Mti mbichikuni ukageuka - na Aron Seni

Imma_Magira

Member
Jan 8, 2022
18
26
MTI MBICHI UKAGEUKA KUNI
Na- Aron Seni

ilikuwa asubuhi tulivu na njema ya mwaka 1977. Baba wa taifa hayati JK Nyerere alipomuita nyumbani kwake msasani-Dar es salaam aliyekuwa Mwanasheria mkuu wa serikali kwa wakati Huo Ndg Joseph Sinde Warioba.

Mwalimu akamwambia Sinde "Nataka unipe majina matatu ya watu wanaofaa kuteuliwa kuwa Jaji mkuu(CJ)."

Sinde akampa mwalimu majina hayo huku akiwa hajui nini kitafuatia Kisha akaondoka zake. Ikafika ijumaa ya wiki hiyo, mwalimu akampigia Simu Sinde na kumpa amri akisema "Nataka Jumatatu Nikutane na Nyalali hakikisha Jumatatu awe amefika dar."

Nyalali muda Huo alikuwa ni Jaji wa mahakama kuu Kanda ya Arusha na alikuwa na uzoefu wa Miaka mitatu tu katika kazi ya Jaji.

Sinde akahaha, kipindi hicho hakuna ndege ya kumuwahisha Nyalali kwani, shirika la ndege la afrika mashariki lilikufa baada ya kuvunjika kwa umoja wa afrika mashariki. Gari lipo Lakini haliwezi kumfikisha Nyalali mapema kwani miundombinu ya barabara haikuwa Rafiki wakati ule.

Genius Sinde akatumia akili zake za tabora boys bwana, Akaingia jeshini akaamuru ndege ya kijeshi imfuate Nyalali chapchap. Ndege ikamleta Nyalali hadi airport. Sinde akamchukua Nyalali hadi nyumbani kwa mwalimu.

Walipofika mwalimu akamuita nyalali faragha, Sinde akaachwa sebuleni akiangalia, Paa na feni zinazopepea.

Baada ya muda mfupi nyalali akatoka faragha akiwa na bashasha kubwa.

Baada ya siku chache Nyalali akaapishwa kuwa Jaji mkuu wa Tanzania. na hapo ndipo mti mbichi ukageuka kuni iliyoivisha chakula pasi kutegemea.

Wapo majaji waliostahili kushika hiyo nafasi kwani walimzidi uzoefu nyalali, Lakini nyalali mbali na uchanga wake aliwapiku kutokana na sifa za Ziada.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Jaji mkuu. Nyalali alipokea Barua kutoka Shirika la kazi duniani - ILO kwenda kufanya kazi hukooo ulaya. Mshahara ulikuwa mkubwa kuliko wa Jaji mkuu, maisha ya juu na ya kifahari kuliko ya Tanzania. Yote hayo aliyapiga chini ili alitumikie taifa lake.

Huyu ndiye Jaji Francis Lucas Nyalali. Alizaliwa mwaka 1935 katika Familia duni ya wafugaji huko mkoani Mwanza. Akasoma hadi makerere. Akawa mwanasheria aliyezipalilia Ndoto zake kwa jembe la mkono.

Leo huwezi kuitaja katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 bila kumtaja Nyalali.

Leo huwezi kuzungumza uhuru wa mahakama bila kumtaja Nyalali.

Leo huwezi kuzungumzia Tume huru ya uchaguzi bila kumtaja Nyalali.

Leo huwezi kuzungumzia mfumo wa usuluhishi nje ya mahakam(Adr) bila kumtaja Nyalali.

Leo huwezi kuzungumzia mfumo wa vyama vingi nchini bila kumtaja Nyalali.

Leo huwezi kuzungumzia mahakama ya rufani ya Tanzania bila kumtaja Nyalali.

Jaji nyalali alifariki mwaka 2003 kwa maradhi.

Mambo ni mengi kuhusu Nyalali. Leo tuishie hapa. Lakini ondoka na hii;
"katika historia ya nchi hii, Kuna viongozi wawili tu walioongoza mihimili ya dola kwa miaka 23 mfululizo, ambao ni Baba wa taifa aliyeongoza serikali kwa miaka 23. Na Jaji Francis Lucas Nyalali aliyeongoza muhimili wa Mahakama kwa Miaka 23."

Aron seni.
LL.B - Mzumbe
 

Attachments

  • IMG-20230722-WA0191.jpg
    IMG-20230722-WA0191.jpg
    34.2 KB · Views: 16
Nimefurahi tu kwamba alishafariki, maana ungekuta na uzee wake bado anashikilia nyadhifa wakati miti mibichi ipo tena mingi kuliko kipindi chake.
 
Back
Top Bottom