Nguvu ya Kisayansi Inayoikinga Pwani ya Afrika Mashariki dhidi ya Vimbunga.

Umkonto

JF-Expert Member
Dec 27, 2018
2,151
3,679
Wakati sehemu mbalimbali duniani ambazo zipo katika upwa ama karibu na bahari kubwa huathirika na misimu ya vimbunga, baadhi ya watu wanaweza kujiuliza kwa nini Tanzania na upwa wa Afrika Mashariki (Kenya na Somalia) haziathiriwi na vimbunga.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya masuala ya hali ya hewa, kimbunga cha mwisho kuipiga Tanzania ilikuwa Aprili 14 mwaka 1952 mkoani Lindi, kipindi hicho bado ikiwa ni koloni la Tanganyika chini ya utawala wa Mwingereza.

Miaka 80 nyuma, yaani Aprili 15, 1872 kimbunga cha mwisho kiliipiga Zanzibar, na kwa mujibu wa maelezo yaliyorekodiwa ya Balozi wa Uingereza visiwani Zanzibar wa miaka hiyo Bw. John Kirk theluthi mbili ya mashamba ya minazi na karafuu visiwani humo yaliharibiwa vibaya.

Hivyo, laiti Jobo kingetua na nguvu, basi kingekuwa kimbunga cha kwanza kurekodiwa kupiga jiji la Dar es Salaam na cha pili kuipiga Zanzibar baada ya takriban miaka 149.

Sababu;

Suali linalosalia ni kwa nini vimbunga hivyo havianzii ama kuathiri pwani ya Afrika Mashariki? Jibu ni kuwa eneo hilo lipo 'kati kati ya dunia'.
Dunia imegawanyika katika mihimili miwili, mhimili wa kusini na mhimili wa kaskazini. Kilichogawanyisha dunia katika mihimili hiyo ni mstari dhahania wa Ikweta. Mstari huo unapita kwenye nchi 13 duniani zikiwemo Somalia, Kenya na Uganda.

"Vimbunga husukumwa na nguvu iitwayo Kani ya Coriolis. Kani hiyo haina nguvu kabisa katika eneo la Ikweta kwa kuwa ndipo mhimili wa Kaskazini na Kusini huapaka, na upepo katika mihimili hiyo huenda katika njia tofauti upande mmoja kushoto upande mwengine kulia," anaeleza Profesa Marshall Shepherd, rais wa zamani wa Jumuiya ya Utabiri wa Hali ya Hewa ya Marekani.

Mtaalamu huyo anaeleza katika makala ya mwaka 2018 iliyochapishwa na jarida la Forbes kuwa nguvu hiyo kinzani ndio huua nguvu ya vimbunga katika eneo hilo.

Japo Tanzania haijapitiwa na mstari wa Ikweta lakini ipo katika ukanda wa Ikweta, masafa machache kusini mwa mstari huo uliopita katika nchi jirani za Kenya, Uganda na hata DR Congo.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Prof Shepherd endapo kimbunga kikali kitajitengeneza mbali na eneo hilo kinaweza kuathiri moja kwa moja eneo hilo, "japo kutokea kwa hali hiyo ingali bado ni jambo la nadra."

Hata hivyo, hali ya mvua kubwa na mafuriko huukumba ukanda wa Ikweta kutokana na athari ya vimbunga vinavyopiga maeneo ya karibu katika msimu wake.

Msimu wa Vimbunga

Eneo la Bahari ya Hindi, kuanzia kusini magharibi ya India mpaka upwa wa mashariki na kusini ya Afrika una msimu wake wa vimbunga ambao huanza mwezi wa Novemba na kuishia mwezi wa Aprili.

Vimbunga vya Zanzibar na Lindi vyote vilitokea mwezi wa nne, hata kwa upande wa Jobo pia huu ni mwezi wa Aprili.

Kimbunga Kenneth kilipiga mwezi wa Aprili 2019 na mwezi mmoja nyuma yake kimbunga kibaya zaidi cha Idai kiliipiga Msumbiji na athari zake kufika mpaka nchi jirani za Malawi na Zimbabwe. Zaidi ya watu 1,000 walipoteza maisha katika kipindi hicho.

Kwa msimu wa mwaka huu (2020/21) ambao unaelekea mwisho zaidi ya vimbunga vikubwa na hafifu 16 vimejitengeneza na kuathiri baadhi ya nchi katika ukanda huo, Jobo ikiwa ni kimoja wapo.

Chanzo; BBC Swahili
 
Back
Top Bottom