Mkapa above the law?: Allegations

Watu wanashindwa ubunge jimboni kwao kwasababu wanashindwa ku deliver, full stop!

Hayo mengine yote ni maneno tu. Mbunge anayejua wajibu wake kwa TZ sio rahisi kabisa
kuangushwa maana anajulikana na pia anakuwa na resources za kutosha.

Mtu kama Mrema hata siku moja asingeliweza kuangushwa ubunge.

Watu wengi wanafikiri ubunge ni kupiga kelele bungeni, sawa kutetea maslahi ya jimbo lako na taifa bungeni ni moja wapo ya majukumu ya mbunge lakini kwa mbunge mchapa kazi hiyo huwakilisha sehemu ndogo sana ya majukumu yake.

Wabunge wanaofanikiwa kwa muda mrefu ni wale ambao wanakuwa na wananchi muda mwingi, wanayaelewa matatizo ya wananchi wao, wanayatatua kila wanapoweza. Sio lazima ujenge barabara za lami lakini at least kule kutatua matatizo yao ya kila siku na kushirikiana nao kujenga jimbo ni jambo kubwa zaidi.

Kundi lingine ni lile la wakaa Dar, ambao wanaenda kwenye majimbo yao kama watalii na kisha utawasikia wakifoka bungeni kama njia ya kufidia muda ambao hawakai kule kwao.

Kimaro kama anataka kuendelea kuwa mbunge asijali akina Mkapa na shemeji zake watasema nini, pamoja na mapambano yake bungeni lakini nguvu kubwa aelekeze kwenye kutatua matatizo ya wananchi wa jimbo lake.
 
Nyie mdanganyeni tu Kimaro, watu kama yeye wanaopiga makelele na kuaibisha wazee wastaafu hawatakiwi ccm. Sasa kibao kimegeuka na itabidi tu aachie jimbo kwa wanaccm wenye kujenga nchi na sio wapiga makelele tu bungeni.

Wakimtoa Kimaro kwa sasa CCM isitegemee kulipata tena hilo jimbo. Hao wananchi wenyewe wa Vunjo shida zimewajaa hadi mdomoni, eti leo waseme wanamwaibisha shemeji yao, Naomba kuwauliza huyo shemeji yao aliwahi kuwasidia nini kwa miaka 10 akiwa Rais?

Nataka kujua kama wakina Papaa Msofe, wakina Richard (RicHill) kama wanaiwakilisha Vunjo yote kwani hawa ndio waliweza kumfaidi huyo shemeji yao .

Kimaro wala usiogope, wenye akili watakupigia debe achana na hao wajinga wachache wanywa mbege na Gongo
 
Hii ni spin tu ya makuwadi wa KIMARO. Kimaro ni tapeli wa kisiasa tu na hilo sitabadilika kulisema. Yeyote anayemjua KIMARO na akawa mkweli moyoni mwake atakubaliana na mimi kuwa alichokifanya KIMARO kilikuwa ni usanii tu. huwezi ukaniambia fisadi wa kimaadili na kiuchumi kama KIMARO akawa na nia nzuri wa watanzania. Ukiangalia mchango wake wenyewe kuhusu fisadi ni wazi ilikuwa ni pre-emptve strike kwa wapinzani na zaidi ni moja ya hatua walizokubaliana wabunge wa CCM kuhakikisha wanatapeli nyoyo za watanzania ili warudishe imani kwao.

Semeni msemavyo lakini kwangu mimi KIMARO is just another Political thug and mediocre waliojaa katika Bunge letu linalopaswa kuwa tukufu.

Nashangaa sana kuwaona watu kama Mzee ES kumshabikia huyu jamaa wakati anajuwa wazi uozo wake. Hata kama ni source ya information na labda mshakaji wa aina fulani lakini ni lazima tuwe makini katika kuwapandisha chati mafisadi kama hawa wanataka tuamini kuwa ni MASIHA wa watanzania........

KIMARO ni fisadi, yale aliyoyasema ni spining tu ya genge lake na hii ni spining tu ya makuwadi wake.....

Tanzanianjema
 
Hii ni spin tu ya makuwadi wa KIMARO. Kimaro ni tapeli wa kisiasa tu na hilo sitabadilika kulisema. Yeyote anayemjua KIMARO na akawa mkweli moyoni mwake atakubaliana na mimi kuwa alichokifanya KIMARO kilikuwa ni usanii tu. Huwezi ukaniambia fisadi wa kimaadili na kiuchumi kama KIMARO akawa na nia nzuri kwa watanzania. Ukiangalia mchango wake wenyewe kuhusu ufisadi ni wazi ilikuwa ni pre-emptve strike kwa wapinzani na zaidi ni moja ya hatua walizokubaliana wabunge wa CCM kuzichukua kuhakikisha wanatapeli nyoyo za watanzania ili warudishe imani kwao.

Semeni msemavyo lakini kwangu mimi KIMARO is just another Political thug and mediocre waliojaa katika Bunge letu linalopaswa kuwa tukufu.

Nashangaa sana kuwaona watu kama Mzee ES kumshabikia huyu jamaa wakati anajua wazi uozo wake. Hata kama ni source ya information na labda mshakaji wa aina fulani lakini ni lazima tuwe makini katika kuwapandisha chati mafisadi kama hawa wanataka tuamini kuwa ni MASIHA wa watanzania........

KIMARO ni fisadi, yale aliyoyasema ni spining tu ya genge lake na hii ni spining tu ya makuwadi wake.....

Tanzanianjema
 
wakati umefika .tanzania tuwachukulie hatua wote wanaovunja sheria za hii nchi yakhe.tusijali kama ni rais uu mbunge.kama uko ushahidi wa kweli ashughulikiwe tu
 
Hivi kusema ukweli bungeni ni kosa! Ndo maana tunajaziwa mitakwimu mingi isiyokuwa na maana na wala haitusaidii watanzania


Mabadiliko huanzia ndani, kuwa na macho sio kujua kusoma
 
Jamani jamani,
Naomba tukumbuke responsibilty inayokuja na priviledge of free media.
tusiseme tu ilimradi tunao uwezo wa kusema.
Lengo liwe kujenga nchi na sio kueneza chuki.
Kama kuna udhaifu wa mtu (au kiongozi) ni bora aambiwe na jinsi ya kujirekebisha si kushangilia kuangika kwake.
Hata fisadi ni mtu, na ameteleza japo kiasi kikubwa.
Simtetei mtu yeyote hapa, kwani tukitafuta mtu ambaye hajafanya kosa ili awe kiongozi tutaishia kutafuta marafiki zetu ambao tutaamua kuficha uovu wao.
Wote waliowahi kupewa nafasi za uongozi kwa kama miaka miwili tu, lazima wameshafanya kosa la kiutawala, hata kama magazetu hayalijui, lakini wananchi wanaathirika.
Kama wananchi hawampendi kimaro, namuonea huruma, kwani hakuna cha kufanya zaidi ya kujiahidi wampende, asifanye kuwa kisingizio cha kutokupendwa ni team ya mashemeji wa old moshi.
hata wapinzani wake kama wanamchukia watoe hoja si kumsingizia anajipendekeza kwa hoja hio moja tu ya mkapa.
 
Aliyemtuhumu Mkapa ajibu mapigo

Francis Chirwa Juni 18, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

Asema ni ukweli daima, fitina mwiko

MBUNGE wa Vunjo, Aloyce Bent Kimaro (CCM), anaamini ametumia haki yake ya kidemokrasia na wajibu wake kama mbunge kumtuhumu rais mstaafu, Benjamin Mkapa kuwa alifanya biashara Ikulu alipokuwa kwenye madaraka.

Akizungumza na Raia Mwema nje ya Bunge wiki hii, jana, baada ya kuwekwa kiti moto na baadhi ya wabunge wenzake waliomtetea Mkapa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) na wabunge wa CCM kilichofanyika hapa mwishoni mwa wiki, Kimaro alisema alichofanya katika suala hilo ni kutekeleza yanayotakiwa na chama chake kwamba mwanachama anatakiwa kusema kweli daima na fitina kwake iwe mwiko.

Alisema kwamba kikubwa kilichomsukuma kusema suala la Mkapa bungeni hivi karibuni ni hali ya Tanzania ya wakati huu kuongozwa kwa sera za uwazi na ukweli katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya Taifa.

Alisema ni wajibu wa Mtanzania mwenye uchungu wa dhati kwa nchi kujitokeza kunyoosha kidole chake kukosoa pale ambapo mambo hayaendi sawa.

“Hakuna ubaya wowote katika kukosoana na kurudishana kwenye msitari kwa manufaa ya Taifa,” alisema Kimaro ambaye hiki ni kipindi chake cha kwanza cha ubunge wa jimbo lake.

Suala hilo la Mkapa ambalo Kimaro alikuwa na ujasiri wa kulisema bungeni na masuala ya sakata la Richmond na EPA yamewagawa wabunge wa CCM ambao dhahiri sasa wako katika makundi yasiyoaminiana.

Raia Mwema imeshuhudia wabunge wawili wa CCM (majina yao yanahifadhiwa), wakifichana walikofikia mjini hapa. Mmoja alimwuliza mwenzake kama amesikia kwamba amefikia Dodoma Hotel hivyo kutaka kujua yuko kwenye chumba gani.

Aliyeulizwa alikiri kwamba amefikia hapo lakini alitaka kuelezwa ni kwani mwulizaji anataka kujua hata chumba alichofikia. “Bwana mimi si swahiba wako? Huwezi kunitajia, unaamini kabisa nitakudhuru? Alimwuliza. Wote waliishia kucheka lakini aliyefikia Dodoma Hotel hakusema chumba chake ni namba ngapi.

Kuwapo kwa makundi dnani ya CCM na kuibuka kwa uvumi wa suala la ushirikina ambalo inadaiwa kwamba mbunge mmoja mwandamizi aliyekuwa na wadhifa wa uwaziri alinyunyuzia dawa kwenye viti kadhaa kikiwamo cha Spika, ni mambo yanayowafanya wabunge wa chama hicho tawala wachekeane ‘kichina’ na hata kufikia kupashana ukweli.

Tayari kuna madai kwamba Mbunge wa Same, Anne Kilango Malecela juzi kabla ya kuanza kikao cha Bunge kuanza alimjia juu Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba. Inadaiwa ya kuwa Mama Kilango alikerwa na mchango wa Mbunge huyo wa Kigoma Mjini ambapo alimtaja kwa jina mbunge huyo.

Raia Mwema imeelezwa ya kuwa Serukamba katika mchango wake kwenye NEC alionyeshwa kukerwa na wabunge wanaoshinikiza wale wanaotajwa katika kashfa mbalimbali wawajibishwe kwani kujiuzulu peke yake nyadhifa zao hakutoshi. Mama Kilango ni mmoja wa wabunge waliotajwa kuwa na msimamo mkali dhidi ya watuhumniwa wa kashfa hizo mbali mbali.

Pia katika suala la ‘kushikana uchawi’, kuna madai kwamba sakata hilo limesukwa na kundi linalotaka kumchafulia jina waziri huyo wa zamani.

Katibu wa Uenezi wa CCCM, John Chiligati, amejaribu kulipoza sakata hilo akidai kwamba ni uvumi tu usiyostahili kupewa nafasi.

Aliwaambia waandishi wa habari kwamba suala hilo lilijitokeza katika mkutano wa NEC na hilo lilipoibuka ikathibishwa kwamba mtu huyo mbunge anayedhaniwa kuwa mshirikina na mtumishi wa Bunge ni kweli waliingia bungeni lakini kwa nia ya ‘mtuhumiwa’ kuonyeshwa kiti chake kipya baada ya kuuvua uwaziri.Hakuna jina lolote lililotajwa.

Lakini ilikuwa dhahiri ya kuwa suala zima la sakata hilo la ushirikina ni utata mtupu kwani hata Spika wa Bunge, Samwel Sitta alikiri kuwapo kwa utata kuhusu siku yenyewe na saa. Alisema kwa vile suala hilo linachanguzwa rasmi na Polisi na Usalama wa Taifa, wananchi wasubiri matokeo ya uchunguzi huo.

Na katika hatua nyingine, Mbunge wa Kigoma Mashariki, Zitto Kabwe amesema kwamba Bajeti ya mwaka huu si ya mwananchi kama inavyoitwa kwa sababu kodi ambazo zilipandishwa mwaka jana hazijashushwa na kurudishwa katika viwango vya mwaka 20006/2007.

Akijadili hotuma ya Bajeti iliyowasilishwa Alhamisi ilioyipita na Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango, Mustafa Mkulo, Zitto ambaye ni Mbunge kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alisema ya kuwa Bajeti hiyo itakuwa ya wananchi iwapo tu kodi hizo zitakuwa zimeshushwa.

“Lakini kitendo cha kuziacha kodi hizo kama zilivyo bado kitaendelea kufanya mfumuko wa bei uweze kuendelea,’’ alisema na kuongeza kwamba uchumi wa Tanzania umebadilika kwa kutoka katika uchumi unaotegemea kilimo kwenda kwenye uchumi unaotegemea huduma kwa asilimia 47.3. Alisema asilimia 28.2 tu ndiyo kilimo.

Akionyesha kushangazwa kwake kwamba mipango ya Taifa bado ni kana kwamba uchumi unategemea kilimo Zitto alisema: “Tumeonyesha wasiwasi wetu kutokana na takwimu ambazo zimetolewa lakini mipango ya nchi ambayo uchumi wake ni takriban zaidi ya nusu inategemea kilimo,” alisema.

Alisema Bajeti ya mwaka huu ni mwendelezo wa bajeti zilizopita ambazo huduma ilikuwa ina mchango mdogo sana katika uchumi. “Kwa hiyo kwa vyovyote vile kutokana na bajeti hii ni vigumu sana changamoto za sasa za nchi kuweza kujibiwa,” aliongeza.

Alilaumu pia mwenendo wa ukuaji wa sekta ya madini nchini. “Sekta ya madini ambayo ndiyo ilikuwa sekta inayoongoza kwa ukuaji, hivi sasa imekuwa sekta ya pili au ya tatu kwa ukuaji. Ukuaji wa uchumi sasa unategemea sekta ya mawasiliano na sekta ya mawasiliano kwa kiasi kikubwa bado haichangii vya kutosha katika mapato ya Serikali.

“Kuna baadhi ya maeneo ambayo Waziri wa Fedha ameonyesha ili Serikali iweze kukusanya fedha zaidi, lakini wakiangalia maeneo hayo bado eneo lenyewe la sekta ya madini halikuangaliwa hata kidogo na huwa tunapata wasiwasi mkubwa sana kwamba baadhi ya mapendekezo yote hayajachukuliwa, matokeo Bajeti inaangalia zaidi kupandisha kodi kwa watu ambao ni walaji na kuacha kabisa kupandisha kodi kwa watu ambao ni wale wazalishaji kwa maana ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi na wawekezaji wa nje peke yake,” alisema.

Alisema bajeti imeshindwa kabisa kukusanya kodi zinazostahili kwenye madini akiongeza: “Nashindwa kuelewa ni kwa sababu gani inafahamika wazi kabisa kwamba mwaka 1997, na mheshimiwa Hamad Rashid Mohammed ameielezea hapa. Bunge hili lilitunga sheria ambayo ilitoa unafuu usio na lazima kwa makampuni ya madini kwa kiasi cha asilimia 15, unafuu ambao umelifanya Taifa lipoteze shilingi bilioni 883 katika kipindi cha miaka 10 tangu sekta ya madini ianze kukua katika Taifa Letu,” alisema.
 
Mtauza magazeti kwa hesabu chanya maana hicho kichwa cha habari na stori iliyomo kwakweli ni shughuli pevu.
Kila la heri na usagaji
 
Mbunge: Msiwasakame Chenge, Lowassa, Mkapa

Habari Zinazoshabihiana
• Mkapa, Lowassa na Chenge waibuliwa mapya 28.05.2008 [Soma]
• Chenge: Wabaya wangu wamenizulia 08.05.2008 [Soma]
• Mbunge aandaa ibada ya miaka 40 bungeni 06.12.2006 [Soma]

*Mwingine ahoji kuhusu suala la Kadhi


Na Amir Mhando, Dodoma

MBUNGE wa Buchosa, Bw. Samuel Chitalilo (CCM), amewashangaa wanaomsakama aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Bw. Andrew Chenge, kwa kuwa hakuvunja nyumba ya mtu na kushangaa pia wanaomsakama aliyekuwa Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa.

Pia Mbunge wa Kigoma Kusini, Bw. Manju Msambya (CCM) naye alitishia
kuwasilisha hoja binafsi bungeni katika mkutano ujao wa Bunge kama Serikali isipolipatia ufumbuzi suala la kuwapo Mahakama ya Kadhi, huku Mbunge wa Viti Maalumu, Bibi Savelina Mwijage (CUF), akisema Rais Jakaya Kikwete anadanganywa na washauri wake kuhusu suala la Muafaka wa Zanzibar, huku Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Bibi Lucy Owenya akihoji ilipo ripoti ya Tume ya Lowassa iliyochunguza suala la ujenzi wa ghorofa.

Akichangia mjadala huo, Bw. Chitalilo alisema kuna hatari ya Bunge kugeuzwa sehemu ya majungu na kutolea mfano kuwa Bw. Chenge anasakamwa bure wakati hakuvunja nyumba ya mtu na kuhoji kama kuna nyumba amevunja kungekuwa na haja ya kulalamika na kusema pia kwamba Bw. Lowassa aliacha wadhifa wake bila kosa, ila alifanya hivyo kutokana na suala la uwajibikaji na kwamba hata angekuwa yeye angeachia.

Pia alishangaa suala la kupakaziwa uchawi na kusema kama mambo hayo yakiachwa yaendelee, ipo siku atapakaziwa Spika, na baada ya kauli hiyo, Spika alimkatisha na kumtaka arejee kwenye hoja.

Pia alihoji suala la baadhi ya wabunge kumsema vibaya Rais mstaafu Benjamin Mkapa, licha ya mambo makubwa aliyoyafanya nchini na kusisitiza kuwa kuna Watanzania hawapendi kusikia akisemwa vibaya.

Katika mchango wake, Bi Owenya aliulizia ilipo ripoti ya Tume ya Lowassa ambayo iliundwa baada ya kuanguka kwa ghorofa la hoteli ya Chang'ombe Village Inn, Temeke Dar es Salaam miaka miwili iliyopita na kutaka iwekwe hadharani.

Pia juzi akisoma maoni ya kambi ya upinzani katika hotuba hiyo, Mbunge
wa Karatu, Dkt. Wilbroad Slaa (CHADEMA), naye alihoji kuhusiana na ilipo ripoti hiyo, huku Watanzania wakizidi kuangamia kwa maghorofa kuendelea kuporomoka.

Kwa upande wake, jana Bw. Msambya alihoji suala la Mahakama ya Kadhi na kuhoji Serikali inapata kigugumizi gani kuhusiana na suala hilo, ambapo alitishia kuwasilisha hoja binafsi katika mkutano ujao kuhusiana na suala hilo kama asipopatiwa ufumbuzi na kwamba watafikishana pabaya.

Naye Mbunge wa Sumve, Bw. Richard Ndassa (CCM) katika mchango wake
alisema anaamini masuala ya EPA na Richmond Serikali imeyachukulia uzito unaostahili.

Katika mchango wake, Bibi Mwijage alisema mazungumzo ya Muafaka kuhusiana
na Zanzibar, washauri wanamdanganya Rais Kikwete na wanampotezea muda, hivyo asiwasikilize, vinginevyo atapoteza imani kwa wananchi wake.

Hali hiyo pia ilizungumzwa na Mbunge wa Gando, Bw. Khalifa Suleiman Khalifa, ambaye alishauri Rais aende bungeni apeleke suala hilo, ili wamsaidie kulijadili na kulipatia ufumbuzi kuliko ilivyo sasa.
 
Hii thread ilipaswa kuwa na heading: "Bunge lawaka moto." Labda hapo watu wengi wangechangia.
 
Hii thread ilipaswa kuwa na heading: "Bunge lawaka moto." Labda hapo watu wengi wangechangia.

Hapana, nadhani imedoda kwa ufinyu wa mtetezi wa hao akina Chenge, Mkapa na Lowassa.
Nani mtetezi wao: Samuel Chitalilo - Mbunge wa CCM Buchosa.
Sifa yake kuu: Ali-forge vyeti vya Form IV na VI wakati elimu yake halali ni Std VII.

Hii ni sawa na Justin Nyari kumtetea Sinclair, au Manji kumtetea Rostam, au Yona kumtetea Mramba, au Babu Sambeke kumtetea Cheupee (wale wakazi wa Moshi wataelewa hapa).
 
Jana bungeni, mbunge machachari wa Kwela na mmoja wa wajasiriamali marufu wa nchi hii Chrissant Mzindakaya alitoa kauli kwa serikali kuwa “…itupe maelezo juu ya mambo yanayoandikwa kuhusu Mkapa…”.Akiongea kwa ujasiri na kuoneshwa kukerwa alidai kuwa siyo vyema kwa serikali kukaa kimya huku kiongozi mahiri kama Mkapa akiendelea kuandikwa na kusemwa vibaya kila siku.Alisisitiza Mzindakaya kuwa “sifa yetu(akimaanisha watanzania) ni kulinda na kuheshimu viongozi wetu wakuu”.

Kauli hii ya Mzindakaya imekuja baada ya kuibuka kwa tuhuma za waziwazi kumhusu Mkapa kuwa alijihusisha na vitendo ambavyo vilikuwa kinyume na maadili ya utumishi wa umma tena kwa ngazi kubwa ya uras.

Mzindakaya anataka serikali itoe tamko juu ya kusemwa huko kubaya kwa rais mstaafu.Kwanini CCM wanaona ajabu sana pale tuhuma zinapokuwa zinarushiwa upande wao? Mara zote wana CCM wamekuwa wakitafuta namna ya kuzigeuza tuhuma zinazotolewa hasa na wapinzani na kuanikwa na vyombo vya habari kuwa uzushi na propaganda.

Mzindakaya ni mmoja kati ya wabunge wenye historia ya kuibua ‘mabomu’ yaliyokuwa yanawahusu vigogo wa serikali.Sina shaka kuwa anaelewa fika uzito wa tuhuma zinazomkabili Mkapa na anatambua ni kwa kiasi gani tuhuma hizo zinahusishwa na mambo nyeti kama vile kuuzwa kwa mgodi wa makaa ya mawe wa kiwira, kuendesha biashara ikulu, kuhusika na skendo la meremeta na TANGOLD pamoja na ishu ya uchotwaji wa mabilioni ya EPA kutokea wakati wa utawala wake.

Kama haya yote anayafahamu Mzindakaya inakuwaje anaita huko ni kusemwa vibaya?
Kwanini Mzindakaya asiiombe serikali kutokukaa kimya na badala yake iruhusu uchunguzi huru wa kimahakama kusudi ukweli na uongo ujulikane?.Kama Mkapa amesemwa vibaya na kuchafuliwa jina ni nani mwenye kuweza kutanabaisha hilo zaidi ya vyombo vya sheria?Mzindakaya ni nani na CCM ni nini hata watoe kauli za kumsafisha au kutaka kumsafisha mtu?.Kwani Mkapa ni nani naye asisemwe vibaya kama katenda vibaya?

Tujuavyo ni kuwa tuhuma zozote zile zinachunguzwa kwa lengo la kuzithibitisha na wala hazizimwi kwa hotuba za kisiasa wala vikao vya kisiasa.Kikwete ndiye aliyekuwa wa kwanza kutuambia tumwache mzee mkapa apumzike.Pamoja na tuhuma dhidi ya Mkapa kuendelea kushikiwa bango kikwete ameendelea kutia pamba masikioni.Kama siyo kufutika mambo ni nini?.

Haya ya Mzindakaya ni mwendelezo wa utamaduni wa CCM kulindana na kufutika maovu yao.Ni ushahidi kuwa kila ovu linalofanywa na viongozi lina baraka za CCM au linaifaidisha CCM pia.Mzindakaya anatukumbusha wapenda haki na utawala bora kuwa sheria tulizonazo siyo ‘msumeno’ kwa kuwa hazikati kuwili.Mzindakaya anataka wanaosema na kuandika kuhusu Mkapa waache kwani tunachafua jina zuri la Mkapa kimataifa.Kauli yake ilikuwa ni sawa na kusema kuwa wanaosema na kuandika kuhusu Mkapa wawajibishwe.

Mzindakaya amefikisha ujumbe kwa jamii kuwa CCM kamwe hakiwezi kurejea zama za Hayati mwalimu Nyerere alipokijengea misingi ya kuwa chama cha wakulima na wafanyakazi.Enzi za Mwalimu Nyerere CCM na serikali havikuwa vyombo vya kusafisha majina na haiba za watu.CCM ya miaka hiyo ilijiheshimu na ikaheshimika.Kilikuwa ni chama kilichojali maslahi ya wanyonge na kupingana na dhuluma na kilijenga serikali adilifu na iliyojali kumtetea mnyonge na siyo mnyongaji.

Mzindakaya ni uzao wa CCM ya wakati wa Nyerere Lakini kauli yake ya kutaka Mkapa atafutiwe mbeleko na serikali inatutoa imani kabisa juu yake.
Hivi ni mpaka lini wanasiasa wetu wataendelea kuyafanya mambo nyeti kama ufisadi na mengineyo porojo za kisiasa?
 
Mbeleko ipi? ipi? kabebewa mbeleko ya kanga kapasua, ya Gunia kapasua, ya Kiloba kapasua,Turubai kapasua, habebeki huyo na sasa mwacheni adondoke kivyakevyake
 
Mkapa aiponza Serikali

2008-06-27 19:53:03
Na Emmanuel Lengwa, Jijini

Sakata la Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Bw. Benjamini Mkapa kuhusishwa na tuhuma mbalimbali za kutumia madaraka kwa kujilimbikizia mali akiwa madarakani sasa limechukua sura mpya baada ya Serikali kugeuziwa kibao na kubanwa ifafanue kuhusu `dili` zote anazotuhumiwa Rais huyo mstaafu badala ya kuendelea kukaa kimya.

Serikali imetakiwa ifafanue kila kitu kuhusiana na tuhuma zinazoelekezwa kwa Mkapa ikiwa ni njia mojawapo ya kuzuia shutuma zinazoelekezwa kwake, ambazo pengine zitakoma baada ya maelezo ya kina kutolewa na kila kitu kuwekwa wazi.

Akizungumza na Alasiri leo asubuhi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Sengondo Mvungi, amesema baada ya mwenyewe Mkapa kuwa kimya na huku tuhuma dhidi yake zikiendelea kuvuma kila kukicha, ni jukumu la Serikali kuingilia kati na kuwaeleza Watanzania juu ya ukweli wa mamabo hayo.

Akasema kwa anvayoamini, mbali na Mkapa mwenyewe, Serikali iliyopo madarakani ndiyo inayoweza kufafanua kwa undani na kwamba kunyamaza kwake, kunajenga hisia kuwa pengine, nayo inaficha baadhi ya mambo yaliyo kinyume na maadili ya uongozi na hivyo kuichafua machoni mwa wananchi.

``Ukimbana Mkapa atakusaidia nini? Suala la Mkapa sio kubwa, kwa sababu yeye ameshaondoka Serikalini... tunapozungumzia ufisadi tunaizungumzia Serikali maana ndiyo itakayoonekana imeshindwa kupambana na ufisadi,`` akasema Dk. Mvungi.

Aidha, Dk. Mvungi ambaye mwaka 2005 aligombea urais kupitia chama cha NCCR- Mageuzi, amesema jambo la busara sasa ni kwa wananchi kuibana Serikali, kwani yenyewe ina dola na mamlaka yote ya kuweza kupata ukweli wa tuhuma zinazoelekezwa kwa Mkapa.

``Serikali iliyopo madarakani ndiyo inayopaswa kuwajibika. Hata kama ni kwa Mkapa, inapaswa kuwatuma tu makachero wake na kupata ukweli sahihi kutoka kwake. Binafsi naona tatizo lipo kwa Serikali yenyewe,`` akasema Dk. Mvungi.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Jimbo la Kwela, Mhe. Dk. Chrisant Mzindakaya, ameitaka Serikali itoe maelezo ya kutosha, ya kwanini imeshindwa kuvikemea vyombo vya habari kwa kile alichosema kuwa ni kwa kumuandika vibaya.

``Nataka Serikali itupe maelezo jinsi anavyoandikwa Rais mstaafu Mkapa huku (yenyewe) ikiwa imekaa kimya,``akasema Dk. Mzindakaya jana,w akati akichangia hotuba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mizengo Pinda.

Baadhi ya tuhuma zinazoelekezwa kwa Mkapa ni pamoja na zile zilizowahi kutolewa na Mbunge wa Vunjo, Mhe. Victor Kimaro (CCM) kuhusiana na Rais huyo mstaafu kushirikiana na aliyekuwa Waziri wake wa Nishati na Madini Bw. Daniel Yona katika kumiliki mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira.

Tuhuma nyingine miongoni mwa zile zinazoelekezwa kwake ni pamoja na kudaiwa kukiuka maadili ya uongozi kwa kufanya biashara akiwa Ikulu, kumiliki shamba kubwa la miwa lililopo Mtibwa Morogoro na kumiliki majumba kadhaa ya kifahari Jijini.

Hata hivyo, mwenyewe alishawahi kusema akiwa kijijini kwao Lupaso kule Masasi Mtwara kuwa yote yanayosemwa juu yake ni uongo!

SOURCE: Alasiri
 
[QUOTE


Hata hivyo, mwenyewe alishawahi kusema akiwa kijijini kwao Lupaso kule Masasi Mtwara kuwa yote yanayosemwa juu yake ni uongo!

SOURCE: Alasiri [/size][/color][/QUOTE]

Nani ataenda kwa waliompa kula na kusema mimi mwizi. Anafahamu fika ni wapi kwa kwenda kama anataka kukanusha ila hafanyi hivyo, tuelewe nini? basi ni kweli hayo yanayosemwa.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom