Msamaha ni Hiyari; Sio lazima

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,340
51,900
MSAMAHA NI HIYARI, SIO LAZIMA.

Kwa Mkono wa, Robert Heriel.

Lengo la Makala: Msomaji atakapomaliza kusoma jumbe hii, awe amejifunza na kuelewa kuwa Msamaha ni jambo la hiyari ambalo aliyekosewa anaweza kuutoa au asiutoe. Mkosaji ajue kuwa msamaha sio haki yake, bali ni neema anayopewa na aliyemkosea. Ni dhamira yangu kuwaambia wasomaji wangu kuwa wasifanye makosa kwa kadiri ya uwezo wao kwa maana watakapofanya makosa suala la msamaha sio haki yao.

Tumekuwa tukifundishwa kwenye majumba ya ibada kuwa Mungu anatutaka tusamehe, zipo aya kadhaa ndani ya misahafu inayotutaka tusamehe; Aya nyingine zimekaa kimlinganyo wa kimahesabu kuwa tusamehe saba mara sabini (7x70) kumaanisha tusamehe mara nyingi hata bila ya kuhesabu. Aya hizi zimekuwa zikitumiwa vibaya ndani ya jamii zetu na hii imesababisha athari mbaya katika familia, jamii na taifa kwa ujumla.

Kwa ngazi ya familia, utashangaa mke au mume anafanya kosa akiwa na akili timamu, akijua kuwa ni kosa, anafanya kwa makusudi kabisa, tena kabla hajafanya anaenda kuomba ushauri kabisa, na watu labda ni rafiki zake wanamuambia asifanye lakini kwaa kiburi anakaidi makusudi anaenda kufanya.

Mwishowe yanapotokea madhara analeta pua na kaptura yake akijilizza kuwa anaomba msamaha. Tena linatumia vifungu kabisa vya Msahafu kama kinga yake kuomba msamaha, na watu wake wapumbavu wanaokuja kuomba naye msamaha wanakushinikiza kwa nguvu umsamehe kwani Binadamu hajakamilika, upuuzi, uongo na ushetani mkubwa. Binadamu amekamilika 100%. Kusema binadamu hajakamilika ni kukufuru Muumbaji kuwa ameumba vitu nusu ambavyo havijakamilika jambo ambalo sio kweli.

Mimi ni binadamu, ninaongea kibinadamu, kila ninachokifanya kikiwa ni kosa nafahamu kabisa hili ni kosa namkosea huyu mtu. Nafahamu kabisa wengi tupo hivyo. Hata wanyama wanajua kabisa wakifanya makosa au kabla hawajafanya kosa wanajua wanaenda kufanya kosa, angalia panya, angalia nyani au Paka akienda kuiba kitu, anajua kabisa hili ni kosa. Hivyo wanafanya makusudi.

Ndani ya jamii yetu zama hizi, Mkosaji anaona Msamaha ni haki yake jambo ambalo sio kweli. Msamaha ni kinyume cha haki, mtu akikosea anastahili kuadhibiwa au kupata matokeo ya makosa yake hiyo ndio kanuni. Neno msamaha linavunja kanuni ya haki, ambayo inasema apandacho mtu ndicho atakachovuna.

Watu siku hizi wamekuwa na desturi ya kufanya makosa kwa makusudi kabisa huku wakijua baadaye watasamehewa. Matokeo yake makosa ya makusudi ndani ya familia na jamii zetu yameongezeka maradufu.

Msamaha umegeuka mzigo wa misumari kwa wakosewa, mtu analazimishwa asamehe hata kama hataki kusamehe, na ninaposema hataki namaanisha moyo wake hautaki hivyo anakuwa na kinyongo sema kwa vile labda hana uwezo basi anajikalia kimya tuu.

Kwa uchunguzi mdogo nilioufanya, watu wanyonge na wadhaifu wa kifedha, kimamlaka, kinguvu na kijinsia mara nyingi ndio hulazimishwa kutoa misamaha pindi wanapokosewa. Watu masikini na wanyonge ndio hutoa misamaha ya kinafiki kwa kulazimishwa.

Na kwa vile hawana jinsi na hawana cha kuwafanya waliowakosea basi hujikuta wanasamehe kinafiki huku moyoni kinyongo kikibakia. Na hii ni sababu kubwa ya masikini na fukara kuwa wanafiki na wasengenyaji kuliko watu wenye fedha na matajiri.

Huwa nina falsafa isemayo; Masikini akikusamehe usimuamini kuwa yameisha, ila tajiri akikusamehe muamini. Kwa sababu masikini anaweza kukusamehe kwa sababu hana jinsi, hana cha kukufanya lakini tajiri au mwenye mamlaka akikusamehe jua amekusamehe kweli kwa sababu uwezo wa kukulipa kisasi anao na wewe unajua hilo wazi kabisa.

Unakuta mume ndani ya ndoa anachepuka makusudi kabisa kwa kujificha na kwa kila aina ya ujanja, rafiki zake wanamshauri aangalie ndoa yake lakini yeye anashupaza shingo. Siku akifumaniwa anaanza kuomba msamaha ati amepitiwa na shetani sijui nini.

Nakuhakikishia hakuna anayechepuka kwa bahati mbaya, wote hufanya makusudi. Hakuna cha kulogwa wala nini, maana wengine hasa wapumbavu na wapuuzi husema wamelogwa. Ukiwa na mume au mke anayejitetea hivi fukuza haraka ndani ya nyumba.

Kama nilivyosema watu dhaifu au tabaka la chini ndio hutoa misamaha ya kinafiki kwa kulazimishwa kwa kuwa hawana jinsi. Wanawake wakifumaniwa na waume zao mara nyingi hufukuzwa na kupewa talaka bila ya msamaha, hii ni kwa sababu wanawake kwa upande wa jinsi ni tabaka la chini ambalo hutawaliwa na wanaume walio tabaka la juu.

Lakini mwanaume afumaniwe utashangaa wengi hawaachwi na wake zao, kwani wake zao hujifanya wamesamehe lakini kiukweli wengi wao hawajasamehe kikweli bali wanakinyongo ambacho mara nyingi hulipa kisasi kwa wao nao kuchepuka. Sababu kubwa ya wanawake kusamehe kinafiki ni kuwa wengi ni tegemezi, wanyonge au wametoka familia duni. Hivyo hawana jinsi zaidi ya kusema wamesamehe ili maisha yaende tuu. Hii inaitwa unafiki.

Wapo wazazi hasa kina Baba ambao kwa makusudi kabisa huzikataa mimba na kutelekeza watoto, alafu mtoto akikua akifanikiwa libaba jinga linakuja na kaptura yake kuomba msamaha, likijiliza kwa unafiki. Mara nyingi watu wa hivi huwa na wafuasi wao nyuma ambao wanashinikiza msamaha, wengine wanaandamana kabisa barabarani kuwa wanataka msamaha kana kwamba ni haki yao.

Hutumia vifungu, sijui Samehe ili Mungu akusamehe,sijui kisasi ni cha Mungu. Sijui mzazi ni mzazi. Hakuna kitu kama hicho. Hakuna mwenye haki ya msamaha pale anapokosea. Msamaha ni hiyari ya mkosewaji kuutoa au asiutoe akiutoa hiyo ni neema tuu umepewa wala sio haki yako.

Msamaha mara nyingi hutolewa ikiwa mtu alifanya kosa kwa kutokujua au alifanya kosa katika mazingira fulani yasiyo na option. Hata Mahakamani msamaha hutolewa kwa kuangalia mazingira ya kosa, kama umefanya kosa kwa kukusudia kamwe huwezi kusamehewa tena unaweza kuongezewa adhabu, kama ulipaswa kufungwa miaka mitano basi wataongeza walau iwe kumi na tano ili iwe fundisho. Lakini yapo makosa ya kutokujua au katika mazingira maalumu, makosa haya ndio unaweza kusamehewa au pia usisamehewe kwa maana kosa haki yake ni adhabu. Ukisamehewa au kupunguziwa adhabu hiyo ni neema wala sio haki yako.

Hata katika maandiko, Yesu aliposema wasamehe alitoa sababu ya kusema hivyo ni kuwa "kwa sababu hawajui walitendalo" kumaanisha mtu ambaye hajui alitendalo ndiye anayeweza pewa neema ya msamaha japo pia sio haki yake kusamehewa hivyo hawezi kudai msamaha kwa lazima kama haki yake kama alikosea kwa kutokujua.

Adamu na Hawa walipoasi pale Bustanini kwa mujibu wa maandiko, walipewa adhabu na wala hawakupewa msamaha wowote ule. Mungu hajawahi kumsamehe Adamu na Hawa. Mungu hajawahi na hatawahi kumsamehe mtu au kiumbe kinachofanya kosa kwa makusudi. Hata kanisani au Misikitini lazima watu wafundishwe kuwa Mungu hajawahi kumsamehe mtu anayefanya kosa kwa makusudi. Huyo mungu atakuwa mpumbavu na asiyejielewa.

Ndio maana mpaka leo tunakufa na tutaendelea kufa kwa sababu Mungu hakumsamehe Adamu na Mama yetu Hawa hii ni kwa mujibu wa maandiko.

Kuna watu watakuja hapa na kuleta vifungu vyao kuwa Mungu alimsamehe adamu, sijui na ndio maana alimvalisha ngozi ya kondoo, sijui Mungu ni mwingi wa huruma uongo mtupu. Mungu hana huruma na wapumbavu, yaani ufanye kosa makusudi alafu awe na huruma na upumbavu wako, unajidanganya. Mungu ni mwenye haki na haki ndio upendo, haki ndio uaminifu. Haki haiendani na huruma. Kumbuka ukikosea nawe unahaki zako kama mkosaji hivyo utatumikia adhabu yako huku ukipewa baadhi ya haki zako.
Na ndio maana hata waliohukumiwa jela bado wanahaki zao wanahudumiwa licha ya kuwa ni wakosaji lakini haiwaondolei adhabu yao.

Mtu akikosea muadhibu kulingana na sheria, kama utamsamehe msamehe kwa moyo wote na dhati yote, sio unasema umemsamehe kumbe kwa shinikizo kutoka kwa watu kuwa usamehe saba mara sabini. Mwishowe unajikuta ukiwa mnafiki, ukiwa na kinyongo na roho ya kisasi.

Mimi mtu anayefanya makosa kwa makusudi lazima awajibike, sinaga misamaha ya kinafiki. Na wala sipendi kusamehewa kinafiki. Nikikukosea kwa makusudi basi nakuruhusu ufanye utakavyo fanya ili unipe haki yangu, sio unaniletea unafiki wako wa kipumbavu.

Pia kuna watu wanakusamehe kinafiki kimkakati ili siku akikukosea na wewe umsamehe. Hivyo anakusamehe leo kumbe anakinyongo chake alafu kesho anakufanyia kosa na wewe la makusudi kisha anakuambia nisamehe, mbona mimi nilikusamehe. Kwangu hiyo haipo.
Nikikukosea makusudi wewe nisamehe kwa moyo wote ukishindwa acha kunisamehe kinafiki maana siku ukikosea sitakulipa kwa kuangalia msamaha wako bali nitaangalia moyo wangu.

Hii huitumia wanandoa wengi, anakusamehe akikufumania, ili nawe ukimfumania umsamehe. Kwa namna hii uovu hauwezi kuisha. Ukimfumania mtu mzingue kisheria kama sheria inazingua mpasue.

Binadamu ni wakamilifu kabisa, wangekuwa sio wakamilifu basi pasingekuwa na haja ya hukumu wala pasingekuwa na dhambi. Dhambi ni uasi, yaani makosa ya kukusudia. Na ili ukusudie lazima uwe na akili toshelevu. Kama huna akili huwezi kukusudia jambo kwani utatenda bila dhamiri.

Wito: Watu waache kuwatishwa mizigo ya misumari wenzao waliowakosea, ukitenda kosa basi subiri matokeo. Ukisamehe shukuru Mungu kwani hiyo ni Neema. Usiposamehewa pia shukuru Mungu kwani ni haki yako kutokusamehewa. Ulitenda kosa kwa hiyari yako basi atakayekusamehe atakusamehe kwa hiyari yake sio umlazimishe na vifungo uchwara vya maandiko.

Maandiko yanasema samehe saba mara sabini. Lakini mimi nawaambia, kama moyo wako hautaki kusamehe usijilazimishe, huo ni unafiki. Mpe adhabu saba mara sabini.

Nimemaliza, leo sitaki maswali. Watu tuache kufanya makosa kwa kisingizio sisi sio wakamilifu. Mimi ukinambia hivyo nitakutwanga makofi mbele ya kikao. Pumbavuu!

Ulikuwa nami;

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
Kwa sasa Dar es salaam
 
Unamakala nzuli na unajitahidi sn kuelimisha jamii hongera kwa Hilo. Tatizo lako unajifanya Sana mjuaji kiasi kwamba wewe umekamilika na mawazo yako tu ndo bola kukiko wengine na unavoonekana unazalau Sana watu maana kwa mawazo yako wewe ni pafect . Kwa kifupi jifunze uandishi wenye hekima na maalifa . Punguza ujuaji hutafika mbali,
Wakati mwingine umekua ukitumiwa lugha ya kuumiza wenzako na kuwazalilisha hii inaonyesha huna hekima.Jifunze kuwa mstalabu, naamin pia hata majilani zako huishi nao kwa amani maana sio kwa ujuaji huo.
Punguza kupenda sifa , shauku watu vizuri na uwape masuluhisho yaliyo ya hekima Hakika utabalikiwa Sana.
Ni ushauli tu Sina Nia mbaya . Ukifata huo ushauli utafika mbali Sana.
 
Pia punguza matusi hii inaonyesha wewe ni mhuni tu.Mwandishi gani wa makala huwa anatumia lugha ya matusi hivo.Naina una msongo was mawazo au pia umetokea katika familia ambayo haujastalabika . Ukimshauli mtu kwa matusi hatakuelewa .
 
Pia punguza matusi hii inaonyesha wewe ni mhuni tu.Mwandishi gani wa makala huwa anatumia lugha ya matusi hivo.Naina una msongo was mawazo au pia umetokea katika familia ambayo haujastalabika . Ukimshauli mtu kwa matusi hatakuelewa .
Msamehe...
 
Back
Top Bottom