SoC01 Namna ya kukabiliana na changamoto za maisha ya kila siku kwa Viziwi

Stories of Change - 2021 Competition

kamwendo

JF-Expert Member
Apr 19, 2012
881
1,852
Utangulizi
Uziwi ni hali ya upotevu wa usikivu. Hali hii hutokana na sababu mbalimbali kama vile magonjwa,ajali,uziwi wa kuzaliwa nao,kuishi sehemu yenye baridi sana na uchafu wa masikio.

Kwa nchi ya ulimwengu wa tatu kama Tanzania Viziwi na walemavu kwa ujumla ni watu waliosahaulika. Ni watu wasioaminiwa kwenye shughuli za uzalishaji mali,wenye kupuuzwa na kudharaulika.

Pamoja na wingi wa taasisi za kiserikali na za binafsi zinazojipambanua katika kuwapambania haki za viziwi na walemavu kwa ujumla bado jitihada hizo hazijazaa matunda.

Katika andiko hili nitaangazia aina za uziwi,changamoto wanazokutana nazo,nini kifanyike na viziwi ili wapate kukabiliana na changamoto za maisha ya kila siku na jinsi jamii inavyopaswa kuwaelewa viziwi na kuwasaidia inapobidi.

Kuna aina tatu za uziwi. Aina hizi hutofautiana kulingana na uwezo wa kusikia sauti,kuitafsiri na kuelewa maana iliyokusudiwa.

Usikivu Mdogo: Ni hali ya kupata shida kuelewa maneno unayoyasikia hasa ukiwa kwenye eneo lenye kelele.

Usikivu wa Kati: Mtu anashindwa kusikia sauti ki ukamilifu ila huweza kusikia kwa msaada wa kifaa cha usikivu (HearingAid).

Uziwi Kamili: Mtu hasikii kabisa huweza kuelewa mazungumzo kwa ishara au kwa kuangalia midomo ya anayezungumza nae(Lips Reading)


Changamoto wanazokutana nazo Viziwi katika Jamii.
  • Kutokukubaliwa; Jamii bado ina muamko mdogo dhidi ya walemavu wa kusikia. Mara nyingi hupuuzwa na kudharaulika iwe kwenye ngazi ya familia na hata kielimu.
  • Kutokupewa nafasi:Idadi ya walemavu wasiosikia maofisini ni ndogo mno.Iwe ofisi ya serikali au binafsi. Jamii inaamini viziwi ni watu wasioweza kufanya kazi kwa ukamilifu kitu ambacho si kweli.
  • Kusengenywa na Kupuuzwa: Kwa kutambua hali ya ulemavu wake jamii humsema na kumpuuza kiziwi kwa kumuona ni mtu asiye na maana,hii hutokea nyumban,shuleni na hata vyuoni.
  • Kutoshirikishwa kwenye mambo muhimu : Kwakuwa jamii inaona ugumu wa kuwasiliana na viziwi hupelekea kuwatenga kwenye maamuzi muhimu kwa mustakabali wa maisha yao na wengine. Maamuzi juu ya elimu na afya zao huamuliwa na wazazi au walezi.

Hatua zinazopaswa kuchukuliwa na viziwi ili kukabiliana na changamoto za kijamii.
  • Kujikubali na kuikubali hali yako: Hii ni hatua ya mwanzo na muhimu zaidi kwa mtu yeyote mwenye ulemavu. Ni hatua muhimu sababu kuikubali na kuielewa hali yako inasaidia kuifanya akili itafute namna ya kukabiliana na tatizo lako.
  • Kwa walemavu wa kusikia kupenda kujifunza vitu tofauti na kuwa na shauku ya kufanikiwa kwa chochote unachokifanya ni hatua muhimu zaidi.
  • Chukulia kudharaulika na kupuuzwa na jamii kama changamoto zaidi za kukujenga ili uwe bora zaidi.
  • Usiruhusu hali ya unyonge ikutawale. Kamwe usiwe na mawazo hasi juu yako kutokana na maoni ya wengine.
  • Fanya kazi kwa bidii,kama unasoma soma kwa bidii ili uweze kuziba madhaifu yako.

Jamii inavyoweza kuishi na viziwi na kuwasaidia inapobidi.
  • Kuwaelewa na kujifunza namna ya kuwasiliana nao kwa lugha za ishara na lugha ya mdomo.
  • Jamii inapaswa kujua viziwi ni binadamu kama binadamu wengine wenye utashi na akili zao ambao wanastahili kupendwa,kuthaminiwa na kusikilizwa.
  • Jamii na serikali kwa ujumla itoe nafasi za ajira kwa walemavu hawa kulingana na utaalamu walionao ili waweze kuwa wazalishaji mali na kuchangia pato la taifa.
  • Serikali na sekta binafsi kupitia taasisi za elimu na afya iweke wakalimani wa lugha ya alama ili kuliwezesha kundi hili la walemavu wa kusikia kupata elimu na matibabu bora.
  • Wazazi,walezi na jamii kwa ujumla isiwafiche watoto wenye uziwi na iwaepushe na unyanyasaji wa kijinsia.
  • Serikali iendelee kuboresha mikopo yake kwa walemavu wa kundi hili kwa kuwapa masharti nafuu ili waweze kupata mitaji ya biashara na kuchangia ukuaji wa uchumi.

Hitimisho.

Jamii, Wazazi na walezi wanapaswa kubadili mitazamo yao mibaya dhidi ya walemavu wa kusikia,kukemea unyanyapaa dhidi yao na kuwapa nafasi ya kwenda shule watoto wasiosikia na kuwalinda dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia.

Serikali inapaswa kuandaa mkakati mpya wa maboresho ya sera dhidi ya walemavu ilikuwawezesha viziwi kupata huduma bora za elimu, kazi na afya.

Serikali inapaswa kuongeza idadi ya shule za viziwi katika kila wilaya ili wazazi na walezi wahamasike kuwapeleka watoto shule. Idadi ya wakalimani katika vituo vya afya iongezwe ili kuleta ufanisi wa mawasiliano katika matibabu.

Serikali itenge nafasi zaidi za ajira kwa viziwi wenye utaalamu wa fani husika. Ni vyema lugha ya alama ikatambulika rasmi na katiba ili iwe rahisi kutiliwa mkazo katika kuwasiliana na walemavu wa kusikia katika nyanja zote.
 
Back
Top Bottom