Ni wakati wa kuonyesha kuwa tuna akili na uwezo wa kufikiri

kivato

Member
Nov 20, 2010
18
2
NIMEVUTIWA na kauli aliyoitoa Waziri wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta Waziri wa Afrika Mashariki ambaye mwanzoni mwa wiki hii aliripotiwa akisema kuwa kuilipa fidia ya Sh 185 bilioni kampuni ya Dowans ni kuhujumu uchumi wa nchi.

Ingawa kauli hiyo imepokewa kwa hisia tofauti lakini binafsi naiona kuwa ni kauli ya kupongezwa kwa sababu Sitta ameweza kuonyesha uzalendo wake halisi. Hiyo ni kauli ya kizalendo na ni kauli nzito kutolewa na mtu ambaye yuko katika mstari wa mbele wa safu ya uongozi wa nchi.

Ameonyesha kuwa kuwa Waziri hakuna maana kuwa ni kufungwa mdomo, waziri anapaswa aonyeshe msimamo wake kuhusu masuala fulani fulani yanayoihusu nchi. Sitta ameonyesha kuwa ni mtu mwenye mawazo huru na mtu kama huyo kamwe fikra zake haziwezi kufa.

Nchi hii inahitaji watu wenye fikra huru za kimapinduzi, wanaopenda kuona mabadiliko yanatokea katika mifumo ya uendeshaji nchi. Bila kisisi au hofu Waziri Sitta ameweka bayana kuwa kuna genge la watu wenye fedha chafu wanaojaribu kuandaa mpango wa kuihujumu nchi, hivyo kusema kwamba hakuna uhalali wowote wa kuilipa Dowans Sh185 bilioni ambazo kimsingi haijazifanyia kazi.

Dowans ni kampuni iliyoirithi kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond ambayo baadaye iligundulika kuwa mkataba wake na serikali ulikuwa na mizengwe mingi na hatimaye baada ya sakata la Richmond kurindima bungeni mwaka 2008 na kusababisha aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa na mawaziri wawili, Nazir Karamagi na Ibrahim Msabah kulazimika kujiuzulu, hatimaye serikali ilifuta mkataba na Dowans.

Kwa mujibu wa Waziri Sitta, Dowans kuishitaki serikali ya Tanzania kwa Mahakama ya Kimataifa ya Usuhishi wa Kibiashara (ICC) na mahakama hiyo kutoa hukumu ya kuwa Serikali ya Tanzania inapaswa kuilipa Dowans kutokana na kuvunja mkataba bila kufuata utaratibu, ni mbinu tu za kutaka kuwahujumu Watanzania na hivyo genge hilo la kifisadi kujipatia fedha kwa ajili ya kujiandaa na uchaguzi wa mwaka 2015.
Sitta amesema kuwa genge hili linawafanya Watanzania wajinga wasio na uwezo wa kufikiri na kwa sababu wameishika nchi…

Kwa hakika Sitta ametufungua macho na ametubainishia kwamba kuna kundi lenye maamuzi na nchi hii ambayo wengi tunadhani kuwa ni yetu sote na tuliowakasimia madaraka wanatuongoza kwa niaba yetu.

Hizi ni nukta tatu zinazohitaji udadavuzi wa kina; kwanza ni genge linalojiandaa kwa uongozi ifikapo mwaka 2015 na pili ni genge la mafisadi wanaotaka kuihujumu nchi na tatu genge hili linataka kuwafanya Watanzania wajinga.

Hivyo pamoja na kuwa kulikuwa na fununu za kwamba kuna watu wanajiandaa kushika nchi mwaka 2015, ijapokuwa wataingia madarakani kwa njia ya kura lakini watafanya uhujumu wa kifisadi ili kupata nafasi hiyo, lakini Waziri Sitta sasa ameziweka bayana tuhuma hizo na kuweka msingi wa kujenga nguvu ya hoja.

Hivi sasa Watanzania wana kazi kubwa ya kulibaini ni lipi hilo genge la mafisadi wanaotaka kuishika nchi? Ikiwa hawa watatumia fedha kuingia madarakani, Waziri Sitta ametutanabahisha Watanzania kuwa tuwe macho na watu hawa, tusikubali kulaghaiwa wala kurubuniwa kwani tukiiacha hali hiyo iendelee tutakumbwa na matatizo makubwa siku za usoni. Ingawa Sitta hakueleza ni matatizo gani, lakini bila shaka hakukuwa na haja ya kutuwekea chakula mdomoni ndipo tutafune.

Lakini Waziri Sitta ameibua nukta nyingine muhimu, kwamba; genge hili linawafanya Watanzania wajinga, wasioweza kufikiri. Hii kwa hakika ni changamoto kubwa kwa Watanzania, sasa wanatakiwa waonyeshe uwerevu wao kuwa wanao uwezo wa kufikiri na wanayo dhima ya kutumia akili na maarifa yao kuikomboa nchi hii isitumbukie katika mikono ya mafisadi.

Kibaya zaidi ni kwamba mafisadi hawa wanataka kuwakaanga Watanzania kwa mafuta yao wenyewe, fedha hizi wanazodai kuwa wanapaswa wafidiwe, zitapatikana kutokana na jasho la Watanzania walipa kodi, hivyo badala ya kodi za wananchi kutumiwa kwa ajili ya kuboresha miundombinu na kuendeleza miradi ya maendeleo, zitatumika kwa ajili ya kuilipa kampuni hewa ya kifisadi, iliyorithi mradi wenye utata wa ufuaji umeme ambao haukuwanufaisha Watanzania bali uliwaingizia hasara ya mamilioni ya fedha, kwani kila siku Serikali ilikuwa inapaswa ilipe Sh 152 bilioni za uzalishaji wa umeme wa Richmond? Je, serikali ilikuwa ikiingiza bilioni ngapi baada ya umeme huo kuzalishwa kwa siku?

Mahakama hiyo ya biashara ya kimataifa bila shaka iliamua kesi bila kuzingatia maslahi ya Watanzania, bali iliangalia upande mmoja tu wa mdai na kuamua kumuongezea aliyenacho, je, ICC iliangalie kipengele cha athari zilizopatikana kwa Mtanzania mvuja jasho kwa serikali kuingia mkataba wa uzalishaji wa umeme wa kidhalimu kama ule wa Richmond na hatimaye Dowans?

Hivi sasa ni jukumu letu Watanzania kulibainisha na kuliumbua genge hili la mafisadi alilolitaja Waziri Sitta ambalo amesema dhamira yake ni kuushika uongozi wa nchi ifikapo mwaka 2015.

Sote tuna wajibu wa kuonyesha uzalendo kupambana na ufisadi wa aina yoyote ile, tusikubali nchi yetu kuangukia katika mikono ya waroho na wabinafsi. Tunataka kuona kuwa jasho la wavuja jasho wa nchi hii linatumika kwa maslahi ya nchi, kwanini tuilipe Dowans? Kwani imetufanyia nini Watanzania?

Ni wakati wetu Watanzania kuonyesha kwamba uwezo wa kufikiri tunao na uwezo wa kumzuia nduli yeyote yule awaye tunao na tunataka dunia ituelewe hivyo!
 
Back
Top Bottom