NEMC: Uchimbaji wa urani (uranium) una athari kubwa

Wambugani

JF-Expert Member
Dec 8, 2007
1,757
276
Na Mwandishi wetu

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc), limeelezea athari zinazotokana na uchimbaji wa madini ya urani kwamba hutoa mionzi hatari inayosababisha athari kwa viumbe hai, ikiwa ni pamoja na kumdhuru binadamu kiafya na hata kusababisha kifo.

Maelezo hayo yalitolewa na Nemc kwa maandishi kupitia Kaimu Mkurugenzi Mkuu wake, Ignace Mchallo, akijibu maombi ya gazeti hili yaliyotumwa kwa Baraza hilo kwa maandishi, kutaka ufafanuzi kuhusu athari za mazingira zinazoweza kutokea kutokana na uchimbaji wa madini hayo.

Mchallo alisema athari za mazingira ziko mbili; za kwanza zikiwa ni zile zinazofanana na uchimbaji mwingine wowote; na za pili zinazohusu madini hayo, ambayo yanatoa mionzi.

Alizitaja athari za kawaida kuwa ni pamoja na kuharibu ardhi kwa kufyeka mimea, kuchepusha mikondo ya maji, kuchimba mashimo makubwa juu na chini ya ardhi, kelele pamoja na mitetemeko kutokana na ulipuaji, vumbi na moshi.
Athari nyingine ni uchafuzi kutokana na taka za kimiminika na

taka ngumu na pia marundo ya mawe taka yanayosababisha madhara mbalimbali katika mazingira kama vile kuzalisha tindikali ambayo uharibu mazingira.

"Athari za aina yake ni zile zinazotokana na ukweli kwamba urani pamoja na watoto wake hutoa mionzi hatari inayosababisha athari kwa viumbe hai ikiwa ni pamoja na kumdhuru binadamu kiafya hata kusababisha kifo," alisema Mchallo.

Alisema kifo kinaweza kutokana na kuishi au kufanya kazi katika mazingira yenye mionzi kwa muda mrefu na kwa binadamu hupata saratani na hatimaye kuugua na kufa.

Mchallo alisema pia kuwa urani ikiingia katika mwili wa binadamu kwa njia ya vumbi, kula au kunywa katika maji yaliyochafuliwa, nayo inaweza kumdhuru hadi kusababisha kifo.

Kutokana na hali hiyo, alishauri udhibiti wa madini hayo ikiwa ni pamoja na mionzi yake, kuingia katika maji na hewa katika viwango vinavyozidi vile vinavyoweza kusababisha madhara.

"Kwa hiyo, inawezekana kuchimba urani katika hali ya usalama kama njia sahihi za kuhakikisha usalama huo zimewekwa, zinafuatwa na pia zinabakia imara siku zote," alisema Mchallo na kuongeza:

"Hii inahitaji uangalizi na ufuatiliaji makini na imara, ikiwa ni pamoja na kuwapo kwa uwezo unaohitajika kukidhi matakwa hayo. Uwezo huo lazima uwapo pande zote; upande wa mchimba madini na pia kwa vyombo vya serikali vyenye dhamana ya kusimamia shughuli za uchimbaji wa aina hiyo."

Pia alishauri kutolewa kwa elimu kwa wadau wote kuhusu athari hizo na jinsi ya kuchukua tahadhari na hatua za kutambua, kuepuka na kuepusha athari zinazoweza kujitokeza katika mazingira mbalimbali, kama vile wakati wa kusafirisha madini hayo.

Hata hivyo, alisema urani inachimbwa ulimwenguni, hivyo inaweza kuchimbwa pia Tanzania kwa mafanikio endapo maandalizi yanayohitajika katika uchimbaji huo yatafanyika kwa ufanisi, kwa faida na kikamilifu na pande zote kabla ya uchimbaji kuanza.

"Kimsingi, maandalizi yalishaanza na tuna imani yatakuwa yamekamilika kabla ya uchimbaji kuanza," alisema Mchallo.

Wakati Nemc ikisema hayo, Desemba 7, mwaka huu, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, akihojiwa na Radio One Stereo, jijini Dar es Salaam, alisema Tanzania ni lazima ichimbe madini ya urani ambayo yanapatikana nchini na haitakatishwa tamaa na alichosema kuwa ni `propaganda' za wanaharakati.

Profesa Muhongo alisema ameshangazwa kusikia kelele zinazopigwa na vikundi vya wanaharakati wa hapa nchini na wale wa Ujerumani juu ya urani kana kwamba ni Tanzania pekee kuna madini hayo.

"Urani siyo kitu kipya duniani. Nchi nyingi zinachimba. Je, wanaharakati wanajua wanachofanya au wanashabikia tu?" alihoji na kusema serikali haijapokea taarifa yoyote kutoka Serikali ya Ujerumani juu ya taarifa za madhara ya urani kama wanaharakati hao wanavyopiga propaganda.

Kauli ya Waziri Muhongo ilifuatia baada ya taarifa za vyombo vya habari zilizonukuu Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwamba, wamepata ripoti kutoka wenzao wanaojishughulisha na ufuatiliaji wa uchimbaji urani kutoka Ujerumani kuwa shughuli hiyo ikiachwa kufanyika nchini, taifa litapata madhara makubwa.

Wanaharakati hao waliitaka serikali kutoruhusu kampuni yoyote kuchimba madini hayo nchini kwa sababu ya athari zake.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa LHRC, Imelda Urio, alisema kulingana na ushauri waliopatiwa ya uzoefu wa uchimbaji wa urani na wataalam kutoka Ujerumani, hakuna namna salama inayoweza kutumika katika uchimbaji wa madini hayo duniani kote.

Akifafanua juu ya athari hizo, Mwenyekiti wa Mtandao wa Uchimbaji wa Madini hayo kutoka Ujerumani, Gunter Wippel, alisema uchimbaji wa madini hayo ni wa gharama kwa kuwa unahitaji vitu mbalimbali, ikiwamo maji mengi. Mbali na maji mengi, alisema pia unahitaji umeme wa kutosha na ardhi kubwa, ambayo itatosha ili kunusuru wakazi wa maeneo ambayo madini hayo yanachimbwa na madhara yanayotokana na uchimbaji huo.

Waziri Muhongo mbali ya kuwataka Watanzania wapuuze taarifa hizo, alisema nchi ya kwanza kwa uchimbaji wa urani duniani ni Kirgizstan ikitoa zaidi ya asilimia 18 ya madini hayo, ikifuatiwa na Canada inayozalisha asilimia 18 ya urani yote duniani.

Nchi nyingine na viwango vya uzalishaji duniani kwa mujibu wa Waziri huyo ni Australia (11%), Namibia (8.4%), Niger (7.8%), Marekani (3.1%), Malawi (1.2%) na Afrika Kusini (1.1%).

"Wanaoogopa Tanzania kuchimba urani waende kufunga migodi Malawi. Hawa wanachimba urani karibu kabisa na mpaka wetu," alisisitiza Waziri Muhongo wakati akihojiwa na kituo hicho cha habari.

Aliwataka wananchi kutokuwa na wasiwasi kwa kuwa uchimbaji utazingatia sheria na kanuni za kimataifa katika kuendesha shughuli hiyo.

Pia alisema ni lazima kampuni za uchimbaji zipate cheti kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) kwa kuwa ndiyo yenye wajibu wa kusimamia kazi hiyo.

Alisema uchimbaji ukishaanza, Tanzania itakuwa imepiku nchi nyingine nyingi na itakuwa ya tano kwa uzalishaji wa urani duniani. Kwa maana kuwa itakuwa inazalisha zaidi ya asilimia 8.4 ya urani yote duniani.

Mbali na madhara hayo, wanaharakati pia walisema: "Madini haya yanapatikana juu ya miamba kwa asilimia 0.01. Kwa hiyo, madini mengi yanapatikana chini ya miamba. Hivyo, inabidi miamba ipasuliwe ili yapatikane. Na hutumia maji mengi kwa ajili ya kupasulia," alisema Wippel na kuongeza:

"Tafiti zinaonyesha kuwa ukitumia maji ya chini ya ardhi kuchimbia madini hayo, baada ya miaka 40 kutakuwa hakuna maji asilia na hivyo kusababisha ukame kwa Taifa."

Alisema uchimbaji wa madini hayo huleta madhara kutokana na vumbi linalochimbwa na mabaki ya madini kuwa na mionzi asilimia 80.

Wippel alisema mionzi hiyo inasababisha kansa na inasambaa kwa njia ya hewa na haraka, hivyo kusababisha madhara kwa watu wengi na kwa muda mfupi.

Alisema mionzi ya madini hayo mbali ya kusababisha kansa, pia huua viungo vya uzazi kwa wanawake na wanaume, hivyo kusababisha kuzaliwa kwa watoto wasiokamilika viungo vyote au waliozidi viungo vya mwili.

Wippel alisema baada ya uchimbaji wa madini hayo, inahitajika kazi ya kufukia mashimo na kusawazisha maeneo yaliyotumika ili kupunguza athari ambazo hudumu kwa muda mrefu.

"Ujerumani imepata hasara ya zaidi ya Sh. trilioni 14 kwa muda wa miaka 20, sasa kwa ajili ya kufanya marekebisho ya maeneo yaliyotumika kwa uchimbaji wa madini hayo, lakini bado hawajafanikiwa," alisema.



CHANZO: NIPASHE
 
Hii serikali inachezea maisha ya watu, ni wakati wa wananchi wa maeneo yatakayochimbwa urani na watanzania wote kuandamana kupinga huu mpango wa serikali wa kuchimba urani kwenye makazi ya watu!
 
kwa viongozi wetu hakuna hatari yoyote itakayo athiri wadanganyika.
 
Jamani, kwa wale mliomfahamu Prof. Muhongo kabla hajawa waziri ndo hivi alivokuwa? Mi naona kama kadri anayouzoea uwaziri anazidi kuwa kilaza vile!
 
Kitu cha msingi hapa kabla ya uchimbaji wa urani ni vyema tuimarishe taasisi zetu za kusimamia usalama zikiwemo hii ya mazingira na ya mionzi. Nilifadhaika sana niliposikia wanasiasa (ambao wengine ni wasomi) wakisema hati madhara ya urani ni pale tu inapobadilishwa kutengeneza nguvu za nuclea; na kwamba ndiyo maana watu wa maeneo ambayo haya madini yalipo wameishi nayo bila athari miaka yote!

Uchimbaji wa urani inahitaji udhibiti wa Hali ya juu ambao kwa vyombo vyetu tulivyo navyo sasa si rahisi kuutoa. Tuviimarishe kwa utalaamu na raslimali, la sivyo tutawaua watu wetu kwa faida ndogo itakayopatikana kutoka kwa hawa wawekezaji.
 
Kwa jinsi tunavyofanya mambo yetu bila kujali kuna hatari kubwa mbele yetu.
 
Uranium ni hatari,ukitaka kujua hebu google na usome uranium ni nini? Sifa za uranium, tabia yake;decay,disintegration,dissemination,half life yake na madhara yake kwa binadamu na mazingira.watawala wetu hawa wanaleta porojo na siasa kwenye mambo ya sayansi. wataalamu wamemezwa na wanasiasa,taaluma na utaalamu wao sio msaada tena ktk taifa hili. mataifa mengi dunia wanatuona ni kituko na uwenda wazimu.Tumekuwa watumwa wa pesa.
 
uchimbaji wa uranium hauhusishi milipuko yeyote. geology ya formation yake ni purely kwenye soft rocks. napata wasiwasi na kwamba taarifa hizi ni za kweli au ushabiki zaidi.
 
Uranium cannot be found as a free element. Uranium can react with water making a complex solution. When reacted with water it makes a colourless;odorless liquid and therefore you can drink water uranium contamination. In the body, the uranium settle in the kidney and Liver. stacking in the kidney would result in some kidney mulfunction. in addition, while in the body can make some reactions with traces of posphorus, Sulphate and nitrate. Compounds of nitrate and Sulphates are radiants even in a very small quantities AND THEREFORE URANIUM IS NOT SAFE!!
 
uchimbaji wa uranium hauhusishi milipuko yeyote. geology ya formation yake ni purely kwenye soft rocks. napata wasiwasi na kwamba taarifa hizi ni za kweli au ushabiki zaidi.

Nani kasema uchimbaji unatumia milipuko? IMESEMWA na NDIVYO ILIVYO kuwa inatumia MAJI MENGI.
 
Back
Top Bottom