Nilirudisha Milioni 3 niliyookota kwa mwenyewe, uamuzi uliobadilisha hatma ya maisha yangu

Mwiba1

JF-Expert Member
Jun 6, 2016
886
1,940
Habarini wana jamvi poleni na swaum lakini pia mfungo mwema kwa wenzetu waislam. Nimependelea nije na mkasa huu hususani katika kipindi hiki cha mfungo kwani ni funzo tosha katika maisha ya kila mmoja wetu.

Mkasa huu sio chai kama wengi walivyozoea kuleta nadharia fikirika.. lahasha huu ni mkasa ulionitokea mwaka 2010 nikiwa katika harakati za kusaka mkate wa kila siku katika stendi kuu ya mabasi Mwanza Nyegezi nikiwa kama utingo na mkatisha tiketi almaarufu kama argent (agent wa mchongo🤣).

Ilikuwa siku ya Jumamosi tarehe 5 mwezi wa pili 2010, nimeamka asubuhi nikiwa na hangover la kutosha lakini pia nikiwa nimechelewa sana kazini kutokana na uraibu wa pombe nilioupata usiku wa jana yake. Geto nilikuwa niko peke yangu tu sikuwa na demu wala hawara maana nilikuwa mnunuaji mzuri sana wa mbususu hivyo sikai na dem mmoja.

Ukutani ni picha ya 2pac na upande wa pili ni picha ya BIG kwani nilikuwa mtu wa hip hop sana, hata maisha yangu binafsi yalikua yanaakisi uhalisia wa hiphop hivyo hata maeneo ya kazini nilijulikana kama maniga pack kutokana na uvaaji wangu lakini pia sikua mchovu wa lugha ya kiingereza especially akitokea abiria wakizungu maeneo yale nilikuwa naletewa mimi.

Nilijiandaa haraka sana ili niwahi posho ya siku kazini shilingi elf10 na endapo nikifeli kuwasili kazini kabla ya saa 2 asubuhi basi inakula kwangu hivyo sikuswaki wala kubath, nikatupia koti langu la jeans, nikavaa na jeans yangu moja pendwa ya rockafella chini timberland boot zangu nikachomoka geto, fasta nikadaka bodaboda, lakini mbali na kufanya jitihada zote hizo za kuwahi lakini nilichelewa kazini na kuikosa posho.

Kichwa kiliniuma sana maana hangover ilinitesa halafu hata hela ya supu sina basi kama kawaida nikaingia kwa mangi nikakopa sigara aina ya embasi nipunguze wenge kwanza( enzi hizo nilikuwa navuta sigara ila namshukuru mwenyezi Mungu niliishaacha), nikaelekea ofisini kuchukua kitabu cha tiketi ili nianze kazi rasmi.

Nikiwa kwenye majukumu yangu alitokea abiria wa kwanza kabisa akiitaji tiketi ya kuelekea Musoma lakini alikuwa amewahi sana maana gari ilikuwa ni ya kuondoka mida ya saa 6 za mchana hivyo nikamwambia ukweli ili kama anakata akate na aendelee na mishemishe zake muda ukifika atafika na atakuta seat yake kama kawaida, basi tulikubaliana hivyo lakini aliomba apumzike kwenye gari maana anahisi uchovu sana hivyo ilinibidi nimfungulie mlango wa basi, binafsi nilikuwa ninakaa na funguo za mabasi na za ofisi maana nilikua nina desturi ya kuwahi sana lakini pia mbali na uhuni nilikuwa mchapa kazi, muaminifu sana, Pindi jua linapowaka sana ilinibidi niingie ndani ya mabasi kufungua vioo hivyo madereva wa kampuni yetu walipendelea kuniachia funguo.

Abiria yule alikuwa mtu wa makamo kidogo, mweusi sana na alizungumza lafudhi ya kabila la kurya binafsi sikujali sana nilimfungulia mlango aingie na apumzike, alikuwa amebeba kimfuko mkononi binafsi sikujali na sikutaka kujua kina nini ndani yake, niliendelea na majukumu na kusahau kabisa kama jamaa alikuwa ndani ya basi huku na kule stori na soga za kijiweni lakini baada ya kama saa moja hivi jamaa alitoka ndani ya gari na kuja uelekeo wangu akiwa kama mtu mwenye haraka hivi, hivyo nilimuuliza kama kuna kitu ninaweza kumsaidia lakini pia nikamwambia kama amechoka akazurure muda ukifika arudi on time asichelewe, lakini jamaa akainsist kuwa anawahi sana hivyo kama usafiri umeshindikana nimrudishie nauli yake achukue hiece mpaka stendi ya Buzuruga(walioishi Mwanza nadhani tutakuwa tumeelewana hapo) pale hatokosa gari kwa muda ule kama kawaida ikanibidi nimletee utata kidogo maana kiendacho kwa mganga hakirudi, lakini yule bwana kama sifa ya kabila lao bwana aliniwashia moto sio wa nchi hii ikabidi niwe mpole hivyo basi nili mrudishia nauli yake na jamaa akaondoka upesi sana.

Ilipofika mida ya saa nne jua lilikuwa limewaka sana hivyo nikaamua kuingia ndani ya basi ili nifungue madirisha hewa iingie ndani. Nikiwa katika zoezi hilo ghafla nikaona mfuko ule aliokuwa nao yule abiria nikaupuuza nikaendela na zoezi langu mpaka nikamaliza nikiwa naelekea kushuka nafsi ikasukuma kwenda kuucheki mfuko ule, nilipoufikia nikapata amshaamsha ya kuufungua ile naufungua tu nikakutana na burungutu la pesa za elfu kumikumi chakushangaza sikupagawa nikaendelea kuudadisi mfuko ule, nilikuta burungutu tatu za makadilio ya mil3.

Chakustaabisha pamoja na kuwa mimi ni mtu wa matumizi lakini sikuwa na tamaa kabisa yaani kuna roho fulani hivi iliniingia ya ustahimilivu, nikawaza sana kuwa huyu jamaa amesahau vipi hizi pesa? Au ni mtego? Au ni uchawi? Lakini nikajipa utulivu wa ajabu sana, huwezi amini niliuchukua mfuko ule na kwenda kuufungia kwenye droo ofisini na nikapiga kufuri na kama kawaida nikarudi katika kitengo changu bila wenge wala nini kama vile sijakutana na tukio lolote.

Niliendelea na kazi mpaka ilipofika mida ya saa kumi na mbili chaajabu nikasahau kabisa kama kuna mzigo niliuacha ofisini, hivyo nikajikataa zangu kuelekea magetoni na Mungu mkubwa siku ile niliondoka na kama elfu20 hivi mfukoni huku elf 10 nikiichezea michezo ya vyama vyetu pale stendi, nikapita bucha kwanza nikachukua nyama ili nikachome geto. Mpaka nafika geto bado sina kumbukumbu ya mfuko ule ofisini, inafika mida ya saa tatu usiku ndio nakumbuka kuwa mzigo nimeuacha kwenye dro...ebwana roho iliniruka sana sio kwa kuupoteza mzigo ule ila kwa kushindwa kuutunza mzigo ule kwani imani yangu ni kuwa bwana yule atarudi na kama hatorudi niishi nazo hizo hela. Kesho yake mapema sana niliamka ili nikafungue ofisi kabla ya mtu yoyote ili nihakikishe kama mzigo uko salama.

Mungu ni mkubwa mzigo niliukuta kama nilivyouweka nikafunga droo kama kawaida na kufuli nikarudi kwenye majukumu yangu.

Kwenye mida ya saa 4 asubuhi bwana yule mkurya nilimuona maeneo ya stendi hapo akiwa amevurugwa sio kawaida anazungumza peke yake na hana uelekeo, yule bwana aliponiona alinifuata uelekeo wangu akiwa amepoa sana. Nilijifanya niko busy huku namsikilizia kama ataleta hasira zake za kikurya ili nimchinjie baharini vizuri. Cha ajabu bwana yule alinisalimia kwa adabu sana wakati huo mimi ni kijana mdogo sana kwake, baada ya hapo yule bwana alianza kulia mfululizo huku akiongea kiluga chake, nilitamani kumtia kofi atoe wenge. Ikanibidi nimuulize tatizo ni nini japo binafsi ninajua ukweli wote, jamaa alianzia mbali sana. Chaajabu katika simulizi zake zote hakuhisi hata kidogo kuwa aliacha mfuko ndani ya basi letu.

Jamaa alidai kwamba baada ya kumrudishia pesa yake ya tiketi aliondoka akiwa na haraka sana kwani alikuwa anawahi mpakani na alikuja Mwanza ili kuchukua mkopo kwa jamaa yake na aliweka nyumba yake kama dhamana, anadai ya kwamba alipoteza mfuko huo ukiwa na kiasi cha mil3 na ana asilimia mia moja ya kwamba kaibiwa akiwa kwenye hiece hivyo amechanganyikiwa hajui afanye nini na hapo alipo ameshindwa kurudi Musoma kwake kwani hana cha kwenda kuiambia familia yake, hana pa kushika na ana mpango wa kukimbilia mbali kusikojulikana. Kiukweli jamaa alikuwa analia sana na alionekana kupagawa sana, nilihisi mtu huyu anaweza hata kujiua na kiukweli alikuwa ananisimulia tu na wala sio kunihisi kwa lolote.

Nikiwa kama mwanaume mpambanaji kiukweli niliingiwa na huruma sana nikapata maswali kadha wakadha kichwani nikajiuliza vipi kuhusu familia yake itakapo nyang'anya nyumba? Vipi kuhusu huyu jamaa atakapoitelekeza familia kwa sababu yangu? Vipi kama mtu huyu atajiua kwa sababu yangu?

Ilinibidi nimkatishe maongezi maana jamaa alionekana kuchoka nikamuuliza kama amekula, jamaa akanijibu hajala tokea jana asubuhi nikamuomba anifate, alinifuata mpaka mgahawani nikamuagizia chai ya maziwa na chapati nne kisha nikamwambia apige menu na asiondoke mimi naenda kuendelea na mishemishe nikiwa free nitakuja ili nione nitamsaidiaje, kiukweli niliitaji uhuru wa fikra ili nipate kutafakari vizuri ili kama napiga mzigo nimpige na kama namrudishia mzigo nimrudishie.

Baada ya kama lisaa limoja hivi nikapita kumchungulia jamaa, nilimkuta amekunywa chai tu chapati hajagusa hata moja, nikamuuliza jamaa akasema ameshindwa kabisa kula, kwa utani nikamuuliza ya kwamba sijawahi kuona mkurya alieshindwa kumaliza chapati nne, nilifanya hivyo ili kuona kama jamaa atapata furaha lakini jamaa alikuwa na hali mbaya sana, jamaa aliniomba aondoke na alinishukuru sana kwa ukarimu wangu.

Nilimuomba asiondoke aendelee kunisubiri jamaa akaendelea kunisubiri, nilipoona ofisini hakuna mtu nilimuomba anifate, tulielekea ofisini wote baada ya kuingia nilifungua droo na kuutoa mfuko ule, nikamuuliza kama anaufahamu mfuko ule kabla sijamaliza jamaa akadondoka na kuzimia aisee nilipagawa sana ikanibidi nikimbilie maji baridi dukani huku nikifunga ofisi.

ITAENDELEA

========

SEHEMU YA PILI NA YA MWISHO:

Muendelezo tulipoishia:

Baada ya kumuonyesha mfuko ule yule bwana, nikamuuliza kama anaufahamu mfuko ule nikaufungua jamaa alipoziona hela tu alianguka na kuzimia, nilitahamaki sana nikajaribu kumpepea lakini jamaa hakurudisha fahamu hivyo ikanibidi nifunge mlango wa ofisi ili nikimbilie maji ya baridi dukani kichwani nawaza kama itakuaje asipo zinduka?

Ila poteleapote nikanunua maji baridi nikarudi ofisini na kumwagia usoni, Mungu si osmani asee yule bwana alizinduka lakini alikuwa kama bubu akiwa pale chini ameketi kitako nikamkabidhi mzigo wake aliubeba lakini mikono ilikuwa inatetemeka balaa mpaka akaudondosha chini. Ilimchukua kama dakika tano hivi jamaa kurudi kwenye ufahamu, ndipo jamaa akaniuliza kama mimi ni binadamu kweli au malaika?

Nilibaki hoi kwa kicheko lakini jamaa alirudia swali lilelile, nilimtoa hofu nikamwambia awe na amani kabisa hivyo nikamwambia ahesabu pesa zake kama ni kamili ama zina mapungufu. Jamaa akagoma kuhesabu ila akasema zozote zilizomo basi azipasue kati anipatie nusu, ebwana huwezi amini nilizikataa katakata maana toka mwanzo nilijua ni pesa za mkopo na zinaenda kwenye biashara hivyo nikitoa kidogo tu nitakuwa nimemuharibia mahesabu yake na ukizingatia marejesho ni palepale.

Nilimuomba jamaa arudi nyumbani kwani kama pesa ameshaipata lakini jamaa hakuridhika kabisa akaniambia basi twende pale mgahawani tumefika mgahawani jamaa akamuamuru mamalishe anihudumie kwa muda wa mwezi mmoja bure kabisa na ampe yeye bill, lakini pia nikaikataa ofa hiyo basi jamaa hakufurahi kabisa ila mimi nilijua tu jamaa anafanya mambo out of excitement au furaha imemzidia, nikamwambia alipie chakula changu cha siku hiyo tu hivyo jamaa alinilipia samaki sato mkubwa na wali akanichukulia na soda, mpaka hapo jamaa alikuwa hanijui jina wala mimi simjui jina hivyo aliniuliza jina langu, nami pia nikamfahamu kwa jina la Paschal tukabadilishana mawasiliano baada ya hapo jamaa aliniaga na kunishukuru sana.

Jamaa akaondoka huku akigeuka mara kwa mara kuniangalia mpaka akatokomea. Kichwani mawazo yananijia duh mtonyo si ningeupiga uleee..wazo lingine linaniambia nilichokifanya ni uungwana, mara bahati hairudi mara mbili lakini potelea mbali nilifurahi kwani nilifanya uungwana kosa lilikuja pale nilipojaribu kusimulia jamaa na marafiki maana wengine walinitukana sana nakumbuka kuna jamaa yangu mpaka akaamua kunichunia kwamba kwanini sikumshirikisha hilo dili huwezi amini jamaa alinipiga chini kabisaa akakataa urafiki na mimi.

Siku ziliendelea na majukumu yaliendelea kusonga kama kawaida lakini yule jamaa alikuwa na desturi ya kunipigia simu hususani akiwa anakuja kuhemea bidhaa za biashara yake hapo Mwanza, jamaa alikuwa kama rafiki lakini yeye alipenda kuniita mimi ndugu yake na pia aliniambia ya kuwa ndugu zake wanayo shauku kubwa sana ya kunifahamu, kaka zake, mke wake na watoto wake woote wananiulizia sana, binafsi nilikuwa nachukulia poa tu na maisha yaliendelea kama kawaida.

Ilikuwa mwezi wa kwanza mwaka 2011, kama kawaida yangu nimeamka nimechelewa sana nikiwa na hofu ya kuchelewa posho ilinibidi nichukue bodaboda ili niwahi posho, nilikuwa naona kama bodaboda haitembei mpaka nikawa namtukana dereva wa boda na kumwambia kama vipi akae nyuma nikanyagie chombo maana naona hatembei kabisaaa, jamaa ikabidi achomoke spidi kwelikweli tukafika kituo kimoja panaitwa nyegezi kona sehemu ambayo sio mbali kabisa na stend kuu huku nikiamini nimeshafika basi costa lililokuwa mbele yetu lilisimama ghafla hivyo boda alihamisha uelekeo akawa kama anaovertake lile costa.

Kilichofuata tulikutana uso kwa uso na prado ambayo nayo ilikuwa moto kwelikweli, ajali ile niliinusa mapema hivyo nilikuwa nawaza niruke, kwa haraka sana nilikanyaga siti ya boda nakuruka juu nilitua juu ya gari nakudondoka nyuma ya gari sikumbuki nilitua vipi lakini nilihamaki kuona mguu mmoja umegeuka nyuma mbele mbele nyuma, kichwani nimepasuka vibaya ukizingatia nilikuwa nanyoa para, huku nikilia kama mtoto nilimuomba jamaa mmoja kati ya watu wengi waliokuwa wametuzunguka pale chini ili aurudishie mguu wangu lakini hakuna aliyeweza kufanya hivyo ilinibidi niukamate mguu mwenyewe na kuurudisha mara moja ebwana maumivu ya hapo sio kwaida nilipoteza fahamu.

Kilichofuata nilizinduka nikajikuta nikiwa hospital nikiwa nimelala pembeni ya jamaa mmoja ambaye alikuwa ameharibika vibaya sana kiufupi hatamaniki nikajiangalia nikagundua mguu mmoja hauna fahamu lakini jeraha kichwani. Nilipiga kelele kidogo kumuita dokta mpaka ikafika muda dokta akaja kuniona, alimuita nesi na kumuuliza ya kwamba huyu na huyo pembeni yake ndio waliopata ajali ya bodaboda? Nesi alikubali, hivyo nikagundua kuwa yule jamaa ni dereva boda boda aliyekuwa amenibeba.

Nilimuuliza dokta kama niko sawa niondoke zangu maana mule ndani palikuwa panatisha sana lakini pia nilitaka kujua niko hospitali gani na wapi? Alinijibu kuwa nipo Bugando hospital wakati ninazungumza na dokta ghafla hali ya yule bodaboda ikabadilika akaanza kurusha miguu so dokta akaita manesi ili apelekwe emergency fasta lakini nakumbuka kabla hata ya zoezi hilo la kumuhamisha halijakamilika bodaboda yule alitulia dokta alienda kumcheki na kusikitika.

Kilichofuata nesi alivuta shuka kumfunika uso hivyo nikapata majibu kuwa jamaa amefariki, hapo wasiwasi ulinipanda ukizingatia sina simu hapo wala nini na ninaishi geto sina mtu japo familia yangu ilikuwa hapo Mwanza lakini ninawajulisha vipi?

Nilimwambia dokta kwamba niko sawa sana naomba niondoke tu dokta alikataa akaniambia bado sijapimwa kujua ajali imeniathiri kwa kiasi gani. Nakumbuka ilipofika asubuhi walikuja jamaa zangu wawili kutokea pale stendi maana taarifa ziliwafikia. Watu kibao pale stendi na uvumi ulikuwa ni kwamba nimepoteza maisha palepale, hivyo walikuja pale Bugando kuhakikisha hivyo baada ya kunikosa mochwari ikabidi waje emergency na mwisho kabisa kwenye wodi za watu wa ajali na walifanikiwa kuniona.

Kiukweli nilifarijika sana kuwaona hao jamaa zangu, nikapata fursa ya kumpigia simu mama yangu pamoja na wanafamilia kuwajulisha jambo lile. Walifika mapema tu na ishu ya vipimo iliendelea hivyo nilipelekwa kufanyiwa kipimo na nikagundulika ya kwamba nimevunjika uti wa mgongo pamoja na mguu mmoja, hivyo daktari alinishauri kama ninaweza niende Muhimbili au nitapata matibabu sahihi, baada ya hapo nilirudi nyumbani na ukizingatia nyumbani penyewe tia maji tia maji, hela za matibabu ikawa kitendawili, hivyo nikawa mtu wa kulala tu na kuhamishwa kutolewa nje jioni kuingizwa ndani, ndio yakawa maisha yangu.

Nakumbuka tajiri yangu pamoja na meneja walikuja kunisalimia siku moja hawakukaa sana na walipotaka kuondoka waliniachia shilingi elfu 10 tu japo ni ndogo ila niliiona ni kubwa mno maana nilikuwa na upweke wa ajabu maana sikuwaona marafiki wala ndugu kunichangia matibabu, hivyo nilikuwa siioni hatma ya maisha yangu na kuna muda niliona kama ndio mwisho wangu, maumivu yalikuwa ni makali sana mpaka ilifika muda nilimuomba mama yangu mwenyewe aniwekee hata sumu ili nife nikikwepe kikombe hiki cha mateso ninayopitia, nakumbuka mama yangu alilia sana aliniambia huo ni mtihani tu yatapita, japo niliona ananienjoy tu maana juzi ni kama jana na jana ni kama leo tu hakuna jipya zaidi ni maumivu kila siku.

Ilipita miezi mitatu hali ilikuwa inazidi kuwa mbaya, mguu wangu ulipona vizuri lakini tatizo lilibaki kwenye mgongo. Nakumbuka ilikuwa ni asubuhi mida ya saa nne nimetolewa kibarazani ilipigwa simu yangu sana simu ilikuwa ndani na hakukuwa na mtu ndani nami sikuwa na uwezo wa kutembea kuifuata hivyo nitulia tu nikisubiri kama atatokea mtu yeyote nimuagize, bimkubwa alirudi kutoka kuchota maji nilimuomba aniletee simu, nilikuta missed calls3 na namba ilikuwa ngeni hivyo nilimuomba bimkubwa simu yake ili niipigie namba ile.

Niliipiga na alipokea katika kumuuliza niligundua ni yule jamaa bwana Paschal mkurya niliemsaidia takribani mwaka mmoja hivi ulishapita jamaa alinijulisha ya kwamba hiyo ni namba yake pia lakini aliniuliza kama nipo stendi maana yupo Mwanza na anahitaji nimkatie tiketi ili akifika stendi tu asigande afike na kuondoka, nilimwambia niko nyumbani na nina matatizo ya kiafya ni miezi takribani minne sifanyi kazi, jamaa alitahamaki sana na akaniomba nimuelekeze nyumbani ili aje kunijulia hali na aliahirisha mpango wa kusafiri mpaka aje anione kwanza.

Basi nilimuelekeza jamaa akachukua boda mpaka mtaani kwetu na alifanikiwa kunikuta nikiwa nimelala nje kwenye mkeka, jamaa alitekewa sana kuniona katika hali ile, nilimsimulia kisa chote yaliyonikuta jamaa alionekana kuguswa sana tulizungumza muda mrefu sana na ilipofikia jioni aliaga kuondoka na kuniachia kiasi cha laki moja lakini aliniambia atarudi kwani kuna ndugu zake kutokea Kenya wapo nyumbani kwake angependa waje wote kunijulia hali kwani wote hao wananifahamu vizuri japo mimi siwafahamu na mara kwa mara hukumbushia tukio langu mimi kumrudishia pesa zake huyu jamaa yangu.

Nilifurahi sana maana tangu niugue sijawahi kupewa laki moja kama pole. Ilipita siku tatu ulikuja ugeni wa maana pale nyumbani, yalikuwa majira ya saa sita mchana ilikuwa discovery nyeusi yenye plate number ya Kenya mbele ya nyumba yetu na kama kawaida nilikuwa nimelazwa nje hivyo nilishuhudia wakishuka wanaume wawili nisio wafahamu, mwanamke mmoja pamoja na yule jamaa yangu. Nilimuita bimkubwa ili aje kuwapokea wageni hao.

Wageni hawakutaka kuingia ndani bali waliomba viti tu, waliketi na kujitambulisha wale jamaa wawili walikuwa ni kaka wa huyu bwana Paschal na yule mwanamke ni mke wa mmoja wa wale ndugu, bwana Paschal aniendelea kwa kuwanadi ya kwamba yule mkubwa anaitwa Marwa ni pilot huko Kenya na huyo mwingine anaitwa Rhobi ni daktari huko Kenya na yule mwanamke ni mke wa bwana Rhobi pia.

Jamaa walipenda kujua kisa na mkasa mpaka niko kwenye hali hiyo, nilisimulia vyote na cha ajabu sasa ni pale ambapo waliniahidi matibabu yangu tena katika hispitali kubwa tu nchini Kenya kiukweli niliona ni drama au labda ninaota tu, walisema wanarudi Kenya baada ya siku mbili na kama sitojali niondoke nao hiyo siku ili nikaanze matibabu jamaa walisema mimi ni kama ndugu kwao kwani kwa nilichomfanyia mdogo wao ni zaidi ya hisani hivyo wala nisiwe na wasiwasi. Mama yangu alibaki midomo wazi, baada ya siku mbili nilisafirishwa kwenda Musoma na walinisafirisha kutoka musoma mpaka nairobi kwa gari.

Naomba kufupisha, nilitibiwa kwa muda wa miezi minne na nikapata nafuu kubwa sana mpaka kuanza kutembea japo taratibu katika hospitali nzuri hapo Nairobi huku matibabu yote nikigharamiwa na huyu bwana Marwa ambae ni pilot by profession akishirikiana na mdogo wake. Niliagwa mwezi wa kumi mwaka 2011 nikiwa nimekumbuka sana nyumbani niliwaomba jamaa hawa nirudi nyumbani nikaendelee na mazoezi, lakini jamaa walinipenda sana hawakuridhia kabisa.

Nakumbuka brother Marwa baada ya mimi kuomba sana ruksa aliniambia ana safari na akirudi ataniruhusu kipindi hicho chote niliishi nyumbani kwake sehemu moja panaitwa Muthaiga ni ushuani kwelikweli, jamaa alikuwa na watoto wakubwa lakini hakuwa na mke kwani mkewe alishafariki kitambo, baada ya wiki mbili alirudi kutoka safarini na tulizungumza nilimshukuru sana kwa hisani yake kwangu, jamaa aliruhusu mimi kuondoka lakini alinipa bahasha na aliniambia nisiifungue mpaka nitakapofika nyumbani, niliwasiliana na bwana Rhobi ambaye alishirikiana bega kwa bega na brother Marwa katika matibabu yangu kumuaga na pia kumshukuru sana kwa hisani yake kwangu.

Nilianza safari kuelekea Silali boda la Kenya na Mara. Nilipovuka niliwasiliana na bwana Paschal naye aliomba sana nikifika Musoma nipite kwake, nilifanya hivyo mida ya jioni nilifika Musoma nilionana na bwana Paschal, jamaa alifurahi kuniona aliniambia kitu kimoja kikanishangaza sana, alisema yeye pia haamini ya kuwa kaka zake wamenifanyia hisani kubwa sana kwani kwa anavyowajua huwa sio watu wa kutoa misaada na hata katika familia huwa hawatoi misaada na wamejitenga kabisa.

Basi tukabaki kucheka na kusema ya Mungu ni mengi na unaweza saidiwa na mtu usiyetarajia. Nililala hapo Musoma na kesho yake alfajiri niliamkia mwanza, nilipofika nyumbani nilimkuta mama yangu pamoja na dada yangu na wadogo zangu wakiwa na shauku kubwa ya kuniona, kiukweli mama yangu alilia kuniona natembea japo taratibu, mimi pia nililia japo mwanaume, yaliendelea mengi hapo nyumbani, nilijisahau kabisa kama nilipewa bahasha na brother Marwa kutokana na furaha niliyoikuta pale nyumbani hivyo ilipofika jioni ndipo nikakumbuka so nikaenda chumbani kuicheki ile bahasha iliyo kuwa ndani ya begi langu la nguo, bahasha ilikuwa haitishi maana ilikuwa haijatuna wala nini.

Nilipoifungua nilikuta bundle la hela za dollar 100 kila moja nilizihesabu zilikuwa ni noti thelathini za dola mia. Nilizichukulia poa kesho yake nilioga freshi nikaenda mjini mwanza kuna hotel moja inaitwa Gold crest, pale kuna duka la kubadili fedha za kigeni sasa pale ndio nilistaajabu ya musa kwani nilipewa kiasi cha shilingi milioni sita na laki nne na thelathini, nilijitahidi kumpigia brother Marwa ila akawa hapatikani nilitamani kumpigia kumshukuru.

Amekuwa mtu busy sana na sikufanikiwa kumpata mpaka leo. Pesa ile ilinibadilishia maisha mpaka leo hii nina mambo yangu ninafanya, nimeoa na nina mtoto. Paschal ni kaka yangu mpaka leo na ninaposema wema wangu ulibadilisha hatma ya maisha yangu ninamaanisha pakubwa sana maana labda ningekuwa mlemavu au labda ningeshapoteza maisha au ningekuwa tingo mpiga debe stendi mpaka leo.

NI WITO WANGU KWA VIJANA WENZANGU TUDUMU KATIKA KUFANYA MAMBO MEMA MUNGU NDIYE AJUAE KESHO YAKO NA MUNGU NDIYE MLIPAJI.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom