Mkasi kusahaulika tumboni yachunguzwa

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili imesema inaendelea kufuatilia kwa kina kubaini ukweli wa madai ya ndugu wa marehemu Scolastica Rwambo (43), ambaye alifanyiwa upasuaji hospitalini hapo na mkasi kusahaulika tumboni baada ya upasuaji wa awali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Uhusiano wa Hospitali hiyo, Aminiel Aligaesha, Scolastica alilazwa wadi namba 10 Kibasila akitoka Hospitali ya Amana Septemba 3 akiwa na maumivu ya tumbo.

Alisema baada ya uchunguzi aligundulika kuwa na tatizo lenye uhusiano na magonjwa ya akina mama na Septemba 6 alihamishiwa Sewahaji wadi namba 21 wanamolazwa wanawake ili kufanyiwa uchunguzi zaidi.

“Septemba 28, baada ya kufanyiwa uchunguzi iligundulika kuwa tatizo lake lilihitaji upasuaji. Ushauri nasaha kwa mgonjwa kupima maambukizi ya Ukimwi ulifanyika wakati huo ambapo
aliridhia na vipimo kufanyika,” alisema.

Aligaesha alisema Oktoba mosi daktari wa upasuaji alimwona mgonjwa akampima, akapitia
vipimo vya uchunguzi akagundua kuwa tatizo alilokuwa nalo lilihitaji upasuaji na Oktoba 4 alifanyiwa upasuaji na jopo la madaktari bingwa.

“Matibabu sahihi kulingana na tatizo alilokuwanalo yalifanyika ukiwamo upasuaji. Mgonjwa alirudishwa wodini baada ya upasuaji na aliendelea vizuri na kuruhusiwa Oktoba 10,” alisema.

Aliongeza kuwa Desemba 27 alilazwa tena Kibasila wadi namba 9 safari hiyo akilalamikia maumivu ya tumbo na uchunguzi ulifanyika na hatimaye kubaini kuwa na tatizo lingine la tumbo na hivyo kufanyiwa tena upasuaji.

Alisema baada ya upasuaji huo alirudishwa wadini kuendelea na matibabu na kwa bahati mbaya juzi saa 1.05 usiku alifariki dunia.

Alisema kutokana na madai ya kusahaulika mkasi tumboni, hospitali hiyo ilifanya uchunguzi kubaini ukweli na uchunguzi wa awali kupitia kumbukumbu za matibabu na taarifa kutoka kwa madaktari na wahusika wa mchakato wa tiba kwa marehemu hauoneshi kusahaulika mkasi tumboni baada ya upasuaji wa awali.

Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu, Masau Bwire ambaye ni ndugu wa marehemu, alidai kuwa Scolastica alikuwa akisumbuliwa na tumbo na kupelekwa Muhimbili na baada ya vipimo alifanyiwa upasuaji na baadaye kuruhusiwa.

Baada ya kurudi nyumbani, alidai mgonjwa aliendelea kulalamikia maumivu makali tumboni
hata kushindwa kutembea, lakini waliporejea hospitalini waliambiwa wasiwe na wasiwasi ni mshono ndiyo ulikuwa unamwuma na hivyo wamfanyie mazoezi zaidi.

Bwire alidai kuwa waliendelea kumfanyia mazoezi ingawa alikuwa hawezi na baadaye walimrudisha hospitalini hapo Desemba 17 baada ya hali yake kuzidi kuwa mbaya na Desemba 21 waliahidiwa kumfanyia vipimo ambapo Desemba 23 aliruhusiwa na kutakiwa kurejea Desemba 27.

Alidai kuwa katika vipimo alivyofanyiwa ndugu yao, madaktari waliona mkasi tumboni na kushirikisha ndugu ambao nao waliushuhudia na Desemba 27 alifanyiwa tena upasuaji.

Aliendelea kudai kwamba wao ndugu walitaka wapewe picha ya vipimo hivyo iliyoonesha mkasi tumboni na stakabadhi ya malipo, lakini madaktari na uongozi wa hospitali hiyo, waliwazungusha hata ndugu yao alipofariki dunia.

Kutokana na hilo alisema ndugu wa marehemu wanahitaji picha ya vipimo kwa sababu ni haki yao na hospitali iseme ukweli kuhusu tukio hilo.
 
Kama ni kweli waliomfanyia upasuaji sio jopo la madaktari bingwa...ni jopo la wazembe bingwa...inasikitisha kweli!Pole kwa wafiwa!
 
Nadhani inahitajika uchunguzi zaidi wa hili jambo ili kuridhisha pande zote. Ninavyolelewa mimi si kitu 'rahisi' kusahau mkasi ndani ya tumbo la mgonjwa baada ya kufanya upasuaji. Kwani vifaa vyote, hata pamba zinazotumika, uhesabiwa kabla ya kuanza upasuaji na pia baada ya upasuaji wakati madaktari wako tayari kufunga tumbo. Na kama idadi inatofautiana, basi tumbo halifungwi mpaka kifaa kilichopungua kipatikane. Hii ni taratibu ya kawaida na ya lazima sana kwa kila upasuaji!
 
Back
Top Bottom