SoC03 Mwanamke uvumilivu Bibi

Stories of Change - 2023 Competition

Mkuki13

New Member
Jun 7, 2023
3
2
MWANAMKE UVUMILIVU BIBI!
TUKOMESHE TABIA ZA KUVUMILIA NA KUHALALISHA VITENDO VYA UKATILI.


Nenda “Kicheni pati” utasikia sifa kuu ya mwanamke ni uvumilivu, “sendi ofu” mwanamke kuvumilia, kwa mama mchungaji nako binti uvumilivu!, bibi nae mvumilivu hula mbivu, mama ndo kabisa atakwambia mimi nisingevumilia tusingefika hapa. Haya sasa we binti usiye na uvumilivu nani atakusikiliza na visingizio vyako visivyo na maana? Sababu zisizo na msingi. Lipi jipya ambalo wenzio hawajapitia? Utaambiwa watoto wa siku hizi mmekosa adabu, kutwa kuachika na waume zenu. Zamani sisi ukiolewa mwiko kurudi nyumbani labda kama hupatiwi unyumba, tena ukiwa hupatiwi unyumba utaenda tu kwa somo wako atawakalisha mambo yatakaa sawa. We kuolewa mke wa pili tu umerudi! Kupigwa kidogo umerudi! Ndoa uvumilivu na kusitiri siri za mumeo. Kwanza mwanamke unyenyekevu, usipigizane kelele na mumeo, mume analindwa kwa maneno matamu na utulivu ndani ya nyumba. Akirudi usiku wa manane na manukato mapya mwambie “shikamoo mme wangu, pole na kazi” huku unampokea alichokibeba hata kama ni kanga iliyochoka, kisha mpatie busu. Muandalie maji mumeo aoge, mkande kisha muongee kuhusu familia kwa furaha mpumzike.

We mwanamke usiwe mwingi wa hasira, maana hasira hasara. Tamaa za mumeo zikiruhusu mwanamke mwingine kwenye maisha yenu utakuwa umebomoa nyumba yako kwa mikono yako wewe mwenyewe tena utakuwa mjinga. Wewe ambae umeambiwa umtii mume wako kwakuwa yeye ni kichwa cha familia! Kwa uelewa wangu kichwa ni makao makuu ya mwili wa binadamu na kichwa kinapopata hitirafu hata mwili hudhohofu.

“Amelaaniwa mwanamke yule anayeishi bila kuolewa siku zote za maisha yake”. Yule naye kazidi ujuaji, nani atamuoa alivyo mjeuri! Watasema watu wanaomzunguka. Aise! Jua linazama na ukali wake, watasema wanaume wanaomtamani. Laana ya ukoo, nguvu za kukataliwa zimuachilie! Watasema viongozi wa dini. Huenda amefungwa na bibi yake babu, tumpeleke kwa babu wa Loliondo apatiwe kikombe! Bibi atamshauri mama. Kwani shida ni nini? Shida ni mwanamke kuamuwa anataka kuishi vipi? Unafikiri kila mtu amejaliwa uvumilivu sababu tu ni mwanamke? Au kila mwanamke mtiifu hata kwa vichwa vibovu? Hivi ni kila kichwa kinafaa kuongoza? Je, unasemaje kuhusu vile vichwa ambavyo vilitakiwa vifanyiwe upasuaji kwasababu vina hitirafu? Na vyenyewe vipewe uongozi?

UPENDO NI NINI?

Hata mimi sijui.

Wengi hutamka neno “nakupenda” lakini uhalisia ni kwamba wanamaanisha “nakumiliki” kwa uelewa wangu upendo husamehe, huchukulia, upendo hufanya mtu ajali furaha ya ampendae haijalishi furaha inabeba maumivu au laa. Hujali zaidi uhuru wa umpendae.

Ila nimeona wengi wakiumiza na kujeruhi miili na miyoyo ya watu wawapendao wakidai walifanya hivyo kwasababu ya upendo. Na walio umizwa na kujeruhiwa walinyamaza kwakuwa waliaminishwa upendo ni kuvumilia. Sisemi wanaume hawaumizwi wala kujeruhiwa.

Hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la ukatili wa kijinsia ambao umekuwa ukiwaathiri wanawake kwa idadi kubwa kuliko wanaume kutokana na matukio yanayo ripotiwa katika mitandao ya kijamii na uswahilini kwetu. Binafsi nimefuatilia visa hivi katika mitandao ya kijamii na maoni mengi kutoka kwa wananchi jinsia zote yalilenga zaidi kumlaumu mwanamke kwa kuwa chanzo cha kuchochea ukatili huo. Wengi walisema “mwanamke hapigwi bila sababu”, wengine wakadai “ukiona mwanamke kapigwa maana yake hana heshima kwa mume, ana mdomo na hamsikilizi mumewe au mwenza wake”. Hii ikanifanya nikagundua bado kuna changamoto kubwa katika jamii zetu. Wengi hutetea vitendo vya kikatili kwa kumhukumu muhanga wa tatizo hilo pasipo kuangalia upande wa mwanaume ambao ndio chanzo cha tatizo hilo. Umewahi kujiuliza ni mangapi wanaume wanafanya kwa wake au wenza wao na bado wanawake wanaishi na hao wanaume kwa upendo? Unadhani wao hawana aibu au moyo wa kuumia? Kwanini mwanamke pekee ndo apewe adhabu anapokosea? Kwanini mwanaume asifiwe na kupongezwa kwa kosa hilo hilo ambalo mwanamke anapondwa akifanya?

Wanawake wengi wanapitia changamoto za kunyanyasika kisaikolojia na kimwili na wenza wao lakini hawasemi kwasababu tayari wameaminishwa wanapaswa kuvumilia, kwasababu wanahisi ni sawa kupigwa au kupewa maneno makali yenye kuondoa utu pale unapokua umekosea. Dini na tamaduni vimeondoa thamani ya mwanamke na kumfanya ajihisi ana nafasi moja tu, ya kunyenyekea hata mahali ambapo hastahili kunyenyekea. Kutokuwa na kipato au shughuli ya kukusaidia kuendesha maisha yako kama mwanamke pia kunachangia kiasi kikubwa wanawake kunyanyasika na kutosema pale wanapo nyanyasika kwa kuhofia kupata fedhea wakiachika.

Japokua siku hizi wanaume wanaotegemea wanawake wanaongoza kunyanyasa wanawake zao kwasababu wanahisi wamezidiwa uwezo kwa kuwa wame aminishwa mwanamke nafasi yake ni ya pili kutoka kwa mwanaume. Wanapohisi hawapo kwenye hio nafasi ya kwanza basi hutafuta namna za kumfanya mwanamke arudi katika nafasi ya pili, hivyo hutumia ukatili wa kisaikolojia au kimwili kumfanya mwanamke amheshimu. Hii hutengeneza hofu na sio heshima. Ukosefu wa maisha mazuri ambao hupelekea wanaume wengi kuwa na msongo wa mawazo na kuchanganyikiwa, mambo ambayo yanapelekea hasira zisizo na kiasi mwisho wanafanya vitendo vya kikatili. Uko wapi upendo?

Katika kupambana na ukandamizaji na ukatili wa kijinsia inabidi kila mmoja achukue jukumu la kuelewa na kukubali kuwa hakuna kosa ambalo ni sawa kwa mwanaume kumuazibu mke. Hakuna mwanamke anapaswa kupigwa wala kufanyiwa vitendo vya kikatili anapokosea, kama mambo yamewazidia ni vizuri kuomba msaada kwa waliowatangulia. Tuelewe pia kuwa hakuna mtu anaemmiliki binadamu mwenzie, maana kufikiri kuwa unammiliki mtu unaempenda kumeleta matatizo mengi sana katika jamii, nchi na dunia kiujumla. Uwekwe mfumo wa upimaji afya ya akili ili kudhibiti tabia za kikatili zinazoweza kusababishwa na matatizo ya akili.

Maana kuna watu wanatembea lakini si wazima vichwani mwao. Wamejaa giza na ukatili ambavyo huwezi kuona hadi siku mashetani yapande, ndo wakishaua utasikia watu mnafanyiwa ukatili hamsemi hadi muuliwe! Na marehemu ndo hajiteteagi. Kama ndo mwanzo kafanyiwa ukatili akafariki je? Tuondoe dhana ya mwanamke uvumilivu, imezika na kujeruhi wengi. Zaidi wanawake tujitambue jamani!

Hata kama hujasoma usiogope kuwa na maisha yako bila kumtegemea mwanaume. Na unapokatiliwa usiogope kusema na kuondoka maana kubaki kunaruhusu mnyanyasaji kukudharau na kuendelea kukunyanyasa. Uhai ni mhimu kuliko mali, usiogope kuanza tena. Mwenzenu uvumilivu ulinishinda, kofi moja tu nikaacha mjengo Masaki nipo zangu Manzese kwenye chumba cha giza. Kikubwa napumua na naamini nna nafasi nyingine tena, nitapambana nitashinda na zaidi. Serikali nayo iongeze nguvu katika kutoa elimu kwa rika zote ili kuweza kutambua thamani ya mwanamke na kujenga kujiamini, kujitambua na kuwe na mafunzo ya jinsi ya kujilinda na ukatili.

MWANAMKE KUJITAMBUA BWANA!
 
Back
Top Bottom