SoC04 Mkombozi wa tatizo la ajira kwa vijana ni vijana

Tanzania Tuitakayo competition threads

ejoh

New Member
Oct 14, 2018
4
0
[GASTON JORDAN LIVIGHA]
[gaejombishi@gmail.com]

UTANGULIZI
Naandika sio kwa dhumuni la kushinda pesa la hasha! lakini naandika nikiwa kama mmoja wa vijana walioathirika na janga la ukosefu wa ajira. Nikiwa kama muhitimu wa chuo cha Dodoma shahada ya mipango na usimamizi wa miradi na maendeleo ya jamii huu ni mwaka wangu wa tatu nikiwa mtaani tangu nilipohitimu mwaka 2021. Natumaini andiko hili litawafikia walengwa nasisi kama vijana tunategemea kufaidika kupitia mawazo yaliyopo katika andiko hili.

MZIZI WA TATIZO
Tunachopitia sasahivi vijana wa kitanzania kimenifanya nikumbuke somo la utawala wa umma (public administration) ambalo lilinipa mwanga na msukumo wa kuandika andiko hili. Ukipitia andiko lililochapishwa mtandaoni na taasisi ya peace child international kuhusu sababu za ukosefu wa ajira kwa vijana unakuta kunasababu mbili ambazo mimi nimeamua kuziongelea zaidi kwasababu nimeona hazitiliwi mkazo na ndio sababu haswa ya haya tunayopitia(mizizi). Sababu hizo ni kutolingana kwa ujuzi( skills mismatch) na ukosefu wa ujuzi wa ujasiriamali na stadi za maisha (lack of entrepreneurship and lifeskills education).

  • KUTOLINGANA KWA UJUZI
Hapa ndio pale kijana kamaliza chuo kozi ya uhasibu halafu kutokana na ukosefu wa ajira anaambiwa nenda kalime na mkopo anapewa pia, lakini baada ya msimu mmoja shamba linakufa na pesa inateketea yote. Mtu ambaye hana ujuzi wa kulima bali ujuzi wa uhasibu analazimika kufanya kitu ambacho hakiendani na ujuzi wake eti kisa tu kuna mkopo. Hii upotevu wa pesa za umma bure kabisa yani ni sawa na kumpa mtoto pikipiki aendeshe wakati hawezi kwa kigezo pikipiki imesaza mafuta (full tank). Kuna maisha baada ya mkopo wa fedha katika kulima pesa ni kitu kimoja lakini kuna ujuzi ambao ndo msingi halisi.

  • UKOSEFU WA ELIMU YA UJASIRIAMALI NA STADI ZA MAISHA
Nafikiri kwenye hili sina mengi ya kuzungumzia kwasababu tumeona michakato mingi ikianza kufanyiwa kazi ikiwa pamoja na kubadilisha mitaala ya elimu ili kuipa nafasi ya kuruhusu elimu ya ujasiariamali na stadi za maisha pamoja na mafunzo mbali mbali ya ufundi na ujasiriamali yakitolewa. Lakini tunatakiwa kuelewa kua sio kila mtu anatakiwa kuwa mfanyabiashara au sio kila mtu anatakiwa kuwa mkulima tunatakiwa kuendeleza vile vitu ambavyo vijana wamesomea ili kukuza soko la ajira. Cha kuzungatia ni kuweka mkazo katika uhalisia katika masomo kuhakikisha yanaleta manufaa kwa vijana katika jamii.

NINI KIFANYIKE KUPUNGUZA TATIZO
Na hapa ndipo naomba umakini mkubwa kwa watu wa wizara husika na wadau wa maendeleo na watanzania kwa ujumla, tatizo la ajira kwa vijana haliwezi kumalizwa kwa kutoa tu mikopo na mafunzo kwa vijana . Tatizo la ajira litamalizwa au kupunguzwa kama serikali yetu itaamua kukaa chini na kufanya uhamasishaji wa rasilimali watu ( human resource mobilization). Ndio najua haujanielewa namaanisha nini , uhamasishaji wa rasilimali watu ni kitendo cha kuhajiri na kuleta pamoja rasilimali watu kwa ajili ya hatua ya pamoja iliyoundwa kuimarisha utendaji wa utawala ( chanzo: wikipedia) . Hapa namaanisha ili kutekeleza jambo unatakiwa ukusanye watu wenye ujuzi mbalimbali kwa pamoja ili kufanikisha jambo husika mfano; unahitaji kufanya uzalishaji wa asali kwa kiwango cha kimataifa kwahiyo utahitaji wataalamu wa ufugaji, wataalamu wa masoko, wataalamu wa usindikaji wa vyakula, wataalamu wa sheria n.k kwahiyo hii itapelekea jambo kufanyika kwa urahisi na pia kutoa fursa kwa watu wenye ujuzi mbali mbali kupata fursa ya ajira.
Ufuatao ni mchanganuo wa wazo langu kwa kufuata hatua:-

UTAMBUZI WA MRADI NA USAJILI
Hatua ya kwanza ni kuandaa wazo la mradi ambalo litatokana na malighafi za eneo husika mfano; mtwara kubangua korosho, shinyanga kusindika nyama. Halafu kutakua na usajili wa wazo kua kampuni, kampuni njiti (lighter companies) ambazo zitakua na usajili wake unaojitegemea na pia zitakua na upendeleo mfano ulipaji wa kodi mpaka pale zitakapo komaa ndipo zitapewa usajili kama wa makampuni mengine . Pia hizi kampuni zitapewa uangalizi maalumu toka wizara ya viwanda na biashara, na wizara ya ajira kwa vijana pamoja na washirika wake kama SIDO,Asasi za serikali, Asasi zisizo za serikali na taasisi za kifedha. Kupitia fungu la asilimia 10% ndilo litakalo dhaminj makampuni haya kwa ushirikiano wa mabenki ya biashara.

WAHUSIKA WA MRADI
Serikali itahusika na mchakato wa kupata Vijana wenye ujuzi wanaoishi kutoka kwenye eneo ambalo mradi husika utafanyika, ndio wahusika wakuu wa mradi utakao anzishwa. Mfano, kama ni kiwanda cha asali tabora basi vijana wa tabora wenye taaluma lakini sio waajiriwa ndio watakua wanufaika namba moja na mradi. Vikundi vya watu kuanzia 10 vitaundwa na wahusika hao watajumuisha vijana wenye ujuzi mbali mbali huku kila mmoja akiwa na kazi yake ndani ya mradi husika, waliosomea uhasibu watafanya kazi za uhasibu, waliosomea sheria watafanya kazi zote zinazohusu sheria nk. Kama kampuni njiti itaanzishwa kwa kila wilaya kulingana na mahitaji tunategemea kuajiri watu wasiopungua 1800 ambapo baada ya muda wa miaka mitatu mpaka mitano watakua na uwezo wa kuajiri wenzao baada ya viwanda kukomaa na kukua.

VIWANDA NJITI
Hivi ni viwanda ambavyo vitakua chini ya wizara ya viwanda na biashara, endapo vitapitishwa basi vitakua chini ya uangalizi maalumu wa serikali na taasisi za fedha kama benki na asasi zingine kama SIDO. Serikali inatakiwa kuhakikisha inasimamia upatikani wa watumishi wa viwanda hivi ambao watakua ni vijana wasio na ajira na ambao wana ujuzi wa kunufaisha mradi. Watakua wanapata mafunzo ya kuendesha mradi husika toka kwa viwanda vilivyoendelea. Tunategemea wahasibu, wanasheria, wataalamu wa masoko, wataalamu wa kilimo, n.k wote wapate ajira kupitia miradi hii. Baada ya miaka 3-5 tunategemea kuvifanyia usajili mkubwa ( full registration) na kuanza kuendeshwa kama viwanda vikubwa ikiwa pamoja na kulipa kodi kama viwanda vingine.


HITIMISHO
Ningependa serikali yangu pendwa ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ielewe kuwa tatizo kubwa kwa vijana sio tu mikopo, mikopo ni muhimu lakini tunahitaji utaalamu wa maeneo mbalimbali ya miradi kuanzia uzalishaji mpaka masoko. Vikundi vingi vinakopa pesa lakini havirejeshi na vinakufa kutokana na kukosa ujuzi wa kuendesha miradi husika hivyo kupelekea miradi kufa. Kupitia wazo hili pia tutapata picha halisi ya kiwango cha elimu yetu , kwani tutakapo anzisha mradi wa kusindika ngozi tunatarajia kupata majibu kuhusu uwezo wa wahasibu, madaktari wa wanyama, wataalamu wa sheria, wataalamu wa masoko n.k watakao pata nafsasi ya kufanikisha mradi husika.
 
ni sawa na kumpa mtoto pikipiki aendeshe wakati hawezi kwa kigezo pikipiki imesaza mafuta (full tank).
Hahahahaaa, ni lazima ataenda spidi na bila breki.... What did we expect!!🤣🤣


Pia hizi kampuni zitapewa uangalizi maalumu toka wizara ya viwanda na biashara, na wizara ya ajira kwa vijana pamoja na washirika wake kama SIDO,Asasi za serikali, Asasi zisizo za serikali na taasisi za kifedha. Kupitia fungu la asilimia 10% ndilo litakalo dhaminj makampuni haya kwa ushirikiano wa mabenki ya biashara.
Unasema kweli kabisa. Taasisi zote zinazojinasibu kudili na uwekezaji, uzalishaji, ujasiriamali na masoko. Zifanye kazi zake.

Na kaka umeiweka vizuri sana kwamba: vijana wenye ujuzi wapo wa kutosha. Taasisi zenye dhamana na serikali vipo. Kilichobaki tu ni ile 'orchestration' ya bendi nzima ili kila mmoja afanye kazi anayojinasibu kuwa ni ya kwake katika timu/kikundi. Ova
 
Back
Top Bottom