Mzimu wa Meremeta wamsumbua Pinda; Mnyika CCM kimetangaza kujivua Magamba nani mmiliki wa Meremeta?

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797




Na Edmund Mihale, Dodoma

MZIMU wa Kampuni ya Meremeta uliibuka tena bungeni Dodoma jana, baada ya Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Bw. John Mnyika kumtaka Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda kuwataja wahusika wa kampuni hiyo lakini akaambulia patupu.

Wahuska katika kampuni hiyo ambao hawajawahi kutajwa hadharani wanatuhumiwa kuchota Dola za Marekani 118,396,460.36 fedha Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Hayo yaliibuka katika kipindi cha maswali ya papo hapo kwa Waziri Mkuu, ambapo Bw. Mnyika alimuuliza Bw. Pinda kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimtangaza kujivua magamba ilikujisafisha na ufisadi hivyo kumtaka kuwataja wahusika wa Kampuni hiyo.

"Mheshimiwa Mkuu uliwahi kulieleza Bunge hili tukufu kwamba usingetaka kabisa kuzungumzia masuala ya Meremeta kwa sababu ni siri za Jeshi. Baada ya kauli hii ya Rais na dhamira hii ya kujivua gamba kuhusiana na masuala ya ufisadi. Je, uko tayari Mheshimiwa Waziri Mkuu kutaja wahusika wa Kampuni ya Meremeta na kuelekeza serikali kuchukua hatua zinazostahili kuhusiana na tuhuma hizo?" aliseama Bw. Mnyika.

Akijibu swali hilo, Bw. Pinda alisema: "Rafiki yangu Mnyika hilo umerukia, hayo ni mambo ya ndani ya CCM la kujivua magamba kwa CCM ni kwa kuwa hayo ni mambo ya ndani ya chama, kwa hiyo halikuhusu na wala hapa si mahali pake."

Pamoja na majibu ya Waziri Mkuu, Bw. Mnyika, alisema katika ytaarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa, kwa nafasi yake ya Uwaziri Kivuli wa Nishati na Madini anaitaka serikali itoe kauli ya kuruhusu ukaguzi maalumu kufanyika katika mahesabu ya kampuni ya Meremeta na kueleza hatma ya mgodi wa Buhemba ambao mali zake zinaendelea kuibwa.

Katika Orodha ya Mafisadi (List of Shame ) iliyotolewa na CHADEMA Septemba 15, 2007 katika Uwanja wa Mwembe Yanga, Dar es salaam ilielezea kuwa katika Ufisadi wa Meremeta Ltd kuwa malipo ya Dola za Marekani 118,396,460.36 zilizopelekwa katika akaunti isiyojulikana ya Benki ya Nedbank Ltd. ya Afrika Kusini kama malipo ya madeni ya kampuni muflisi iliyokuwa inachimba dhahabu katika eneo la Buhemba wilaya ya Musoma, Mkoa wa Mara.

Awali, serikali ilikuwa ikisema kwamba Meremeta Ltd. ilikuwa ni kampuni ya Kitanzania iliyokuwa ikimilikiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa ajili ya mradi wake wa Nyumbu, Kibaha, Mkoa wa Pwani. Hata hivyo, nakala ya usajili iliyotolewa na Msajili wa Makampuni wa Uingereza na Wales inaonyesha kwamba kampuni hiyo iliandikishwa nchini Uingereza Agosti 19, 1997 na ilifilisiwa huko huko Uingereza Januari 10, 2006.

Aidha, taarifa ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ya Mei 31, 2005 inaonesha kwamba Meremeta Ltd. ni tawi la kampuni ya kigeni iliyosajiliwa Tanzania kama tawi, Oktoba 3, 1997. Vile vile taarifa hiyo inaonesha kwamba hisa 50 za Meremeta Ltd. zilikuwa zinamilikiwa na Kampuni ya Triennex (Pty) Ltd. ya Afrika Kusini na hisa 50 zilizobaki zilikuwa zinamilikiwa na Serikali ya Tanzania kwa kupitia kwa Msajili wa Hazina katika Wizara ya Fedha.

Hata hivyo, kuna utata mkubwa juu ya nani ni mmiliki hasa wa Meremeta Ltd. kwa kuwa taarifa ya BRELA inaonesha pia kwamba kampuni mbili za Kiingereza – London Law Services Ltd. na London Law Secretarial Ltd. – nazo zinamiliki hisa moja kila moja, za Meremeta Ltd. Kampuni hizo zinatumia anwani moja iliyoko 84 Temple Chambers, Temple Avenue, jijini London.

Benki Kuu iliruhusu fedha za umma kutumika kulipia madeni yote ya kampuni ambayo Serikali ilikuwa inamiliki hisa 50 tu wakati makampuni mengine ya kigeni yalikuwa yanamiliki hisa 52. Na kama ilivyosema barua ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, uhalali wa Serikali kulipa madeni ya Meremeta Ltd. kwa Nedbank Ltd. badala ya kuiacha benki hiyo kudai malipo hayo kutoka kwa mfilisi wa kampuni hiyo sawa na wadeni wengine haujulikani;

Kwa mujibu wa barua ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Benki Kuu iliruhusu au kunyamazia malipo mengine ya Dola za Marekani 13,736,628.73 kwa kampuni ya Tangold Ltd. Katika hotuba yake bungeni ya tarehe 27 Juni 2007, Waziri wa Madini na Nishati Bw. Nazir Karamagi alidai kwamba"… mali na madeni ya MEREMETA yamehamishiwa kwenye kampuni mpya ya TANGOLD ambayo inamilikiwa na Serikali kwa asilimia mia moja.”

Hata hivyo, barua ya BRELA ya Julai 4, 2007 inatamka wazi kwamba “Tangold Limited ni kampuni ya kigeni iliyosajiliwa kwa mara ya kwanza nchini Jamhuri ya Mauritius, na baadaye kuandikishwa nchini Tanzania kama tawi la kampuni ya kigeni.” Barua hiyo inaongeza kwamba kampuni hiyo ilipewa hati ya kutimiza masharti ya Tanzania Februari 20, 2006 na kwamba Katiba ya kampuni hiyo haikuonyesha “majina ya wanahisa wa kampuni na mgawanyo wa hisa.”

Barua hiyo ya BRELA inaonyesha kwamba wakurugenzi wa Tangold Limited ni pamoja na Gavana Balali (Marehemu), Bw. Gray Mgonja na Bw. Andrew J. Chenge. Aidha fomu Na. 1F inayohusu usajili wa kampuni za kigeni iliyowasilishwa BRELA na mawakili wa Tangold Limited na kusainiwa na Gavana Balali Mei 20, 2005 inaonyesha kwamba kampuni hii ilitokea “Jamhuri ya Mauritius” na anwani yake iko Suite 520, Barkly Wharf, Le Caudan, Waterfront, Port Louis, Mauritius.

Akijibu swali la Mbunge Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe, alitaka kujua serikali imechukuwa hatua gani baada ya ripoti ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikili kuhusu taarifa ya upotevu wa sh. bilioni 48 zilizotolewa na serikali kusaidia walioathirika na mdorodoro wa uchumi, Bw. Pinda alisema kuwa hadi sasa hana taarifa ya jambo hilo, hivyo yuko tayari kulitolewa ufafanuzi baada ya kupata taarifa.
 
mimi nawaulizeni watanzania wenzangu, tuyaache mambo kama haya yaendelee hadi lini? pesa zetu watu wanagawana halafu tunasubiri kila kitu kinachohusu maisha yetu kifanyike " kwa hisani ya watu wa Marekani!!!" hadi lini? tumelemaa akili sisi, kabisa! jana kuna kiongozi mmoja wa taasisi ya lugha ya kiswahili, bila aibu analalamika kuwa eti wafadhili wengi wa nje hawataki kutoa fedha zao kwa ajili ya kukuza kiswahili!!! niliona aibu sana. kumbe uwezo wa kujifanyia mambo yetu upo ila tu kuna walafi tumewapa dhamana badala ya kuwapa pingu na magwanda ya pink!
 
Back
Top Bottom