Nini kilitokea kati ya Mwalimu Nyerere na Kolimba

mukizahp2

JF-Expert Member
Jul 28, 2012
706
377
HORACE Kolimba ni miongoni mwa viongozi waandamizi nchini ambaye Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alitofautiana naye na baadhi ya wenzake kuhusu masuala ya msingi katika uongozi na mwelekeo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Lakini mbali na Mwalimu, Kolimba alitofautiana na chama chake (CCM), angali Katibu Mkuu, akiweka bayana chama hicho kimepoteza dira.

Kwa ujumla, hakuna ubishi kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa akifahamu mifumo yote ya uongozi wa nchi kwa sababu ameshiriki kuibuni n kuiridhia, akiwa kiongozi mkuu.

Bila shaka, alielewa wapi apate taarifa ipi na kuhusu nani au nini. Kubwa zaidi, watoa taarifa katika vyombo nyeti nchini walijitolea kumdokeza kwa kadiri ilivyowezekana wakiamini ndiye mtu wa uhakika asiye na hila kwa nchi yake. Asiye na mikono michafu dhidi ya nchi.

Lakini pia hakuna ubishi Mwalimu huyo huyo, alifahamu tabia na mienendo ya viongozi karibu wote waandamizi nchini. Ikumbukwe, asilimia kubwa ya viongozi ‘aliwalea' baada ya kuwaingiza katika mfumo wa uongozi.

Kwa hiyo, ni sahihi kusema Mwalimu alitambua uhodari na udhaifu wao na alijenga mazingira ya kuingilia majukumu yao kwa kadiri mambo yanavyoanza kwenda kombo katika ofisi alizowakabidhi chini ya kauli mbiu; "cheo ni dhamana."

Na pengine tatizo lililokuwapo ni kwamba wakati mwingine; ‘ndoto' nzuri alizokuwanazo Mwalimu kuhusu Tanzania bora isiyotegemea wahisani kujiendesha na isiyoongozwa na mchanganyiko wa viongozi wezi na waadilifu wanaovumiliana na hata kuwa genge moja dhidi ya umma, hazikusambaa vizuri kwa baadhi ya viongozi wenzake.

Na kwa hiyo basi, pengine alikuwa akihisi wenzake wanavuruga ‘ndoto' yake bila kujua kwamba ndoto hiyo haieleweki kwao au inaeleweka lakini kwao haina ‘mashiko'. Kwamba wakati yeye akiwa ameridhia hata mshahara wake upunguzwe ili kukabili hoja za mgomo wa wanafunzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) bila kulalamika maisha yake yatakuwa magumu (Msasani sio Dodoma kama sasa), wenzake wengi walitamani mshahara mkubwa zaidi.

Na kwa mantiki hiyo kutokana na baadhi ya hatua alizokuwa akichukua kama kiongozi wa nchi na hata baada ya kustaafu, wengi wanaamini ilikuwa vigumu kwa viongozi wengi waandamizi kubishana hadharani na Mwalimu Nyerere.

Ni kama vile uadilifu wa Mwalimu ulikuwa kikwazo au silaha kwa baadhi kumshambulia hadharani, ingawa kwa nadra ilijitokeza wachache kufanya hivyo huku wengine wakiishia kulalamika pembeni (mitaani).

Kati ya ambao miongoni mwao hawakuridhiki na walitumia mbinu nyingine za kumjibu Mwalimu ni pamoja na Horace Kolimba, kama tutakavyoona katika mfululizo wa makala hizi.

Kimsingi, inawezekana viongozi wengi waandamizi waliamini kwamba mbele ya umma, nguvu za Nyerere ni kubwa zaidi hasa kwa kigezo cha uadilifu na kwa hiyo, si rahisi kumpinga katika hali ya kumdhalilisha na ukabaki salama.

Imani hii ya uadilifu wa Nyerere ndiyo bila shaka, iligeuzwa na Watanzania kuwa dhamana kwa Benjamin Mkapa asiyekuwa ‘mwenyeji' kwao, na wakampigia kura za urais 1995.

Urais ambao baadhi ya machapisho yanabainisha kuwa Kolimba naye alikwishaonesha nia mapema zaidi, takriban miezi 10 kabla (mwishoni mwa mwaka 1994).

Lakini hata hivyo, ni dhahiri kuwa nyuma ya nguvu hizi za Mwalimu Nyerere katika jamii aliyoshiriki kusaka uhuru wake dhidi ya watawala wa kigeni, kulikuwa pia na nguvu za dola zilizokuwa na jukumu la kusukuma na kusimamia hoja zake za kitaifa.

Wengi mtakumbuka jinsi Mwalimu alivyotofautiana dhahiri na aliyekuwa Waziri Mkuu, John Malecela, achilia mbali Katibu Mkuu wa CCM (chama tawala), Horace Kolimba.

Na kwa namna ya kipekee, Mwalimu pia alitofautiana kuhusu namna Mzee Ali Hassan Mwinyi alivyokuwa akiongoza nchi katika baadhi ya masuala ya msingi, ingawa wakati mwingine alimtetea kuwa anashauriwa vibaya.

Nini hasa kilitokea?

Kutokana na tofauti hizo na hasa kwa kuangalia viongozi hao watatu, Kolimba, Malecela na Mwinyi, itakumbukwa Mwalimu aliandika kitabu; Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania.

Sijui kwa sababu zipi hasa ambazo pengine Mzee Ali Hassan Mwinyi na Mzee John Malecela wanaweza kuzieleza kwamba hawakutaka kujibishana na Mwalimu Nyerere, tofauti na alivyofanya Horace Kolimba.

Hata hivyo, Kolimba naye hakufanya majibizano na Mwalimu moja kwa moja hadharani, anadaiwa kutumia vyombo vya habari vya Chama cha Mapinduzi (magazeti ya Uhuru na Mzalendo) akiwa Katibu Mkuu, kumjibu Nyerere.

Inaaminika katika hali inayothibitisha nia ya Kolimba kuwania urais mwaka unaofuatia (1995), mwaka 1994 mwanasiasa huyo alijipanga kwanza kujinasua na mashambulizi ya Mwalimu Nyerere kwake na hata kwa wenzake (Mwinyi na Malecela ambao walikaa kimya). Mashambulizi hayo yamo kwenye kitabu cha Nyerere; Uongozi wetu na hatima ya Tanzania.

Maswali zaidi yanajitokeza katika mkakati huo wa Kolimba kama ambavyo pia tutazidi kubaini katika mufululizo wa makala hizi.

Kwa mfano, wakati Kolimba akidaiwa kutumia vyombo vya chama kumjibu Nyerere katika ‘staili' ya kipekee ambayo ilifichuliwa na magazeti mengine nchini, Mzee Mwinyi akiwa Mwenyekiti wa chama, alikaa kimya.

Kupitia magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Kolimba anadaiwa kuwatumia waandishi ambao inadaiwa pia walikuwa wakitumia majina tofauti, kama ilivyopata kufichuliwa na gazeti jingine la binafsi baadaye.

Baadhi ya makala hizo ni zile zilizotolewa katika gazeti la Uhuru la Novemba 8, mwaka 1994 ukurasa wa saba na Novemba 18, mwaka huo huo, pia ukurasa wa saba. Makala hizi inaelezwa ziliandikwa na Kolimba lakini kwa jina la mwandishi aliyejiita Alex Kowe.

Makala hizi (ambazo nitazichambua siku zijazo) ziliandikwa katika wakati ambao kwanza ni mwaka mmoja kuelekea Uchaguzi Mkuu huku Kolimba akidaiwa kutaka kuwania urais.

Lakini pia ni yeye ambaye kuelekea uchaguzi huo huo wa 1995, aliweka bayana chama anachokiongoza kimepoteza dira, ikielezwa angegombea kwa chama kingine.

Na kwa namna ya kipekee katika kile kinachoelezwa ni kujibu mapigo ya Mwalimu Nyerere kwa kitabu chake cha "Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania" Novemba 4, mwaka 1994, Kolimba alijigamba mbele ya waandishi kuwa; hajioni kuwa na kasoro kama Mtendaji Mkuu wa CCM na kwamba uamuzi ni wa wananchi.

Kauli yake kwamba; "uamuzi ni wa wananchi" ilizua maswali mengi kwa baadhi ya watu na hasa waliopata kuhisi au kuelezwa kuwa Kolimba anataka kuwania urais mwaka 1995. Kwamba alitaka awe Amiri Jeshi Mkuu wa tatu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

Maswali ni mengi na miongoni mwa hoja zilizoibuka ni kwanza; Kolimba ambaye si kiongozi wa kuchaguliwa (mteule) ni kwa vipi aseme wananchi wawe waamuzi wakati hawakuwahi kumchagua?

Je, alitaka kwenda kujipima kwa wananchi kwa njia ya kupigiwa kura baada ya kuachana na wadhifa wa kuteuliwa? Na je, kupigiwa kura katika nafasi ipi ya uongozi? Je, ni urais?

Swali kubwa zaidi ni; je, kwa kauli hiyo kama Kolimba angekwenda kugombea urais, asingeungwa mkono na Mwalimu Nyerere? Kama jibu ni hapana, je, angeungwa mkono na Mwinyi pamoja na viongozi wengine waliotofautiana na Mwalimu kuhusu uongozi wa nchi na hususan kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995?

Lakini katikati ya kile kinachoelezwa kuwa ni majibu ya Kolimba kwa Nyerere kupitia vyombo vya habari vya chama, wapo waandishi wa habari waliodokezwa kuhusu mipango ya Kolimba na ‘wakachochewa' ili kwenda kumuuliza Mwalimu.

Wamuulize kwanza; kama amesoma mfululizo wa makala kwenye magazeti ya chama ambazo ingawa zimeandikwa na ‘waandishi' (kwa majina mengine si Kolimba) lakini zinamjibu na hata kumshambulia.

Pili, nini majibu yake. Tatu, anadhani Kolimba anapata wapi ‘ujasiri' huo wa kutumia hata vyombo vya chama kwa maslahi yake kisiasa? Yalikuwa maswali ya kumchokoza Mwalimu na hata kupima upeo wake wa busara.

Majibu ya Mwalimu Nyerere ambayo pia yamenukuliwa katika baadhi ya machapisho nchini yanaeleza kwa kifupi lakini katika hali ya upeo mkubwa wa busara, pengine kinyume cha hata matarajio ya wanahabari hao kwamba Mwalimu angehamaki.

Mwalimu Nyerere ananukuliwa kuwajibu waandishi waliomfuata katika hali ya utulivu akitamka maneno sita tu. Akawajibu akisema; mwacheni aendelee, tutajibizana hoja kwa hoja."

Majibu haya ya Mwalimu bila shaka hayakukidhi matarajio ya waandishi wa habari waliokuwa wakifuatilia sakata hilo kwa kina, na hapa bila shaka, Katibu Mkuu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa sasa, Kajubi Mukajanga, anafahamu hili kwa namna fulani, wakati huo akiwa Mhariri wa gazeti la kila wiki la WAKATI ni HUU.

Lakini pia maneno hayo sita tu ya Mwalimu katika suala pana la mgogoro wa kiuongozi, yalithibitisha Mwalimu alikuwa na taarifa za Kolimba kutumia vyombo vya chama kumjibu, kisichojulikana dhahiri ni je, ‘wakubwa' gani walikuwa kambi ya Kolimba dhidi ya Nyerere?

Kwa kuzingatia mazingira hayo, wanahabari walizidi kuhoji kwa mfano; pamoja na kwamba Rais Ali Hassan Mwinyi, ni Mwenyekiti wa CCM na ameelezwa kuhusu ‘matatizo' hayo ya Kolimba kutumia vyombo vya chama kwa kadiri anavyotaka, kwa nini hafanyi lolote?

Maswali hayo na mengine yaliongeza joto na kwa kipekee, ukali wa joto uliongezwa na majibu ya Nyerere; mwacheni tutapambana kwa hoja. Hatimaye, kutokana na joto hilo Mzee Mwinyi akapewa tafsiri kuwa alikuwa akimuunga mkono Kolimba na hasa ikieleweka kuwa naye ni majeruhi katika kitabu cha Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania.

Wiki ijayo tutaangalia hoja za Kolimba katika kujibu mapigo ya Mwalimu Julius Nyerere, akitumia magazeti ya chama angali akiwa Katibu Mkuu, huku kimya cha Mwenyekiti wa chama, Ali Hasssan Mwinyi kikizidi kubeba tafsiri ya kumuunga mkono Kolimba.


PART 2


WIKI iliyopita katika sehemu ya kwanza ya mfululizo wa makala hizi, nilieleza katika hali ya kudadisi zaidi ni kwa nini viongozi wengi hawakuwa tayari kumkosoa Mwalimu Julius Nyerere hadharani na kama baadhi walithubutu, basi, walikuwa wachache mno na ukosoaji ulikuwa wa nadra.

Nilieleza kuwa wengi hawakuwa katika ‘mizani' sawa na Mwalimu kwa kigezo cha uadilifu mbele ya umma na hata wale waadilifu, ilitokea wakiiga njia ya uadilifu wa Mwalimu Nyerere. Lakini pia nilieleza licha ya nguvu hizo za kiuadilifu, Mwalimu alikuwa na ushawishi mkubwa katika mifumo ya kidola nchini.

Mifumo ya kidola ambayo alishiriki kuibuni na kuiridhia, akiwa Mkuu wa Nchi wa kwanza baada ya Uhuru wa iliyokuwa Tanganyika na hata Tanzania (baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar).

Nilieleza ni Mwalimu Nyerere ambaye ujasiri wake wa kumkosoa yeyote hadharani, ulivunja mipaka na hadi kumgusa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais aliyekuwa madarakani, Ali Hassan Mwinyi.

Ukosoaji huo pia uliwagusa bila woga, aliyekuwa Waziri Mkuu, John Malecela na aliyepata kuwa Katibu Mkuu wa chama tawala (CCM), Horace Kolimba. Hawa wote aliwakosoa kupitia kitabu chake cha Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania.

Makala ilieleza kuwa ni Kolimba pekee kati ya viongozi hao watatu ndiye aliyejitokeza kujibu mapigo dhidi ya Mwalimu kupitia makala maalumu katika magazeti ya chama (CCM), akiwa Katibu Mkuu, huku Mwinyi na Malecela wakibaki kimya.

Nikaeleza, Mwalimu alijua hilo hasa pale alipoulizwa wanahabari na kujibu akitamka maneno sita tu; mwacheni nitajibizana naye hoja kwa hoja. Hata hivyo, katika makala hiyo ya kwanza katika mfululizo wa makala hizi, kulikuwa na makosa.

Nilieleza Kolimba alitamka CCM kupoteza dira akiwa angali Katibu Mkuu wa chama hicho, ukweli ni kwamba alitamka hivyo lakini wakati akiwa tayari ameondoka kwenye nafasi hiyo.

Leo tunaendelea na sehemu hii ya pili ya mfululizo wa makala hizi. Katika sehemu hii ya pili, naanza kuchambua hoja za Kolimba katika kujibu mapigo dhidi ya Mwalimu Nyerere.

Kolimba ambaye kama tulivyoona katika sehemu ya kwanza ya mfululizo wa makala hizi, tayari alikuwa na nia ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995. Inawezekana ukosoaji wa Mwalimu dhidi yake aliutafsiri kama kikwazo na kwamba Mwalimu ameingilia nia yake hiyo (lugha ya siku hizi kumchafua-sio kumkosoa).

Inadaiwa kuwa Kolimba kupitia kwa mwandishi aliyetambulishwa kwa jina la Alex Kowe, aliandika makala katika gazeti la Uhuru, Novemba 8, 1994, takriban miezi 10 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 1995.

Miongoni mwa hoja zake katika makala husika ni malalamiko dhidi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Anamlalamikia Nyerere kwa kile anachokieleza kuwa ni hatua yake ya kumlazimisha Rais Ali Hassan Mwinyi, asipokee ushauri wake (Kolimba).

Ni Nyerere pekee angeweza kufafanua hili ingawa pia inawezekana alimuonya Mwinyi kutopokea ushauri wa Kolimba pengine baada ya kubaini ni aina ya kiongozi asiyeaminika kwa kiwango cha kuridhisha katika baadhi ya masuala ya kiuongozi.

Ni kutokana na maelezo ya Nyerere kwa Mwinyi kwamba ushauri wa Kolimba ni wa shaka, Kolimba mwenyewe anapinga hilo akisema haikuwa sahihi kwa sababu anaamini si wakati wote angekuwa na ushauri mbaya au ushauri wenye nia mbaya kwa Rais Mwinyi.

Ni katika mazingira hayo ya kumuonya Mzee Ali Hassan Mwnyi kutoamini moja kwa moja ushauri wa Kolimba, kuna maelezo pia yanayodai kwamba Nyerere alikuwa akimwona Rais Mwinyi kuwa ni kiongozi aliyezongwa na udhaifu wa kiuongozi.

Udhaifu aliouona Nyerere kwa Mzee Mwinyi unadaiwa ni kuhusu namna ya kuchuja (kupima) ushauri kutoka kwa viongozi wengine wanaomsaidia na hapa, izingatiwe kuwa, ushauri mbovu ni msingi wa uamuzi mbovu.

Kwa hiyo, Kolimba kupitia makala hiyo ambayo inadaiwa kuandikwa naye ingawa ilipewa jina (by-line) la Alex Kowe, anapingana na Nyerere kuhusu hoja ya udhaifu wa Mwinyi kiuongozi. Katika kupinga, Kolimba anadai kwamba udhaifu wa Mwinyi si kushindwa kuchuja (kupima) ushauri bali ni uungwana wake kupita kiasi.

Anasema Mwinyi ni muungwana kupita kiasi. Kwa mujibu wa Kolimba, msingi wa uungwana huo wa Mwinyi uliovuka mipaka ni mwelekeo wake wa kuchelea kumuudhi (kutompinga) Baba wa Taifa na hivyo kumpa mwanya wa kumyumbisha.

Kwa lugha nyingine, wakati Nyerere anaamini Mzee Mwinyi ni dhaifu katika baadhi ya masuala ya kiuongozi na hasa kupima ushauri anaopewa na wasaidizi wake, Kolimba aliamini huo si udhaifu kwa tafsiri halisi ya udhaifu, bali ni uungwana uliopita kiasi ambao Nyerere ‘aliutumia' kumyumbisha Mwinyi kiuongozi.

Kolimba anamgeukia Nyerere akijibu mapigo kutoka kitabu cha Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania dhidi yao (Kolimba na wenzake Mwinyi, Malecela) akimwelezea (Nyerere) kuwa ni mtu ambaye haambiliki na ni king'ang'anizi.

Katika mashambulizi yake kwa Nyerere ambaye tayari katika makala iliyopita tuliona alifuatwa na waandishi wa habari na wakamuuliza kuhusu mashambulizi dhidi yake kutoka kwa Kolimba naye akawajibu; mwacheni aendelee nitajibishana naye hoja kwa hoja, Kolimba anasema Nyerere akishikilia jambo lake huwa hashauriki kwa urahisi na wala hashawishiki.

Katika sentensi fupi akimwelezea Nyerere, Kolimba kupitia makala anayodaiwa kuiandika na kubandika jina la Alex Kowe, anamtafsiri akisema kwake (Nyerere); "msimamo kwanza na maslahi baadaye."

Kolimba anatetea tafsiri yake hiyo dhidi ya Nyerere (msimamo kwanza na maslahi baadaye) akiorodhesha mambo ambayo anaamini Nyerere aliyasimamia kwa kutanguliza msimamo badala ya maslahi ya nchi na hivyo, hayakuwa na mafanikio mazuri kwa nchi.

Mambo hayo ambayo Kolimba anaamini yalitekelezwa kwa msimamo usioridhia ushauri ni kwanza; Azimio la Arusha. Pili, operesheni vijiji. Tatu, kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyokuwa ikiundwa na nchi tatu- Tanzania, Kenya na Uganda (mwaka 1977).

Nne, mapambano yake (Nyerere) ya muda mrefu dhidi ya sera za Shirika la Fedha duniani (IMF), kwa wakati huo Mwalimu akikerwa mno na masharti ya shirika hilo kwa nchi masikini akifikia hatua kutamka IMF si Wizara ya Fedha ya Dunia.

Kolimba katika makala hiyo anayodaiwa kuiandika yeye, anamkabili Mwalimu akisema mambo hayo manne ni mifano na vielelezo vya misimamo mikali ya kisiasa ya Mwalimu Nyerere, ambayo haikutanguliza mbele maslahi ya taifa na watu wake. Hii ni sehemu ya pili ya mfululizo wa makala hizi kuhusu nini kilichotokea kati ya Kolimba na Mwalimu Nyerere?

Wiki ijayo tutachambua namna wakati fulani Kolimba alipofurahia ‘kusita' kwa Mzee Mwinyi kukidhi haja za shinikizo la Mwalimu Nyerere, kutaka yeye (Kolimba) na Malecela waondolewe madarakani. Tutaangalia je, Kolimba alichukuliaje uamuzi huo wa Mwinyi ambao hata hivyo, baadaye waliondolewa madarakani.

Kwake yeye Kolimba, kitendo cha Rais Mwinyi kukataa shinikizo la Mwalimu Nyerere kutaka Malecela na yeye waondolewe madarakani (jambo kuchelewa kutekeleza shinikizo hilo) ni kitendo cha ujasiri na wala si kielelezo cha udhaifu kama ambavyo Nyerere angetaka Watanzania waamini.


PART 3

WIKI iliyopita niliahidi kuendelea na sehemu hii ya tatu ya mfululizo wa makala hizi kuhusu nini hasa kilichotokea kati ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na aliyepata kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Horace Kolimba, ambaye pamoja na aliyepata kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Rais, John Malecela na Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, walikosolewa na Mwalimu kupitia kitabu chake maarufu cha Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania.

Kama tulivyoona katika makala zilizopita, ni Kolimba ambaye hakuwa tayari kukaa kimya kutojibu mapigo ya Mwalimu Nyerere tofauti na wenzake Mwinyi na Malecela ambao walikaa kimya, ingawa haijulikani walikuwa wakiunga mkono uamuzi huo wa Kolimba au la. Hata hivyo, tuliona Kolimba alijibu mapigo ya Mwalimu japo si kwa kujitokeza moja kwa moja hadharani. Alimjibu akitumia magazeti ya chama (CCM) ya Uhuru na Mzalendo, kwa kuandika makala zilizopewa jina la mwandishi Alex Kowe.

Leo tutaendelea na uchambuzi wa hoja za Kolimba ikiwa ni majibu dhidi ya mapigo ya Mwalimu Nyerere kupitia kitabu cha Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania. Kama nilivyodokeza wiki iliyopita, yapo maelezo kutoka duru za kiserikali kuwa wakati fulani Rais Mwinyi alisita kuufanyia kazi moja kwa moja ushauri au shinikizo la Mwalimu Nyerere kutaka Kolimba na Melecela waondolewe madarakani.

Uzito huo wa Rais Mwinyi kuwaondoa madarakani Malecela na Kolimba unathibitishwa na maelezo ya Kolimba katika makala zake, akitafsiri kuwa kitendo hicho cha Mzee Mwinyi cha kukataa shinikizo la Mwalimu Nyerere kuwaondoa wao madarakani ni cha ujasiri. Kwa mujibu wa Kolimba, kitendo hicho si kielelezo cha udhaifu kama ambavyo Mwalimu Nyerere angetaka Watanzania waamini.

Katika makala yake ya Novemba 18, mwaka 1994, Kolimba, kupitia kwa mwandishi Alex Kowe, anamshambulia Mwalimu kuhusu hoja ya Serikali tatu, ambayo Mwalimu alipata kuichambua vizuri kwa mwelekeo wa kuainisha kigezo cha udhaifu wa viongozi hao. Kolimba anamshambulia Mwalimu Nyerere akidai kuwa ameshindwa kuona ukweli juu ya hoja ya Tanganyika na Serikali tatu.

Kwa mujibu wa Kolimba ukweli alioshindwa kuuona Mwalimu ni kwamba; "hoja ya serikali tatu ndani ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar imetokana na ubovu wa misingi ambayo Muungano huo umesimikwa na si udhaifu wa viongozi. Mtazamo wa Kolimba ni kwamba kuzidi kuwakosoa viongozi kuwa ni dhaifu kwa sababu ya hoja hiyo ni sawa na "kumwaga damu" za viongozi husika na kwa hiyo, Kolimba anasema kwamba, bila kurekebisha misingi hiyo (ambayo Muungano umesimikwa juu yake) basi, "damu za viongozi zitazidi kumwagika".

Katika makala yake hiyo, Kolimba anarejea kile kilichopata kumkuta aliyekuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Aboud Jumbe. Anasema Aboud Jumbe alikumbwa na maafa mwaka 1984 pale hoja ya Serikali tatu ilipojitokeza. Lakini mbali na Jumbe, Kolimba anasema maafa hayo pia yalimfika aliyekuwa Waziri Kiongozi, Seif Sharrif Hamad, baada ya kuhisiwa kwamba alikuwa mchochezi wa chini chini wa kuitisha kura ya maoni Zanzibar, kuhusu uhalali wa Muungano.

Katika kufikisha ujumbe wake bila kubainika ni yeye aliyeandika makala hizo na kuzipa jina la Alex Kowe, Kolimba anaandika; "Safari hii, Mwalimu ameamua kuwakalia shingoni Malecela na Kolimba. Na inaelekea mzimu wa Tanganyika bado utaendelea kuhitaji damu zaidi."

Lakini anaendelea mbele kujibu mapigo ya Mwalimu Nyerere akihoji na kutafakari ni kwa nini Mwalimu Nyerere huyo huyo, hakumshambulia aliyekuwa Jaji Mkuu, Francis Nyalali, ambaye aliongoza Tume ya Mfumo wa Vyama na kujikuta akichambua masuala ambayo hayakuwa sehemu ya hadidu za rejea kwa tume hiyo, kwa sababu Nyalali naye alipendekeza kuwapo kwa Serikali tatu.

Hapo Kolimba anaandika; "...na sijui kwa nini Mwalimu hakudai kwamba damu ya Jaji Mkuu, Francis Nyalali nayo imwagike kwa kufufua hoja ya Tanganyika bila hata kutumwa na wananchi? Lakini baada ya kujiuliza na kutafakari, Kolimba mwenyewe anabuni majibu ambayo Mwalimu angeweza kuyatoa kuhusu "damu ya Nyalali" kutomwagwa kwa hoja ya Tanganyika. Anaingia katika fikra za Mwalimu na kubahatisha kuwa pengine Mwalimu angejibu kwa kusema "mjumbe hauawi," na kutokana na jibu hilo, Kolimba anaendelea kuhoji; "...lakini Jaji Nyalali katumwa na nani?"

Lakini kwa upande mwingine wakati Kolimba akiingia katika kile kilichopata kuelezwa na gazeti la WAKATI ni Huu kwamba ni malumbano dhidi ya Mwalimu Nyerere, katika wakati ambao Waziri Mkuu na Makamu wa Rais, Malecela na Mwinyi wakitajwa kukaa kimya, duru za habari serikalini zilikuwa zikitafakari mazingira ya mgawanyiko mkubwa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho kilikuwa katika ukingo wa safari kuteua mgombea urais ambaye atakuwa mrithi wa Ali Hassan Mwinyi ambaye mbele ya Mwalimu Nyerere, hakuwa kiongozi imara kiasi cha kutosha.

Na hapa ikumbukwe nafasi ya Mwalimu Nyerere katika mgawanyiko huo ambao ulikwishaanza kuonyesha dalili za wazi ndani ya CCM. Nafasi ya Mwalimu inayopaswa kukumbukwa hapa ni kwamba, ndiye kiongozi ambaye kwa wakati huo alikuwa na ushawishi mkubwa katika mifumo ya kidola na hususan idara nyeti ya usalama wa taifa, ikielezwa kuwa maofisa wengi wa idara hiyo waliamini katika uadilifu wa Mwalimu na uzalendo wake kwa nchi katika kiwango tofauti na Rais aliyekuwa madarakani kwa wakati huo.

Kwa hiyo, nguvu ya Mwalimu mbele ya umma na ndani ya mifumo wa kidola ilikuwa kubwa mno kiasi hata cha kutishia uhai wa CCM kuendelea kukamata dola katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, kama ingetokea Mwalimu Nyerere ambaye alipata kutamka CCM si mama yake na hivyo angeweza kukihama chama hicho na huku akionyesha mwelekeo wa kuvutiwa kwa kiasi fulani na chama ambacho hakikuwa na umaarufu wowote, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), lakini kikiongozwa na mtu ambaye alikwishawahi kufanya kazi na Mwalimu, Edwin Mtei.

Hata hivyo, kwa wakati huo CHADEMA kilichoonekana kumvutia Mwalimu kuliko vyama vingine maarufu kikiwamo NCCR-Mageuzi na CUF, hakikuwa kikiunga mkono wazi wazi na kwa ‘sauti' kubwa Muungano wenye sura ya Serikali tatu, ambazo Mwalimu Nyerere aliamini ni mwelekeo wa kuvunja Muungano na kubwa zaidi, ni udhaifu wa viongozi ambao wakati nchi kubwa zikihangaika kujenga mazingira ya kuungana, "vi-nchi" vidogo vinafikiria kutengana na hasa kwa sababu ya uroho wa madaraka na si maendeleo ya wananchi ambao umoja miongoni mwao ni nyenzo muhimu zaidi.

Wiki ijayo katika mwendelezo wa makala hizi, tutarejea mikasa au vituko alivyowahi kukumbana navyo Mwalimu Nyerere Ikulu ya Magogoni, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni pamoja na siku ambayo alifika Ikulu kwa ajili ya kukutana na aliyekuwa Rais wa Ireland, Bi. Mary Robinson, Oktoba 1994.

PART 4
WIKI iliyopita katika mfululizo wa makala hizi, nilirejea baadhi ya hoja za aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Horace Kolimba, katika kujibu mapigo dhidi ya ukosoaji wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwake na wenzake ambao ni Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na aliyekuwa Waziri Mkuu, John Malecela, kupitia kitabu chake maarufu, Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania.

Niliahidi pia wiki hii kurejea baadhi ya vituko alivyokutana navyo Mwalimu Nyerere, ikiwa ni pamoja na siku alipofika Ikulu, Dar es Salaam, kuzungumza na aliyekuwa Rais wa Ireland, Bi. Mary Robinson.

Itakumbukwa kuwa katika makala zilizopita na hasa makala ya kwanza, nilieleza namna ambavyo haikuwa ikijulikana wazi kama Rais Mwinyi kwa wakati huo na Waziri Mkuu Malecela, walikuwa wakiunga mkono mapigo ya Kolimba dhidi ya Nyerere, na hasa ikizingatiwa Kolimba alijibu akitumia magazeti ya chama (Uhuru na Mzalendo), akiwa Katibu Mkuu na mwenyekiti wake, Rais Mwinyi akibaki kimya.

Katika ukimya huo, kuna mambo tunaweza kuyatafakari. Kwanza, inawezekana Mwinyi na Malecela na baadhi ya viongozi wakubwa walikuwa nyuma ya Kolimba lakini hawakutaka kumkabili Mwalimu moja kwa moja na kwa hiyo, wakatumia matukio mengine kuzidi kumkosesha ‘raha' Mwalimu Nyerere ambaye hakuwa na madaraka zaidi ya kuwa mstaafu, ingawa aliendelea kuwa na ushawishi katika mifumo ya dola.

Hebu turejee baadhi ya mikasa inayoweza kuhusishwa na ‘hasira' dhidi ya Mwalimu ambaye aliamini uongozi umefeli katika masuala muhimu ya kuongoza nchini kwa wakati huo hadi kutunga kitabu cha kuukosoa uongozi huo.

Jumanne ya Oktoba, 11 mwaka 1994, moja ya magazeti ya binafsi nchini lilichapisha habari ikiwa na kichwa cha habari; "Nyerere akosa mapokezi Ikulu."

Lilikuwa ni gazeti la kila wiki (WAKATI ni Huu), wakati huo likitamba katika kuibua habari zenye mitafaruku (controversies), Mhariri wake akiwa Katibu Mkuu wa sasa wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga.

Ikumbukwe kuwa kwa wakati huo, tayari Mwalimu alikwishaanza kuwakosoa viongozi waandamizi wa Serikali, akiwamo Rais kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa kiuongozi na nchi ilikuwa ikielekea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995.

Mwandishi wa gazeti hilo ambaye hakutajwa jina aliripoti kwamba; "katika hali isiyokuwa ya kawaida, maofisa wa Ikulu mwishoni mwa wiki walishindwa kumpokea rais mstaafu, Mwalimu Nyerere wakati alipowasili katika ofisi za Ikulu kwa mazungumzo na Rais wa Ireland , Bi. Mary Robinson.

"Ingawa ratiba ya ziara ya Rais wa Ireland iliyotolewa siku moja kabla ya kuwasili kwake ilikuwa inaonyesha wazi wazi kuwa Mwalimu angekuwa na mazungumzo na Rais huyo, hakuna kiongozi wa Ikulu aliyeonyesha kujishughulisha kumpokea".

Mwandishi anaendelea kuandika; "Mwalimu ambaye alifika Ikulu saa kumi na moja na robo, jioni Ijumaa, alijikuta hana mtu wa kumlaki na kumwelekeza."

Lakini swali jingine ni je, hali ilikuwaje katika kumnusuru Mwalimu? Hapo, mwandishi huyo anaandika kwamba, ili kumuepusha Mwalimu Nyerere na balaa la kuendelea kuduwaa, mpambe (msaidizi) wake alimpeleka kwenye makochi inapofanyika mikutano ya kila wiki ya waandishi wa habari na mwandishi wa Rais (Patrick Chokala).

Katika hali inayothibitisha mwandishi alikuwa akishuhudia kile ambacho yeye na waandishi wenzake walikiita ni udhalilishaji dhidi ya Mwalimu Nyerere, mwandishi huyo anaandika; "….kabla ya kuketi, Mwalimu alichukua muda kuangalia huku na kule kulitazama jumba lililokuwa ofisi yake miaka tisa iliyopita."

Na baadhi ya waandishi wa habari waliokuwapo wakati Nyerere anawasili Ikulu, walisema kuwa kitendo hicho cha kutokuwapo mtu wa kumlaki Nyerere kilikuwa cha kumdhalilisha.

Waandishi hao wananukuliwa wakisema; "Huu ni udhalilishaji. Haiwezekani viongozi wa itifaki wa hapa washindwe kuwa na mawasiliano kwamba Mwalimu anawasili."

Pengine tuzidi kukumbushana, hatupo nje ya mada kuu kwamba nini kilichotokea kati ya Kolimba na Nyerere, kwa sababu, tunalo swali la msingi, je, mapigo ya Kolimba dhidi ya Nyerere yalikuwa yakiungwa au kutoungwa mkono na viongozi wengine waandamizi ambao Nyerere aliwashambulia kwa pamoja?

Na kabla ya kuachana na kisa hiki kinachotusogeza katika nafasi ya kutafakari kama ukosoaji wa Mwalimu dhidi ya viongozi waandamizi, ikiwamo Ikulu, uliwakasirisha kiasi cha kumfanyia vituko, tutazame nani aliokoa jahazi la udhalilishaji.

Inaelezwa kuwa, siku hiyo kama asingekuwapo aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Ali Mchumo, Mwalimu angezidi kuzubaa hapo Ikulu.

Alikuwa msaidizi wa Mwalimu ndiye aliyemuona Balozi Mchumo, akamwita kutoka katika chumba (ofisi) alimukuwamo Rais Mwinyi na mgeni wake, Bi. Robinson na kwa mujibu wa ofisa mmoja wa Ikulu aliyezungumza na mwandishi huyu, basi Nyerere angeendelea kusubiri kwa muda mrefu na iliaminika kuwa uvumilivu ulianza kumwishia Mwalimu na alikuwa akijiandaa kuondoka Ikulu, bila kuonana na mgeni, kama ilivyopangwa kwenye ratiba.

Taarifa ya habari RTD ‘yazimwa'

Iliripotiwa na moja ya magazeti na tena bila kukanushwa siku zilizofuata, kwamba aliyekuwa Waziri wa Habari na Utangazaji, Dk. William Shija, alizuia taarifa ya habari ya saa mbili usiku, kutosomwa kwa habari iliyotokana na mkutano kati ya Nyerere na waandishi wa habari, waliokutana nyumbani kwake, Msasani, jijini Dar es Salaam.

Kwa wafuatiliaji wa mambo, itakumbukwa kuwa kulikuwa na mvutano mkubwa kati ya msimamo wa Mwalimu Nyerere na Serikali ya Tanzania, chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi, kuhusu mauaji yaliyokuwa ya raia yaliyokuwa yakiendelea nchini Rwanda, na mvutano huu ni kati ya mambo ambayo, Nyerere aliamini uongozi wa nchi ulikuwa ukiyumba si tu kutokana na udhaifu wa Rais, bali hata washauri wake wakuu.

Ilikuwa Julai 4, mwaka 1994, Mwalimu alikutana na waandishi wa habari na akishinikiza Serikali ya Tanzania , nchi aliyokuwa akiifahamu kuwa madhubuti katika kutetea haki za watu popote duniani, iweke wazi msimamo wake kuhusu Rwanda .

Hadi Mwalimu anazungumza, tayari takriban watu 700,000 walikwishauawa katika vita ya wenyewe kwa wenyewe Rwanda, tangu Aprili 6, 1994 alipouawa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Juvenal Habyarimana.

Mwandishi wa habari wa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) aliyehudhuria mkutano huo wa Nyerere alirudi ofisini, akaandika kilichojiri huko kwa ajili ya kurushwa hewani katika habari ya saa 2:00 usiku kama kawaida.

Lakini licha ya habari hiyo kupitiwa na mhariri wa zamu na mhariri mkuu na kuridhiwa, inadaiwa kiongozi mmoja wa zamu (studio) alimpigia Waziri Shija, kumuuliza habari hiyo itangazwe au la. Ikabidi Waziri Shija akasomewe kwanza habari hiyo kabla ya kuamua na baada ya kusomewa, akakataa itangazwe.

Swali muhimu ni je, kwa nini habari ya Mwalimu ilizuiwa? Je, ni kwa sababu inaishinikiza Serikali? Je, ni kwa sababu imetamkwa na Nyerere bingwa wa kuwakosoa viongozi waliokuwapo madarakani? Au je, ni kwa sababu kuna viongozi walijenga mtandao wa kumuasi Mwalimu? Na kama kulikuwa na mtandao huo, je, ulikuwa nyuma ya mapigo ya Kolimba dhidi ya Nyerere?

Kimsingi, katika mkutano wake na waandishi wa habari, Mwalimu ambaye baadaye alikuwa msuluhishi wa mgogoro huo wa Rwanda , aliilaumu Serikali kwa kushindwa kueleza msimamo wake wa wazi katika vita hiyo ya Rwanda .

Waandishi waliokuwapo kwenye mkutano huo wa Mwalimu waeleza alichosema Nyerere kuwa; "…anashindwa kuelewa ni vipi nchi iliyokuwa huko nyuma inao msimamo unaoeleweka ilikuwa inayumba kiasi hicho katikati ya wimbi lenye kasi kubwa ya mauaji ya raia wa nchi jirani.

Ikulu yasema ni hisia za Nyerere

Kama tulivyojiuliza maswali machache hapo awali, je, kwa nini Mwalimu aliandamwa? Sasa baada ya mkasa huo wa Nyerere na RTD, mkasa ambao ni wenye mwelekeo wa kuzidi kukosoa uongozi mkuu wa nchi, aliyekuwa mwandishi wa habari wa Rais, Patrick Chokala, alikutana naye na waandishi wa habari, Ikulu siku chache baadaye.

Lakini katika mkutano huo, Chokala hakutoa nafasi kwa waandishi kumuuliza maswali zaidi, ingawa mada ya mkutano wake huo ilikuwa kuhusu suala la Rwanda , ambalo kwa mujibu wa ukosoaji wa Mwalimu, uongozi wa nchi ulikuwa unayumba kimsimamo.

Chokala pengine akitambua kuwa waandishi walikuwa wanazo taarifa nyingi zaidi ambazo ni mbaya kwa Serikali, alimpinga tu Mwalimu kwa kusema alichopata kueleza ni "hisia zake" tu na kukwepa maswali.

Nyerere ‘alimkumbuka' Karume?

Bila shaka, ukosaji wa Nyerere dhidi ya akina Kolimba na wenzake kupitia kitabu cha uongozi wetu na hatima ya Tanzania , umezingatia mambo mengi.

Bila shaka, ukosoaji wake haukuzingatia tu mwenendo alioamini wa ovyo kuhusu namna uongozi unavyoamua, kudhibiti au kutolea msimamo mambo mazito ya nchini na kimataifa, bali pia ulizingatia namna walivyoihangaikia nchi, yeye na waasisi wenzake, akiwamo Abeid Amani Karume na hasa zinapojitokeza dalili za kuhujumu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar .

Utaona kwamba, licha ya Mwalimu kuchukizwa na namna uongozi ulivyoyumba kusimamia Muungano, lakini pia alichukizwa na namna uongozi unavyoshughulikia mambo mengine ya msingi yenye kujenga taswira ya nchi kimataifa. Yote haya yalimfanya kuwakosoa washauri wakuu wa Rais na Rais mwenyewe, kupitia kitabu chake.

Ni kweli, yapo mengi yanayoelezwa kuonyesha pengine Karume alichoshwa na Muungano ambao Nyerere aliutetea na hata kuwakosoa baadhi ya viongozi.

Lakini hata hivyo, ni Karume huyo huyo, ambaye aliwahi kunukuliwa na gazeti la The Nationalist (sasa Daily News), akisema Muungano unanufaisha wananchi, asiyeutaka ahame nchi."

Gazeti la Julai 30, mwaka 1964, The Nationalist, liliandika habari hiyo kutokea Zanzibar nami ninukuu katika lugha iliyotumika; "The first vice president of the United Republic, Abeid A. Karume told a mammoth rally here yesterday (July 29) that anyone who did not like the union between Tanganyika and Zanzibar "should quit the soil of the United Republic immediately."

Na katika hali ya msisitizo kwenye mkutano huo uliotajwa kuhudhuriwa na watu zaidi ya 50,000, gazeti linaandika katika lugha ya Kiingereza likimnukuu Karume; "The Union has been created for the benefit of the people of the two countries. It embraces their aspirations…..The doors of the United Republic are open to any of our brothers who want to unite with us.

Kwa kiongozi aliyetambua malengo halisi ya Muungano kama hivi ambavyo Karume alivyonukuliwa akisema; bila shaka, si ajabu kumwona Nyerere akipingana na waliokuwa wakitishia uhai wa Muungano lakini kubwa zaidi, kuona Serikali na uongozi wa nchi ukiyumba katika masuala ya msingi ya kiuongozi, kama tulivyoona kupitia makala ya leo kuhusu vituko dhidi ya Mwalimu.

PART 5
WIKI iliyopita katika sehemu ya nne ya mfululizo wa makala hizi nilieleza baadhi ya vituko alivyokumbana navyo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, katika mwelekeo unaodhihirisha ni mwendelezo wa mapigo kwa ukosoaji wake dhidi ya viongozi waandamizi nchini.

Nilieleza namna aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Ali Mchumo, alivyomuepusha na balaa Mwalimu Nyerere, aliyefika Ikulu kukutana na aliyekuwa Rais wa Ireland, Bi. Mary Robinson.

Nilieleza namna aliyekuwa Waziri wa Habari na Utangazaji, Dk. William Shija, alivyozuia kipengele cha taarifa ya habari ya saa mbili usiku Redio Tanzania, kilichohusu mkutano kati ya wanahabari na Mwalimu Nyerere, kwake Msasani Dar es Salaam.

Hata wiki nalazimika kufanya masahihisho, kwanza Nyerere baadaye hakuwa msuluhishi wa mgogoro wa Rwanda bali Burundi, pili; gazeti la The Nationalist nililonukuu na kusema ndilo Daily News kwa sasa, si sahihi ukweli ni kuwa, Daily News imetokana na gazeti la The Standard.

Leo tujikite katika kauli ya Kolimba kuhusu hoja ya serikali tatu ndani ya Muungano, kwa sababu hoja hiyo ni kati ya mambo yaliyomfanya Mwalimu Julius Nyerere kukosoa uongozi wa nchi (akina Kolimba, Malecela na Mwinyi mwenyewe), kupitia kitabu chake cha Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania.

Tuendelee na mfululizo wa makala hizi kwa kugusa moja ya hoja iliyotumiwa na Kolimba, kujibu mapigo ya ukosoaji kutoka kwa Mwalimu.

Itakumbukwa katika moja ya makala zilizopita, tulieleza majibu ya Kolimba dhidi ya Nyerere na hasa alipojenga hoja kuwa, Mwalimu hataki kutambua, mantiki ya serikali tatu inatokana na misingi mibovu ambayo Muungano umesimikwa juu yake na kwamba tatizo si viongozi.

Nilieleza, kwa sababu Nyerere aliwaandama viongozi waandamizi waliokuwa wakishabikia serikali tatu ndani ya Muungano, Kolimba pia alihoji ni kwa nini Nyerere huyo huyo, hakumwandama aliyekuwa Jaji Mkuu, Francis Nyalali?

Nyalali ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa tume kuhusu mfumo wa vyama vya siasa na nje ya hadidu za rejea za tume hiyo, Nyalali na wenzake walipendekeza serikali tatu na hapo Kolimba akahoji; "Kwa nini damu ya Nyalali haikumwagika?" Yaani kwa nini Nyerere hakumwandama?

Leo, tuingie kwenye fikra za Kolimba kwa wakati huo kwa kurejea mahojiano kati yake na aliyekuwa mwandishi wa gazeti la Mzalendo, Joseph Kulangwa, yaliyochapishwa Juni 26, mwaka 1994.

Joseph Kulangwa (sasa ni Mhariri Mkuu-gazeti la Serikali la HabariLeo), alifanya mahojiano na Kolimba yaliyochapishwa katika safu ya "ana kwa ana" kwenye gazeti la Mzalendo.

Kulangwa alimuuliza Kolimba maswali tisa.

Lakini kabla ya kuanza kuuliza swali lake la kwanza, mwandishi alitoa maelezo akisema; "Wabunge hivi sasa wameanza kulipenyeza suala la Serikali ya Tanganyika katika majadiliano ya Bunge, wakati huo huo, utaratibu uliokubaliwa kutumika kuliamua suala hilo katika kikao cha pamoja, haieleweki umefikia wapi."

Lakini kwa maelezo haya tu ya mwandishi, ukifanya tafakari fupi utabaini; mosi, kulikuwa na nguvu fulani nyuma ya wabunge, kusukuma suala la serikali tatu liingie bungeni.

Lakini je, nguvu (external force) hiyo inajumuisha viongozi gani ambao si miongoni mwa wabunge? Je, ni pamoja na wale ambao Mwalimu aliwakosoa na kueleza bayana, ushauri wao kwa Rais si mzuri, akiwamo Kolimba na hata Waziri Mkuu, John Malecela?

Pili, utabaini pia kuna nguvu nyingine tofauti inayoelekeza kupambana kuzima suala hilo kwa kutengeneza "utaratibu wa namna ya kuliamua suala hilo" kwa mujibu wa maelezo ya mwandishi aliyemuhoji Kolimba.

Kwa hiyo, kwa kuzingatia maelezo hayo ya mwandishi ambaye bila shaka alikuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu kadhia hiyo, ni dhahiri kulikuwa na ‘kambi' ya Mwalimu Nyerere na kambi pinzani (inawezekana ni akina Kolimba na wenzake). Baada ya tafakari hiyo fupi kutokana na maelezo ya mwandishi, turejee katika swali.

Swali la mwandishi kwa Kolimba lilikuwa; "Chama kinatarajia kulikabili vipi shinikizo la wabunge kuhusu hoja hiyo?

Kabla ya kujua Kolimba alijibu nini, ndani ya swali hili utabaini kuwa; ni kama vile ‘kambi' ya Mwalimu Nyerere (kama ilikuwapo) ilikuwa ikitumia mbinu mbalimbali kuzima suala hilo lisizidi kugawa nchi na hata kuifanya isitawalike na hatimaye kuvunga Muungano kupitia ‘uchochoro' wa serikali tatu.

Na mbinu mojawapo ni hiyo, kutumia chama (chenye hatamu na wabunge wake) kulikabili suala hilo mbinu ambayo hivi karibuni pia ilitumika kuzima wabunge wenye uchu wa posho nono, kwa chama kutoa kauli ya kupinga suala hilo.

Je, Kolimba alijibu nini? Baada ya maelezo na swali hilo, Kolimba akajibu: "Suala la serikali tatu ni hoja kubwa ambayo haitakiwi kuchukuliwa kwa pupa. Kwa hiyo, naamini bado tunao muda wa kutosha kulifanyia kazi.

Akaendelea; "Maoni ya wana-CCM tayari yamepokewa na Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM inayotarajiwa kukutana baadaye mwezi ujao (Julai, 1994) itayatafakari maoni hayo.

"Nina uhakika pia kwamba Serikali itajipa muda ili yapatikane maelewano kati ya wabunge, Serikali na CCM yenyewe. Siwezi kusema muda huo utakuwa upi, lakini ikumbukwe kwamba Azimio la Bunge lilisema suala hilo litakuwa limepatiwa ufumbuzi ifikapo Aprili, mwakani (1995).

Hayo ndiyo majibu ya Kolimba ambayo bila shaka, wakati wote wa chama kushughulikia suala hilo iwe kwa kusikiliza maoni ya wadau au vyovyote, ilikuwa ni wakati ambao misiguano ya mabishano ilikuwa ikiendelea chini kwa chini.

Inawezekana, kwa kadiri vuguvugu hili lilivyokuwa likishika kasi sambamba na jaribio la kutaka kulizima kwa kutumia chama likiendelea huku Kolimba akiwa Katibu Mkuu wa chama; je, Mwalimu Nyerere alikuwa na sababu za msingi kusaidia kulizima suala hili?

Ingekuwaje kama Nyerere angebaki kijijini Butiama akipalilia mahindi shambani kwake? Sauti ya ukosoaji kwa nguvu ya hoja na hata ikibidi hoja za nguvu kutoka kwa Mwalimu Nyerere ilikuwa na ulazima?

Pengine akikumbuka kilichowahi kutokea mwaka 1984, chini ya ‘mkono' wa Aboud Jumbe, Nyerere aliamini hicho ndicho kilichokuwa kikielekea kutekelezwa na Rais wa wakati huo Zanzibar, Dk. Salmin Amour Juma na hivyo, na hivyo ilibidi kuingilia kati.

Ikumbukwe, kiini cha masuala haya ni pamoja na Dk. Salmin ambaye alionekana kuwa na ‘mabavu' kiuongozi kuliko uongozi wa juu wa Jamhuri ya Muungano.

Salmin, pamoja na mambo mengine alitaka kuiburuza Zanzibar kujiunga na Umoja wa nchi za Kiislamu (OIC), bila kujali kufanya hivyo ni kuutia nyufa Muungano.

Swali la pili kwa Kolimba

Kabla ya kuendelea kuuliza swali la pili, mwandishi aliyemuhoji alitoa maelezo mafupi ya utangulizi kwa akisema; "kauli na vitendo vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar badala ya kutafuta muafaka vinaelekea kuchochea hisia za ‘wabara' kudai Serikali yao.

Anatoa mifano akisema; "mifano ya hivi karibuni ni suala la ushuru wa makontena ambalo limeamuliwa nje ya sheria za Serikali ya Muungano na hivi juzi uamuzi wa kuanzisha kitengo cha Usalama wa Taifa maalumu kwa Zanzibar." Kisha anamuuliza Kolimba; "unasemaje kuhusu hali hiyo?

Lakini kabla ya majibu kama tulivyofanya kwa swali la kwanza, tutafakari maelezo haya. Ni kwamba, mifano yote hiyo imejikita katika kudhihirisha uongozi wa Zanzibar ulilenga kuvunja sheria zilizokuwapo na si kupendekeza zifanyiwe marekebisho.

Kwa uongozi makini wenye malengo ya maridhiano na ustaraabu na hasa uongozi ambao uko madarakani, sheria hazivunjwi bali hupendekezwa kufanyiwa marekebisho kwa kadiri inavyofaa.

Uongozi kushabikia na kutekeleza uvunjaji wa sheria zinazokera kwao si ishara njema.

Ni kiashiria cha mpasuko, tena mpasuko wenye kuzongwa na maslahi yanayotarajiwa baada ya kutengana.

Baada ya tafakari hiyo fupi; je, Kolimba alijibu nini? Kwa swali hilo, alijibu: "Naamini kuwa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya Rais wa Zanzibar wanaupenda Muungano.

Wao ni viongozi ambao tunaweza kuwategemea kutatua matatizo ya mahusiano yaliyopo katika Muungano.

Hiyo ni sehemu ya majibu ya Kolimba na kabla ya kuendelea na sehemu nyingine ya majibu kuhusu swali aliloulizwa, tutafakari; Kolimba anasema anaamini viongozi Zanzibar wanaupenda Muungano.

Swali hapa ni je, kama waliupenda Muungano ni kwa nini walivunja baadhi ya sheria za Jamhuri (rejea uamuzi kuhusu makontena) badala ya kupendekeza zifanyiwe marekebisho?

Je, Kolimba alikuwa akiwalinda licha ya kutambua kasoro nyuma ya viongozi hao kuhusu Muungano?

Na je, kwa namna hiyo ya Kolimba ‘kufunika' kombe badala ya kuwa muwazi, ilitosha kwa Mwalimu Nyerere kumtilia shaka na hasa ushauri anaoweza kumpa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wakati huo, Ali Hassan Mwinyi?

Kitengo cha usalama wa taifa Zanzibar

Tuendelee na sehemu ya majibu ya Kolimba kuhusu kitengo cha usalama; "...suala hilo nimeliona tu kwenye magazeti. Sina uhakika na madaraka ya kitengo hicho.

Siamini kuwa kimeondoa ama kuchukua au kuingilia kazi za idara za ulinzi na usalama katika Muungano. Kitengo hicho kinazuia uvujaji wa siri za Serikali toka ofisi mbalimbali za Serikali visiwani.

Anaendelea; "...chombo chochote kitapenda kuhakikisha kwamba taarifa za serikali zinazotoka ni sahihi na kuwa zinatolewa kwa utaratibu unaotakiwa.

Nadhani ndiyo nia kubwa ya kitengo hicho. Lakini nasisitiza kwamba sina taarifa kamili ya kitengo chenyewe.

Hayo ndiyo majibu yake, lakini cha kutafakari ni je, kwa nini atoe majibu hayo yenye mwelekeo wa kulinda ‘kasoro' ya SMZ ilihali akikiri kutokuwa na taarifa kamili kwa mfano, kitengo cha usalama wa taifa alichoanzisha Dk. Salmin Amour?

Je, hii pia ni sababu iliyomfanya Nyerere kumhesabu Kolimba kuwa ni kati ya viongozi ambao Rais hapaswi kuamini moja kwa moja ushauri wao kama tulivyopata kuona katika makala zilizotangulia na hasa pale Kolimba alipolalamika kwamba Nyerere anamshawishi Mwinyi kutoamini ushauri kutoka kwake?

Wiki ijayo tutaendelea na uchambuzi wa maswali kwa Kolimba hali itakayotuweza kubaini kama Kolimba kwa majibu yake mwenyewe alikuwa na mawasiliano na kundi la wabunge waliokuwa wakitaka serikali tatu ndani ya Muungano, maarufu kama G55?

`


WIKI iliyopita, katika mfululizo wa makala hizi tulijadili majibu ya Kolimba wakati wa mahojiano kati yake na mwandishi wa habari wa gazeti la Mzalendo, Joseph Kulangwa (kwa sasa ni Mhariri Mkuu gazeti la Serikali la Habarileo.

Tulichambua mantiki ya maelezo ya mwandishi na hata baadhi ya hoja katika majibu ya Kolimba, tukizidi kutafakari kwa nini Mwalimu Nyerere amewahi kuwakosoa viongozi wakuu akiwamo Kolimba, kupitia kitabu chake cha "Uongozi wetu na hatima ya Tanzania."

Tuliwahi kuona kwenye makala zilizotangulia, Kolimba kupitia kwa mwandishi wa makala aliyepachikwa jina lisilo halisi la Alex Kowe, akimlalamikia Nyerere kwa hatua yake ya kumtaka Rais Ali Hassan Mwinyi, asiamini ushauri wa kiuongozi kutoka kwa Kolimba.

Leo, tutamilizia baadhi ya maswali kwa Kolimba kutoka kwa mwandishi aliyemhoji. Maswali ambayo yanahusu kiini cha hoja iliyoleta mtafaruku kwa Mwalimu Nyerere, kiasi cha kuwakosoa wazi wazi viongozi aina ya Kolimba na wenzake.

Kati ya maswali yake tisa, mwandishi alimuuliza Kolimba; "Kauli za baadhi ya wabunge ndani na nje ya Bunge hazionyeshi kuheshimu na kuzingatia kanuni zinazotawala mwenendo wa wabunge wa CCM ndani ya Bunge. Chama kitaidhibiti vipi hali hii na wakati huo huo, kuepusha hofu ya kutokea mgawanyiko kama inavyodhaniwa na baadhi ya Watanzania?"

Hapa, kabla ya kuingia kwenye majibu ya Kolimba, ikumbukwe kuwa swali hili lililenga zaidi kundi maalumu la "kushinikiza" kupatikana kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano, maarufu kama G55 na Kolimba akiwa Katibu Mkuu wa CCM, wadhifa ambao baadaye aliupoteza (kutokana na shinikizo la Mwalimu Nyerere?).

Lakini kwa upande wa majibu ya Kolimba, maelezo yake ya mwanzo kulingana na swali hilo ilikuwa ni kukiri kuwapo mawasiliano kati yake na baadhi ya wabunge wanaounda G55. Katika kauli ambayo kwa namna fulani inaweza kutoa tafsiri ya msimamo wa Kolimba kuhusu sakata hilo, alijibu akisema; ingawa wanadai Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano, wabunge hao hawapendi kuonekana waasi.

Kolimba anajibu; "Nabahatika sana kupata fursa ya kuongea na wabunge wetu na wale walioko katika kundi la wabunge 55. Jambo ambalo linafurahisha ni kwamba wabunge wote nilioongea nao wanaonyesha mapenzi makubwa kwa chama chao na hawapendi waonekane kuwa waasi.

"Zipo tofauti zinazohusu suala la serikali tatu, kazi ya CCM ni kuhakikisha kwamba tofauti hizo zinachambuliwa na kutolewa maelekezo wazi wazi kabisa.

"Miongoni mwao sijawahi kumsikia hata mmoja anayependelea kuvunjika kwa Muungano au kuvunjika kwa CCM. Lakini kwa upande wa CCM kipindi hiki itasisitiza nidhamu ya viongozi wote wakiwamo wabunge wetu.

"CCM haitasita kumsuta au kumrekebisha kiongozi yeyote ambaye mwenendo wake utaathiri maadili ya chama. Huu ni wakati wa viongozi wa CCM, wakiwamo wabunge, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, wenyeviti na makatibu wote wa CCM kuikubali dhana ya nidhamu ya chama, kwa maana ya kuheshimu maamuzi rasmi na sera za CCM." Hayo ndiyo majibu yake kwa swali hilo.

Lakini kabla ya kuingia katika swali na majibu yake mengine, tutafakari haya kwanza. Mosi, kwenye majibu hayo tunaona Kolimba akikiri kuwasiliana na wabunge na hasa wale G55 (jambo ambalo si kosa akiwa mtendaji mkuu wa chama, bali udadisi ujikite katika nia ya hatua yake hiyo).

Lakini pili, tunaona namna Kolimba ‘akiwatumia' wabunge hao katika hali ya kueleza anachokiamini yeye binafsi (kuwa msemaji wao kwa kauli yenye tafsiri pana) anaposema; "hakuna anayependa kuvunja Muungano.

Hapa, kwa tafsiri ya maelezo ya Kolimba, hadi anajitokeza kueleza kwamba hakuna anayependa kuvunja Muungano (kati ya wana-G55), maana yake tayari kulikuwa na hoja kwamba wabunge hao wana ajenda, malengo au dalili za kuvunja Muungano.

Swali katika tafakari yetu ni je, nani aliyekuwa akidhani wabunge hao walikuwa wakitaka kuvunja Muungano hadi Kolimba atoe maelezo hayo tena akisisitiza anakutana na wahusika? Je, ni Nyerere na kama ni Nyerere; je, Kolimba alikuwa akimjibu (Nyerere) kwa ‘kivuli' cha wabunge hao?

Kwa lugha rahisi; wakati Nyerere akiamini kuna dalili hoja za G55 zinalenga kuvunja Muungano, Kolimba aliamini kinyume chake.

Tatu; tunaona katika majibu yake Kolimba akisisitiza nidhamu ya chama kwa wabunge, kwamba uamuzi wa chama ndiyo wa mwisho.

Awali, tumeona Kolimba akikiri mawasiliano yake na wabunge wa G55, hapa tujiulize zaidi; Je, tayari Kolimba alikuwa na msimamo wake binafsi kuhusu serikali tatu ndani ya Muungano kila alipokuwa akikutana na wabunge hao?

Au je, alikuwa hana msimamo binafsi, isipokuwa alikuwa akiwasikiliza tu ili kupima uzito wa hoja zao? Na je, kama hakuwa na msimamo wowote ilikuwaje wapishane na Mwalimu Nyerere aliyekuwa na msimamo wa wazi dhidi ya G55?

Na je, mawasiliano hayo ya Kolimba yalikuwa katika mfumo rasmi wa kiuongozi ndani ya chama au ni mawasiliano ambayo msingi wake ni utashi na msimamo wake binafsi? Au vyote viwili?

Lakini kama ni mawasiliano yaliyokuwa yakisukumwa na utashi wake binafsi, bila shaka Kolimba alikuwa na anachokiamini katika hoja ya serikali tatu, hata kama hicho alichokuwa akikiamini ni tofauti na msimamo wa chama chake kwa kadiri alivyokuwa akihisi au kuona dalili.

Lakini katika tafakari ya pili Kolimba anaposema; "hakuna anayependa Muungano uvunjike" je, hapa alikuwa akitetea msimamo wake binafsi kwa ‘kutumia' wabunge wa G55?

Je, maelezo haya yalikuwa ni kudhoofisha msimamo wa Mwalimu Nyerere kupinga madai ya Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano? Kwa lugha nyingine; ni kama Kolimba alikuwa amesogea mstari wa mbele tayari dhidi ya Nyerere.

Hapa, ikumbukwe kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa akipinga sababu zinazotumika kutetea kuwapo kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano, akiamini sababu hizo zimejengwa juu ya msingi usiokuwa na hoja zenye maslahi ya kitaifa.

Ni Nyerere ambaye aliwahi kuzungumza wakati akieleza sifa za mrithi wa Rais Ali Hassan Mwinyi, akisema ni lazima kupata mtu anayetambua Muungano umetikiswa na nyumba (taifa) kwa ujumla wake, imepata nyufa nyingine katika paa, kuta na hata katika msingi.

Kwa hiyo, kwa kuoanisha misimamo ya Nyerere kuhusu madai ya Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano na kauli hizi za Kolimba, zenye mwelekeo wa kutetea msimamo wa G55, akisema si kweli wanataka kuvunja Muungano au kuonekana waasi, ni dhahiri, msuguano kati ya Mwalimu na Kolimba haukujificha.

Lakini je, Kolimba alisisitiza nidhamu ya chama (katikati ya kukolea kwa hoja za G55) akijua kwamba baadaye chama kitatumika ‘kuua' hoja hiyo ya madai ya Serikali ya Tanganyika?

Je, alikumbusha nidhamu ya chama kwa hiari na muono wake kama mtendaji mkuu wa chama au alisukumwa na nguvu nje ya utashi wake kama tulivyoona katika makala zilizopita, akimjibu Nyerere kwamba tatizo si viongozi bali ni misingi ambayo Muungano umesimikwa juu yake.

Lakini je, nini hasa ufafanuzi wa Kolimba kuhusu nidhamu ya chama? Mei 28, mwaka 1994, katika hotuba yake iliyotangazwa moja kwa moja na Redio Tanzania (RTD), Kolimba alitishia baadhi ya viongozi kufukuzwa CCM.

Akiwasilisha salamu za "chama" katika mkutano mkuu wa nne wa Umoja wa Vijana wa CCM, ukumbi wa Kilimani, mkoani Dodoma, Kolimba alisema, "....kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita CCM kimeshuhudia baadhi ya viongozi wakifanya mambo kinyume cha maadili ya uongozi wa CCM lakini walivumiliwa kubaki katika nafasi zao kutokana na ukweli kwamba CCM ilikuwa ikijifunza mbinu mpya za uongozi katika kipindi cha mageuzi."

Akatishia akisema; "Kuanzia sasa CCM hakitasita kupendekeza kwa NEC-Taifa juu ya haja ya kumuondoa madarakani kiongozi atakayebainika kuwa vitendo na tabia yake vinakiharibia CCM sifa zake za kuliongoza taifa.

"Ninaposema tujenge nidhamu ndani ya chama chetu haina maana kwamba tusitofautiane kimawazo, lakini mawazo yetu lazima yawe na lengo la kupanua demokrasia na kukiendeleza chama," alisema Kolimba katika mkutano ambao, aliyekuwa Katibu Mkuu wa UVCCM, Sukwa Saidi Sukwa, alizitaka Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mapinduzi Zanzibar, zijitahidi kutatua tatizo la ajira hali itakayofanya vijana kuendelea kukipigania CCM.

Katika mjadala wa leo, kuna mambo mawili makubwa; kwanza, ni kama vile Kolimba alikuwa upande wa G55, wakati Nyerere hakuwa upande huo na wakati huo huo, Kolimba akiwa mtendaji mkuu wa chama ambacho ndicho chenye jukumu la kuzima madai ya Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano. Ilikuwa abaki, kupigania na kutafsiri "nidhamu ya chama" au akae pembeni ili chama kidhibiti hali ya hewa.

Na hapo, tunaona alijaribu kwa nyakati tofauti kupigania nidhamu ya chama iwe kwa utashi binafsi au kwa shinikizo, kama hotuba yake hiyo ya Dodoma inavyojieleza. Pili, tunaona Mwalimu Nyerere ni kama ndiye aliyeonekana kikwazo, kwa utashi wa akina Kolimba kutimia na hii inajionyesha kwenye makala zilizopita kuhusu maelezo ya Kolimba binafsi na hata majibu yake kwenye makala ya leo, akigeuka msemaji wa G55, katika mwelekeo wa kumjibu Nyerere, hasa anaposema G55 hawataki Muungano uvunjike.


Chanzo: Rai Mwema
 
Back
Top Bottom