Nchimbi atema cheche Aonya polisi 'wanaobambika' kesi, amsifu IGP

Kakke

JF-Expert Member
Dec 4, 2010
1,883
1,482
na Tamali Vullu | Tanzania Daima

WAZIRI mpya wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, amezungumza kwa mara ya kwanza na kuonya kutokuwa na huruma na mtu yeyote au chama chochote cha siasa kitakachohatarisha uvunjifu wa amani nchini.

Amesema mtu yeyote atakayetumia vibaya madaraka yake awe mwanachama wa CCM, CHADEMA, CUF au chama kingine chochote atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria, ili kuhakikisha amani nchini inaendelea kutawala.

Akizungumza na watumishi wa Jeshi la Polisi jana jijini Dar es Salaam, Waziri Nchimbi alisema jeshi hilo halipaswi kuwavumilia wanaochochea vurugu zinazohatarisha uvunjifu wa amani kwa misingi ya kikabila, rangi, ukanda na dini, kwani taifa linahitaji kuwa salama.

"Kazi ya Jeshi la Polisi nchini ni kulinda amani na mali za wananchi, hivyo mtu yeyote awe mwanachama CCM, CHADEMA, CUF au chama chochote ashughulikiwe kwa mujibu wa sheria, tunahitaji kuwa salama nchini," alisema.

Pamoja na hilo, aliwataka watumishi wa jeshi hilo kwenda na kasi yake na kwamba hatakuwa na urafiki na mtu yeyote asiyetimiza wajibu wake.

Alisema kwa muda mrefu jeshi hilo limekuwa likilalamikiwa na wananchi, hivyo linapaswa kujipanga ili kuondoa malalamiko hayo.

"Kuna malalamiko ya wananchi kusingiziwa kesi, kuchelewesha upelelezi wa kesi kwa lengo la kutaka rushwa.

"Pia baadhi wa askari wa usalama barabarani nao wanalalamikiwa kwa kuwabambikizia wenye magari makosa, ili kujipatia fedha. Nataka kuona vitendo hivi vinakomeshwa na wahusika wanachukuliwa hatua," alisema Dk. Nchimbi.

Aidha, alisema jeshi hilo linapaswa kupongezwa kwa sababu katika kipindi cha kuanzia Desemba mwaka 2011 hadi sasa limepunguza uhalifu kwa asilimia 19.

Alimmwagia sifa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Said Mwema, kwa uchapaji kazi na uadilifu wa hali ya juu na kutaka askari wengine kuiga mfano huo.

Waziri Nchimbi alilihakikishia jeshi hilo kwamba atafanya awezavyo kuwa karibu na jeshi hilo na pia atalivalia njuga suala la bajeti finyu, vifaa vya kazi na madai mengine, ili kuondosha kero zilizopo.

Awali IGP Mwema alisema jeshi hilo linapaswa kupatiwa bajeti ya kutosha, ili liweze kuwa na vifaa vya kutosha, maslahi bora na kuajiri askari wengi zaidi.

Alisema katika jeshi hilo hakuna uwiano kati ya idadi ya askari na idadi ya Watanzania wapatao milioni 45 katika shughuli za kila siku za kuwalinda na kukabili vitisho mbalimbali vikiwemo vya ugaidi, uharamia, wizi wa silaha na ajali.
 
Back
Top Bottom