SoC01 Mwenendo wa Demokrasia Tanzania

Stories of Change - 2021 Competition
Nov 15, 2015
5
2
Demokrasia ni mfumo wa utawala ambao watu wana sauti ya juu kabisa katika kuisimamia serikali yao wakati inatekeleza majukumu ambayo muhimiri wa madaraka unabebwa na nguvu ya umma kupitia wawakilishi. Tangu kuingia madarakani kwa serikali ya awamu ya tano 2015-2020 kumekuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu na utawala bora, kutofuata mwongozo wa katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho yake hususani ya mwaka 1984 yaliyoingiza haki za binadamu katika katiba, Jumuiya za Kimataifa ambazo Tanzania pia ni mwanachama. Pia mikataba ya kimataifa mfano Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu(ACHPR), Mkataba Unaoanzisha Afrika Mashariki(1999) ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa haki za Binadamu(ICCPR).

Marekebisho madogo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaliyofanywa mwaka 1992 yaliruhusu mfumo wa vyama vingi ili kurudisha demokrasia na kuwapa fursa wanachi kujiunga na vyama na kuchagua Viongozi wanao wataka, mfumo ambao matakwa yake ni vyama vingi na ushiriki wa wananchi katika siasa, unaolenga kuwapa uhuru katika maamuzi yanayogusa maeneo ya kiutawala kwa mstakabari wa maendeleo yao.

Kutokana na matakwa ya kidemokrasia ukiukwaji wa haki za binadamu umedhihirika kutokana na kuingiliwa kwa Uhuru wa kujieleza, uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kukusanyika na haki ya kuishi katika maeneo haya kumekuwa na mwingiliano na kupelekea uvunjifu wa amani , pia kupelea Raia kupoteza haki nyingine za msingi ikiwepo ya kuishi na ya kiusalama.

Mhe. Edward Lowassa akiwa Waziri mkuu Tanzania aliwahi kusema ili kupima ukomavu wa demokrasia katika Taifa inapaswa kufanyika tathmini kupitia vigenzo vifuatazo;​
  • Uimara wa asasi za siasa;​
  • Ulinzi wa haki za raia kisheria;​
  • Urari katika mgawanyo wa mamlaka;​
  • Ushiriki wa wananchi katika siasa;​
  • Uenezi wa habari;​
  • Kujengeka kwa utamaduni wa kidemokrasia; na​
  • Ushindani wa amani.​

Mapendekezo haya yalitolewa na Mh Edward Lowassa (Mb) katika “Mkutano wa Hali ya Siasa Tanzania”, chuo kikuu cha dar es salaam, tarehe 25 Julai, 2006 mapendekezo yote haya yalilenga kuthamini iwapo vigezo tajwa ni imara, miaka kadhaa baadaye imedhihirisha kujua kwamba taasisi tajwa hazina uimara wa kutosha katika suala la kutoa mchango katika eneo la demokrasia Tanzania kwasababu yaliyojitokeza katika utawala wa 2015-2020 yamepelekea Tanzania kuonywa mara nyingi na Jumuiya za kimataifa, asasi za kiraia na vyama vya siasa. Kutokana na hali hii Tanzania imepitia katika kipindi kigumu ambacho matukio yafuatayo hayatasahaurika kwa Watanzania hasa wapenda haki na maendeleo ya Demokrasia nchini​
  • Matukio ya utekwaji wa Raia ambayo hayajapatiwa ufumbuzi mpaka sasa.​
  • Uvamizi katika taasisi za kisheria mfano IMMA​
  • Vurugu katika mikutano ya kisiasa na mazuio yanayokiuka haki za kisiasa.​
  • Mauaji ya KIBITI na miili ya watu kukutwa katika fukwe za bahari ya hindi ikiwa kwenye viroba.​
  • Kushambuliwa kwa Rais wa TLS, Mbunge wa Singida Mashariki (Tundu Lisu)​
  • Kuminywa kwa uhuru wa vyombo vya habari(fungia fungia ya magazeti, Radio na Vituo vya Television)​

VYOMBO VYA DOLA DHIDI YA DEMOKRASIA
CHADEMA, CUF na ACT Wazalendo wameripoti kuingiliwa na jeshi la polisi hata kwenye mikutano yao ya ndani ambayo ipo kikatiba. Kamata kamata ya viongozi wa siasa na ubambikizaji wa kesi, kuteswa na kuachiwa bila kufikishwa mahakamani. Unyang’anyi wa haki ya msingi ya kujieleza ikiwa pamoja na kunyimwa dhamana kinyume na taratibu za kisheria , ikumbukwe kwamba muendesha mashtaka wa serikali (DPP) alikuwa akitumia kifungu namba 148(4) ambapo mwaka 2015 mahakama ilitamka kwamba kifungu kinakwenda kinyume na katiba ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jeshi la polisi liliendelea kuwanyima dhamana baadhi ya wanasiasa.

Haya jaanza leo, mwaka 2001 visiwani Zanzibar ukirudi katika utawala wa Mh Benjamin Wiliam Mkapa* inaonesha miongoni mwa matukio ya kukumbukwa sana ni katika tukio la maandamo ya amani yaliyofanyika mwaka 2001, maandamano ambayo ni maokeo ya kukosekana kwa haki katika uchaguzi uliofanyika oktoba 2000, ambapo ilidaiwa kutokuwa huru na wa haki, ulikumbwa na udanganyifu na dhuruma.

Wengi walifariki kutokana na jeshi la polisi kuingilia na kuweka vizuizi, shirika la Human Right Watch(HRW) lilidai kuwa zaidi ya watu 35 waliuawa na wengine kujeruhiwa ambapo baadhi ya wanasiasa walikimbilia nchi jirani kutafuta hifadhi, idadi iliyotolewa na serikali ilikuwa tofauti na idadi iliyotolewa na CUF lakini pia taarifa zilitofautiana na ya HRW, taarifa ya serikali ilidai kuwa watu waliofariki walikuwa 23 huku majeruhi wakiwa 82 ndani yake wakiwa maaskari 10, na 352 kukamatwa kwaajili ya mahojiano, huku chama cha wananchi CUF kikidai kwamba watu 67 walipoteza maisha, wakati HRW wakisema 600 walijeruhiwa.

Kutokana na idadi kamili kutoeleweka HRW walihitmisha kuwa idadi ya Waliokufa, waliojeruhiwa na waliokimbia nchi haijulikani kwasababu ya msigano baina ya pande tatu katika takwimu, pili kutokana na kukosekana kwa ushirikiano kutoka kwa viongozi.[HRW Report 2001]​

VYOMBO VYA HABARI NA WANAHABARI.
Magazeti, Redio na Runinga ni baadhi ya vyombo vya habari vilivyofungiwa na kupigwa faini mara kadhaa pamoja na kukamatwa Waandishi wa habari, wahanga wengine ni watumia mitandao ya kijamii ambao walikutana na joto kupitia kivuli cha sheria ya 2015, Cyber Crime Act, yaliibuka maswali mengi, ambayo yalihitaji majibu.

Mambo haya yalichangia pakubwa watu kukumbuka tukio la kule Nyororo mkoani Iringa katika Wilaya ya Mfindi ambapo Daudi Mwangosi aliuawa, na uchunguzi wake ukaibua maswali mengi, mgogoro wa Cloud Media na mkuu wa mkoa, kutekwa Azory Gwanda mwandishi wa habari za uchunguzi ni ushahidi tosha kwamba palikuwa na shambulio katika eneo la habari lililolenga kufifisha demokrasia nchini Tanzania, uhuru wa habari uliibua hisia kali kutokana na aina ya miisho ya matukio.​

DHIDI YA WANASIASA
Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 3. -(1) Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, kwa bahati mbaya vyama hivi na wanasiasa wake wamepitia katika mkono wa chuma kwa mateso pamoja na kuwekwa kizuizini bila kupelekwa mahakamani, kunyimwa haki ya kujieleza, haki ya kukusanyika, na kuzuiwa kufanya mikutano na maandamano yanayotambuliwa kisheria.

Tangazo la nchi yenye Mfumo wa vyama vingi Sheria ya 1992 Na.4 ib.5 inatambua haki ya kila chama na nafasi zake katika majukwaa ya kisiasa, isivyo bahati ni kwamba imekiukwa mara kadhaa katika suala la haki za kidemokrasia, mfano; haki na uhuru wa kukusanyika, kufanya mikutano ya kisiasa, maandamano na kuingiliwa uhuru wa vyombo vya habari.Watanzania wanaopenda demokrasia watakuwa mashuhuda kwamba nyakati zote tangu 1992 kulikuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu, sheria na Utawala bora lakini katika kipindi cha 2015-2020 kimekuwa kipindi chenye upekee sana kwa wanasiasa kutoka katika vyama mbalimbali kukumbana na mikasa inayovunja haki na misingi ya kidemokrasia.

Viashiria hivi bila shaka havina afya sana katika maendelea ya haki za binadamu, uhuru wa kujieleza, na utawala bora, kwasababu katika kesi nyingi ambazo wanasiasa wamekumbana nazo wameshinda, tafsiri yake ni kwamba kesi hizi zilitengenezwa kwa maksudi ili kurudisha nyuma nguvu ya vyama na demokrasia.​

TASWIRA YA DEMOKRASIA NA BUNGE
Katiba ya Tanzania ibara 63.-(2)Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hii.

Kwa msingi huu bunge linawajibika kuhoji iwapo serikali inafanya jambo ambalo linatafsiriwa kuwa halina maslahi kwa Wananchi kwasababu serikali ni mamlaka ambayo kwa mujibu wa sheria ipo chini ya wananchi, katiba ya mwaka 1977 ibara ya 8.-(1).-(a) “wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii;” turudi nyuma sasa kwenye udhaifu wa bunge kupitia ripoti iliyotolewa na CAG ambaye ni Prof, alisema bunge ni dhaifu kwa vigezo vya kitaalamu, alionesha kwamba bunge limeshindwa kuwajibika ipasavyo katika sehemu ya kuisimamia serikali kwasababu ndani ya serikali kulikuwa na ubadhilifu wa fedha, bunge lilianza kukabiriana na CAG mpaka kumuita kwenye kamati ya maadili.

Bunge lilijiondoa kwenye nafasi ya kuwawakilisha wananchi ambao kwa nafasi yao walitarajia kuona bunge lao linahoji vyema ni kwanini mabilioni ya fedha hayaonekani. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kilichoitwa Bunge Maalumu ambalo majukumu yake yalitarajiwa kuiletea Tanzania katiba mpya lilishiriki katika mchakato wa mabadiliko ya katiba mpaka kupatikana kwa “Katiba Pendekezwa” , baadaye Mheshimiwa JPM akasema hicho si kipaumbele, kwa udhaifu wa bunge halikusimamia upande wa Wananchi huku wakisahau kwamba mabilioni ya fedha za umma yalitumika kwaajili ya mchakato ambao mwishowe sasa unaonekana hauna maana, je nani alipaswa kuihoji serikali ya JPM juu ya hili?.

Miongoni mwa majukumu ya Msingi ya Bunge ni kutunga sheria, suala la kutunga sheria ni jukumu linalohitaji macho ya kitaalamu na ushirikishaji, katika hali ya kushangaza bunge limehusika kutunga sheria zilizokosolewa vikali, na utunzi wa baadhi ya sheria unaonekana kukusudia kunyamazisha ukosoaji, mfano wa sheria iliyopata ukosoaji mkubwa ni pamoja sheria ya mitandao, the cyber Crime Act , 2015 sheria hii ilitungwa mahsusi kwaajili ya mitandao ambapo upatikanaji wake unadaiwa na wakosoaji kuwa haukuwa shirikishi hata kupelekea kupatikana kwa sheria kandamizi kwa watumiaji wa mitandao, watu wengi walikamatwa na polisi na kufikishwa mahakamani na miisho ya kesi zao imekuwa tofauti kutokana na namna ya matumizi na maudhui ya ujumbe ulioandikwa. Ili kukuza demokrasia tunapaswa kufanyia kazi yafuatayo.​
  • Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania​
  • Uhuru wa vyombo vya habari​
  • Utendaji kazi wa Jeshi la Polisi​
  • Kuondoa mgongano ya mihimiri Mikuu katika Taifa​
  • Haki za binadamu na Mfumo wa Utawala.​

Yakifanyiwa kazi yataleta tija
 
Back
Top Bottom