarehe 24 June, 2011, upande mmoja kwenye hayo makubaliano (mshtakiwa), Masoud Mohamed Nasser, akafungua maombi kwenye Mahakama Kuu hiyo hiyo chini ya kifungu cha 68(e) na 95 cha Sheria ya Mwenendo wa kesi za Madai (CPC) kuiomba Mahakama itengue (set aside) Makubaliano hayo (consent judgement), kwa sababu eti yalifikiwa kwa ushawishi wa kimazingira (duress), vitisho (intimidation), kulazimishwa (coercion) na kutumia vibaya mamlaka au nafasi waliyo nayo viongozi wa mlalamikaji (undue influence).

- Mlalamikaji, Mohamed Enterprises (T) Limited akaweka pingamizi kwa sababu zifuatazo:

1: Kwamba, kifungu cha 68(e) cha CPC hakiwezi kutumika kuiomba Mahakama itengue makubaliano yaliyofikiwa, kwa sababu tayari kuna TUZO ya Mahakama (decree) ilishatoka kwenye hii kesi, na hamna kesi nyingine inayosubiri kusikilizwa, na hicho kifungu kinahusu maombi na maagizo mengine ya Mahakama ambayo hayaamui kesi mpaka mwisho (interlocutory applications and orders).

2: Kwamba, kifungu cha 95, (kinachoipa Mahakama Mamlaka ya asili (inherent power) yasiyo na mipaka kufanya maamuzi yoyote ili kutenda haki au kuzuia matumizi mabaya ya Mahakama) hakiwezi kutumiwa hapa kwa sababu kesi husika ilishaisha.

-Awamu hii Jaji alikuwa mwingine (Mheshimiwa Jaji Fauz Twaib, ambaye sasa ameshastaafu)

-Huyu Jaji wa pili, akapokea maombi haya mapya, akakubaliana na Pingamizi la kwanza, lakini akakataa pingamizi la pili, akasema alikuwa na sababu za kutosha kutumia Mamlaka yaliyopo kifungu cha 95 ambayo yanaipa Mahakama Uhuru mkubwa kuamua.

-Mheshimiwa Jaji Twaib, akakitumia kifungu hicho, kuendelea kusikiliza haya maombi ya mara ya pili, akatengua na kuweka kando (set aside) yale maamuzi ya mwanzo ya Jaji mwenzake, (Mwarija J), yaliyotambua na kusajili yale makubaliano (consent decree), akatengua pamoja na tuzo (decree) iliyotokana na makubaliano hayo na akairejesha kesi mwanzo. (restored the original suit)

-Hapo ndipo mlalamikaji kwenye hii kesi hakuridhika, akaenda Mahakama ya Rufaa kuomba Revision (mapitio) kwa sababu ni aina ya uamuzi ambao huwezi kukata rufaa. Soma Order XL ya CPC.

- Akaiomba Mahakama Ya Rufaa iitishe na kupitia upya kumbukumbu na mwenendo mzima wa kesi kutoka Mahakama Kuu, ili ifanye uchunguzi na kujiridhisha yenyewe kuhusu usahihi na uhalali kisheria wa uamuzi wa Mheshimiwa Jaji Twaib.

HOJA ZA MAWAKILI

Upande wa Mlalamikaji walisema kwamba:

- Baada ya kufikia Makubaliano na wakayapeleka Mahakamani yasajiliwe na yakasajiliwa na Mwarija J, basi Mahakama ilikuwa FUNCTUS OFFICIO - Hii ni kanuni kwamba, kama kesi imesikilizwa imeisha na Mahakama imetoa hukumu, basi Mahakama hairuhusiwi kurudia tena kukaa kusikiliza kitu hicho hicho na kubadilisha au kuja na hukumu nyingine, hivyo Mheshimiwa Jaji Twaib, hakuwa na Mamlaka kusikiliza yale maombi ya awamu ya pili yaliyofuatia.

“That Twaib, J., was not competent to reopen a matter which had been concluded and a decree drawn up by his fellow judge of the High Court.”

- Pia wakasema, vifungu alivyotumia Jaji sio Sahihi.

- Na kwamba njia pekee aliyo nayo yule ambaye anapinga walichokubaliana na mwenzake ni kufungua kesi mpya.

- Upande wa Pili wa Mawakili ukajibu kwamba, vifungu alivyotumia Jaji ni sahihi kwa sababu kwanza hakuna kifungu cha sheria kinachotoa Mamlaka ya kutengua (set aside) kile walichokubaliana watu wenyewe (consent decree) hata kama makubaliano hayo yalifikiwa kupitia udanganyifu (fraud), upotoshaji (misrepresentation), vitisho (intimidation) au matumizi mabaya ya nafasi au cheo (undue influence).

- Kwa hiyo Jaji alikuwa sahihi kutumia kifungu cha 95 kinachotoa Mamlaka ya asili kwa Mahakama kwa kumpa Jaji uhuru wa kuamua usio na mipaka ili kutenda haki, na vile vile hakuna kifungu kinachomzuia Jaji wa Mahakama Kuu kutengua amri iliyotolewa na Jaji mwingine wa Mahakama Kuu.

Hizo zilikuwa hoja za Mawakili.

UAMUZI WA MAHAKAMA YA RUFAA

- Kwanza, Mahakama ya Rufaa ilikubali kwamba Sheria ya mwenendo wa kesi za Madai (CPC) haina kifungu kinachotoa fursa ya kutengua (set aside) TUZO ya Mahakama inayotokana na MARIDHIANO ya watu wenyewe.

- Hivyo CPC haijitoshelezi (haina kila kitu), na katika mazingira hayo (ambapo CPC iko kimya), ndipo Mahakama inabidi itumie sheria za nje ya nchi na maamuzi yaliyotokana na Mahakama za Uingereza (common law) kama inavyoruhusiwa chini ya kifungu cha 2(2) cha JALA (the Judicature and Application of Laws Act),

- Hata hivyo, Mahakama ikasema (Kwa hii kesi ilivyo) lazima itoe (shule) utaratibu sahihi wa kufata, kwa sababu haiwezekani Jaji mmoja wa Mahakama Kuu atoe hukumu au tuzo kwenye kesi moja, (ambapo hiyo kesi inakuwa imeisha), alafu baadaye tena aje Jaji mwingine wa Mahakama Kuu, atengue hiyo hukumu au tuzo na kuja na hukumu au tuzo nyingine mpya badala yake.

- Kufanya hivyo itakuwa ni matumizi mabaya ya mfumo wa Mahakama.

- Mahakama ya Rufaa ikasema, Hukumu au tuzo ikishatolewa na Mahakama, basi Jaji au Hakimu wa Mahakama hiyo anakuwa “functus officio” yaani hana mamlaka kuendelea na kesi hiyo hiyo.

- Kama ikitokea baada ya kesi umegundua kitu kipya ambacho unaona kilitakiwa kisemwe wakati kesi inasikilizwa, sheria inaruhusu kuomba marejeo (Review). Soma Order XLII au unaweza kuomba Revision (mapitio).

- Kwa hiyo kama hujaridhika unaruhusiwa kufungua kesi mpya kupinga uamuzi kwenye kesi ya kwanza.

Mahakama ya Rufaa ikarejea kitabu cha mwandishi nguli wa sheria za Madai “Mulla” Toleo la 16, Juzuu ya 1, Kurasa za 299, 653 na 1066.

Ambapo ukurasa wa 299, anasema “Labda wanaoshtakiana wakubaliane, vinginevyo huwezi kuiomba iliyokuwa Mahakama ya kwanza kusikiliza kesi, itengue tuzo yake, INGAWA UNAWEZA KUFANYA HIVYO KWA ZILE AMRI AMBAZO HAZITOI UAMUZI WA MWISHO WA KESI (interlocutory orders).”

Ukurasa wa 653 anasema, “Njia pekee iliyopo kwa mtu anayetaka kupinga tuzo inayotokana na makubaliano, kwa kigezo kwamba kulikuwa na udanganyifu ni KUFUNGUA KESI akiomba kutengua hiyo amri”

Katika ukurasa wa 1066 ambao unahusu Utaratibu wa kutengua tuzo ya Mahakama inayotokana na makubaliano ya watu wenyewe (Procedure for setting Aside Consent Decrees). Mulla anasema, “kwa kuwa kifungu kidogo cha 3, kinakataza mtu kukata rufaa kwenye amri ya Mahakama inayotokana na makubaliano ya watu wenyewe, hii inatoa kanuni kwamba, tuzo ambayo watu wamekubaliana wenyewe, ni kizuizi cha kigeugeu (a judgment by consent, acts as an estoppel).

-Amri ya Mahakama inayotokana na makubaliano yenu wenyewe, ingeweza tu kutenguliwa kupitia kesi sahihi kwenye hiyo nafuu husika (could only be set aside by substantive proceedings appropriate to that particular remedy).

-Na inaweza kutenguliwa kwa sababu yoyote ambayo huwa inabatilisha makubaliano (mkataba) kama vile upotoshaji, udanganyifu au makosa (mistake).

“Hii inaweza tu kufanyika kupitia kesi.”

“TUZO ya Mahakama inayotokana na makubaliano yenu wenyewe, HAIWEZI KUTENGULIWA KWA KUKATA RUFAA (APPEAL) au KUOMBA MAREJEO (REVIEW).”

“Lakini, Mahakama kwa mamlaka yake ya asili inaweza kutengua amri ISIYOAMUA KESI HADI MWISHO inayotokana na makubaliano yenu wenyewe (interlocutory consent order) yaani amri ambayo sio amri au hukumu ya mwisho (which is not a final order or judgment) [all the above emphasis provided].” Huyo Ni Mulla.

- Mahakama ya Rufaa ikasema inakubaliana na mawazo ya Mulla.

- Hii ina maana kwamba, Mheshimiwa Judge Twaibu, angekuwa na mamlaka ya kutumia kifungu cha 95 cha CPC (kinachotoa Mamlaka ya asili kwa Mahakama na kumpa Jaji uhuru wa kuamua usio na mipaka ili kutenda haki), kama tu kesi iliyokuwa mbele yake ingekuwa haijasikilizwa na kuisha kule mbele ya Jaji mwenzake wa Mahakama hiyo hiyo Kuu.

- Au kama uamuzi wa Jaji mwenzake (Mwarija J.) ungekuwa hautoi tuzo au hukumu ya mwisho (if the matter before him had not been finally concluded by a fellow judge of the same High Court, or if the decision of Mwarija, J. was interlocutory in nature).

-Mahakama ya Rufaa ikasema, kwa maelezo yaliyoko mbele yetu, yanaonesha wazi kuwa kesi husika ilikuwa imeamuliwa hadi mwisho, hati ya makubaliano (a deed of settlement) ilikuwa imeshaletwa Mahakamani na amri ya Mahakama ikatolewa dhidi ya Mshtakiwa.

- Baada ya hapo, Mahakama ilikuwa hairuhusiwi kuendelea tena na hiyo kesi (functus officio). Wote wawili, Mwarija na Twaib, JJ. hawakuwa na mamlaka ya kusikiliza tena maombi ambayo yangefuata baada ya hapo kwenye hii kesi.

- Ingawa, hakuna sheria (kwa ufahamu wetu kama Mahakama ya Rufaa), ambayo inamzuia Jaji mmoja kutengua uamuzi wa Jaji mwenzake mwenye mamlaka kamili, lakini utaratibu wa siku zote (practice), busara na mwenendo wa taaluma vinazuia hicho kitu.

- NJIA PEKEE ILIYOPO KWA MSHTAKIWA HAPA NI KUFUNGUA KESI UPYA.

- Lakini hakufanya hivyo, badala yake akafungua maombi mengine mbele ya Mheshimiwa Jaji Twaib kwenye Mahakama ile ile. Hiyo haikuwa sahihi.

- Ni kweli kwamba vitu kama udanganyifu, kulazimishwa, upotoshaji vinaweza kubatilisha makubaliano yaliyofikiwa (matters of fraud, coercion or misrepresentation do vitiate a consent decree).

- Ni lazima ushahidi utolewe kuthibitisha hayo madai. Ushahidi wa kiapo hautoshi.

- Mwisho, Mahakama ya Rufaa ikakubali maombi ya Revision (Mapitio), ikatengua na kuweka kando uamuzi na amri ya Mahakama Kuu ya mheshimiwa Jaji Twaib.

- Mahakama ya Rufaa ikaurudisha (restore) kama ulivyokuwa ule uamuzi wa kwanza wa Mahakama Kuu wa Mwarija, J. (Hii ilikuwa tarehe 23/08/2012.

------MWISHO------

Angalizo: Position au maelezo haya ni kwa mujibu wa kesi zilizokuwa zimeamuliwa mpaka siku ya kupost hili andiko. Hivyo unaposoma leo hii kesi soma na kesi zingine zilizopo sasa hivi, ili ujue utaratibu bado ni ule ule au la! Mimi sifahamu umesoma lini haya maelezo, lakini Sheria zinarekebishwa na nyingine mpya zinatungwa kila siku, pia Mahakama ya Rufaa inaweza kupindua huu uamuzi kupitia kesi nyingine muda wowote

Disclaimer: Lengo la hii makala ni kutoa elimu kwa jamii. Huu sio ushauri wa kisheria kwa mtu yeyote. Ikiwa utaamua kufungua kesi kwa kufata haya maelezo na ukapata hasara, mwandishi wa maelezo haya hatawajibika kwa vyovyote vile. Kama unahitaji ushauri wa kisheria wasiliana na Mawakili.

Pia natoa angalizo, wale wazee wa kukopi machapisho ya watu na kuweka majina yenu. Ni kosa kisheria. Hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayejimilikisha andiko hili. Unaruhusiwa tu kushare lakini usibadili yaliyomo. Ni heri uanze kuandika ya kwako mpya.

Tafsiri hii ya Kesi imeandaliwa na kuletwa kwako nami Zakaria Maseke,
Advocate Candidate,
(0754575246 WhatsApp).
zakariamaseke@gmail.com
 
JF ya zamani ilikuwa na vitu kama hivi. JF was a forum of knowledge kabla ya kuvamiwa na chekechea na siasa za chawa wa CCM!

Kesi hii nimeisoma sana lakini ilikuwa haijakaa sawa kichwani maana kulikuwa na vitu vinanichanganya. Now it is as clear as a translucent sheet! Asante sana.
 
JF ya zamani ilikuwa na vitu kama hivi. JF was a forum of knowledge kabla ya kuvamiwa na chekechea na siasa za chawa wa CCM!
Kesi hii nimeisoma sana lakini ilikuwa haijakaa sawa kichwani maana kulikuwa na vitu vinanichanganya. Now it is as clear as a translucent sheet! Asante sana.
Una mimba ya mwana CCM sio bure
 
Back
Top Bottom