Njaa za cuf kuivuruga znz

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,956
22,149
MENGI yameandikwa na yanaendelea kuandika kuhusu

"Maridhiano" yanayoelezwa kuwa yamefikiwa baina ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Amani Karume na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif; maridhiano ambayo hayakubainishwa kwa kauli ya mdomo na wala hayakuandikwa popote pale.


Katika kuelezea kutoridhika kwangu na hali ya usiri na ukimya inayoendelea kuyakumba hayo 'maridhiano' yanayozungumziwa hapa, niliwahi kumuomba Maalim Seif Shariff katika kikao cha Kongomano lililofanyika hivi karibuni katika Hoteli ya Bwawani kuhusu Mustakbali wa Zanzibar atuwekee wazi nini hasa kilichozungumzwa na kukubaliwa kati yake na Rais Amani Karume.


Alicheka tu bila ya kusema lolote. Baadaye nilifahamishwa kuwa ili maridhiano hayo yaweze kutekelezwa, kulikuwa na haja kubwa ya kuiwacha hali ya ukimya na usiri kuendelea mpaka hapo baadaye mambo yatakapojikita wenyewe...


Hivi karibuni, tumelisikia pendekezo kutoka vyama vya upinzani na jumuiya za kidini la kutaka Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu uahirishwe hadi mwaka 2012; na shinikizo baada ya shinikizo linalomtaka Amani akubali kuongozewa muda wa kutawala, sio kwa kipindi kingine cha miaka mitano, bali kwa miaka miwili ya ziada akiwa ni kiongozi wa serikali ya mpito kuelekea katika uchaguzi ujao.


Katika hotuba yake aliyoitoa kule Pemba katika sherehe za kuadhimisha miaka 46 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Amani alisema kuwa hatagombea kipindi cha tatu cha urais na huku akisisitiza haja ya kulinda na kutetea katiba ya Zanzibar ambayo inamzuia kugombea tena urais wa Zanzibar.


Lakini, kauli yake hiyo haimaanishi hata kidogo kuwa hayuko tayari kuiongoza Zanzibar kwa kipindi cha miaka miwili kama kiongozi wa serikali ya mpito kuelekea katika uchaguzi ujao ikiwa ataombwa kufanya hivyo. Na hii ndiyo hasa hoja ya Maalim Seif. Na, kwa hivyo, mpaka hapo Amani atakapoweka wazi kuwa hana dhamira ya kuiongoza serikali ya mpito hata kwa siku moja, basi hoja ya Amani kutokugombea kipindi cha tatu cha urais, itabaki palepale.


Lakini inawezekana kabisa akakubali kuiongoza serikali ya mpito kwa muda wa miaka miwili ikiwa Baraza la Wawakilishi litapitisha sheria ya kuahirisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu na kumtaka yeye kuiongoza serikali ya mpito kuelekea katika uchaguzi ujao; mamlaka ambayo Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanayo kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar na kanuni za Baraza la Wawakilishi.


Kauli za akina Pius Msekwa, Yusuf Makamba na wengineo ni sawa sawa na kelele za mpangaji ambazo haziwezi kumkosesha mwenye nyumba usingizi. Kwa lugha nyingine, urais wa Zanzibar si jambo la Muungano; kwa hivyo, ni jukumu la Wazanzibari kujiamulia wenyewe jinsi waonavyo; tena bila ya kuingiliwa na yeyote yule kutoka nje ya Zanzibar.


Hata hivyo, hebu tujiulize: nini hasa madhumuni ya kuwa na serikali ya mpito? Ni jambo la kawaida kabisa kuwa serikali ya mpito huwa inaundwa kila pale inapotokea migogoro ya kisiasa au hali ya dharura katika nchi. Hatuna haja ya kwenda mbali kujifunza mifano iliyo hai na iliyowahi kutokea ili kupata maana halisi ya serikali ya mpito.


Kwa mfano, baada ya kujiuzulu kwa Alhaj Aboud Jumbe mnamo April 1984, Ali Hassan Mwinyi aliteuliwa na Halmashauri Kuu ya CCM kuziba pengo lililoachwa wazi na Jumbe na kuongoza Serikali ya mpito kwa muda wa karibu miezi mitatu hadi uchaguzi ulipofanyika na hatimaye Mwinyi kuchaguliwa rasmi kama Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.


Isitoshe, serikali ya mpito pia iliwahi kuundwa nchini Afrika Kusini Septemba 2008 baada ya kujiuzulu kwa Rais Thabo Mbeki kutokana na tuhuma dhidi yake ya kuingilia katika jitihada za kumfungulia mashtaka bandia, hasimu wake mkuu wa kisiasa Jacob Zuma; na baada ya Bunge la nchi hiyo kupiga kura kumchagua Makamu Mwenyekiti wa ANC Kgalema Motlanthe kushika nafasi ya Mbeki mpaka Uchaguzi Mkuu ulipofanyika mwaka jana na Jacob Zuma kuchaguliwa rasmi kuiongoza Afrika Kusini.


Hali kama hiyo iliwahi kutokea nchini Liberia mnamo Agosti 2003 baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Charles Taylor na nafasi yake kushikiliwa kwa muda wa karibu mwaka mmoja na Makamu wa Rais Moses Blah ambaye aliongoza serikali ya mpito mpaka uchaguzi ulipofanyika na kuchaguliwa Ellen Johnson-Sirlief, mwanamke wa kwanza kabisa kushikilia nafasi ya urais katika Bara la Afrika.


Kwa hivyo, kama tuonavyoona hapo juu, serikali zote hizo za mpito ziliundwa baada ya kutokea migogoro ya kisiasa au dharura za aina fulani katika nchi hizo husika. Kwa upande wa Zanzibar, kujiuzulu kwa Jumbe kulisababishwa na “kuchafuka kwa hali ya hewa” na hivyo kusababisha kulazimika kujiuzulu kwake nafasi zote za uongozi alizokuwa nazo.


Nchini Afrika Kusini, kujiuzulu kwa Mbeki mwaka mmoja tu kabla ya kumalizika kwa muda wake wa urais kulililazimisha Bunge la nchi hiyo kumteua Rais wa muda kushika nafasi hiyo kwa sababu nchi haiwezi kujiendesha bila ya kiongozi. Hiyo ilikuwa ni dharura kubwa ambayo isingeliweza kuachwa bila ya kushughulikiwa.


Nchini Liberia mambo yalikuwa kama ilivyofanyika nchini Afrika Kusini. Liberia ilihitaji kupata kiongozi wa muda mpaka uchaguzi utakapofanyika kutokana na kujiuzulu kwa Rais wake kabla ya kumaliza muda wake. Hiyo nayo ilikuwa ni dharura kubwa ambayo iliikuta Liberia katika hali mbaya ya mgogoro wa kisiasa iliyosababishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoendelea kwa zaidi ya miaka 14.


Sasa, tukirudi nchini kwetu Zanzibar; hivi kweli kuna haja ya kuundwa kwa serikali ya mpito? Nauliza hivi kwa sababu hakuna dharura au mgogoro wa kisiasa unaomlazimisha Rais Amani Karume kuachia ngazi kabla ya muda wake kumalizika. Hili la kwanza.


Lakini, la pili ni kuwa ikiwa hoja inayojengwa hapa ya kutaka kuahirisha uchaguzi ujao kwa madhumuni ya kumpa rais Karume muda wa kutosha ili kuhakikisha kuwa uchaguzi ujao unafanyika kwa misingi ya uhuru na haki na hasa zaidi, kama alivyohoji Prof.


Issa Shivji hivi karibuni katika gazeti la Mwananchi toleo la Januari 16, 2010, kwa madhumuni ya kuondokana na "mazingira ya siasa za uhasama na chuki tuliyonayo":na kuelekea katika jitihada za kujenga utamaduni wa "mazingira ya siasa za ushindani tunayoyataka"inakubalika, basi la kujiuliza hapa ni kwanini muda huo uwe miaka miwili ya ziada badala ya rais Karume kutumia muda aliobakia nao kutekeleza yote hayo kabla ya kumalizika kwa kipindi cha pili cha urais wake mwishoni mwa mwezi Oktoba 2010?


Ikiwa kweli Rais Karume ana nia ya kufanya hivyo, mimi ninaamini kwa dhati kabisa kuwa anaweza kurekebisha kasoro zote zilizojitokeza katika zoezi la uandikishaji wa wapiga kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura; na pia kuhakikisha kuwa kila mwenye sifa za kupewa kitambulisho cha Uzanzibari anapewa kama ipasavyo mnamo muda huo huo uliobakia wa urais wake.


Kwa lugha nyepesi, sioni sababu ya kuamini kuwa Serikali au Tume ya Uchaguzi inahitaji miaka miwili ya ziada kukamilisha zoezi la kuandikisha wapiga kura wasiozidi 500,000 nchini kote.


Isitoshe, hivyo ni kweli kuwa Amani Karume hana muda wa kutekeleza hayo maridhiano kati ya hivi sasa na mwezi Oktoba 2010? Na ni maridhiano gani hasa yanayozungumziwa hapa ambayo yanaendelea kuwa siri? Na ikiwa kweli kuna haja ya kutekeleza maridhiano, kwanini lazima awe Amani Karume tu na si mtu mwingine wa kutekeleza maridhiano hayo?


Kwa kuendelea kuiongoza Zanzibar kwa muda wa miaka miwili mingine baada ya kumaliza vipindi viwili vya uongozi wake, pamoja na nia njema aliyonayo, Amani Karume haoni kuwa ataonekana anataka kujiongezea muda wa kutawala kwa mlango wa nyuma; na hivyo kuweka utamaduni mbaya kwa viongozi wajao ambao nao pia wataweza kabisa kujenga mazingira yanayofanana na hayo; ilimradi tu wapate fursa ya kujiongezea muda wa kutawala kinyume na katiba ya nchi?


Na ikiwa hili litaruhusiwa kufanyika, hivi Zanzibar itakuwa inaelekea wapi? Kuna haja gani, kwa hivyo, kuwa na katiba ya nchi ambayo haithaminiwi na wala kutekelezwa ipasavyo?


Kwa upande mwingine, ikiwa Maalim Seif na CUF watashiriki kikamilifu katika kuunda hiyo serikali ya mpito kama inavyotarajiwa, hapana shaka yoyote kuwa nao watajiwekea mazingira mazuri katika uchaguzi ujao kuliko wagombea wengine kutoka katika vyama vingine.


Hii inatokana na ukweli kuwa Maalim Seif ni mgombea mtarajiwa wa urais wa Zanzibar kupitia chama cha CUF, wakati Amani hatokuwa mgombea tena. Serikali ya mpito ndiyo itakayoweka hayo "mazingira" mazuri yatakayohakikisha kuwa uchaguzi ujao utakuwa huru na wa haki.


Kwa hivyo, ikiwa dhana ya serikali ya mpito ni kuweka mazingira mazuri kwa kufanyika uchaguzi ulio huru na wa haki, kushiriki kwa Maalim Seif katika serikali hiyo kutaonekana kama kuna mgongano wa kimaslahi (conflict of interest situation) kwa upande wake.


Kwa maana nyingine, huwezi kuongoza au kushiriki katika serikali inayopaswa kuandaa uchaguzi ulio huru na wa haki na papo hapo wewe ukawa ndiye mmoja katika wagombea watarajiwa wa uongozi wa nchi katika uchaguzi huo.


Hiki ndicho kilio cha CUF cha muda mrefu dhidi ya serikali inayoongozwa na CCM.


Kitu gani kitatufanya tuamini kuwa Maalim Seif na viongozi wenzake watakuwa mara hii waadilifu zaidi kuliko walivyokuwa viongozi wa CCM?


Kwa hivyo basi, naamini kwa dhati kabisa kuwa ni vyema akateuliwa mtu mwingine ambaye hatokuwa mgombea urais wa Zanzibar, muadilifu na mwenye sifa zifaazo, kuiongoza hiyo serikali ya mpito.


Vinginevyo, jitihada hizi zote zinazoendelea hivi sasa za kutaka kuakhirisha uchaguzi na kumtaka Rais Amani Karume kuongoza serikali ya mpito, zitakuwa si chochote zaidi ya mbinu mpya ya kutaka kuendelea kutawala kwa mlango wa nyuma. Na hili, kwa maoni yangu, si jambo la busara hata kidogo.


Zanzibar haiwezi kujiwekea utamaduni mbaya ambao utaweza kutumiwa na viongozi wajao kila pale watapotaka kujiongezea muda wa kutawala baada ya kumaliza vipindi vyao vya uongozi kwa mujibu wa katiba.


Ikiwa Amani Karume, kwa kuitumia CUF na hasa zaidi Maalim Seif, ataruhusiwa na kufanikiwa kufanya hivyo, kitu gani kitawazuia viongozi wengine kufanya vivyo hivyo siku za baadaye?


Makala hii imetoka kwa mara ya kwanza katika mtandao wa Zanzibar Institute for Research and Public Policy-ZIRPP) zirpp@googlegroups.com
 
Back
Top Bottom