Mtambuzi
Platinum Member
- Oct 29, 2008
- 8,810
- 15,398
Wiki iliyopita niliandika mada kuhusu dalili za hisia za usaliti katika mapenzi, unaweza kujikumbusha kwa kufungua hapa: https://www.jamiiforums.com/mahusia...sia-za-usaliti-katika-mahusiano%85%85%85.html
Niliahidi kwamba wiki hii nitaweka mada kuhusu jinsi ya kushinda hicho kishawishi na ndoa au uhusiano wako ukaendelea kuwa imara. Kama unajikuta uko kwenye mtego huo wa kuisaliti ndoa yako kwa kujikuta ukiwa na hisia za usaliti wa mapenzi (emotional Infidelity) unaweza kuchukua tahadhari kabla ya hatari kwa kufanya yafuatayo:
1. Jiweke mbali na kishawishi hicho kwa kuweka mipaka ya kukutana na mtu huyo, na hakikisha unajitahidi kumfuta katika mawazo yako……. Katu asitawale mawazo yako.
2.. Kamwe usimshirikishe kwenye matatizo yako, wasiliana na mumeo au mpenzi wako pindi upatapo tatizo linalohitaji msaada wa haraka
3.Kama kuna ulazima wa kutoka naye kwa jambo lolote, basi usitoke naye ukiwa peke yako, hakikisha mtoko wenu unawahusisha watu wengine, mnaweza kuwa kundi la marafiki au wafanyakazi wenzako, usije ukaruhusu mazingira ya kuwa peke yenu.
4.Hamisha mawazo yako yote kwa mpenzi wako au mumeo, na hakikisha unampa mpenzi wako kipaumbele kuliko huyo rafiki mpya.
5.Panga mtoko na mumeo au mpenzi wako ambao utawasha moto wenu wa mapenzi wa awali kama unaoekana kufifia.
6..Iwapo unafanya naye kazi ofisi moja na kama huwa inatokea mnafanya kazi muda wa ziada, kwepa kubaki ninyi wawili tu hapo ofisini…. Jambo hilo litakufanya uwe naye karibu na hivyo kuendelea kumpa nafasi ya kutawala mawazo yako
7. Kama ni mtu unayemtegemea kumuomba msaada kikazi na huwa anakusaidia, basi tafuta mtu mwingine atakayekuwa anakusaidia, lakini usimuonyeshe kama unamkwepa, anaweza kufanya udadisi na jambo hilo likakupa wakati mgumu.
8. Jitahidi kuwa unawasiliana na mpenzi wako au mumeo mara kwa mara kwa simu uwapo ofisini ili kurejesha ukaribu wenu
9. Jiepushe na kumweleza matatizo yako na mwenza wako hata kama ni jambo ambalo unahitaji ushauri, tumia vituo vya ushauri na kama ushauri huo ni lazima utoke kwa mtu wa jinsia tofauti na yako basi tafuta mtu wa mbali usiyekutana naye mara kwa mara.
10. Hakikisha unaimarisha uhusiano wako na mwenza wako kwa namna yoyote na hata kama ikibidi kujishusha…………
Ni vyema kila mtu akajua kwamba kila mtu yuko kwenye hatari ya kukumbwa na hisia za usaliti wa mapenzi (emotional Infidelity) hata kama una uhusiano imara kiasi gani, hilo hakuna awezaye kulikwepa. Hiyo ni kwa sababu mvuto wa kimapenzi kwa mtu mpya mwenye jinsia tofauti ni jambo la kawaida sana, na linaloleta msisimko. Kinachotokea ni kwamba wapo wanaomudu kushinda kishawishi hicho na ndoa zao zikaendelea kuwa imara, lakini wapo ambao hushindwa na kujikuta wakiwasaliti wenza wao.
Lakini pia hisia za usaliti wa mapenzi zina faida zake, kwani hutukumbusha ni kitu gani tunakikosa kwa wenzi wetu na hivyo kutuweka katika nafasi nzuri ya kudai hicho tunachokikosa kwa wenzi wetu na kuziba pengo hilo. Kumbuka kwamba hisia za usaliti wa mapenzi (Emotional infidelity), maana yake ni kwamba unaruhusu mtu mwingine wa jinsi tofauti azibe pengo la hisia ambalo lingetakiwa lizibwe na mpenzi wako au mume wako.
Hivyo usijisikie vibaya iwapo utajikuta ukikabiliwa na hali hiyo, kinachotakiwa ni kufanya hayo niliyoeleza hapo juu kisha boresha uhusiano wako na huyo mpenzi wako au mumeo umpendaye. Ni pale tu utakapojiwekea mipaka na marafiki wa jinsia tofauti ndipo utakapokuwa salama na kishawishi hicho cha hisia za usaliti wa mapenzi.
Tukutane wakati mwingine……………Nitakapokuja na mada ya namna ya kujitoa katika hisia za kumpenda mpenzi uliyeachana naye…….!