Mwalimu Nyerere hakuwa na insafu juu ya Muungano

Hamid Rubawa

Member
May 23, 2018
72
202
BARAZANI KWA RAJAB
Na Ahmed Rajab
MARA ya mwanzo kabisa kukutana na Mwalimu Julius Nyerere, uso na macho, ilikuwa 1968 jijini London ndani ya ukumbi mmoja wa hoteli iitwayo Hyde Park. Hoteli hiyo iko mkabala wa uwanja wa Hyde Park na iko mwendo wa dakika chache kutoka Hertford Street ulipokuwako siku hizo ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza.

Sikumbuki iwapo Nyerere alikuwa akipita njia London kuelekea kwingine au iwapo alikuja kwa ziara mahsusi nchini Uingereza.

Wakati huo Nyerere alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar ulikuwa na umri mdogo wa miaka minne. Ukumbi wa mkutano wa Nyerere na Watanzania ulijaa lakini Wazanzibari tuliokuwako tulikuwa wanne tu.

Mahusiano baina ya ubalozi na Wazanzibari hayakuwa mazuri, kwa hakika yalikuwa duni kama yalivyo sasa. Wazanzibari waliokuwa wakiuzuru ubalozi, na walikuwa wachache, wakitiliwa shaka na maofisa wa ubalozi.

Kwa upande wao, Wazanzibari wenyewe wakijihisi kama ni Watanzania wa daraja ya chini. Hata leo, miaka zaidi ya nusu karne baada ya kuundwa Muungano, hali kwa jumla imeselelea kuwa vivyohivyo. Mengi yanapita kwenye ubalozi huo na Wazanzibari waishio Uingereza hawahusishwi.

Sisi Wazanzibari wanne tuliohudhuria mkutano wa Nyerere tulialikwa kwa sababu tulikuwa na Mzee Tawakali Khamis, Mzanzibari aliyekuwa waziri mdogo wa mambo ya nje wa Tanzania na aliyekuwa katika msafara wa Mwalimu kutoka Dar es Salaam. Siku hizo ofisi ya waziri mdogo wa mambo ya nje ilikuwa Zanzibar.

Mwaka wa 1968 Tanzania ilikuwa maarufu kwa Azimio la Arusha na siasa yake ya Ujamaa. Kadhalika, Tanzania, kama zilivyokuwa nchi nyingi za Kiafrika, lilikuwa taifa lililoruhusu chama kimoja tu cha siasa. Kwa hakika, kulikuwa vyama viwili, Tanganyika African National Union (TANU), cha Tanganyika, na Afro-Shirazi Party (ASP), cha Zanzibar.

Ingawa vikisema vilikuwa vyama vya kidugu, ukweli wa mambo ni kwamba vilikuwa vyama viwili tofauti kwa nchi mbili tofauti, kila nchi ikiwa na chama chake na sera zake. Na kila chama kikiitawala nchi yake kilivyotaka. Kila nchi ilikuwa na yake.

Siku hizo Zanzibar, ikiwa chini ya Rais Abeid Amani Karume, haikujihisi hata dakika moja kwamba ikikaliwa kichwani na Tanganyika. Mambo yalianza kubadilika mwaka 1977 wakati Nyerere alipoviunganisha vyama vya TANU na ASP na kuanzisha Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hatua hiyo ilikuwa sehemu ya mkakati wake wa kuidhibiti Zanzibar.

Mwaka 1968 jungu la siasa za dunia likitokota na kufuka. Ulimwengu uligawika pande mbili: upande wa waliokuwa wakifuata sera za nchi za Magharibi na ule wa waliokuwa wakijiita wanamaendeleo, ambao kwa jumla wakifuata sera za mrengo wa kushoto. Hawa wa upande wa pili wakipinga ukoloni na ukoloni mamboleo.

Marekani ilikuwa inabwagwa vitani huko Vietnam na Tanzania ikionekana kama taifa linalojenga jamii mpya yenye usawa barani Afrika. Ilikuwa Tanzania ya matumaini. Sio hii ya leo.

Baadhi yetu tukimuangalia Nyerere kwa jicho jengine. Tukimuona kwamba alikuwa anabadilika na badala ya kuwa “mwana mwema” wa nchi za Magharibi alijitumbukiza kwenye handaki moja na wakombozi dhidi ya nchi za Magharibi. Bado ukoloni wa Magharibi ukishamiri katika nchi kadhaa za Kiafrika.

Serikali ya walowezi wachache wa kizungu waliikaba Rhodesia, (Zimbabwe ya leo), na makaburu nao wakiongoza serikali ya wachache Afrika Kusini. Angola, Comoro, Guinea-Bissau na Cape Verde, Msumbiji, Namibia, zote zikitawaliwa na wakoloni.

Dar es Salaam ulikuwa mji wa ukombozi kwa vile ulikuwa na makao makuu ya Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika. Na Nyerere akionekana kuwa ni “Baba wa Ukombozi”. Wakombozi wengine nje ya Afrika akina Malcolm X wa Marekani, Michael Manley wa Jamaica na Che Guevara kutoka Cuba walikanyaga jiji la Dar kumzuru.

Wasomi wa kimaendeleo kutoka nje miongoni mwao akiwa Walter Rodney walipiga maskani jijini humo wakisomesha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Ilikuwa kana kwamba makao makuu ya ukombozi wa Afrika yaligura kutoka Algiers na kuhamia Dar.

Nyerere alizungumzia mengi kuhusu ukombozi alipokuwa akituhutubia pale Hyde Park Hotel. Yote yaliingia akilini. Siku hiyo, kama ilivyokuwa kawaida yake ulimi wake ulikuwa mtamu na alitufanya tusichoke kumsikiliza hasa pale alipotufanya tuhisi kama hakuwa akibania kitu.

Nayakumbuka maswali yangu mawili niliyomuuliza. La kwanza lilihusika na Jeshi la Tanzania jinsi lilivyokuwa likifunzwa na Wachina na wakati huohuo Kikosi cha Anga (Air Wings) kikifunzwa na Wacanada walichokianzisha kikosi hicho. Takriban marubani wote wa jeshi wakifunzwa Canada.

Swali langu la pili lilihusika na tangazo la Sheikh Karume kwamba Wazanzibari wote wenye asili ya visiwa vya Comoro si raia wa Tanzania na kwamba lazima wakate tajnisi kuomba uraia.

Nyerere hakuliunga mkono tangazo hilo la Karume na ilikuwa wazi kutokana na jibu lake kwamba alikwishaanza kukerwa na yaliyokuwa yakijiri Zanzibar.

Zilikuwa kero za kujitakia. Kwa hakika, balaa lote hii lililoikumba Zanzibar tokea 1964 ni lake. Lilianza tangu alipokwenda Zanzibar kwa mara ya mwanzo katika miaka ya 1950 kutia shinikizo ziungane jumuiya za Washirazi na Waafrika kwa madhumuni ya kuunda chama kimoja cha kisiasa. Nyerere alifanikiwa katika jitihada zake na kuungana kwa jumuiya ya Washirazi (Shirazi Association) na ya Waafrika (African Association) ndiko kulikokizalisha chama cha ASP kilichoongoza mapinduzi ya Zanzibar ya 1964.

Ukunga wa Nyerere katika mazazi ya ASP mnamo 1957 ulizidisha ushawishi wake juu ya chama hicho. Historia inatuonyesha kwamba tangu kiundwe chama cha ASP kilikuwa kikitegemea sana ushauri wa wanasiasa wa Tanganyika, hususan wa viongozi wa TANU chini ya Nyerere.

Chama cha ASP kilihisi kwamba kililazimika kuwategemea wanasiasa wa Tanganyika kwa ushauri kwa sababu, hasa mwanzoni mwa uhai wake, kilikuwa hakina wasomi wa Kizanzibari wa kukishauri. ASP iliwapata wasomi hao baada ya Wazanzibari kama Othman Sharif Musa, Aboud Jumbe, Hasnu Makame na Idris Abdulwakil kuacha kazi zao katika serikali ya kikoloni na kujiunga na chama hicho.

Baada ya mapinduzi ya 1964 ushawishi wa Nyerere juu ya Karume uliongezeka. Kwa siri kubwa Nyerere alimtega Karume akubali nchi yake iungane na Tanganyika. Nyerere alitumiliwa na madola ya Magharibi, hususan Marekani na Uingereza, afanye juu chini kuziunganisha nchi hizo kwa kisingizio cha kuyazuia mapinduzi ya Zanzibar yasiusambaze “ukomunisti” kwingineko Afrika.

Nyerere naye kwa kutumia hoja hizo hizo alizitumilia nchi za Magharibi katika jitihada zake za kuibana Zanzibar. Sura inayojitokeza ni ya pande hizo mbili, nchi za Magharibi kwa upande mmoja na Nyerere kwa upande wa pili, zikitumiliana ili Nyerere aweze kuidhibiti Zanzibar katika Muungano.

Kwa namna mambo yanavyoibuka inaonyesha kwamba tangu mwanzo Nyerere hakuwa na nia njema kuhusu Muungano. Ni wazi kwamba alikuwa na lake. Alikuwa na ajenda yake mwenyewe, aliyoijua yeye mwenyewe na aliyoisimamia mwenyewe.

Mfano mmoja wa udhibiti wa Nyerere juu ya Zanzibar ni ile kadhia ya uanachama wa Zanzibar katika Jumuiya ya Kiislamu (OIC). Zanzibar ilishinikizwa ijitoe kutoka Jumuiya hiyo kwa vile Nyerere alikuwa hataki iwe mwanachama. Alikuwa na sababu zake zisizoeleweka, ingawa akishikilia kwamba Zanzibar kujiunga na jumuiya hiyo ilikuwa inafanya mambo kinyume na katiba ya nchi.

Baada ya kumlazimisha kwa nguvu Rais wa siku hizo wa Zanzibar, Dkt. Salmin Amour, abadili uamuzi wa serikali yake na Zanzibar ijiondoe kutoka jumuiya hiyo ya Kiislamu, Nyerere alitoa ahadi ambayo hadi leo haijatimizwa kwamba Tanzania nzima itajiunga na OIC.

Dhamira za Nyerere zinazidi kufichuka kila miaka ikisonga mbele. Wa karibuni kuzifichua ni mbunge wa zamani wa Chunya, Njelu Kasaka, aliyeongoza kundi la wabunge wa CCM waliotaka pawepo na muundo wa muungano wa serikali tatu.

Kundi hilo, maarufu kwa jina la G55, liliibuka wakati wa utawala wa awamu ya pili chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi. Kasaka ndiye aliyewasilisha hoja yao bungeni ya kutaka pawepo serikali ya tatu, ya Tanganyika, katika muundo wa muungano.

Kasaka anastahiki kupongezwa kwa kuandika kitabu kiitwacho “Maisha, Siasa na Hoja ya Tanganyika”, ambacho, miongoni mwa mengine, kinaelezea mchakato mzima wa kundi la G55 wa kudai papatikane serikali ya Tanganyika na jinsi Mwalimu Nyerere alivyouzima mchakato huo. Kwa simulizi hiyo, Kasaka ameibua mengi yenye kudhihirisha jinsi Nyerere alivyowapiga chenga wahubiri wa serikali tatu na kuhakikisha kwamba taifa la Tanzania litaendelea kuwa na serikali mbili na wakati huohuo kuiweka wazi njia ya kuelekea serikali moja.

Mantiki ya haja ya serikali tatu ikimkodolea macho Nyerere lakini aligeuza uso hakutaka imsute kwani lengo lake lilikuwa kuwako kwa serikali moja ya Tanzania. Mwenyewe hakuwahi kulitamka wazi hadharani lengo hilo. Akiwa mwanasiasa mahiri akitambua hatari na athari za kufanya hivyo.

Kwa nguvu alizokuwa nazo alipokuwa Rais na alipokuwa mwenyekiti wa CCM na hata baada ya kutokuwa na madaraka yoyote, serikalini au katika chama kinachotawala, ingekuwa jambo jepesi kwake kuiambia serikali ikae na irekebishe mapungufu yaliyokuwa yakijitokeza mara kwa mara katika Muungano.

Hakufanya hivyo. Badala yake alihakikisha kwamba polepole Tanganyika, ikijivisha juba la serikali ya Muungano, inayanyemelea na kuzidi kuyapora mamlaka ya Zanzibar. Siku zote nia yake ilikuwa pawepo serikali moja ili Tanganyika iimeze Zanzibar moja kwa moja na pasiwepo na isimu ya nchi iiitwayo Zanzibar.
Hakuwa na insafu (nia njema) kwa Zanzibar kwenye Muungano huu tangu siku ya kwanza.
Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter; @ahmedrajab
Mwandishi wa makala haya ni Mwandishi wa Habari mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 50; akiandikia na kuhariri majarida tofauti ya kimataifa. Ahmed pia ni mshairi na mwandishi wa insha. Kwa sasa anaishi jijini London, Uingereza.


Screenshot_20230424-164323_Chrome.jpg
 
ifike wakati CCM uturudishie nchi yetu Tanganyika inawezekana nia ilikuwa nzuri kuwa na Tanzania lakini ndani ya safari imezaliwa Danganyika!
 
Zanzibar ina watu milioni 2 iwe tu mkoa wa Tanzania kama Mwanza au Mtwara! MWALIMU ALIKOSEA kuipa Zanzibar mamlaka kidogo tangu mwanzo ndo maana hizi hoja zinajitokeza hadi leo!
 
Zanzibar ina watu milioni 2 iwe tu mkoa wa Tanzania kama Mwanza au Mtwara! MWALIMU ALIKOSEA kuipa Zanzibar mamlaka kidogo tangu mwanzo ndo maana hizi hoja zinajitokeza hadi leo!
Lakini Nyerere aliikuta Zanzibar ni nchi huru iliyojipatia uhuru wake na ilikuwa na Rais na utawala uliokamilika,usipoelewa haya ni kujivesha unyerere juu ya muungano.
 
Pamoja na uandishi mtamu ila TANZANIA yetu inabaki nchi ya mfano barani Afrika....UTULIVU NA AMANI YAKE yote ni jitihada za baba wa taifa hayati JKN na wazalendo wenzake wa TANU na ASP......

Ukitaka kinyume cha mazuri haya hebu yaangalie ya akina HERMETI na Sudan yao........

#SiempreJMT
#SiempreAmaniYaTanzania
#SiempreUtulivuWaTanzania

#SiempreSerikaliMbiliZaTanzania

Sent from my TECNO F1 using JamiiForums mobile app
 
Nyerere angekuwa hai ilibidi atuambie Tanganyika ilienda wapi baada ya muungano.
Ardhi ya iliyokuwa Tanganyika ipo.....ila haina serikali.....

Yote ni bora kwani kwa mujibu wa maneno ya hayati baba wa taifa JKN kuwa "naogopea kuimeza Zanzibar kutokana na udogo wake...."

Wanaoulizia iwapi Tanganyika ....waulizie pia iwapi "N/S RHODESIA".....

Muungano wetu ni wa kipekee kabisa....si lazima tufanane na miungano ya nchi nyingine ilihali TUKO HURU....TUNA AMANI...NA UTULIVU.....

Tuwaangalie SUDAN...
Tuwaangalie ETHIOPIA....


#SiempreSerikaliMbiliZaTanzania



Sent from my TECNO F1 using JamiiForums mobile app
 
Zanzibar ina watu milioni 2 iwe tu mkoa wa Tanzania kama Mwanza au Mtwara! MWALIMU ALIKOSEA kuipa Zanzibar mamlaka kidogo tangu mwanzo ndo maana hizi hoja zinajitokeza hadi leo!
Maneno ya hayati baba wa taifa JKN....

"Zanzibar ilipata uhuru wake 1963...na kuwa taifa kamili....hatuwezi tukalifuta hilo eti kwa kigezo cha udogo wake na huu Muungano tulionao..."

#SiempreMuunganoWetu

Sent from my TECNO F1 using JamiiForums mobile app
 
ifike wakati CCM uturudishie nchi yetu Tanganyika inawezekana nia ilikuwa nzuri kuwa na Tanzania lakini ndani ya safari imezaliwa Danganyika!
Mkuu tema mate chini....

Tanganyika ikirudi....wako watakaotaka mikoa yao ijitenge na kuanzisha nchi nyingine.....

Hayati baba wa taifa aliliona hilo siku nyingi.....kwani aliijua dhambi ya UBAGUZI NA AKAZIJUA HADAA ZA BAADHI YA WANASIASA MUFLISI wenye mrengo wa UKANDA ,UDINI NA UKABILA.....

#TanzaniaSiEthiopia
#TanzaniaSiSudan

#TanganyikaIkoKaburini
#TanganyikaIsifufukeMpakaKiama

Sent from my TECNO F1 using JamiiForums mobile app
 
Kwani Muungano wetu ni mbaya?!!

Hauna faida kwetu na vizazi ?!!!

Sent from my TECNO F1 using JamiiForums mobile app
Hoja kuu siku zote sio faida na/au hasara za Muungano. Hoja ni kuwa muungano wetu ulijengwa kwenye misingi ya hila na ujanja ujanja tu. Haihiitaji akili kubwa kubaini madhaifu ya muungano. Inahitaji busara na utashi tu kuurekebisha na kuufanya uwe imara na wa manufaa zaidi kwa pande zote 2.

Hivyo ni budi ifike mahali tuujadili kwa upana na uwazi, kisha tuweke misingi ya ukweli na ya kudumu badala ya hicho alichokileta Nyerere.
 
"Hila "zake hazikuwa kwa ubaya...

Sent from my TECNO F1 using JamiiForums mobile app
Hakuna hila Nzuri wala Njema. NEVER!

Muungano lazima ujadiliwe upya, ujengwe upya kwa misingi ya ukweli na haki kwa maslahi ya wananchi wote sio wanasiasa au viongozi wachache. Nyakati, mazingira na mahitaji vyote vimebadilika, so ni budi uwekwe meaning.
Mwananchi wa kawaida hafaidiki na huu wa sasa. Na pia kama hakuna hila, hofu, kigugumizi na nguvu ya kuzima mjadala vya nini??

Uliopo ni muungano wa Nyerere na Karume, au at best wa TANU na ASP. Sasa tunataka muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kwa maslahi halisi ya Watanganyika na Wazanzibar. Na tukitaka hata jina pia tunaweza tafuta jingine (ni kawaida nchi kubadili majina ya nchi, miji mikuu, bendera nk) na tupate muundo mwingine tofauti na huu.

NB: Muungano sharti uwe wa hiari na haki.
However, history reminds us that Communist didn't have nor understand the word "voluntary will"; they only have the word Force. Hakuna muungano wala mkataba wa kulazimisha/shwa.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom